Mabaki ya nyumba baada ya kufukiwa na maporomoko
 Baadhi ya nyumba zilizofukiwa na maporomoko
 Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere akiangalia baadhi ya nyumba zilizofukiwa na kifusi
 Mkuu wa wilaya ya Ludewa Adrea Tsere akisaidiwa kuvuka mto unaomwaga maji yake ziwani na baadhi ya  wanakamati ya ulinzi na usalama
Baadhi ya makaburi yaliyofukuliwa na maporomoko
 
Na Shukrani Kawogo, Njombe

Wakazi wa kata ya Lifumo iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kuhama na kuacha kulima maeneo yaliyopo katika mkondo wa maji ili kuepuka kusababisha maporomoko ambayo hutokea kipindi cha mvua na kusababisha maafa.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Ludewa Andrea Tsere alipotembelea kambi ya wahanga wa maporomoko hayo yaliyotokea siku chache zilizopita na kusababisha vifo vya watoto wawili waliofahamika kwa majina ya Julietha Nkwera (16) na Farida Haule (5) pamoja na majeruhi tisa ambao wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo.

Maporomoko hayo yamepelekea nyumba 13 kusambaratishwa na nyingine kujaa vifusi vya maporomoko hayo pamoja na zaidi ya hekari 60 za mashamba ya mihogo yakiwa yameharibiwa huku makaburi 20 yakifukuliwa na kupelekea mafuvu kuonekana.

Alisema kuwa watu wamekuwa wakiufuata mkondo wa maji na kujenga makazi yao pasipo kuangalia athari wanazoweza kuzipata kipindi cha mvua.

“Tatizo la watu wakiona eneo liko wazi wanakimbilia kujenga pasipo kufanya uchunguzi kama eneo hilo linafaa kwa ujenzi au la! matokeo yake zinapotokea athari kama hizi wanaanza kutafuta msaada wakati wao ndio walioufuata mkondo wa maji wenyeye”, Alisema Tsere.

Aliongeza kuwa katika milima kuna mifereji ambayo inamwaga maji yake ziwani hivyo wananchi wanapojenga nyumba zao kwenye njia za mifereji hiyo huyazuia maji kupita kwa urahisi na inapofika msimu wa mvua kubwa maji hulazimika kubomoa nyumba zao ili kuweza kupita kwenye mkondo wake.

“ Ili kupata suluhu ya hili janga wananchi mnapaswa kuungana na kutanua mkondo wa maji ambao ni mpana ili maji yapite kwenye njia yake, na waliopo kwenye njia ya maji wapishe kwakuwa wao ndiyo walio ufuata mkondo huo na si mkondo wa maji uliwafuata wao”. Alisema Tsere.

Aidha kwa upande wa diwani wa kata hiyo Bw. Herbert Haule alisema kuwa vijiji vilivyoathirika katika kata hiyo ni vitatu ambavyo ni Lifumo, Kilindi na Luambo ambapo waliopatwa na maafa hayo wamelazika kuwahifadhi katika shule ya msingi Lifumo kama kambi ya muda na kuwasimamisha masomo wanafunzi kwa kipindi kifupi wakati wanaendelea na mipango mingine ya kuwasaidia.

Aliongeza kuwa wahanga hao wanahitaji msaada mkubwa wa chakula, malazi na mavazi kwakuwa vitu vyote walivyokuwa navyo vimeharibiwa.

Naye mmoja wa wahanga hao Bi. Adehema Stephano alisema kuwa jambo hili limewarudisha nyuma kimaendeleo na kuwaletea umasikini hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuwasaidia kuwachangia mahitaji mbalimbali ikiwemo mavazi.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ambaye aliambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya ametoa mchango wa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, maharage, Unga wa mahindi pamoja na mashuka mia moja, pia alisema ameongea na mbunge wa Ludewa Deo Ngalawa ambapo aliwasiliana na ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa na kuahidi kuwasaidia mahema, mikeka, maturubai pamoja na mablanketi ili kuweza kuwaweka katika hali nzuri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...