JUMLA ya mbegu 5,000 za Vanilla zimetolewa kwa wakulima wa Shehia za Mtambwe Kusini na Kaskazini Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini  Pemba kwaajili ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Viungo, Mboga na matunda unaotekelezwa Zanzibar.

Akikabidhi mbegu hizo Bwana shamba Msaidizi wa shehia hizo, Hamad Mwitani amesema mbegu hizo zimetolewa ikiwa kufuatia kukamilika kwa mafunzo maalum ya kuwafundisha wakulima wanufaika wa mradi huo juu ya mbinu bora za uzalishaji wa mazao shambani.

Amesema wakulima walionufaika na mbegu hizo ni wakulima 50 kutoka shehia za Mtambwe Kusini na Kaskazini ambapo kila mkulima amefanikiwa kukabidhiwa mbegu 100 kwaajili ya kuanza uzalishaji katika shamba lake kwa kuzingatia taaluma aliyofundishwa.

Maryam Hamad Sharif mmoja wa wakulima waliopatiwa mbegu hizo amesema kupitia taaluma ya kilimo cha kisasa waliyofundishwa na wataalam wataitumia kuanzisha shamba la mivanilla ambalo litawafanya kuwa wakulima bora na kuongeza uzalishaji wa zao hilo Zanzibar.

Naye Rashid Abdalla Salum ameshukuru mradi wa Viungo kwa kutambua changamoto za wakulima na  kuwapatia mbegu bora kwani wengi wao wanashindwa kufanikiwa kupitia kilimo kutokana na kukosa mbegu bora za uzalishaji wa mazao hayo.

 “Nawashukuru sana wafadhili waliotuletea mradi huu kwasababu nilikuwa sijawahi kupata mbegu kama hizi kwaajili ya kujiendeleza. Nashukuru sana naahidi kwamba nitazalisha zaidi na nitawaita waje kunikagua kuona hatua niliyofikia.”

Mapema mkurugenzi mtendaji wa Community Forests Pemba, Mbarouk  Mussa Omar amewataka wakulima waliokabidhiwa mbegu hizo kuziendeleza kulingana na maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili malengo ya mradi yaweze kufikiwa kama ilivyokusudiwa. 

Aidha amewataka wakulima wa shehia ambazo mradi unatekelezwa kuendelea kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi huo kwani unalenga kumfikia kila mkulima aliyepo katika shehia hizo.

Mapema  meneja uendeshaji wa mradi kanda ya Pemba, Sharif Maalim Hamad amesema kutolewa kwa mbegu hizo ni mwendelezo wa juhudi za mradi katika kuhakikisha wakulima wa mazao ya Viungo, Mboga na Matunda  wanazalisha mazao bora kupitia upatikanaji wa mbegu bora za kilimo.

Mradi wa Viungo, Mboga na Matunda unatekelezwa Zanzibar na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Community Forests Pemba (CFP) na People’s Development Forums (PDF) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU.)


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...