WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa wataalamu wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi duniani ni ishara ya dhamira ya nchi hiyo kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kutumia sayansi katika kujenga maendeleo endelevu.
Amesema athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi si tishio la siku zijazo pekee, bali tayari zinaonekana duniani kote, hasa katika nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika na visiwa vidogo.
Mbarawa amesema hayo leo Novemba 2, 2026 wakati akiwasilisha hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika ufunguzi wa Mkutano wa tatu wa Wataalamu wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), jijini Arusha.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha sahihi na inayozingatia unyeti wa kisera katika mawasilisho ya kisayansi ya IPCC, akieleza kuwa waandishi wanapaswa kuchagua maneno kwa umakini ili kuhakikisha taarifa zinabaki kuwa sahihi kisayansi, zinaaminika na zinachangia katika michakato ya maamuzi na sera za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Mkutano huo umeanza leo Novemba 2 na utamalizika Novemba, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha PAPU jijini Arusha, ukiwakutanisha wataalamu bingwa wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kutoka nchi 75 duniani.
Lengo la mkutano huo ni kuimarisha mchango wa Kikosi Kazi namba Moja cha Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi katika kuandaa Tathmini ya Saba ya IPCC kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi.
Mkutano huo umeandaliwa na IPCC kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TMA, ukiwa na lengo la kutoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya wanasayansi wa Tanzania, Afrika na wa kimataifa, pamoja na kuongeza ushiriki wa Afrika katika mchakato wa IPCC.





.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...