Hayo yamesemwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Algeria leo asubuhi katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers.
Balozi Matinyi amesema sekta ambazo zimepiga hatua katika kipindi cha miezi michache iliyopita ni viwanda vya dawa, nishati, elimu ya juu, biashara ya mazao ya kilimo na ufugaji wa nyuki.
Amesema hatua hizo zinafuatia maelekezo ya viongozi wa nchi hizo mbili ya kugeuza maeneo ya ushirikiano yaliyobainishwa kuwa fursa halisi za maendeleo kwa wananchi.
“Nilipowasilisha hati zangu za utambulisho mnamo Juni 10, 2026, Rais Abdelmadjid Tebboune alisisitiza kwamba sasa umefika wakati wa kuuweka ushirikiano wetu katika vitendo. Nilipokuja Algeria, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pia alisisitiza kwamba kutokana na ushirikiano wetu wa kimkakati, sasa ni wakati wa kupata manufaa kwa ajili ya wananchi wetu,” amesema Balozi Matinyi.
Ushirikiano katika dawa
Akizungumzia sekta ya dawa, Balozi Matinyi amesema Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP) pamoja na Saidal Group, kampuni ya dawa inayomilikiwa na Serikali ya Algeria, zinatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi Oktoba kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Amesema ziara hiyo inalenga kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya taasisi hizo.
Ameeleza kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha juu cha ML3 katika mfumo wa ukaguzi wa dawa mwaka 2018, kwa mujibu wa tathmini ya Shirika la Afya Duniani (WHO), huku Algeria ikiwa na takribani theluthi moja ya viwanda vya dawa vilivyopo barani Afrika.
Balozi Matinyi amesema hali hiyo inaweka msingi mzuri wa nchi hizo mbili kushirikiana na kufikia mafanikio makubwa katika sekta ya dawa.
Aidha, amesema kampuni ya dawa ya Hikma iko katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya ushirikiano katika biashara na uwekezaji na Medipharm, kampuni tanzu ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kwa lengo la kuhudumia masoko ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Amesema kampuni nyingine ya Algeria, Frater Razes, inatarajiwa kufika Tanzania mwezi Oktoba kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Serikali kuhusu fursa za biashara na uwekezaji.
Nishati
Katika sekta ya nishati, Balozi Matinyi amesema Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO), kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ilifanya ziara nchini Algeria mwezi Julai kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano wa kiufundi.
Amesema wakati wa ziara hiyo, wataalamu wa ETDCO walitembelea maeneo ya kiufundi ya Shirika la Umeme na Gesi la Algeria (SONELGAZ), pamoja na kiwanda cha vifaa vya umeme cha GISB Electric.
Algeria kutoa nafasi 176 za masomo
Katika sekta ya elimu ya juu, Balozi Matinyi amesema Algeria imetoa nafasi 176 za masomo ya juu kwa wanafunzi kutoka Tanzania.
Amesema Serikali ya Tanzania imeamua kuchagua wanafunzi 150 wenye ufaulu wa juu chini ya mpango wa Samia Scholarship Extended, ambao wataenda kusoma masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na tiba nchini Algeria.
Korosho na usindikaji wa mazao
Akizungumzia biashara ya mazao ya kilimo, Balozi Matinyi amesema kampuni ya Algeria ya Sarl Anacard’Or imenunua ghala la kuhifadhia korosho mkoani Mtwara kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa korosho kwenda Algeria.
Amesema kampuni hiyo pia iko katika hatua za kukamilisha mipango ya kuanza shughuli za ubanguaji wa korosho nchini Tanzania.
Aidha, amesema kampuni nyingine ya Algeria inayotengeneza mashine za kusindika mazao ya kilimo, dawa na vifaa vya kufungashia, CAM Sarl, imekubali kushirikiana na Tanzania katika upatikanaji wa mashine hizo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao kabla ya kupelekwa katika masoko ya kimataifa.
Ushirikiano katika ufugaji wa nyuki
Balozi Matinyi amesema Tanzania na Algeria pia zinatarajia kuanza ushirikiano katika sekta ya ufugaji wa nyuki na mazao yake.
Amesema hatua hiyo imefuatia ziara ya maafisa na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na wadau wa sekta binafsi nchini Algeria mwezi Septemba 2026, ambapo pande hizo zilikubaliana kuanza ushirikiano katika eneo hilo.
Akihitimisha mazungumzo yake na waandishi wa habari wa Algeria, Balozi Matinyi amewakaribisha wananchi wa Algeria kutembelea Tanzania na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Hifadhi za Taifa za Serengeti na eneo la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro pamoja na fukwe za Zanzibar.




.jpeg)









.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)








.jpeg)



