Diwani wa Ngorongoro, Diwani Jonnas Tiams aliyehamia  Msomera  akizungumza na waandishi wa habari   hawapo pichani hapo akiwa katika eneo la nyumbani kwake Msomera, Wilayani Handeni Mkoani Tanga

Mwananchi ambaye amehamia Msomera  akitokea Ngorongoro akioenesha waandishi wa habari hati ya umiliki wa nyumba yake aliyopewa na serikali  mara baada ya kuhamia Msomera.

Mwananchi akipata huduma  ya Posta katika Kijiji Cha Msomera kilichopo Wilayani Handeni  Mkoani  Tanga.
Mwanafunzi Neema Ming'ata wa kidato cha pili akitoa shukrani zake kwa serikali  kwa kuwapa fursa ya kupata elimu huku akiomba kujengea shule za mabweni.
Jengo la Hospitali  inayoitwa jina la Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa  iliyopo Msomera.
Na Khadija Kalili, MSOMERA
WAMASAI wanaoishi katika makazi mapya  ambayo wamehamia kwa hiari  wameonesha kufurahia maisha hayo wanayoishi kutokana kupata faida lukuki ikiwemo kupata chakula cha kutosha na lishe bora kwa familia zao.
Wakizungumza na Waandishi  wa Habari kutoka vyombo mbalimbali  ambao wako kwenye ziara iliyoratibiwa na Idara ya Habari  MAELEZO na kufadhiliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa  Ngorongoro  wamesema wanaishkuru serikali kwa sababu hali ya maisha yao imebadilika kutokana na kubadili mfumo wa maisha waliyokuwa wakiishi awali na wanyama ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
"Afya zetu zimeimarika kusema kweli  nashkuru mara baada ya serikali kutuhamishia huku Msomera nimeweza kuwatosheleza watoto wangu kwa kuwapa chakula bora tofauti na maisha ya awali ambapo ilikuwa vigumu kuwashibisha kutokana na kutokuwa na chakula cha kutosha sababu ndani ya hifadhi kwani haturuhusiwi kulima, huku tumelima mahindi, maharage na pia mifugo nayo imepata malisho ya uhakika na hailiwi na wanyama." Amesema  mwananchi mmoja ambaye ni miongo mwa waliohamia kwa hiari Msomera.
Akizungumza  na waandishi wa habari  Diwani  wa Ngorongoro Johannes Tiams ambaye amehamia Msomera awamu ya kwanza huku akiwa amenufaika kwa kupata nyumba tatu kwa sababu ana wake watatu amekiri kuwa maisha ya Msomera ni mazuri na shuhuda ni nyingi ikiwa ni pamoja na kuimarika kiafya na uchumi.
"Mimi nilihamia hapa katika awamu ya kwanza naishi vizuri na familia yangu kama jinsi mnavyoona ila napenda  kuwaeleza  kuwa shuhuda ni nyingi kutoka kwa kila kila kaya watawaeleza namna hali zao za maisha zilivyobadilika japo kule Ngorongoro  kuna wanafamilia wamebaki ila ninaamini watahama tu siku moja kwa hiari yao kutokana na sisi tumekuwa tunafanya mawasiliano nao na kuwaasa waachane na propaganda hasi zinaenezwa na baadhi ya watu ambao  hawajui athari za kuishi ndani ya hifadhi na wanyama.
Aidha Waandishi  wa Habari wameshuhudia wananchi hao wanamiliki nyumba za kisasa zenye vyumba vitatu zenye umeme eneo kubwa la kuhifadhi mifugo yao  kuwa na eneo la kulima huku  wakipata  mahitaji mengine yote muhimu ikiwemo kujengewa Hospitali, watoto  wanakwenda shule kusoma, huduma za usafirishaji vifurushi kwa njia ya Posta.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekua ikiwahamisha kwa utaratibu wa kufanya  tathmini ya kuwalipa kila mwananchi mwenye mali anayomiliki   ndani ya ya  hifadhi ya Ngorongoro na baada ya kuwalipa kila kaya ikiwa ni pamoja na kupewa kiasi cha fedha cha Milioni 10, huku mamlaka ya hifadhi  ya Ngorongoro huwa inawahamisha kwa gharama zake bila kulipisha muhusika yeye, mali zake ikiwemo mifugo pamoja  na familia yake kwenda kwenye makazi mapya  Msomera  Mkoani Tanga.
Afisa Mwandamizi Mkuu  wa Kitengo Cha Mawasiliano  Ngorongoro, Kassim  Nyaki amesema kuwa awamu ya kwanza ya kuwahamisha  wananchi hao kutoka Ngorongoro kwenda Msomera imefanyika  Februari 2022 na kukamilika Januari 2023 huku utekelezaji awamu ya pili ambayo  umefanyika Julai 2023 na ukitarajiwa   kwenda mpaka  Machi, 2024 huku lengo kubwa la Serikali ni kujenga nyumba 5,000 katika  eneo  linalojumuisha maeneo ya  Kitwai, Sauni na  Msomera kwa ajili ya wakazi wa Ngorongoro wanaohamia  kwa hiyari eneo la Msomera.
Nyaki ameongeza kwa kubainisha  kuwa  tayari wananchi wamejengewa bwawa ambalo wanalitumia kuchota maji ya matumizi mbalimbali ya kibinaadamu, pia wamejengewa majosho ya kuogesha mifugo yao  jambo ambalo ni tofauti na walivyokuwa wakiishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro  huduma hizo hawakuzipata.


.jpeg)




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...