"HABARI JAMII"
Showing posts with label HABARI JAMII. Show all posts
BALOZI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema katika kipindi cha miezi michache iliyopita nchi hizi mbili zimepiga hatua katika sekta muhimu tano na kuweka matumaini ya ushirikiano zaidi katika sekta zingine.

Akizungumza leo asubuhi na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Algeria kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers, Balozi Matinyi alizitaja sekta hizo ambazo Ubalozi umefanikisha zipige hatua kuwa ni za viwanda vya dawa za tiba, nishati, elimu ya juu, biashara ya mazao ya kilimo na ufugaji wa nyuki.

Balozi Matinyi alisema juhudi za sasa za serikali za nchi hizi mbili zinafuatia maelekezo ya marais wa nchi hizi kwamba baada ya kuainisha maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Algeria sasa ni wakati wa kuyaweka katika vitendo kwa maendeleo ya wananchi wake.

“Nilipowasilisha hati zangu za utambulisho mnamo tarehe 10 Juni, 2026, Rais Abdelmadgid Tebboune alisisitiza kwamba sasa umefika wakati wa kuuweka ushirikiano wetu katika vitendo na wakati nikija Algeria Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza kwamba kutokana na ushirikiano wetu wa kimkakati sasa ni wakati wa kupata manufaa kwa ajili ya wananchi wetu” alisema Balozi Matinyi.

Akielezea mafanikio hayo, Balozi Matinyi alisema katika sekta ya viwanda vya dawa za tiba Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP) na kiwanda cha dawa cha Serikali ya Algeria cha Saidal Group, zitafanya ziara nchini mwezi Oktoba kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ya Tanzania (TMDA) ili kujadili namna ya kushirikiana kitaalamu.

Balozi Matinyi alisema kwa kuzingatia kuwa katika ukaguzi wa dawa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha juu (ML3) mwaka 2018 kwa mujibu wa tathmini ya kimataifa (GBT) ya Shirika la Afya la Dunia (WHO) huku Algeria ikiwa na theluthi moja ya viwanda 690 vya dawa Afrika, nchi hizi mbili zinaweza kufikia mafanikio makubwa.

“Kampuni ya dawa ya Hikma nayo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya ushirikiano katika biashara na uwekezaji na kampuni tanzu ya Bohari Kuu la Dawa (MSD) ya Medipharm ili kuhudumia nchi za ukanda wa mashariki, kati na kusini mwa Afrika,” alisema Balozi Matinyi na kuongeza: “Kampuni nyingine binafsi ya Frater Razes inakuja nchini mwezi Oktoba pia kujadiliana na Serikali namna ya kuanza ushirikiano katika biashara na uwekezaji,” alisema Balozi Matinyi.

Katika sekta ya nishati Balozi Matinyi alisema Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), ilifanya ziara nchini Algeria mwezi Julai kujadiliana namna ya kushirikiana kiufundi na kutembelea maeneo ya kiufundi ya Shirika la Umeme na Gesi la Algeria (SONELGAZ) na kiwanda cha vifaa vya umeme cha GISB Electric.

Katika ushirikiano kwenye sekta ya elimu Balozi Matinyi alisema: “Algeria ilitoa nafasi 176 za masomo ya juu kwa wanafunzi wa Tanzania ambapo Serikali imeamua kuchagua wanafunzi wenye ufaulu wa juu 150 chini ya mpango wa Samia Scholarship Extended na wanakuja kwa ajili ya masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na tiba.”

Akizungumzia ushirikiano kwenye biashara ya mazao ya kilimo, Balozi Matinyi aliitaja kampuni ya Sarl Anacard’Or ya Algeria kwamba imenunua ghala la kuhifadhia korosho mkoani Mtwara kwa ajili ya kuzileta Algeria. Kampuni hiyo pia inakamilisha mipango ya kuanza ubanguaji korosho nchini Tanzania.

Aidha, Balozi Matinyi alisema kampuni nyingine ya Algeria ya kutengeneza mashine za kusindika mazao ya kilimo na dawa pamoja na kufungasha ya CAM Sarl imekubali kutoa ushirikiano kwa Tanzania wa kupata mashine hizo ili kuongezea thamani mazao ya kilimo kabla ya kuuzwa kwenye soko la dunia.

Balozi Matinyi alitaarifu zaidi kuwa Tanzania na Algeria zinatarajia kuanza ushirikiano katika sekta ya ufugaji wa nyuki na mazao yake kufuatia ziara ya maafisa na wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na wadau wa sekta binafsi mwezi Septemba 2026 ambapo walikubaliana na wenzao wa Algeria kuanza ushirikiano.

Balozi Matinyi alimaliza taarifa yake kwa waandishi wa Algeria kwa kuwakaribisha wananchi wa Algeria kuja nchini kujionea fahari ya hifadhi za bonde la Ngorongoro na Serengeti, mlima Kilimanjaro na vilevile kuja kufurahia fukwe maridhawa za Zanzibar.

Algiers, Septemba 30, 2026.
Na. Mwandishi Wetu, Tabora
WATENDAJI wa uchaguzi wamesisitizwa kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele leo tarehe 29 Septemba, 2026 mkoani Tabora wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo la Chamwino Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma na Kata 11 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Novemba, 2026.

“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewaelekeza watendaji hao kuhakikisha kuwa wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huo, wanavishirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa.

Ameongeza kuwa watendaji hao wanapaswa kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala.

“Ni muhimu kwenu pia, kuhakikisha mnayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika vituo vya kupigia kura,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewaasa watendaji hao kuhakikisha kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi, wanaepuka kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine.

Jaji Mwambegele amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye sifa, weledi, wanaojitambua na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

“Mhakiki vifaa vya uchaguzi mnavyopokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema na kuhakikisha siku ya uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi,” amesema.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata, maafisa uchaguzi, maafisa ununuzi na wahasibu.

Kata 11 za Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi wa Udiwani ni Nonde iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Nyingine ni Igalula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele akizungumza leo tarehe 29 Septemba 2026 mkoani Tabora wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na Kata 11 za Tanzania bara.(Picha na INEC).

Sehemu ya washiriki ambao ni watendaji wa Uchaguzi kutoka katika Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma na Kata 11za Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. (Picha na INEC).


Na Chalila Kibuda , Bagamoyo
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), limefanya zoezi la majaribio ya Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini Tanzania Bara kwa mwaka 2026 katika maeneo ya Pwani ya Bagamoyo.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sensa hiyo, kwa lengo la kupima uelewa na uwezo wa washiriki katika kutekeleza mafunzo waliyopatiwa, pamoja na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ukusanyaji wa taarifa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu Wanaoratibu Sensa hiyo, Nahodha Alex Katama, amesema zoezi la majaribio limekwenda vizuri na washiriki wameweza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maelekezo na mafunzo waliyopatiwa.

Amesema Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini inatarajiwa kuanza Oktoba Mosi na kukamilika Oktoba 25, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katama, zoezi la majaribio limewapa washiriki wanaohusika na ukusanyaji wa taarifa fursa ya kufanya kazi kwa vitendo, hatua iliyowasaidia kujenga uelewa na uzoefu wa namna ya kukusanya taarifa sahihi kutoka kwa wadau wa sekta ya usafiri majini.

“Kwa ujumla, zoezi limekwenda vizuri. Washiriki wanaokwenda kukusanya taarifa wameweza kufanya majaribio kama walivyofundishwa, jambo ambalo linatupa imani kuwa watakuwa tayari kutekeleza zoezi la Sensa kwa ufanisi,” amesema Katama.

Kwa upande wao, wavuvi pamoja na wajenzi wa vyombo vya usafiri majini, wameeleza utayari wao wa kutoa ushirikiano katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa zinazohitajika ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye ubora kuhusu sekta ya usafiri majini nchini.

Mtengenezaji wa vyombo vya majini, Said Doto, amesema watatoa ushirikiano wakati zoezi hilo litakapoanza ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa zitakazosaidia katika kupanga na kuendeleza shughuli za karakana za ujenzi wa vyombo vya majini.

“Tutatoa ushirikiano ili Serikali iweze kupata taarifa sahihi na kupanga mipango mizuri kwa upande wa karakana za vyombo vya majini,” amesema Doto.

Naye Mtakwimu wa TASAC, Ally Njama, amesema zoezi la majaribio limefanikiwa na kutoa uzoefu muhimu kwa washiriki kabla ya kuanza kwa zoezi rasmi.

Amesema ushirikiano wa wadau wakati wa Sensa hiyo utasaidia kuhakikisha taarifa zitakazokusanywa zinakuwa sahihi na kuwezesha zoezi kufanyika kwa ufanisi.

Sensa hiyo inalenga kupata taarifa muhimu kuhusu idadi na aina ya vyombo vya usafiri majini, pamoja na shughuli za ujenzi wa meli na vyombo vingine vya majini Tanzania Bara.

TASAC na NBS zimeendelea kuhamasisha wadau wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu zitakazosaidia katika kupanga, kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri majini nchini.







Na Mwandishi Wetu
TAWI la Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU–T) la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), tarehe 25 Septemba 2026 lilifanya Mkutano Mkuu wa Tawi kwa lengo la kujadili masuala ya ustawi wa wafanyakazi pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wa Tawi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Hamid Mbegu,
amewaahidi wajumbe ushirikiano, umoja na mshikamano, pamoja na kufanya kazi kwa ukaribu na Menejimenti ya Shirika ili kuimarisha ushirikiano, kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi na kuhakikisha TASAC inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa COTWU (T), Bi. Juliana Mpanduji, amewahimiza wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi na mawasiliano kujiunga na COTWU–Tanzania ili kuwa na sauti moja katika kutetea maslahi yao mahali pa kazi na kunufaika na Mkataba wa Hali Bora.

Kabla ya uchaguzi, Katibu wa Tawi la COTWU (T) – TASAC, Nahodha George Mnali, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Tawi kwa kipindi cha miaka mitano na kujibu hoja mbalimbali za wanachama.

Katika uchaguzi huo, Bw. Mohamed Kapera amechaguliwa kuwa Mwenyekiti na Nahodha George Mnali kuwa Katibu wa COTWU (T) – TASAC. Wajumbe wa Kamati Tendaji waliochaguliwa ni Hashimu Awadh, Salma Mohamed, Nahodha David Chiragi, Nahodha Mzee Mvihanga, Juma Mwacha na Chester Kapinga.

Aidha, Bi. Martha Ngasha amechaguliwa kuwa Mjumbe Maalum Mwanamke; Mhandisi Kelvin Kami, Mwenyekiti wa Vijana; Aggrey Koni, Katibu wa Vijana; huku Richard Nyasenga na Wilfred Chawene wakiwa Wajumbe wa Kamati ya Vijana.

Kwa upande wa Wanawake, CPA Edda Mwakatobe amechaguliwa kuwa Mwenyekiti na Florence Marick kuwa Katibu, huku Selina Mokiti na Victoria Myonga wakiwa Wajumbe wa Kamati ya Wanawake.

Akizungumza baada ya uchaguzi, Mwenyekiti mpya, Bw. Kapera aliahidi kufanya kazi kwa ukaribu na menejimenti ili kuendeleza umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Shirika na kulinda maslahi ya wafanyakazi.



 Dkt. Yonazi Charles, Mkurugenzi Mtendaji wa Masaki Wellspring Hub, ambao ni waandaaji wa Masaki Health Expo ( wa nne kushoto mwenye miwani) pamoja na wadau wengine wakimsikiliza Dr.Living Dennis Nyaki  katika maonesho hayo yaliyofanyika Masaki, jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa wananchi akichangia damu wakati wa maonesho ya Afya ya Masaki ( Masaki Health Expo 2026) katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa Seli Mun

Na Mwandishi Wetu
JAMII imetakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, ikiwemo kupima ugonjwa wa seli mundu (sickle cell), huku vijana wakihimizwa kupima vinasaba vya ugonjwa huo kabla ya kuingia kwenye ndoa ili kupunguza uwezekano wa kupata watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa matembezi na maonesho yaliyolenga kuelimisha umma kuhusu ugonjwa wa seli mundu, Mratibu wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza mkoani humo, Dkt. Living Dennis Nyaki, amesema seli mundu ni ugonjwa wa kurithi unaoweza kumpata mtoto pale wazazi wote wawili wanapokuwa na vinasaba vinavyosababisha ugonjwa huo.

Dkt. Nyaki amesema vijana wanapaswa kupima na kufahamu hali zao za vinasaba kabla ya kuingia kwenye ndoa, ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya na uzazi. Pia amesisitiza umuhimu wa kuwapeleka watoto kupima ili kutambua hali zao mapema na kuwawezesha kupata huduma stahiki.

“Ni muhimu vijana kupima kabla ya kuingia kwenye ndoa ili kujua kama wana vinasaba vya seli mundu. Hii itasaidia kuongeza uelewa na kuchukua hatua sahihi za kiafya kabla ya kupata watoto,” amesema.
Aidha, Dkt. Nyaki ameitaka jamii kubadili mfumo wa maisha ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kuzingatia ulaji salama na kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Masaki Wellspring Hub, Dkt. Yonazi Charles Senkondo, ambao ni waandaaji wa matembezi na maonesho hayo kwa kushirikiana na Ruge Mutahaba Foundation, amesema shughuli hiyo imelenga kuhamasisha jamii kuwa na uelewa kuhusu seli mundu na umuhimu wa kupima, sambamba na kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaoishi na ugonjwa huo.


Naye Dkt. RhobiJeremiah Zakaria kutoka Ruge Mutahaba Foundation amesema inakadiriwa kuwa kati ya watoto 11,000 na 14,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa wa seli mundu, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za mapema kupitia elimu na upimaji.

Katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kupima, Balozi wa Seli Mundu na Miss Universe Tanzania 2026, Queen Elizabeth, amesema kuwa yeye anaishi na changamoto hiyo na ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kupima afya na kufahamu hali zao za vinasaba kabla ya kuingia kwenye mahusiano na ndoa.

“Mimi ni mama wa mtoto mwenye changamoto hiyo, hivyo ni ugonjwa ambao nimekuwa nikiishi nao. Naiasa jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya na kujua vinasaba vyetu tunapokutana na wenza wetu. Ni muhimu kupima,” amesema.


Queen Elizabeth amesema ugonjwa wa seli mundu unaweza kuwa na gharama kubwa za matibabu, akieleza kuwa baadhi ya matibabu yanaweza kugharimu kiasi kikubwa ambacho familia nyingi haziwezi kumudu.

Amesema Serikali inatoa huduma ya upandikizaji wa uboho katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, lakini gharama ya huduma hiyo, inayokadiriwa kufikia takribani Sh milioni 75, bado ni changamoto kwa watu wengi, huku akieleza kuwa ni watu wachache tu wameweza kupata huduma hiyo hadi sasa.
“Katika uhalisia wa maisha ya kawaida, kwa Watanzania zaidi ya milioni 60, watu wengi hawawezi kumudu gharama hizi. Hivyo ni muhimu kupima mapema ili ujue kama unabeba kinasaba na kuchukua hatua ili kuzuia mtoto kuzaliwa akiwa na ugonjwa huo,” amesema.

Queen Elizabeth ameipongeza Masaki Wellspring Hub  kwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za mapema dhidi ya seli mundu, huku akiwataka Watanzania kuendelea kupima afya zao na kuchukua hatua stahiki.


Hii ni mara ya tatu kwa Masaki Wellspring Hub kuandaa uko hilo ili kuongeza uelewa , kuima na kutoa ushauri juu ya magonjwa yasiyoambukiza
Wadau waliounga mkono tukio hilo mwaka huu ni pamoja na Kanisa la Waadventista wa Sabato Masaki, Elveth Group, Choplife Foundation na Fortune Management Consulting.


Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue kuhusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira, utakaofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ukiwa ni mkutano wa kwanza kufanyika ndani ya bara la Afrika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alisema kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika na GCC+ katika masuala ya uhamaji wa nguvu kazi na ajira.

Mkutano huo utawakutanisha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC+), ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, pamoja na Jordan na Lebanon.

Sangu alisema mkutano huo ni jukwaa la kimataifa linalolenga kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa uhamaji wa nguvu kazi na kukuza ajira zenye staha, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Na katika mkutano huu mkuu kabisa, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Alisema Mkutano wa Kwanza wa Doha Dialogue ulifanyika jijini Doha, Qatar, Mei 21 na 22, 2024, ukihusisha nchi 33, ikiwemo nchi 25 za Afrika, nchi za Ghuba pamoja na Jordan na Lebanon, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizoshiriki.

Kwa mujibu wa Sangu, mkutano huo ulipitisha azimio lililoitwa Doha Declaration, lililoweka msingi wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nchi za Kiarabu kuhusu uhamaji wa nguvu kazi.

“Tanzania ni nchi ya pili kuwa mwenyeji wa Doha Dialogue, mkutano huu ambao unafanyika kila baada ya miaka miwili. Na kwa mara ya kwanza ndio unafanyika ndani ya bara la Afrika,” alisema.

Alisema maeneo muhimu yatakayojadiliwa ni pamoja na uimarishaji wa mikataba ya ajira baina ya nchi, uoanishaji wa ujuzi wa wafanyakazi na mahitaji ya soko la ajira na ujenzi wa mifumo ya uhamaji wa nguvu kazi inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, mahitaji mapya ya soko la ajira na kazi zenye staha.

Sangu alisema mkutano huo pia utatoa fursa kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhamaji wa nguvu kazi, kupanua fursa za ajira nje ya nchi, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika na GCC+.

“Mkutano huu pia utaongeza ushindani wa nguvu kazi ya Tanzania na kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050,” alisema.

Alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kupitia balozi pamoja na kuwa na siku maalum za kukutana na Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi ili kupata mrejesho kuhusu mazingira yao ya kazi.
Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
SERIKALI imeahidi kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya bidhaa za uzazi wa mpango kwa angalau asilimia 10 kila mwaka, ikiwa ni hatua ya kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Ahadi hiyo ilitolewa Septemba 28,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Wizara ya Afya, Ziada Sellah, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Grace Magembe.

Sellah alisema uzazi wa mpango ni uwekezaji muhimu katika afya ya watu, ustawi wa familia na maendeleo ya Taifa, kwa kuwa unaziwezesha familia kufanya maamuzi kuhusu idadi ya watoto na muda wa kupanga kati ya uzazi mmoja na mwingine.

“Ahadi ya Tanzania ya Uzazi wa Mpango 2030 inatoa msingi muhimu wa kuimarisha ufadhili endelevu wa ndani wa uzazi wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuongeza rasilimali za ndani kwa ajili ya bidhaa za uzazi wa mpango kwa angalau asilimia 10 kila mwaka na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatolewa kikamilifu,” alisema.

Alisema kuongeza uwekezaji katika uzazi wa mpango kutasaidia pia kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan Lengo la Tatu linalohusu afya bora na ustawi.
Naibu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Melissa McNeil-Barrett, alisema uzazi wa mpango haupaswi kuangaliwa kwa upande wa upatikanaji wa bidhaa na huduma pekee, bali pia kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi na wanaweza kufanya maamuzi yenye uelewa kuhusu afya yao ya uzazi.

“Uzazi wa mpango hauhusu tu upatikanaji wa bidhaa na huduma. Pia ni kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi, wanaweza kupata huduma hizo na wako huru kufanya maamuzi yenye uelewa kuhusu afya yao ya uzazi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MSI Tanzania, Patrick Kinemo, alisema mabadiliko katika ufadhili kutoka kwa wafadhili yameongeza umuhimu wa Serikali kuimarisha uongozi, ushirikiano na umiliki wa kitaifa katika kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kupatikana.

Alisema uzazi wa mpango ni sehemu muhimu ya afya ya mama, mtoto mchanga na afya ya uzazi, huku akibainisha kuwa huduma hizo za hiari zinaweza kuchangia ujauzito wenye afya na kupunguza vifo vya akina mama vinavyoweza kuzuilika.

Kinemo alisema bado kuna vikwazo vinavyoathiri upatikanaji wa huduma hizo, ikiwamo ukosefu wa taarifa, taarifa potofu, changamoto za kifedha na kijiografia pamoja na vikwazo vya kijamii na ndani ya mfumo wa afya.

Alisema washirika wanaendelea kushirikiana na Serikali kusogeza huduma karibu na jamii, hususan maeneo ya pembezoni, pamoja na kujenga uwezo wa wahudumu wa afya na kuboresha ubora na upatikanaji wa huduma.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya “Hakuna Vikwazo, Chaguo Pekee” inalenga kuhimiza upatikanaji wa taarifa sahihi, huduma bora na chaguo mbalimbali za uzazi wa mpango kwa wanawake, wasichana, vijana, wanandoa na watu binafsi.

Siku ya Uzazi wa Mpango huadhimishwa duniani kote Septemba 26 kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu uzazi wa mpango na kuwawezesha watu kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya yao ya uzazi.











Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SERIKALI imetenga Sh milioni 90 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga dhidi ya saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino, huku ikiagiza wadau wote kuhakikisha Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu wenye Ualbino (MTHUWWU) unatekelezwa kwa vitendo na kwa wakati.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Joy Maongezi, amesema fedha hizo zimetengwa katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

Amesema tayari chupa 339 za mafuta hayo zimesambazwa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau.

Maongezi amesema Serikali pia ina wataalamu takribani 403 wa ngozi katika halmashauri pamoja na madaktari bingwa wa ngozi 98 katika hospitali za kanda na rufaa za mikoa.

Akizungumza leo, Septemba 28, 2026, wakati akifungua Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa MTHUWWU jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema hatua hizo zinapaswa kuambatana na utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yote yanayohusu haki na ustawi wa watu wenye ualbino.

Kabudi amesema Serikali na wadau wana wajibu kuhakikisha mpango huo hautabaki kwenye nyaraka, bali utekelezwe kwa vitendo, ukipewa rasilimali na kutekelezwa kwa wakati.

“Ni muhimu kuweka mipango madhubuti ya utekelezaji wa mpango na kuhakikisha kuwa mikakati na afua zilizoainishwa katika mpango zinapatiwa rasilimali na kutekelezwa kwa wakati,” amesema.

Amesema shughuli zilizopangwa zinapaswa kutekelezwa na taarifa zake kutolewa kwa wakati ili kuwezesha Serikali na wadau kufuatilia maendeleo, kubaini changamoto, kupima matokeo na kuchukua hatua za kuboresha utekelezaji.

Kabudi amesema mpango huo una nguzo nne ambazo ni ulinzi, kinga, usawa na kutobagua pamoja na uwajibikaji, huku mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ukitakiwa kufanya kazi kuanzia ngazi ya Taifa hadi Mkoa, Halmashauri, kata, kijiji na mtaa.

Amesema jukwaa hilo la siku tatu linapaswa kwenda zaidi ya kutathmini yaliyofanyika, bali kubaini mambo yanayotakiwa kutekelezwa, maeneo yenye upungufu na hatua mahsusi za kuziba mapengo hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wambura Kizito, amesema sasa ni wakati wa kutoka katika hatua ya kuwa na mpango kazi na kuingia kwenye utekelezaji unaopimika, unaoratibiwa na wenye uwajibikaji.

Amesema masuala ya watu wenye ualbino ni mtambuka na hayawezi kutekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu au taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa sekta za afya, elimu, ajira, haki na ulinzi, ustawi wa jamii, uwezeshaji wa kiuchumi, ulinzi wa mtoto na usalama.

Amesema jukwaa hilo litabaini shughuli zilizotekelezwa, zinazoendelea na ambazo hazijatekelezwa pamoja na sababu zake, taasisi zinazohusika, rasilimali zinazohitajika na changamoto zinazokwamisha utekelezaji.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa MTHUWWU, Yohana Sali, amesema jukwaa hilo litatoa nafasi kwa Serikali na wadau kujadili mafanikio, changamoto, fursa na vipaumbele vya utekelezaji wa mpango huo.

Amesema siku ya kwanza itajikita katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mpango huo, historia yake, maudhui na hali ya utekelezaji, huku siku ya tatu ikijikita katika uratibu, masuala mtambuka na maandalizi ya mpango wa utekelezaji.

Kabudi amesema Serikali pia inaendelea kuboresha mifumo ya taarifa za watu wenye ulemavu hadi ngazi ya kijiji na mtaa.

Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania Bara ina watu wenye ualbino 71,631, wakiwemo wanaume 41,203 na wanawake 30,428.

Amesema taarifa hizo zinaisaidia Serikali kufahamu idadi na maeneo wanakoishi watu wenye ualbino ili kupanga huduma kwa kuzingatia mazingira na mahitaji yao.








Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WATANZANIA 8,408 wameunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, huku jumla ya Watanzania 15,715 wakinufaika na fursa hizo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alisema Septemba 28,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Sangu alisema Tanzania imeingia mikataba na nchi mbalimbali, zikiwemo za Ghuba, kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira katika fani za kilimo, mifugo, udaktari, ujenzi, uhandisi, ufundi mchundo, udereva, upishi na huduma za majumbani.

Alisema kwa sasa Watanzania wameanza kupata ajira za kitaalamu katika nchi za nje, zikiwemo za walimu wa vyuo vikuu, madaktari na wahandisi, tofauti na hapo nyuma ambapo wengi waliokwenda katika nchi za Kiarabu walifanya zaidi kazi za majumbani.

“Hivi karibuni tutatangaza fursa za ajira kwa mainjinia 650, ma-engineer na ma-technician, ambazo ni fursa tuliyoenda kuzungumza nao wenzetu na wakatupatia hizo fursa,” alisema.

Alisema kampuni kubwa ya ujenzi nchini Qatar, Holding Power, inatarajia kutoa fursa za ajira zipatazo 4,500 kwa Watanzania.

Aidha, alisema Serikali imeendelea kuwaunganisha vijana na fursa katika nchi za Ulaya, zikiwemo Poland, Sweden, Norway na Ujerumani, huku baadhi yao wakiwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika fani za kilimo na mifugo.

Sangu alisema Serikali imeweka mifumo ya kuhakikisha vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanalindwa dhidi ya changamoto zilizokuwa zikijitokeza hapo nyuma, ikiwemo unyanyasaji na kunyang’anywa pasipoti.

Alisema kwa sasa hakuna wakala binafsi anayeweza kumkusanyisha mfanyakazi kwenda kufanya kazi nje ya nchi bila kupitia mifumo ya Serikali.

“Tumehakikisha kwamba wote wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi wanapewa mikataba, na mikataba hiyo itakuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano,” alisema.

Alisema mikataba hiyo inalenga kulinda haki za wafanyakazi, ikiwemo kuhakikisha ujira na kiwango cha malipo vinaendana na kazi anayokwenda kufanya mfanyakazi.

Sangu alisema Serikali pia inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia balozi zake, huku mwajiri akitakiwa kuwa na mawasiliano na ubalozi.

“Tumehakikisha kwamba balozi wetu anakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mwajiri. Na hii imepunguza sana changamoto ya vijana wetu kunyanyaswa, kunyang’anywa paspoti, na kwa kipindi hiki kuanzia mwezi Januari mpaka sasa hatuna kesi yoyote iliyoripotiwa kwamba kuna unyanyasaji,” alisema.

Alisema Serikali imeweka pia utaratibu wa kuwaaga vijana kabla hawajaondoka nchini kupitia Special Departure Day, ambapo hupewa maelekezo kuhusu mazingira ya kazi na namna ya kupata msaada wanapokutana na changamoto.

Aidha, Serikali imeweka kanzidata ya wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, na hakuna mfanyakazi anayekwenda kufanya kazi nje bila kupitia kanzidata hiyo.

Sangu alisema fursa nyingine zipo kwa manesi kutoka Saudi Arabia, huku Qatar ikitarajiwa kutoa nafasi nyingine kwa manesi zitakazotangazwa hivi karibuni.

“Fursa za nje zikipatikana ni jukumu letu Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira kuhakikisha tunawalinda vijana wetu na kuwaunganisha na fursa za ajira,” alisema.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Shirika hilo Nahson Sigalla wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) akifungua mafunzo kwa mawakala wa Sensa ya Vyombo vya Majini yaliyofanyika mjini Bagamoyo.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo kwa ajili ya kuendesha Sensa ya Vyombo vya Majini

Na Chalila Kibuda ,Michuzi TV
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kufanyika kwa Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini kutaiwezesha Serikali na wadau wa sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TASAC, Nahson Sigalla, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini inayofanyika nchini kote.

Sigalla amesema Sensa iliyofanyika mwaka 2021 ilikuwa na mafanikio, ambapo jumla ya vyombo 52,800 vya usafiri majini vilibainika, huku Sensa ya mwaka 2026 ikilenga kutoa hali halisi ya idadi na mwenendo wa vyombo hivyo nchini.

Amesema taarifa zitakazopatikana kupitia sensa hiyo zitasaidia Serikali kupata picha ya mahitaji ya sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji na kuweka mikakati inayolenga kutekeleza dhamira ya Serikali ya kukuza uchumi wa buluu.

“Sensa hii itatoa picha halisi ya hali ya vyombo vya usafiri majini na mahitaji yaliyopo katika sekta, jambo litakalosaidia Serikali na wadau kupanga mipango inayokidhi mahitaji hayo,” amesema Sigalla.

Ameongeza kuwa, mbali na kuhesabu vyombo vya usafiri majini, TASAC inalenga kukusanya taarifa kuhusu maeneo muhimu yanayohusika na ujenzi wa vyombo hivyo, ikiwa ni pamoja na kubaini idadi ya wataalamu wanaohusika na uzalishaji wake.

Kwa mujibu wa Sigalla, taarifa hizo zitasaidia kuhakikisha vyombo vinavyozalishwa vinazingatia viwango vinavyotakiwa vya usalama na mahitaji ya sekta ya usafirishaji majini.

Amesema Sensa hiyo pia itasaidia kutoa picha ya hatua iliyofikiwa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 katika sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji.

Mshiriki wa Mafunzo hayo Afisa Uvuvi Mkoa wa Lindi, Abdallah Kawambwa, amesema alishiriki Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini iliyofanyika mwaka 2021 na kwamba zoezi la mwaka 2026 linatarajiwa kuwa na ufanisi zaidi kutokana na maboresho yaliyofanyika na changamoto zilizobainika katika zoezi lililopita.

Baadhi ya maafisa kutoka sekta ya uvuvi walioshiriki mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yatawawezesha kutekeleza zoezi la sensa kwa weledi na usahihi, hatua ambayo itasaidia kuboresha huduma kwa jamii.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka taasisi na idara mbalimbali, zikiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), sekta ya Uvuvi na Mifugo, TASAC pamoja na Ofisi ya Rais–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


Picha za makundi za matukio mbalimbali ya Mgeni rasmi na washiriki wa mafunzo wataondesha Sensa ya Vyombo vya Usafiri majini.


Na Mwandishi Wetu, Lindi

WATU wenye mahitaji maalum mkoani Lindi wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Lindi, Alusaria Mushi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, wakati akifungua kongamano la siku moja la ushirikishwaji wa wazawa jumuishi.

Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA).

Mushi amesema makundi hayo hayapaswi kujiona yameachwa nyuma, bali yanapaswa kutambua nafasi ya Kanda ya Kusini katika kuchangia ukuaji wa uchumi na kutumia fursa zinazotokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika eneo hilo.

Amesema awali miradi ya Serikali ilikuwa ikibainisha mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi, lakini kwa sasa wananchi wana wajibu wa kuibua mahitaji yao ili Serikali iweze kuhakikisha makundi yote yanahudumiwa kwa usawa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watu wenye mahitaji maalum, wanawake, vijana na wazee.

Amesema lengo ni kuhakikisha makundi hayo yanapata fursa ya kushiriki na kunufaika na miradi ya mafuta na gesi asilia nchini.

“Katika utekelezaji wa miradi, kila mtu ana nafasi yake ya kushiriki na kunufaika. Hata kama kuna wawekezaji kutoka nje, wazawa wana nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na miradi hiyo,” amesema Nyangi.

Aidha, ameyataka makundi hayo kuwa na biashara zilizosajiliwa ili yaweze kushiriki katika fursa zitakapotangazwa katika maeneo yanayotekelezwa miradi, hususan mkoani Lindi.

Kongamano hilo la siku moja lilikuwa sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Viziwi, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro.

Katika kuunga mkono maadhimisho hayo, PURA imegharamia ushiriki wa watu watano kutoka CHAVITA Wilaya ya Kibiti pamoja na kugharamia vifaa vya kusaidia usikivu.




Na Mwandishi Wetu, Kigoma

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Ofisi ya Mkoa wa Kigoma, limekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuzama kwa boti iliyodaiwa kuwa imebeba watu 40 katika Ziwa Tanganyika.

TASAC imesema taarifa hizo ni za uzushi na hazina ukweli, huku ikifafanua kuwa taarifa iliyotolewa na Ofisi hiyo Septemba 23, 2026, ilihusu tukio la meli nyingine iliyokuwa ikijulikana kwa jina la MV MJP, iliyokuwa imeondoka Bandari ya Kigoma kuelekea maeneo ya Mto DRC.

Kwa mujibu wa taarifa ya TASAC iliyotolewa jana, Septemba 25, 2026, meli hiyo iliondoka Bandari ya Kigoma majira ya saa mbili usiku wa Septemba 22, 2026, ikiwa na mzigo mchanganiko wenye uzito wa tani 492.838, abiria 34 na mabaharia 15.

TASAC imeeleza kuwa ilipokea taarifa kuhusu meli hiyo Septemba 23, 2026, na kufanya mawasiliano na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhusu ajali hiyo.

“Mpaka kufikia leo tarehe 25 Septemba 2026 saa 2:26 alasiri, mabaharia wote 15 tayari wameokolewa na jitihada za kuwatafuta watu wengine zinaendelea,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, TASAC imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na mamlaka za DRC kufuatilia tukio hilo na endapo kutakuwa na taarifa nyingine, umma utajulishwa kupitia njia rasmi za mawasiliano.

Shirika hilo pia limezitaka vyombo vya habari kuthibitisha taarifa zake kwa mamlaka za Serikali kabla ya kuzisambaza, ili kuepusha taharuki na hofu miongoni mwa wananchi.

TASAC imewahimiza wananchi wanaohitaji taarifa sahihi kuhusu usalama wa usafiri majini kutumia vyanzo rasmi vya TASAC na mamlaka husika.

Vilevile, TASAC imevitaka baadhi ya vyombo vya habari vilivyochapisha taarifa hiyo kurekebisha kupitia mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo ili kutoleta taharuki kwa umma.


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kwa kufanya doria za kubaini na kuzuia uhalifu. Pia oparesheni na misako imeendelea kufanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu wa makosa mbalimbali.

PROGRAMU YA ONGEA NA KAMANDA YAZAA MATUNDA MBEYA.
Septemba 23, 2026 saa 11 alfajiri, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Tumaini John Matimba, mkazi wa Iyela One, Jijini Mbeya alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Iyunga kuwa Pikipiki yake ya Mizigo ya Magurudumu matatu maarufu Guta yenye namba za usajili MC 240 FVV iliyokuwa imeegeshwa katika maeneo ya Iyunga Jijini Mbeya imeibwa na mtu/watu wasiofahamika.

Kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Askari wa Kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu lilianza mara moja ufuatiliaji na ilipofika saa 6:30 mchana liliweza kubaini kuwa Pikipiki hiyo [Guta] iliyoibwa maeneo ya Iyunga ipo maeneo ya Itezi Jijini Mbeya.

Askari pamoja na Mhanga walifika eneo la Mtaa wa Mwasote, Kata ya Itezi, Jijini Mbeya kwenye nyumba moja na kufanikiwa kuikuta Pikipiki ya Mizigo ya magurudumu matatu maarufu Guta yenye namba za usajili MC 240 FVV iliyokuwa imefichwa ndani ya nyumba.

Aidha, katika upekuzi uliofanyika katika nyumba hiyo, zilipatikana mali mbalimbali za wizi ambazo ni Pikipiki moja aina ya Kinglion yenye namba za usajili MC725 ESL rangi nyekundu, Television moja Flat Screen aina ya Alitop nchi 43, Computer moja aina ya Acer rangi nyeusi na Simu Smartphone 15 za aina mbalimbali.

Mali nyingine ni Ving’amuzi viwili, Plate Number 03 za Pikipiki zenye usajili MC 691 FMN, MC 127 DHF na moja namba zake hazisomeki, Spika 2 za Redio aina ya Lg, Stendi 07 za Television, Bracket 25 za kufungia Television ukutani, Begi moja la Spanner mbalimbali pamoja na vifaa mbalimbali vya kuvunjia.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wawili waliokuwepo ndani ya Nyumba hiyo ambao walikimbia muda mfupi kabla ya Askari kufika eneo la tukio.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali na badala yake watafute shughuli halali kwa ajili ya kujipatia kipato halali kwani uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii. Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kufika kituo cha Polisi Mbeya kutambua mali zao walizoibiwa.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.