Na Janeth Raphael - MichuziTv
Ikiwa taifa liko katika juhudi za kujenga jamii yenye maadili, amani, mshikamano na uwajibikaji, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limetakiwa kuendelea kutumia nafasi yake katika kuimarisha misingi hiyo na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose Mary Senyamule, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 6 wa Wachungaji wa KKKT unaofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, jijini Dodoma.
Senyamule amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa KKKT katika maendeleo ya taifa, ikieleza kuwa kwa miaka mingi kanisa hilo limekuwa mshirika muhimu katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.
Amesema huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, malezi ya vijana, huduma kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na misaada ya kijamii na juhudi za kupambana na umaskini.
Senyamule amesema pamoja na huduma za kijamii, KKKT imeendelea kuwa mdau katika shughuli za kiuchumi na uwekezaji, huku viongozi wa dini wakiwa na nafasi ya kipekee katika kujenga maadili mema, kudumisha amani na kuimarisha umoja wa kitaifa.
“Viongozi wa dini tunatambua kuwa mnaaminika sana na wananchi kuliko taasisi na watu wengine. Kwa sababu hiyo, mafundisho na matendo yenu yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika familia, jumuiya na taifa kwa ujumla,” amesema.
Amesema taifa linahitaji viongozi wa dini wanaoweza kuwa sauti ya matumaini na faraja kwa wananchi, hususan wale wanaopitia changamoto mbalimbali za maisha.
Senyamule amewataka wachungaji na viongozi wa dini kwa ujumla kuendelea kuwa sauti ya faraja kwa wenye huzuni, matumaini kwa waliokata tamaa na msaada kwa watu walio katika mazingira magumu.
Katika eneo la malezi, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha malezi ya kiroho na kimaadili, hasa kwa watoto na vijana, ili kuwaandaa kuwa kizazi chenye maadili, uwajibikaji na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Aidha, amewataka wachungaji kuendelea kutoa elimu inayowajenga wananchi katika nyanja za kiroho, kijamii na kiuchumi, huku wakihimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, kutumia fursa zilizopo na kushiriki katika shughuli halali za maendeleo.
“Imani iendelee kusambaa sambamba na matendo yanayoleta ustawi wa mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla,” amesema.
Mkutano Mkuu wa 6 wa Wachungaji wa KKKT umehusisha wachungaji kutoka Dayosisi 28 za KKKT na umefunguliwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Alex Malalusa.
Mkutano huo unatarajiwa kuendelea hadi Septemba 17, 2025, ukiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya kanisa, malezi ya kiroho na nafasi ya kanisa katika jamii na maendeleo ya taifa.



































.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)








.jpeg)
.jpeg)

