Na Mwamvua Mwinyi, 

WANAFUNZI wa shule za msingi na sekondari katika Kata za Pichandege na Viziwaziwa, Manispaa ya Kibaha, wametakiwa kutokubali vitisho wanapofanyiwa vitendo vya ukatili, ulawiti, ubakaji na unyanyasaji, bali watoe taarifa kwa polisi, viongozi wa serikali za mitaa na kata, walimu pamoja na wazazi ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Wito huo umetolewa Novemba 3, 2026 na timu ya wataalamu wa sheria na ustawi wa jamii kupitia Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), Manispaa ya Kibaha, inayoongozwa na Wakili Revocatus Thadeo Mathew, iliyofika katika shule za sekondari za Filbert Bay, East Coast na Pichandege pamoja na shule za msingi na sekondari katika Kata ya Viziwaziwa.

Akitoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, Wakili wa Serikali Modykauye Benedict alisema ukatili dhidi ya watoto hauwahusu wasichana pekee, bali wavulana pia wanaweza kuwa waathirika wa vitendo hivyo.

Aliwataka wanafunzi kutokubali vitisho vinavyotolewa na watu wanaowafanyia ukatili, huku akiwahimiza kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa wanapoona dalili za ukatili badala ya kusubiri madhara yatokee.

“Msioogope kutoa taarifa za vitendo vya ukatili, msiharibu vielelezo kwa sababu vitasaidia kutoa ushahidi wakati wa kesi za ukatili, ili tukomeshe vitendo hivi visiendelee,” alisema.

Kupitia kampeni hiyo, wanafunzi katika kata hizo wamepatiwa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uelewa wa kutambua, kujikinga na kutoa taarifa dhidi ya vitendo hivyo katika jamii.

Watoa huduma ya msaada wa kisheria wa Mama Samia wamewafundisha wanafunzi kutambua aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia, haki zao na namna ya kuchukua hatua wanapokumbana na vitendo hivyo, huku wakisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Sambamba na elimu hiyo, watoa huduma walitoa mafunzo kwa Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata za Pichandege na Viziwaziwa kuhusu namna bora ya kushughulikia na kutatua migogoro inayojitokeza katika jamii kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Aidha, wananchi walipata fursa ya kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili, kusikilizwa na kupatiwa ushauri pamoja na ufafanuzi wa masuala ya kisheria, yakiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, familia na haki za watoto.

Akifafanua kuhusu kampeni hiyo, Wakili Revocatus Thadeo Mathew alisema wananchi wanapata fursa ya kueleza kero zao na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sheria, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa haki zao na kuimarisha upatikanaji wa haki katika jamii.

Huduma hizo zinaendelea kutolewa katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao, kuimarisha upatikanaji wa haki na kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...