KASI ya ukuaji wa Teknolojia ya Akili Unde (AI) imeibua mjadala kuhusu uwezo wa sera, taasisi na mifumo ya uongozi nchini kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia hiyo.

Hoja hiyo imeibuliwa katika Mkutano wa Tatu wa Vyuo Vikuu Vitano (5UCC) unaofanyika katika Taasisi ya Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST), Arusha, kuanzia Septemba 23 hadi 25, 2026.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema mjadala kuhusu AI haupaswi kuangalia uwezo wa teknolojia hiyo pekee, bali pia namna taasisi, sera na mifumo ya uongozi inavyopaswa kuitikia fursa na changamoto zake.

“Huu ndio hasa aina ya mjadala tunaouhitaji, si kuhusu tu kile ambacho teknolojia inaweza kufanya, bali pia namna taasisi zetu, sera zetu na mifumo yetu ya uongozi inavyopaswa kuitikia fursa na changamoto zinazoletwa na teknolojia hiyo,” amesema.

Katika mkutano huo, Dkt. Philbert Nyinondi, mhadhiri na mtafiti wa mawasiliano ya sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amewasilisha utafiti unaochunguza uwezo wa miongozo ya AI kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia hiyo katika elimu ya juu.

Utafiti huo umechambua National Guidelines for AI in Education (NGAIE) na National Digital Education Guidelines for Universities (NDEGU), zote za mwaka 2025, na kubaini kuwa Tanzania tayari ina msingi wa kisera unaotambua ufuatiliaji, mrejesho na maboresho ya sera.

Hata hivyo, Dkt. Nyinondi amesema bado kuna mapungufu, ikiwamo kutokuwepo kwa vichocheo vilivyoainishwa wazi vya kufanya mapitio ya haraka ya sera, muda wa kushughulikia changamoto za dharura, mfumo wa tahadhari za awali kuhusu teknolojia zinazoibuka na utaratibu wa wazi wa kuunganisha taarifa za ufuatiliaji na maamuzi ya kisera.

Amesema kadiri AI inavyoendelea kubadilika, matumizi yake katika elimu ya juu yanaweza kuleta changamoto ambazo hazikutarajiwa wakati miongozo hiyo ilipoandaliwa, hivyo mifumo ya kisera inahitaji kuwa na uwezo wa kutambua mabadiliko hayo na kuchukua hatua kwa wakati.

Dkt. Nyinondi amesema hoja si kwamba Tanzania haiwezi kubadilisha sera, bali ni kama mifumo iliyopo inaweza kufanya mabadiliko hayo kwa kasi inayolingana na maendeleo ya AI.

Kwa upande wake, Profesa Raffaella Cagliano wa Politecnico di Milano, Italia, amesema maendeleo ya teknolojia yanapaswa kuendana na mahitaji na mazingira ya kijamii na kiuchumi ya watu.

“Hatuwezi kutenganisha uendelezaji wa teknolojia na uhalisia wa mazingira na mifumo ya kijamii,” amesema.

Naye Profesa Tushar Shinde wa IIT Madras Zanzibar amesema AI haipaswi kupimwa kwa ukubwa wa mifumo pekee, bali pia kwa ufanisi, upatikanaji na gharama yake.

“Lengo si kujenga mfumo mkubwa zaidi. Lengo ni kuufanya mfumo uwe mdogo, wa haraka na wa gharama nafuu,” amesema.

Amesema mustakabali wa AI unapaswa kupimwa kwa kiwango cha athari inayozalisha, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga teknolojia inayoweza kuwafikia watu wengi zaidi.

Mijadala hiyo imeonesha umuhimu wa kujiandaa kwa matumizi ya AI katika ufundishaji, ujifunzaji, tathmini, utafiti na huduma za kitaaluma, sambamba na kuimarisha uwezo wa mifumo ya kitaifa kukusanya ushahidi, kufanya maamuzi na kurekebisha sera kwa wakati.





 


Na Karama Kenyunko Michuzi tv 

SERIKALI imebadilisha ratiba ya Upimaji na Mitihani ya Taifa ya mwaka 2026, kwa kurudisha nyuma  mitihani hiyo kutoka Novemba hadi Oktoba, kutokana na utabiri wa mvua kubwa za El Niño unaotarajiwa kuathiri maeneo mbalimbali nchini.

Hatua hiyo imetangazwa leo Septemba 25, 2026, huku Serikali ikieleza kuwa hatua hiyo imelenga kulinda usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine, pamoja na mitihani, vifaa na nyaraka zake.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Amneir, amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuzingatia uwezekano wa mvua kubwa kunyesha mwezi Novemba 2026, kipindi ambacho baadhi ya mitihani ilikuwa imepangwa kufanyika.

Amesema kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wa Agosti 18, 2026, kuna uwezekano wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu, inayotarajiwa kuathiri mvua za Vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba 2026 na kuendelea hadi Januari 2027.

“Kwa mujibu wa utabiri huo, mvua hizo zinatarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026, huku mwezi Novemba 2026 ukitarajiwa kuwa na mvua nyingi zaidi,” amesema

Amesema Serikali, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), imeona umuhimu wa kufanya marekebisho ya ratiba ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

Wanu amesema mvua kubwa zinaweza kusababisha mafuriko, kuathiri barabara na usafiri, hali ambayo inaweza kuchelewesha au kuzuia ufikishaji wa mitihani, vifaa na nyaraka katika vituo vya mitihani.

Amesema pia mvua hizo zinaweza kusababisha wanafunzi, wasimamizi na maofisa wengine kushindwa kufika vituoni kwa wakati, huku kukatika kwa umeme na kuathirika kwa mawasiliano kukiwa ni changamoto nyingine inayoweza kujitokeza.

Aidha, amesema mvua na unyevunyevu vinaweza kuathiri mazingira ya afya na usafi katika baadhi ya vituo vya mitihani, hususan maeneo yenye changamoto katika mifumo ya maji, vyoo na taka.

Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili unahusisha shule 21,353, huku wa Darasa la Nne ukihusisha shule 21,008, hivyo athari za mvua katika vituo vya upimaji zinaweza kuwakabili wanafunzi wengi.

Amesema wanafunzi wanaofanya upimaji huo wengi wao wana umri wa chini ya miaka 11, hivyo wanahitaji mazingira salama na rafiki wakati wa kufika na kushiriki katika upimaji.

Wanu ametoa wito kwa Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri pamoja na Wakuu wa Shule kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na NECTA katika kutekeleza maelekezo yatakayotolewa.

Pia amewataka wanafunzi, wazazi na walezi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zitakazotolewa na Wizara na NECTA kuhusu ratiba na maelekezo ya uendeshaji wa Upimaji na Mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne ambao awali ulipangwa kufanyika Oktoba 21 na 22, sasa utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026.

Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili uliokuwa ufanyike Novemba 17 na 18, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026.

Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili uliopangwa kufanyika Novemba 2 hadi 13, sasa utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026.

Kwa upande wa Mtihani wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kuanza Novemba 9 hadi 27, sasa utaanza Oktoba 19 na kukamilika Novemba 6, 2026.

Profesa Said amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha kalenda ya mitihani na mihula katika sekta ya elimu haiathiriki, huku wanafunzi wakifanya mitihani katika mazingira salama.

“Uamuzi huu umezingatia zaidi usalama wa watoto, usalama wa mitihani na kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, hasa mwezi Novemba ambao unatabiriwa kuwa na mvua nyingi zaidi,” amesema.



 


Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetunukiwa tuzo maalum  katika Jukwaa la Fungua fursa mkoa wa Geita, ikiwa ni kutambua mchango  wa Ofisi  katika utoaji wa  huduma za Elimu na Ushauri wa Kisheria nchini na  kwa wananchi na  Washiriki wa Maonesho ya Kitaifa ya Madini yanayofanyika Mkoani Geita.

Tuzo hiyo imetolewa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Septemba 25, 2026, na kukabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita,  Mhe. Hashim Abdallah Komba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Alexander Mnyeti, Tuzo hiyo  imepokelewa na Wakili wa Serikali Mkoa wa Kagera  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw.  Richard Nkaina.

Aidha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashiriki katika Jukwaa la Fungua Fursa mkoa wa Geita kwa Kutoa elimu na Ushauri wa  Kisheria kwa Wananchi wa Mkoa huo.

Uzinduzi rasmi wa  Jukwaa la Fungua Fursa unafuatiwa na Maonesho ya Kitaifa ya Madini yalioanza tarehe 23 Septemba, 2026 na yataendelea hadi tarehe 3 Oktoba 2026 katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mjini Geita.

NEW YORK, Marekani.

Rais wa Namibia Mhe. Netumbo Nandi-Ndeitwah amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya na utu wa wanawake na watoto inagusa moja kwa moja mustakabali wa Afrika, akisisitiza kuwa uwekezaji katika afya ya mama na mtoto si matumizi ya kawaida bali ni uwekezaji katika watu, uchumi na maendeleo endelevu.

Rais Netumbo amesema hayo wakati wa mkutano wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wenye ajenda isemayo “Uhamasishaji kwa Ajili ya Enzi Mpya: Wanawake Wanaoongoza katika Afya ya Mama na Mtoto kwa Wote” (Advocacy for a New Era: Women Leading Maternal and Child Health for All, “SHE RISES) ulioandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa Umoja wa Afrika katika afya ya Mama na Mtoto, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 81), New York nchini Marekani.

Ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia huduma hizo badala ya kutegemea misaada ya nje pekee, akisisitiza kuwa maendeleo ya Bara la Afrika hayawezi kutenganishwa na afya ya watu wake.

Namibia imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa jukumu hilo la Umoja wa Afrika.

Akiwasilisha uzoefu wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema uwekezaji huo tayari umeanza kupata mafanikio, ambapo kati ya mwaka 2015 na 2022 vifo vya uzazi vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000. 

Bajeti ya afya imeongezeka kutoka takribani Sh bilioni 780 mwaka 2015 hadi Sh trilioni 1.8 mwaka wa fedha 2026/27, wakati mfumo wa M-Mama ukiwa umewezesha zaidi ya rufaa 150,000 za dharura kwa akina mama na watoto wachanga hadi Agosti 2026. Hatua hizo, amesema, zinaonesha kuwa utashi wa kisiasa unapounganishwa na rasilimali na utekelezaji, unaweza kuleta mabadiliko yanayogusa maisha moja kwa moja.

Katika ngazi ya bara, Mhe. Ndejembi amesema Rais Samia, akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, anatumia nafasi hiyo kusukuma Mpango wa Umoja wa Afrika wa Mama, Mtoto mchanga, Mtoto na afya ya vijana balehe (African Union Champion Roadmap for Maternal, Newborn, Child and Adolescent Health), ikiwemo ajenda ya “sifuri tatu” ambayo inalenga kutokuwepo kwa kujifungulia nyumbani, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.

Kupitia ya ajenda ya “SHE RISES”, Tanzania pia inataka wanawake wasibaki kuwa wapokeaji wa huduma pekee, bali wawe sehemu ya uongozi na maamuzi yanayoamua mwelekeo wa mifumo ya afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), Bi. Diene Keita, amepongeza uongozi wa Rais Samia na nafasi ya Tanzania katika kuifanya afya ya mama na mtoto kuwa ajenda ya kisiasa ya Afrika.

 Amesisitiza kuwa mafanikio yanahitaji utashi wa kisiasa unaoonekana kwenye bajeti, uwekezaji katika huduma za uzazi na kuimarishwa kwa wakunga kama nguzo muhimu ya kuokoa maisha. UNFPA imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo, ikisisitiza umuhimu wa viongozi na nchi vinara zinazoweza kugeuza dhamira za kimataifa kuwa huduma na matokeo halisi kwa wanawake na watoto.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Dkt. Mohamed Janabi amesema dhamira ya kisiasa ikiendana na uwekezaji, uwajibikaji na vitendo, maisha ya mama na mtoto yataendelea kuokolewa. Amempongeza Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake katika afya ya mama na mtoto kwa kuwa suala hilo ni la kimaendeleo, kiuchumi na haki.

Amesema Wanawake ndio nguzo katika mifumo ya afya kwa kuwa wanachangia kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma za afya ikiwa asilimia 70 ya watendaji katika sekta ya afya barani Afrika ni wanawake. Dkt. Janabi amesema licha ya hayo bado idadi ya wanawake katika utoaji wa maamuzi imebaki asilimia 25 pekee.

Amesema ajenda ya “SHE RISES” ni kuhakikisha wanawake wanashiriki katika kutunga sera, kupanga bajeti, vipaumbele na uongozi utakaotoa matokeo bora kwa afya ya mama na mtoto.

Awali akitoa maelezo kuhusu Mkutano huo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa New York, Mhe. Togolani Mavura amesema mkutano huo unapaswa kuwa chachu ya wajibu kwaajili ya kuhakikisha ajenda ya afya ya mama na mtoto inapewa kipaumbele na huduma kuwa bora na sawa katika maeneo mbalimbali duniani.

Kwa Tanzania, SHE RISES inabeba hoja pana zaidi ya afya: kwamba kuokoa maisha ya mama na mtoto kunahitaji uongozi, fedha na uwajibikaji, lakini pia sauti ya mwanamke katika meza ambako maamuzi hayo yanafanyika. Ndiyo msingi wa ujumbe unaosukumwa kutoka New York kwenda Afrika na duniani mwanamke anapoinuka, Mama anaishi; Mama anapoishi, Mtoto anastawi; na Mtoto anapostawi, Taifa linainuka.

Mkutano huo, umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Bara la Afrika, Viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau wa sekta ya afya duniani pamoja na watunga sera.













Kampuni ya JETOUR Tanzania imezindua JETOUR Club na kutambulisha magari mawili mapya yenye teknolojia ya plug-in hybrid, JETOUR G700 na JETOUR F700, hatua inayolenga kuwapa Watanzania chaguo zaidi katika matumizi ya usafiri unaozingatia ufanisi wa nishati.

Uzinduzi huo unafanyika wakati dunia ikikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mafuta na kuongezeka kwa gharama za nishati, hali inayosukuma matumizi ya teknolojia zinazolenga kupunguza utegemezi wa mafuta.

Tanzania nayo inaendelea kuchukua hatua katika kuhamasisha matumizi yenye ufanisi ya nishati na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa JETOUR Tanzania, magari hayo mapya yanachanganya matumizi ya umeme na mafuta, hivyo kumpa mtumiaji fursa ya kutumia umeme katika safari fupi na mafuta kwa safari ndefu, kulingana na mahitaji ya safari.

Hatua hiyo inalenga kuongeza chaguo kwa Watanzania wanaohitaji magari yenye uwezo wa kufanya kazi katika mazingira mbalimbali, huku wakipata fursa ya kutumia teknolojia inayoweza kusaidia kupunguza matumizi ya mafuta ikilinganishwa na magari yanayotegemea mafuta pekee.

Uzinduzi huo umefanyika chini ya kaulimbiu “Africa Expedition 2025”, ikiwa ni sehemu ya mpango wa JETOUR Tanzania kwa kushirikiana na Africarriers Group wa kuimarisha uwepo wa chapa hiyo katika soko la Tanzania, sambamba na kuunganisha teknolojia ya magari ya kizazi kipya na uzoefu mpana wa umiliki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JETOUR Tanzania, Zain Pirbhai, amesema kampuni hiyo inalenga kuwapatia wateja magari yanayokidhi mahitaji ya matumizi ya kila siku, safari za masafa marefu pamoja na shughuli za nje.

Amesema teknolojia ya plug-in hybrid inatoa unyumbufu zaidi katika matumizi ya nishati, kwa kumwezesha mtumiaji kutumia umeme na mafuta kulingana na aina na umbali wa safari.

“Tunataka kuwapa wateja wetu magari yanayokidhi mahitaji yao ya kila siku, safari ndefu na shughuli mbalimbali za nje, huku wakinufaika na teknolojia ya kisasa inayowapa unyumbufu katika matumizi ya nishati,” amesema Pirbhai.

















 


Mgeni Rasmi, Waziri Ridhiwani Kikwete, akikabidhi tuzo ya shukrani  kwa PSSSF iliyopokelewa na Meneja wa PSSSF  Kanda ya Kati Bw. Sayi Lulyalya wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA).

Picha ya maafisa kumbukumbu na nyaraka kutoka PSSSF, waliohudhuria Mkutano Mkuu wa 14 wa TRAMPA

Wanachama wa PSSSF wakihudumia kandoni mwa Mkutano Mkuu wa 14 wa Maafisa Kumbukumbu na Nyaraka kutoka Ofisi za Umma jijini Dodoma

Dodoma, Septemba 23, 2026

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeshiriki katika Mkutano wa 14 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofunguliwa rasmi Jumatano, Septemba, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe, Ridhiwani Kikwete ambaye aliwataka wanachama wa TRAMPA kuhakikisha historia ya Taifa inalindwa, pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika katika ofisi za umma.

Mhe. Ridhiwani Kikwete ameiagiza Taasisi za Umma kuanzisha vituo vya kisasa vya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, huku akisisitiza matumizi ya mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office).

“Naagiza  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufuatilia mara kwa mara matumizi ya mfumo huo na kubaini ofisi ambazo hazitumii mfumo huo ili hatua zichukuliwe” aliagiza Mhe. Kikwete  

Aidha, Mhe, Ridhiwani Kikwete alihitimisha hotuba yake kwa  kuagiza Ofisi za Umma kuwekeza nguvu katika matumizi sahihi ya kumbukumbu na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Pembeni mwa mkutano huo wa, PSSSF ilishiriki kwa kutoa huduma kwa wanachama wa TRAMPA ambao ni wanachama wa PSSSF. Mfuko hutumia majukwaa kama haya ili kutoa elimu na huduma kwa wanachama wake.

Afisa Matekelezo Mkuu wa PSSSF Mkoa wa Dodoma, Juma Milinga, amewasisitiza wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka nchini (TRAMPA) kuendelea kujisajili na kutumia mifumo ya kidigitali katika kupata huduma za mfuko huo badala ya kutegemea matumizi ya makaratasi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa 14 wa TRAMPA uliofanyika jijini Dodoma leo Septemba 24, 2026.

Milinga amesema matumizi ya mifumo ya kidigitali yamesaidia kupunguza ucheleweshaji wa madai pamoja na kupunguza changamoto ya upotevu wa nyaraka, hatua inayowezesha wanachama kupata huduma kwa wakati.

Kwa upande wao, baadhi ya wanachama wa TRAMPA wameiomba Serikali kupitia PSSSF kuendelea kutoa elimu kuhusu huduma za PSSSF, sambamba na kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili wanachama walioko maeneo ya vijijini waweze kupata huduma za mfuko huo kwa ufanisi


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, jana Alhamisi Septemba 24, 2026, alitembelea Vatican City akiwa jijini Roma, Italia, katika ziara ya kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo, uliofanyika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Akiwa Vatican City, Waziri Mkuu alikutana na Mkuu wa Itifaki wa Sekretarieti ya Nchi ya Vatican, Monsinyori Javier Domingo Fernández González.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mwigulu pia alitembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria na kiutamaduni ya Vatican City, yenye umuhimu mkubwa katika historia ya Kanisa Katoliki duniani.





Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MANISPAA ya Kibaha imeendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya utunzaji wa mazingira kwa viwanda, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Niño zinazotarajiwa.

Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda kuboresha mifumo ya kuchuja na kutiririsha maji taka, ili kuzuia maji hayo kusambaa katika maeneo ya wananchi na kusababisha madhara kwa jamii na mazingira.

Dkt. Mawazo ametoa wito huo wakati akikagua kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Fortune, kilichopo Misugusugu, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Manispaa kuhusu utunzaji wa mazingira.

Amesema kiwanda hicho awali kilikuwa na mashimo manne makubwa yaliyotumika kutiririsha maji taka, hali iliyokuwa ikihatarisha wananchi wanaoishi maeneo ya jirani, lakini katika ukaguzi huo amebaini kuwa maagizo ya Manispaa yametekelezwa kwa mashimo hayo kufukiwa na mfumo wa majitaka kuboreshwa.

Meya Mawazo amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wawekezaji kwa kuwa viwanda vinachangia pato la Serikali na kutoa ajira, huku akiwataka kuzingatia sheria na miongozo ya utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Saeni, Edward Kitale, amesema wananchi walikuwa wakikabiliwa na kero ya harufu mbaya pamoja na maji taka kuelekea mashambani, lakini hali hiyo imeanza kuimarika baada ya mashimo hayo kufukiwa.

Naye Ofisa Mazingira wa kiwanda hicho, Daudi Tito, amesema wamepokea maelekezo ya Serikali na Manispaa na wataendelea kuzingatia sheria na miongozo ya mazingira ili changamoto hiyo isijitokeze tena.

Meneja Biashara wa kiwanda hicho, Colin Tang, amesema kiwanda kimeboresha mifumo yake kwa kujenga mitambo ya kisasa ya kuchuja maji taka, hatua inayolenga kuzuia madhara kwa wananchi na mazingira.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Meya Dkt. Mawazo pia amekagua kiwanda cha kutengeneza mabati na bidhaa za chuma cha Kinglion, pamoja na Shule ya Sekondari na Shule ya Msingi Misugusugu.





Mkurugenzi wa Shirika la INADES Formation Tanzania, Jacqueline Nicodemus, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuweka mikakati ya kuwa na vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuhakikisha yanaendelea kutekeleza shughuli zake bila kutegemea zaidi fedha kutoka kwa wafadhili.

Akizungumza leo Septemba 24, 2026, jijini Dodoma kwenye Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Dodoma, amesema ushiriki wao katika jukwaa hilo ulianza katika ngazi za wilaya, ambapo walishiriki katika majukwaa yaliyofanyika katika wilaya tano kabla ya kufikia ngazi ya mkoa.

Amesema ajenda kubwa iliyojadiliwa ni uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, hususan changamoto ya kuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato ili kupunguza utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili.

Aidha, amesema mashirika yanaweza kutumia fursa zilizopo kuendeleza bidhaa na huduma mbalimbali zinazoweza kuzalisha mapato, hatua ambayo itasaidia kupanua wigo wa mapato na kuimarisha utekelezaji wa shughuli zao.

Kwa upande mwingine, amesema kupitia majukwaa hayo, wadau wameweza kujadili na kuweka mikakati ya kuhakikisha mashirika yanapata fursa zaidi za mapato na kuwa na uwezo wa kujiendesha kwa uendelevu.

Ameongeza kuwa mjadala huo utaendelea katika ngazi ya kitaifa mwezi Oktoba, ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka maeneo mbalimbali Nchini yataendelea kutoa mchango kuhusu namna ya kujenga uendelevu wa sekta hiyo nchini Tanzania.

Naye Rajab A. Rajab, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali NACONGO, kutoka Wilaya ya Kondoa, ameeleza kuwa INADES Formation Tanzania imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo mazingira, kilimo, ufugaji, elimu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Amesema kupitia shughuli za mazingira, shirika hilo limefanikiwa kupanda zaidi ya miti 80,000 katika mkoa wa Dodoma, huku likiendelea kuwafikia wakulima na wafugaji kwa kutoa elimu na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Aidha, amesema katika maeneo ambayo shirika halifiki moja kwa moja, hutumia njia mbalimbali kuwafikishia wananchi elimu na taarifa muhimu, ikiwemo tafiti na machapisho yanayowasaidia wakulima kupata uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

Ameeleza pia kuwa matokeo ya shughuli za shirika yanaonesha kuwa zaidi ya vikundi saba vinaendelea kutekeleza shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini, huku vikifikia zaidi ya watu 150,000.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Khatibu Kazungu, amezitaka mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia masharti ya sheria, kushiriki mikutano na vikao vya wadau, kuwasilisha kwa wakati taarifa za robo mwaka na mwaka pamoja na kulipa ada kwa wakati.

Kazungu pia amesisitiza mashirika hayo kulinda maslahi ya nchi, kuheshimu mila, desturi, utamaduni na maadili, kuhakikisha wanufaika wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi na kuzingatia mipango na vipaumbele vya Serikali, hususan Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Kwa upande wake, Patrick Mafuru, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, amesisitiza mashirika kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza, akieleza kuwa lengo kuu linapaswa kuwa kuisaidia Serikali kufikisha huduma kwa jamii katika maeneo ambayo bado haijafika.