-Asema mikakati ya maendeleo ya sekta iwe na matokeo yanayopimika

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameitaka Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi na taasisi zake kuhakikisha tathmini, mipango na uwekezaji katika sekta ya hiyo vinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuchochea mageuzi ya kiuchumi, kuimarisha ushindani wa Tanzania na kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema hayo leo, Novemba 16, 2026, wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Uchukuzi, akisisitiza umuhimu wa wadau kuweka mikakati yenye uhalisia, inayotekelezeka na inayozingatia vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ina dhamira ya kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni muhimu kuimarisha muunganiko wa bandari, reli, barabara, viwanja vya ndege na usafiri wa majini ili kurahisisha biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza tija ya uchumi.

“Mafanikio ya uwekezaji katika sekta hii hayapaswi kupimwa kwa idadi ya miradi inayotekelezwa pekee, bali kwa mchango wake katika kupunguza muda na gharama za safari, kuimarisha usalama, kurahisisha biashara na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi”.

Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia na kuendesha miradi ya miundombinu kupitia mifumo bunifu ya ufadhili na ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) ili Serikali iweze kuelekeza rasilimali zake katika maeneo mengine muhimu ya utoaji huduma za kijamii.

Amesisitiza kuwa Mkutano wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Uchukuzi unapaswa kuwa jukwaa madhubuti la uwajibikaji na kupima matokeo ya utekelezaji badala ya kuwa mkutano wa kawaida wa mwaka.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya uchukuzi unakuwa jumuishi, salama, wenye ufanisi na endelevu kifedha ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Mapema, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, alisema Serikali imepiga hatua katika kuendeleza miundombinu na kuboresha huduma za uchukuzi kwa kuendelea na ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa (SGR), maandalizi ya kuimarisha Reli ya TAZARA, kuboresha barabara, kupanua huduma za bandari na usafiri wa anga na majini.

Amesema uwekezaji huo unaimarisha muunganiko wa maeneo mbalimbali, kuchochea biashara ya kikanda na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati ya kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki na Kati. Hata hivyo, amebainisha changamoto za upatikanaji wa fedha endelevu, matengenezo ya miundombinu na ufanisi wa utekelezaji wa miradi.

“Pamoja na mafanikio hayo, kipaumbele chetu hakipaswi kuwa ujenzi wa miundombinu pekee, bali kuhakikisha kila uwekezaji unaleta manufaa halisi ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu,” amesema Profesa Mbarawa.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...