Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkoa wa Simiyu umejipanga kuhakikisha hakuna maambukizi mapya ya VVU ifikapo mwaka 2020, kwa kuwaanzishia dawa za kufubaza VVU wote watakaopimwa na kubainika kuwa na VVU bila kujali wingi wa CD4 kama mwongozo mpya unavyoeleza.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Mageda Kihulya wakati akitoa taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi katika Uzinduzi wa Kampeni ya Huduma Jumuishi za kuzuia maambukizi ya VVU uliofanyika kimkoa katika viwanja vya Sabasaba Mjini Bariadi.
Dkt Mageda amesema hadi kufikia Septemba 2016 Mkoa umesajili wateja 40,426 kwenye huduma za tiba na matunzo (CTC) na kati ya hao 34,838 tayari walikuwa wameanzishiwa dawa za ARV sawa na asilimia 86,huku wagonjwa wanaoendelea na dawa za kufubaza VVU ni 18,246 sawa na asilimia 52.
Katibu Tawala mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini (wa pili kulia) akikata utepe katika Uzinduzi wa Kampeni ya Huduma Jumuishi za Kuzuia Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Kimkoa, uliofanyika katika uwanja wa Sabasaba Mjini Bariadi, (wa tatu kulia) Meneja wa AMREF Tanzania, Dkt.Amosi Nyirenda.
Dkt. Mageda ameongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2015 wananchi wapatao 262,862 walipata huduma ya ushauri nasaha na upimaji na kati yao 8,631 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU sawa na asilimia 3.3 chini ya kiwango cha maambukizi cha kitaifa ambacho ni asilimia 5.1.
Aidha, akina mama wajawazito wapatao 92,964 katika kipindi cha Januari- Desemba 2015, waliohudhuria kliniki walipimwa kujua hali ya afya zao ikiwa ni kutekeleza mpango kabambe wa kuzuia maambukizi yaVVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kati yao akinamama 1,459 waligundulika kuwa na virusi sawa na 1.6%.
Sanjari na hilo Mganga Mkuu huyo wa Mkoa ameanisha mikakati ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU ifikapo 2020 Mkoani Simiyu, kuwa ni pamoja na kutoa huduma za ushauri nasaha na upimaji kuwawezesha watu kujua hali zao na kujikinga na kukinga wenzao wasipate maambukizi mapya, sambamba na kuwaanzishia dawa za kufubaza virusi wale wote watakaopimwa na kubainika na VVU bila kujali wingi wa CD4 kama mwongozo mpya unavyoeleza.
Katibu Tawala mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini akipokea taarifa kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Muungano Mjini Bariadi, alipotembelea kituo hicho kujionea utoaji wa huduma za afya kabla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Huduma Jumuishi za Kuzuia Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Kimkoa, uliofanyika katika uwanja wa Sabasaba.
Mikakati mingine ni na kupima na kuanzisha dawa za kufubaza VVU kwa akinamama wote wajawazito na wanao nyonyesha watakaobanika na VVU, kutoa huduma ya tohara ya hiari kwa wanaume na kuwafanyia uchunguzi wa Kifua Kikuu na kuwatibu mara kwa mara watakaobainika kuwa na Kifua Kikuu kwani ni moja ya magonjwa nyemelezi yanayoua watu wengi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, amesema kuwa Kampeni ya Huduma Jumuishi za kuzuia Maambukizi ya VVU itatekelezwa hadi Juni 2017, ambapo inalenga kufikia watu zaidi ya 6,000 katika wilaya zote za mkoa huu, huku akitoa rai kwa wadau kufuata sera, miongozo na sheria za Nchi katika kutoa huduma za VVU na Ukimwi wakati na baada ya kampeni hii.
Kwa upande wake Meneja wa AMREF Tanzania Dkt. Amosi Nyirenda amesema Shirika hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI na amewaomba wakazi wa Mkoa wa Simiyu kujenga utamaduni wa kupima ili kujua afya zao wanapobaini wameathirika ni vema kuanza dawa mapema.
“Sisi kama AMREF tunafanya kazi na Serikali kuhakikisha tunashirikiana katika mapambano maeneo yote, tunakwenda zaidi maeneo yenye uhitaji leo tumezindua kampeni hii hapa na tutaendelea na kata 25 mpaka Desemba mwaka huu na mwaka ujao tutaenda kata 18 za mkoa wa Simiyu tutashirikiana na timu ya mkoa kuanisha kata husika” alisema Dkt.Nyirenda.
Uzinduzi wa Kampeni ya Huduma Jumuishi za kuzuia Maambukizi ya VVU Mkoa wa Simiyu, umeenda sambamba na uchangiaji wa damu kwa hiari, huduma za upimaji VVU, Toharakinga kwa wanaume, huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, huduma za magonjwa ya ngono na via vya uzazi, upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na huduma za ushauri wa lishe bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...