.jpeg)
Na Khadija Kalili Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohammed Mchengerwa, ametangaza rasmi kupandishwa hadhi kwa Halmashauri ya Bagamoyo na kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo.
Tamko hilo limetolewa leo, Agosti 22, wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nia Njema, wilayani Bagamoyo.
Mhe. Mchengerwa amesema tangazo hilo linatokana na maelekezo rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameridhia mabadiliko hayo muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Bagamoyo.
“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Halmashauri ya Bagamoyo ipandishwe hadhi kuwa Halmashauri ya Mji. Ninyi sasa ni mji kamili na maandalizi ya mipango ya mji yataanza mara moja,” alisema Mchengerwa.
Kwa kutekeleza agizo hilo, Waziri Mchengerwa amewaagiza wataalamu wa mipango kutoka TAMISEMI kufika Bagamoyo na kuanza maandalizi ya kitaalamu ya upangaji wa mji huo. Pia amemuagiza Katibu Mkuu wa TAMISEMI kuandaa tangazo rasmi katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuthibitisha kisheria kupandishwa hadhi kwa Bagamoyo.
Serikali Kuwekeza Bilioni 1 Katika Miundombinu ya Afya
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa ametangaza kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika maeneo ya Bagamoyo. Ametoa agizo kwa Katibu Mkuu TAMISEMI kuhakikisha shilingi milioni 700 zinapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika eneo la Kisutu, pamoja na shilingi Milion 300 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya katika eneo la Kitame.
TARURA Kuboreshwa Miundombinu ya Barabara Bagamoyo
Waziri pia ameielekeza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya mapitio ya kina ya mtandao wa barabara za mji wa Bagamoyo ili kuandaa mpango wa kuongeza barabara za lami kwa ajili ya kuboresha usafiri, biashara na ustawi wa wakazi wa mji huo mpya.
Wananchi Wamshukuru Rais Samia
Akimkaribisha Waziri Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, aliwasilisha shukrani kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo kwa hatua mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Sisi wakazi wa Bagamoyo tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kutufungulia fursa mpya za maendeleo. Ameturidhia kujenga Bandari ya Bagamoyo, reli ya SGR kutoka Bagamoyo hadi Kwala kwa ajili ya mizigo, pamoja na njia ya kusafiraha umeme kutoka Chalinze hadi Bagamoyo Kv 220 ” alisema Kunenge.
Aidha, aliongeza kuwa Serikali imeanza pia ujenzi wa barabara ya Makofia–Mlandizi kwa njia mbili, hatua inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri katika. mkoa huo na kukuza uchumi wa wananchi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...