
NAIBU Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania kuhakikisha kuwa ujenzi wa maabara ya mbolea
unakamilika kwa wakati.
Ametoa agizo hilo leo Julai 8, 2022
alipotembelea ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili
kupata taarifa na kuona hatua ya ujenzi wa maabara hiyo ulipofikia.
Naibu
Waziri Mavunde amesema kukamilika kwa jengo hilo la maabara kutaifanya
Tanzania kuwa na maabara kubwa inayojihusisha na upimaji wa mbolea
Afrika mashariki na kati.
Aidha, ameitaka kamati ya ujenzi pamoja
na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa TFRA kuhakikisha wanasimamia
ipasavyo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ili ifikapo mwezi Agosti ujenzi
wa maabara hiyo uwe umekamilika.
“Suala la ujenzi mwisho iwe
mwezi wa saba, mwezi wa nane nitafika ili kuona hatua mliyofikia kwani
serikali ina shauku kubwa kuona maabara inafanya kazi hivyo mfanye kazi
usiku na mchana”, Mavunde alisisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo alisema ofisi yake itahakikisha
ujenzi huo unakamilika kwa wakati kwani kukamilika kwake kuna manufaa
kwa nchi, taasisi anayoisimamia na jamii ya watanzania kwa ujumla.
Akitoa
taarifa ya ujenzi wa ma baraaba hiyo Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi na
Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa
Pamoja, Joseph Charos amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 70 na kuwa
tayari vifaa vyote kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo vimenunuliwa.
Ujenzi
wa maabara hii ni katika kuhakikisha TFRA inatekeleza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa mbolea na
kuzisajili kwa matumizi ya kilimo, kufanya uchambuzi wa udongo na mimea
pamoja na kuitambulisha maabara kimataifa kutokana na uwezo wake katika
kuchambua mbolea Afrika Mashariki na Kati.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...