Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa akizungumza na walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa NIC mara baada ya kukabidhiwa viti na meza 200 vilivyotolewa na shirika hilo na kuwataka wanafunzi kulinda rasilimali hizo kwa matumizi ya sasa na baadaye, Leo jijini Dar es Salaam.



Meneja Uhusiano wa Shirika la Bima Tanzania (NIC,) Karimu Meshack akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya viti na meza, yaliyofanyika katika shule ya sekondari Aboud Jumbe na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa, leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Aboud Jumbe Rose Mkono akizungumza katika hafla hiyo ambapo ameishukuru NIC kwa kutatua kabisa changamoto ya viti na meza kwa wanafunzi wa kidato cha tano wa shule hiyo, leo jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa (katikati) akikata utepe kuashiria mapokezi rasmi ya viti na meza  zilizotolewa na Shirika la Bima la Taifa (NIC,) leo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa akikabidhi viti na meza kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Aboud Jumbe, kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Dalmina Mikaya na katikati ni Meneja Uhusiano wa NIC Karimu Meshack. Leo jijini Dar es Salaam. 




SHIRIKA La Bima la Taifa (NIC,) limetoa msaada wa viti na meza 200 vyenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa shule tatu za Sekondari za Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ikiwa ni sehemu ya kutekeleza sera ya shirika hilo ya kurudisha kwa jamii pamoja na kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya mbalimbali muhimu zinazoigusa jamii ikiwemo elimu kwa shule za msingi na sekondari pamoja na afya.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Mkuu wwa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa amesema NIC imekuwa ikishiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kwa kutoa msaada huo wa viti na meza 200 wameweza kutatua kabisa changamoto  ya viti na meza  kwa wanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya Aboud Jumbe na sekondari za Kisarawe II na Minanzini.

"Taasisi, jamii na wadau wa elimu tunawaomba wafuate nyayo za NIC kwa kushiriki katika kusaidia miundombinu rafiki ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi katika Halmashauri yetu kusoma katika mazingira wezeshi ili waweze kufanya vyema katika mitihani yao ya kuhitimu.....Nawaomba NIC mnifikishie salamu za shukrani kwa Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Bima la Taifa- NIC, Dkt. Elirehema Doniye tutarudi tena  tunaomba mtupokee.'' Amesema Nyangasa.

Aidha amewataka walimu na wanafunzi wa shule hizo kutunza rasilimali hizo kwa manufaa ya waliopo na watakaofika ili kuwapa moyo zaidi wanaotoa misaada hiyo kwa kuendelea kushiriki  katika kuboresha sekta hiyo muhimu ya elimu na kuwataka wanafunzi hao kuzingatia masomo na kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Manispaa hiyo kitaaluma.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Meneja Uhusiano wa Shirika hilo Karimu Meshack amesema wamekuwa wakitekeleza sera ya shirika hilo la kurudisha kwa jamii pamoja na sera ya Serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM,) katika kuunga mkono jitihada katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari.

Amesema kuwa NIC imefarijika kwa kutatua changamoto ya viti na meza kwa wanafunzi wa kidato cha tano wa Aboud Jumbe sekondari na kunufaisha shule  za Sekondari za Kisarawe II na Mianzini na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala yanayoigusa jamii wanayoihudumia.

Akitoa taarifa kwa niaba ya shule zilizonufaika na msaada huo mkuu wa shule ya sekondari Aboud Jumbe Rose Mkono amesema NIC walitoa shilingi milioni 20 zilizoelekezwa katika miundombinu ya viti na meza zoezi lililosimamiwa na ofisi ya Mkurugenzi na ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kuleta manufaa kwa wanafunzi wa shule hizo.

Amesema katika msaada huo wanafunzi 200 wamenufaika na msaada huo, huku ikielezwa kuwa thamani ya kila kiti na meza imegharimu shilingi laki moja na kwa mgawanyo wa Sekondari ya  Aboud Jumbe kupata viti na meza 110, Kisarawe II 40 na Minanzini 50 na kuwasilisha changamoto ya samani kwa walimu wa shule hiyo ambayo ilichukuliwa na Meneja Uhusiano wa NIC kwa hatua zaidi.

Bi. Mkono ameishukuru NIC kwa kuona umuhimu wa kushiriki na kutoa msaada kwa wanafunzi wa shule hizo na kuiomba jamii, taasisi mbalimbali na wadau wa elimu kufuata nyayo za shirika hilo ili kuboresha zaidi sekta ya elimu nchini kama Serikali ilivyodhamiria.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...