"MADINI"
Showing posts with label MADINI. Show all posts

 


Pwani, 13 Aprili 2025 - Kampuni ya Solar Nitrochemicals Limited (SNCL) leo imezindua rasmi kiwanda chake kipya cha kisasa cha kutengeneza baruti na vilipuzi katika Eneo la Viwanda Kisarawe, ikiwa ni kielelezo cha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya viwanda na ukuaji wa sekta ya madini nchini Tanzania.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mhe. Anthony Mavunde (Mb.), Waziri wa Madini, ambaye aliipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wake na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuunga mkono viwanda vya ndani.

“Uwekezaji katika kiwanda hiki ni wa kimkakati na umekuja katika wakati muafaka. Mbali na kuboresha ukuaji wa viwanda nchini, kiwanda hiki kinaunga mkono ajenda ya kitaifa ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa,” alisema Waziri Mavunde. “Tunakaribisha mchango wa Solar Nitrochemicals na tunahimiza kampuni nyingine kuiga mfano huu ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.”

Kiwanda hiki cha kisasa kimejengwa mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa vilipuzi vinavyotumika katika uchimbaji wa madini, uchorongaji wa miamba, ujenzi na tafiti za kijiolojia kwa kutumia mitetemo (seismic exploration). Kikiwa kimejengwa jirani na mikoa yenye shughuli za uchimbaji wa madini, kiwanda hiki kitahakikisha upatikanaji wa haraka wa bidhaa, kupunguza gharama za usafirishaji, na uhakika katika mnyororo wa usambazaji katika sekta za uchimbaji hapa nchini.

Mbali na uwezo wake wa uzalishaji, kiwanda hiki kipya kinatarajiwa kuleta matokeo chanya kijamii na kiuchumi. Kiwanda kinakadiriwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zipatazo 300 na zaidi ya ajira 1,000 katika mnyororo wa thamani. Kiwanda hicho kinatarajiwa kukuza mchango wa kampuni hiyo katika mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali. Tangu kuanza kwa shughuli zake mnamo Novemba 2021, kampuni ya SNCL imechangia kiasi cha Shilingi Bilioni 17.104 katika mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali, na mchango huu unatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2030.

Vilevile, kiwanda hiki kitawezesha matumizi ya teknolojia mpya na kukuza utaalamu kwa Watanzania. Kwa kuzalisha bidhaa hizi muhimu hapa nchini, SNCL italiwezesha taifa kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na hivyo kukuza uwezo wa Tanzania kujitegemea katika vifaa muhimu kwenye sekta ya madini.

“Madhumuni ya Solar Nitrochemicals ni kuchangia jitihadi za maendeleo ya taifa kupitia uzalishaji wa ndani. Kiwanda hiki ni kielelezo cha dhamira yetu ya muda mrefu ya kuchangia katika maendeleo ya Taifa sambamba na kuzalisha bidhaa salama, za uhakika na zenye gharama nafuu” alisema Bwana Milind Deshmuk, Mkurugenzi Mtendaji wa Solar Group.

Solar Nitrochemicals ambayo ni sehemu ya kampuni mashuhuri na mzalishaji mkubwa zaidi wa vilipuzi nchini India, imeanza shughuli zake nchini Tanzania tangu mwaka 2021, na inaendelea kuwa mshirika muhimu katika uzalishaji wa vilipuzi salama na vya bei nafuu. Kiwanda hiki kipya ni hatua nyingine muhimu katika mkakati mzima wa kampuni ya kupanua shughuli zake barani Africa na kuunga mkono maendeleo endelevu katika nchi zilizoko Mashariki na Kusini mwa Afrika.






• Maeneo zaidi ya wachimbaji wadogo kutengwa

TUME ya Madini imetoa jumla ya leseni za uchimbaji madini 54,626 katika kipindi cha miaka saba.

Kaimu Mkurugenzi wa Leseni na Tehama Mhandisi Aziza Swedi amesema katika kipindi cha kuanzia 2018/2019 hadi Septemba 30, 2024, Tume ya Madini imetoa jumla ya leseni 54,626 kati ya leseni hizo, leseni za utafutaji wa Madini (Prospecting Licence-PLs) 1,683, leseni za uchimbaji wa kati (Mining Licences-MLs) 144 na leseni za uchimbaji mkubwa (Special Mining Licences-SMLs) tano.

Aidha amesema, leseni za uchimbaji mdogo (Primary Mining Licences-PMLs) zilizotolewa ni 35,536 leseni za uchenjuaji (Processing Licences-PCLs) 216, leseni za usafishaji Madini (Refinery Licences-RFLs) saba, leseni za uyeyushaji Madini (Smelting License’s-SLs) sita, leseni ndogo za biashara ya Madini (Brokers Licences-BLs) 12,273 na leseni kubwa za biashara ya Madini (Dealers Licences-DLs) 4,756.

Amesema, Tume imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo ikiwemo kuwatengenezea mazingira rafiki kwa ajili ya kupata Leseni za uchimbaji pamoja na kuwaunganisha na Taasisi za kifedha ili wapate Mikopo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji

“Hadi kufikia Oktoba, 2024 Tume imefanikiwa kutenga maeneo 65 kwa ajili ya Wachimbaji wadogo katika mikoa mbalimbali yenye shughuli za uchimbaji madini,”amesema Mhandisi Aziza.

Asema, Tume ya Madini imeendelea kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika kuyafanyia utafiti maeneo mbalimbali ili kuwawezesha Wachimbaji kupata taarifa za uwepo wa rasilimali madini na kufanya uchimbaji wenye tija.

Mhandisi Aziza amesema ili kuimarisha mfumo wa usimamizi wa utoaji wa leseni, Tume ya Madini imejenga mfumo mpya wa kuboresha uchakataji,usimamizi na utoaji wa leseni za madini.

“Baada ya maboresho yote kukamilika itafuata hatua ya uunganishwaji wa mifumo mingine ya Serikali na uhamishaji wa data kutoka mfumo wa zamani kwenda mfumo mpya pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo,”amesema Mhandisi Aziza.






Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akizungumza wakati akizindua chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA) jiji Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), Peter Kumalilwa akizungumza machache wakati wa uzinduzi wa chama chao.
Meneja wa Barrick Tanzania, Melkiory Ngido akizungumza machache.
Mjumbe wa Bodi ya TPSF, Octavian Mshiu.
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akifuatilia jambo.
Mwakilishi wa Kituo cha Uwekezaji akizungumza machache.
Wadau mbalimbali sekta ya Madini wakifuatilia uzinduzi huo.
Viongozi wa TAMISA wakizungumza Mhe. Mavunde.
Wadau wa Sekta ya madini wakizungumza na Mhe. Mavunde.


Na Mwandishi Wetu


Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amezindua chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), shirika jipya lililoanzishwa ili kusaidia wasambazaji wa sekta hiyo.


TAMISA imeanzishwa ili kutetea maslahi ya wasambazaji katika sekta ya madini, kuboresha maudhui ya ndani, kuimarisha mazingira ya biashara, kukuza utamaduni wa uvumbuzi, ushirikiano kati ya wadau na uendelevu wa biashara ndani ya mfumo wa maudhui ya ndani.


Dhamira ya TAMISA ni kuimarisha sekta ya ugavi na huduma za madini kwa kuwapatia wanachama wake fursa muhimu, kutetea maslahi yao, na kukuza utamaduni wa ubunifu na uendelevu.


Akizindua TAMISA, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi, amepongeza dhamira ya TAMISA na kuzingatia sera za maudhui ya ndani. “Kuunganisha Watanzania katika sekta ya madini kupitia maudhui ya ndani ni muhimu kwa ukuaji endelevu na kutaiwezesha serikali kutatua changamoto za mahudhui ya ndani kupitia umoja huo ambao ndio sauti rasmi ya pamoja ya wasambazaji wa sekta madini.


Uwepo wa TAMISA utachagiza azma ya serikali katika kuhakikisha kuwa utajiri wetu wa madini unawanufaisha wananchi wetu moja kwa moja na kukuza maendeleo ya kiuchumi,” alisema Mhe. Mavunde.


Pia ameiangazia maono mapana ya serikali: “Serikali inataka kuona makampuni ya Tanzania yakijitosa katika kuanzisha viwanda na kutengeneza bidhaa muhimu katika kuchimba madini. Serikali inatoa kipaumbele kipaumbele katika uwekezaji wenye tija kupitia ajira za ndani na matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kwani tunalenga kukuza ukuaji wa uchumi na kupunguza utegemezi wa pembejeo za nje. Juhudi hizi zitachangia sana katika kuleta ajira, ukuzaji wa ujuzi, na ukuaji wa tasnia zinazohusiana, na hivyo kuunganisha sekta ya madini kwa undani zaidi katika uchumi wa ndani.


Aidha Waziri Mavunde amefurahishwa na uzinduzi wa taasisi hiyo iliyoko chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania akisema kwamba sasa wasambazaji wa sekta ya madini wana sauti rasmi katika masuala muhimu jambo litakalohakikisha kwamba haki zao zinalindwa na kuimarishwa kupitia uboreshaji wa mazingira ya biashara na utatuzi wa chan


Aidha Waziri Mavunde amefurahishwa na uzinduzi wa taasisi hiyo iliyoko chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania akisema kwamba sasa wasambazaji wa sekta ya madini wana sauti rasmi katika masuala muhimu jambo litakalohakikisha kwamba haki zao zinalindwa na kuimarishwa kupitia uboreshaji wa mazingira ya biashara na utatuzi wa changamoto zao.


Awali Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa alifafanua kwamba TAMISA imeanzishwa ili kuwawezesha na kuwaleta pamoja wasambazaji wa sekta ya madini, kutetea maslahi yao na kuimarisha mazingira ya biashara. Malengo yetu makuu ni pamoja na kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji, na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia. Tunalenga kuendesha uvumbuzi na uendelevu ili kuweka wanachama wetu kama viongozi katika tasnia.


“Sekta ya madini nchini Tanzania kwa muda mrefu imekuwa nguzo ya uchumi wetu. Hata hivyo, ili kutumia kweli uwezo wa sekta hii, ni lazima tupite zaidi ya uchimbaji; ni lazima tuhakikishe kuwa manufaa ya uchimbaji madini yanaenea hadi kwenye uchumi mpana kupitia uendelezaji na uwezeshaji wa mnyororo wa ugavi wa ndani. Ndio maana TAMISA ilizaliwa: ili kutetea ukuaji na mafanikio ya wasambazaji wa sekta ya madini," amesema Kumalilwa.



●Kiasi cha Tsh Bilioni 2 zalipwa kwa vijiji vitano
●Wilaya ya Tarime yanufaika na Malipo ya Tsh 69bn kwa miaka mitatu
●Mavunde aipongeza kampuni Twiga Minerals kwa uwazi wa malipo
●Aelekeza malipo ya Mrabaha yakachochee maendeleo ya Vijiji husika
●Rais Dkt. Samia apongezwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji

Nyamongo - Tarime
WAZIRI wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde ataka fedha zinazotolewa kama sehemu ya gawio la mrabaha kutoka katika mgodi zitumike katika miradi iliyoibuliwa na wananchi katika sehemu husika kwa ajili ya kuendeleza mipango ya maendeleo kwa wananchi .

Hayo yamebainishwa leo Agosti 20, 2024 na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde wilayani Tarime mkoani Mara wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi tano za malipo ya mirabaha kwa vijiji vitano kutoka katika mgodi wa dhahabu wa North Mara.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Serikali kupitia mpango wa CSR inatambua mchango wa migodi kwa jamii, hivyo fedha hizi zinazotolewa katika vijiji vitano zikatumike kikamilifu katika maeneo husika ili kuleta uhalisia na kuonesha umuhimu wa uwekezaji uliopo ndani ya sekta ya madini nchini.

Akielezea kuhusu ushirikishwaji wa Vijana , Wakina mama na Wazee katika sekta ya madini eneo la Nyamongo , Waziri Mavunde ameigiza Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Tarime kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Mara kutenga maeneo maalum yatakayofanyiwa utafiti na kugawiwa kwa makundi hayo kwa ajili kufanya uchimbaji wenye tija.

Akifafanua kuhusu mpango wa utekelezaji wa Maudhui ya Ndani (Local Content), Waziri Mavunde amesema , Wizara ya Madini itashirikiana na Wizara ya Kilimo kwenye mradi wa uchimbaji visima vya maji kuchimba visima katika eneo la Nyamongo ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa maji kwa kilimo cha mbogamboga kama walivyoanza.

Awali , akiwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya utoaji wa gawio la mrabaha wa asilimia moja kwa vijiji vitano Meneja Mkuu wa Mgodi wa NorthMara Ndg.Apolinary Lyambiko amesema kampuni ya Twiga katika Robo ya Pili ya mwaka 2024 imetoa mrabaha wa zaidi ya shilingi bilioni 1.1 katika vijiji vitano ikifanya jumla ya Shilingi Bilioni 2.2 kutolewa kwa vipindi vya robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.

Lyambiko amevitaja vijiji hivyo nufaika kuwa ni pamoja na Kerende,Kewanja,Nyamwaga,Nyangoto na Genkuru.North Mara Gold Mine Limited imeendelea kutoa gawio la Mrabaha kwa vijiji 5 ambavyo vilikuwa vikimili maeneo yenye leseni za uchimbaji (PML) wakati mgodi unaanzishwa na Kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mines Limited (Sasa North Mara Gold Mine Limited) mnamo tarehe 27 April 1996

Lyambiko ameongeza kuwa, kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 kiasi cha bilioni 69 kimelipwa kwa Serikali ikiwa ni malipo mbalimbali yanayotokana na Mgodi.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe.Masache Kasaka ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya madini hususani kwenye uwazi katika utoaji wa mirabaha.

Nae, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja. Edward Gowele ameipongeza Serikali kupitia wizara ya madini kwa kazi nzuri inayofanya katika kushirikisha jamii kwenye miradi ya kitaifa ikiwa ni mipango na mikakati ya kuwanufaisha kwenye rasilimali zinazowazunguka katika maeneo yao na kuhaidi kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro yote iliyopo katika wilaya ya Tarime.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Lemi Mkapa ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wa Nyamongo kwa kuweka mpango wa wazi katika utoaji wa mrabaha ambapo kupitia fedha hizo jamii itaibua miradi ya kijamii na kutatua changamoto zilizopo.
















WIZARA ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na kampuni ya Kidee Mining Ltd wanaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati wa madini wanaotembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, namna ya kutumia mfumo wa ‘Monorope System Winchi’

Mfumo huo ni wa kutoa udongo kwenye mgodi kwa kutumia vifaa maalum ambavyo vitamuwezesha mchimbaji kutoa tani 10 hadi tani 13 kwa saa moja tofauti na mfumo wa kizamani wa kutumia ndoo na viroba kutoa udongo mgodini.

Akizungumza Mkurugenzi wa Kampuni ya Kidee Mining (T) Limited, Fey Kidee amesema mfumo huo wa zamani mchimbaji anatoa udongo kilo 60 kwa siku na kumuongezea mzigo mkubwa wa kazi tofauti na mfumo huo wa Monorope ambao unarahisisha.

“Tumekubaliana na Tume ya Madini kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati nchi nzima ili waufahamu huu mfumo wa kisasa uliopo na kuachana na mfumo wa zamani wa kutumia ndoo na viroba,”amesema Kidee.

Aidha, amesema mfumo huo wa kisasa unasaidia kuongeza mapato kwa Serikali na mchimbaji mmoja mmoja ikiwemo kuokoa muda.

“Kutokana na jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alizozifanya kwenye Sekta ya Madini, tumeweza kuinuka wachimbaji kutoka uchimbaji mdogo hadi kufikia uchimbaji wa kati hivyo ni muhimu sisi kama Kidee Mining kuunga mkono juhudi za Rais Samia kwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo tukishirikiana na Tume ya Madini ili nao wapande kutoka uchimbaji mdogo kuja uchimbaji wa kati,”amesisitiza.

Kidee Mining (T) Limited inayojihusisha na uchimbaji madini na uuzaji na usambazaji wa vifaa vya uchimbaji madini, uchimbaji wa kisasa, ilianzishwa mwaka 2000 ambapo mpango ni kutanua zaidi matawi yake kwa kuongeza migodi na kutengeneza ajira nyingi kwa watanzania.

Mpaka sasa imeshafungua ofisi katika mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Geita.

 

 



Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick walioshiriki mbio za riadha za NBC DodomaMarathon 2024 wakifurahi baada ya kumaliza na kukabidhiwa medali za ushiriki

Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick walioshiriki mbio za riadha za NBC DodomaMarathon 2024 wakifurahi baada ya kumaliza na kukabidhiwa medali za ushiriki.
Wafanyakazi wa kampuni ya Barrick nchini wameshiriki katika mbio za riadha za NBC DodomaMarathon 2024 zilizofanyika mkoani Dodoma ambapo wamemudu kukimbia mbio za masafa mbalimbali.

Kampuni ya Barrick nchini imekuwa na program za mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa na nguvu na afya bora.

Kila mwaka kampuni imekuwa ikiwezesha wafanyakazi wake kushiriki riadha mbalimbali na michezo ikiwemo mbio za kilomita 42 ya Bulyanhulu Healthy Lifestyle Marathon zinayofanyika kila mwaka.

Migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu pia imewekeza kujenga miundombinu ya michezo na mazoezi ili kuwawezesha wafanyakazi wake kushiriki michezo na mazoezi katika mazingira rafiki kwa ajili ya kujenga afya zao.

Lengo kuu la mbio hizi zilizowashirikisha maelfu ya wakimbiaji kwa mujibu wa waandaaji lilikuwa ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.







• Yawataka kuzingatia sheria
TUME ya Madini katika kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kutoa huduma kwa wazawa ya kuwasajili katika mfumo wa uombaji leseni mtandaoni huku wakitahadharishwa kuzingatia sheria ya madini ili wasipoteze sifa za kumiliki leseni.

Huduma hiyo inatolewa katika Banda la Tume ya Madini kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam 'Sabasaba' yanayofikia tamati kesho.

Mhandisi Daniel Mdachi akizungumza leo Julai 12, 2024 amesema Tume ya Madini inasimamia shughuli zote za utoaji wa leseni za uchimbaji na biashara ya madini, mipango ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.

Amesema, waombaji leseni ni sharti kuzingatia sheria ya madini sura ya 123 ili kuepuka kufutiwa leseni na kuepuka kupoteza sifa za kumiliki leseni.

Mhandisi Mdachi amesema wapo wananchi wanaomba leseni lakini hawalipi ada stahiki, wengine hawawasilishi nyaraka muhimu.

Mdachi amesema ili mtu awe na sifa za kuomba leseni ni lazima azingatie Sheria ya Madini na kanuni zake.

Ambapo ameeleza kuwa kuna makundi mbalimbali ya leseni za madini ambazo ni leseni za uchimbaji mdogo, leseni za utafiti, Leseni za uchimbaji wa kati, Leseni za uchimbaji mkubwa na Leseni za uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji wa madini.

Amesema leseni za uchimbaji mdogo hutolewa kwa watanzania pekee waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Madini wakati leseni za utafiti zinatolewa kwa wageni au wazawa kwa ajili ya mwekezaji kufanya utafiti na kubaini uwepo wa mashapo yanayoweza kuchimbwa kwa faida.

“Baada ya kujiridhisha uwepo wa mashapo yanayoweza kuchimbwa kwa faida ataomba Leseni ya uchimbaji: uchimbaji wa kati (ML) au Uchimbaji mkubwa (SML) kulingana na ukubwa wa mtaji wa uwekezaji,”amesema na kuongeza,

“Mwekezaji anayeomba leseni ya uchimbaji wa kati au mkubwa anatakiwa kuambatisha cheti cha mazingira ‘Environmental and Social Impacts Certificate’, Taarifa ya upembuzi yakinifu –‘Feasibility Study’, mpango wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye uchimbaji, mpango wa fidia na uhamishaji wa makazi, uthibitisho wa utaalam na fedha,”amesema.

Aidha, Mdachi amesema leseni za biashara ya madini zipo za aina mbili:Leseni ndogo (Brokers) za biashara na leseni kubwa (Dealers) za biashara ya madini.

Amesema leseni ndogo za biashara hutolewa kwa watanzania pekee waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123.

Pia, leseni kubwa za biashara ya madini hutolewa kwa wazawa au wazawa na wageni wenye kampuni ambapo mzwa ana hisa zisizopungua asilimia 25.

Imeelezwa kuwa uhai wa leseni za biashara ya madini ni miezi kumi na mbili kuanzia tarehe 1 Julai hadi tarehe 30 Juni ya mwaka unaofuata.