Na Fatma Salum-GCLA
MKEMIA Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amewahimiza wajasiriamali kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazotumia katika uzalishaji wa bidhaa zao ili kulinda afya za binadamu na mazingira.

Dkt. Mafumiko ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea maonesho ya wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambayo yanafanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.

Aliwaeleza wajasiriamali hao kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikitoa mafunzo kuhusu matumizi salama ya kemikali kwa wadau wake mbalimbali wanaotumia kemikali wakiwemo wajasiriamali ili kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali pamoja na namna bora ya kuhifadhi bidhaa zao.

“Kwa nafasi yetu kama wasimamizi wa sheria ya kemikali tuna jukumu la kuhakikisha watumiaji wa kemikali kama vile watengeneza batiki na wanaosindika bidhaa za vyakula pamoja na dawa asili wanazingatia taratibu za kiusalama, hivyo tunawaahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau hao,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila alisema kuwa katika zoezi la kuwafikia wajasiriamali, taasisi yake inapata ushirikiano mzuri kutoka GCLA kwenye kuwaelimisha wajasiriamali hao namna bora na salama ya kutumia kemikali katika uzalishaji wa bidhaa.

Aidha, baadhi ya wajasiriamali waliowahi kupata mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kutoka GCLA walieleza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kuboresha bidhaa zao na kulinda afya zao bila kuchafua mazingira.

Naye mjasiriamali kutoka Zanzibar, Salma Othman ameiomba GCLA iendelee kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi kupitia njia mbalimbali ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inazingatia usalama wa afya za watu na mazingira.

Maonesho hayo ya pili ya wajasiriamali wanawake yaliyoandaliwa na TWCC yalianza Machi 3 mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika Machi 8, 2022 ambayo ni Siku ya Wanawake Duniani.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko akieleza jambo katika moja ya Banda kwenye maonesho ya Wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Mmoja wa Afisa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) akitoka maelekezo kwa mmoja wa Wananchi waliopita kwenye Banda hilo kupata maelekezo na kujifunza masuala mbalimbali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...