Na Joseph Lyimo, Hanang’
MKOA wa Manyara umepokea dozi mpya 175,000 ya chanjo ya UVIKO-19 aina ya Jonsen Jonsen ambapo sasa mkoa unaanza kampeni ya kutoa chanjo hiyo kwenye wilaya tano za mkoa huo.

Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara Dkt Damas Kayera ameyasema hayo, wakati akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' akiwa ameambatana na wataalamu wa afya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ambao wanafanya uhamasishaji wa chanjo hiyo.

Dkt Kayera anaeleza kwamba chanjo hiyo ni salama hivyo madiwani wapate chanjo hiyo na kuwahamasisha wananchi wao kwenye kata mbalimbali kuchanja ili wawe salama kiafya.

"Hii elimu ya chanjo tunaomba tuifikishe kwa wananchi wetu na muwaambie wenyeviti wa vitongoji na vijiji ili wasaidie kuhamasisha katika maeneo yao," anaeleza Dkt Kayera.

Anasema kuwa lengo lao la haraka wanatakiwa ifikapo Julai 30 mwaka huu kuwa wamefikia asilimia 40 na kwa sasa bado wako chini ndio maana wameamua kuanzisha Kampeni hiyo iliyoanza Juni 27 hadi Julai 30.

Anasema dozi za chanjo hizo zimegawanywa kwenye wilaya zote tano za mkoa wa Manyara, ambazo ni Babati, Kiteto, Simanjiro Hanang’ na Mbulu, ambapo wananchi wake wanaendelea kupata chanjo hivi sasa.

Mshauri wa ugonjwa wa UVIKO-19 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt Chima Onuekwe anasema kwamba kuna nchi 10 Afrika ambazo hazijafikia asilimia 10 ya chanjo ya COVID 19 ikiwemo Tanzania ndiyo sababu maana wamekuja ili waweze kufanya uhamasishaji.

Dk. Onuekwe anaeleza kuwa UVIKO-19 bado ipo hivyo wanatakiwa watoe hamasa ya wananchi wengi kuchanja ili kuwakoa na janga hilo.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere akizungumza na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' amekiri bado UVIKO-19 ipo hivyo wananchi wapate chanjo.

Makongoro anasema kwamba UVIKO-19 ikimshika na kumkuta mtu ameshapata chanjo inakuwa ni rahisi kupambana nayo, tofauti na yule ambaye hajapatiwa chanjo.

“Tutumie nafasi hii kwa kuhamasisha wananchi wetu tukitumia mikutano ya hadhara, nyumba za ibada, wazee wa kimila, masoko na magulio ili waweze kupata chanjo ya UVIKO-19 ambayo inatolewa bila malipo,” anaeleza Makongoro.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Dawar, Charles Akonaay anaeleza kwamba Diwani anaaminika sana kwa wananchi kuliko hata daktari hivyo hawatakiwi kunyamazia hilo kwani watakosa watu.

“Wataalam wa afya hakikisheni kuwa hii chanjo inapatikana kwani watu walio wengi wameikubali hivyo mjipange vizuri katika kutoa chanjo hadi huku vijijini kwetu," anaeleza Akonaay.

Mkazi wa kata ya Ganana, Rosemary Jacob anaeleza kwamba amepata chanjo hiyo ya UVIKO-19 kwenye hospitali ya Tumaini ya wilaya hiyo baada ya yeye kupatiwa elimu kwanza.

“Sikuona madhara makubwa zaidi ya kichefuchefu na kahoma kamuda mfupi ila hivi sasa nina amani moyoni kwani nimeshapata chanjo yangu na sina hofu tena juu ya UVIKO-19,” anasema Rosemary.

Mkazi wa kata ya Katesh, Magdalena Ombay anasema kuwa, amepata chanjo ya UVIKO-19 baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalam wa afya hivyo hana hofu yoyote juu ya maambukizi ya ugonjwa huo.

“Elimu ikishatolewa kwa wananchi na wakaelewa inakuwa rahisi kwao kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 mradi tuu wahamasike kupata maelezo ya wataalam wa afya,” anamalizia kwa kusema Ombay.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...