Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo kipya cha Polisi Mavurunza, Wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, Septemba 3, 2023. Watatu kulia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba na wapili kushoto ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Murilo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza baada ya kufungua Kituo kipya cha Polisi Mavurunza, Wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, Septemba 3, 2023.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akiwaaga wananchi wa Kimara, Wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, baada ya kufungua Kituo cha Polisi Mavurunza Wilayani humo, leo Septemba 3, 2023. Katikati ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akitoa cheti cha pongezi kwa kiongozi wa ulinzi shiriki kata ya Kimara, Hamidu Kimtu baada ya ufunguzi wa Kituo kipya cha Polisi Mavurunza, Kimara Wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, Septemba 3, 2023. Kulia ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Murilo.


* Kamanda Murilo awataka askari kuzingatia nidhamu, maadili na haki katika kituo kipya Mavurunza

WAZIRI Wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi. Hamad Masauni ametoa onyo kwa wahalifu kote nchini kutofikiri kufanya uhalifu badala yake watafute shughuli nyingine za kiuchumi kwa kuwa hawatavuka katika Jeshi la Polisi ambalo lipo macho katika kuhakikisha ulinzi na usalama unadumishwa.

Masauni ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua kituo cha Polisi cha Mtaa wa Mavurunza Kata ya Kimara ambacho hadi kukamilika kwake kimegharimu Shilingi million 100 huku wananchi wa Mtaa huo wakichangia shilingi milioni 70.

"Hakuna mhalifu atakayevuka katika mipaka ya Jeshi la Polisi, Hatushindwi! juzi Njombe walitubip shughuli yao imeisha usiku wa leo.. Jeshi la Polisi na makamanda ni imara na wananchi wanaonesha mshikamano katika kipindi hiki chenye shughuli nyingi za kiuchumi..Dar es Salaam ni tulivu, Tanzania ni salama." Amesema.

Pia amelitaka jeshi la Polisi kutoa huduma nzuri na kuhakikisha haki inatolewa sambamba na kushughulikia kero za wananchi kwa haraka.

"Wapo baadhi ya askari wanafanya mambo kinyume na kanuni za jeshi la Polisi, Jeshi linafuatilia na kuchukuwa hatua...Na kwa upande wa Serikali baada ya malalamiko ya wananchi Rais Samia Suluhu Hassan aliunda kamati ya Tume ya Haki Jinai kuangalia nini kifanyike ili kuimarisha zaidi Jeshi la Polisi."Ameeleza.

Vilevile amesema, kituo hicho kilichojengwa kwa nguvu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Mbunge hadi kukamilika kwake kutapunguza adha ya wanachi kwa kufuatia huduma katika vituo vilivyo mbali na makazi yaonikiwemo vituo vya Gogoni na Urafiki.

"Wananchi wa Mavurunza ni mfano wa kuigwa katika kuonesha Nia na kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuweka usalama mbele, kitunzeni kituo hiki na jeshi litatoa huduma kwa haki na wakati." Amesema.

Kuhusiana na kuimarisha usalama kwa ngazi za Kata Mhandisi. Masauni amesema dhamira ya Serikali ni kuimarisha vyombo vya usalama na ongezeko la bajeti la asilimia 32 pia imeelekezwa katika kupeleka usafiri kwa Polisi Kata na Wilaya, na ameelekeza uendelezwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi na kuwataka vijana kujiunga na vikundi hivyo ili kudumisha ulinzi na usalama katika mitaa wanayoishi.

Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Murilo amewashukuru wananchi wa Mavurunza kwa kutambua masuala ya kiusalama na kushiriki katika ujenzi wa kituo hiki." Amesema.

"Niwahakikishie kuwa kituo hiki kitatumika kama ilivyokusudiwa kiusalama na kutoa haki...Askari watakaotoa huduma kituo hiki wazingatie nidhamu na uadilifu,Sitegemei wananachi kukasirika na kuchoma moto kituo hiki kwa huduma mbovu zitakazotolewa na nitafuatilia hili kwa ukaribu zaidi." Amesema Kamanda Murilo.

Pia amesema, Jeshi la Polisi halina huruma na wahalifu na litaendelea kuhakikisha wananachi wanafanya shughuli zao za kiuchumi kwa amani na usalama usiku na mchana ili kukuza uchumi wa Nchi na uwekezaji kama Serikali ya awamu ya sita ilivyodhamiria.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashim Komba amesema katika kuhakikisha usalama unadumishwa atashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha jijini hilo linakuwa salama na wananchi wanafanya shughuli zao kwa amani.

Aidha ameagiza kuendeleza kwa vikundi vya ulinzi shirikishi na kushughulikia changamoto zao ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuimarisha usalama katika mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji amewashukuru wananchi wa Mtaa ya Mavurunza kwa kujitoa katika ujenzi wa kituo hicho ambacho kilidumu kwa muda wa mrefu na kupitia kampeni ya uchaguzi ya 2020 waliahidi kuongeza chachu ya ujenzi huo kabla ya 2025.

"Askari hawana chama na hawatatoa huduma kwa upendeleo ila kituo hiki kimejenga kwa nguvu kubwa na chama cha Mapinduzi kupitia uongozi wa Kata...tuna ahadi kubwa tano ambazo tuliahidi kwa wananchi wa Kimara ikiwemo ujenzi wa kituo hiki, barabara ya Kikwete highway ya Kilomita Saba itakamilika kabla ya mwaka 2025, Bilioni 17 imeidhinishwa kwa ujenzi pamoja na hospitali ya Wilaya Baruti...tutakamilisha miradi hii kabla ya 2025 ili wananchi wapate huduma bora." Amesema.

Aidha amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia.Suluhu Hassan ameidhinisha Wilaya za Ubungo na Kigamboni kuwa kuingia katika miradi ya DMDP ya ujenzi wa barabara ambapo Jimbo la Ubungo limepata Kilomita 55 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 88.5.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Cleophance Malima amesema wazo la kituo hicho lilitokana na Umoja wa wananchi wa mtaa wa Mavurunza 'Wanaume Upendo Group' kwa kushirikiana na wananchi wa Mtaa wa Mavurunza.

"Hadi kukamilika kwa mradi huu jumla ya shilingi milioni 100 zimetumika, ambazo shilingi milioni 70 zilichangwa na wananchi wa Mavurunza, milioni 20 zilitoka katika Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo na wadau mbalimbali walichangia vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 10 katika kufanikisha ujenzi huu" Amesema.

Malima amesema, wananchi wa Kata ya Kimara Mtaa ya Mavurunza kwa kushirikiana na Serikali wamejitoa na kuhakikisha kituo hicho kinajengwa kwa ajili ya usalama ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinafanyika kwa usalama.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...