Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameitaka Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuhakikisha inaweka mifumo madhubuti ya utunzaji na matengenezo ya miundombinu ya chuo hicho ili iendelee kutoa huduma bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa mafunzo ya Udaktari wa Wanyama katika chuo hicho, amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya SUA. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha miradi inayotekelezwa inasimamiwa ipasavyo ili thamani ya fedha zilizowekezwa ionekane.

Akitoa taarifa ya chuo  Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Dkt. Philip Isdori Mpango, amesema tafiti nyingi zinazofanywa na chuo hicho bado zinategemea ufadhili kutoka kwa wadau wa nje ya nchi.

Aidha ameiomba Serikali, kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine wa ndani, kuongeza fedha za kugharamia tafiti kupitia vyanzo vya ndani ili kupunguza utegemezi wa ufadhili wa nje na kuhakikisha tafiti hizo zinaakisi vipaumbele vya kitaifa pamoja na mahitaji ya maendeleo ya nchi.

Pia, Dkt. Mpango ameiomba Serikali kusaidia ujenzi wa barabara ya kuingia chuoni hapo kwa kiwango cha lami ili iendane na hadhi ya chuo hicho kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) na Mkuu wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya ya SUA, Profesa Esron Karimuribo, amesema maadhimisho hayo ya miaka 50 yanaweka kumbukumbu muhimu ya mchango wa madaktari wa wanyama waliohitimu katika chuo hicho.

Profesa Karimuribo ameiomba Serikali kufanya marekebisho ya muundo wa kiutawala katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Sekretarieti za Mikoa kwa kuimarisha huduma za afya ya wanyama kuanzia ngazi ya wizara hadi vijijini. Ameshauri kuanzishwa kwa vitengo maalumu vya huduma za mifugo katika halmashauri zote nchini, vitakavyoongozwa na madaktari wa wanyama katika ngazi za wilaya na mikoa.

Vilevile, ameiomba Serikali kugharamia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Udaktari wa Wanyama, akieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya lazima ya mchakato wa kitaaluma na mwanafunzi hawezi kuhitimu bila kuyatekeleza.

Maadhimisho hayo yalianza Novemba 22 na kutamatishwa Leo November 2027, 2026, kwa shughuli mbalimbali zikiwemo mbio za marathon, zilizofuatwa na huduma za uchunguzi na matibabu ya wanyama zilizotolewa na madaktari wa wanyama katika kata na wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro.


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...