Na Mwamvua Mwinyi, Mafia
KATIKA mwambao wa Mashariki mwa Tanzania, Kisiwa cha Mafia kinajulikana kwa utulivu wake wa asili, mandhari ya kuvutia ya bahari na matumbawe yaliyojaa uhai.
Hata hivyo, chini ya uso wa samawati wa maji yake, changamoto ya uchafuzi wa mazingira ya baharini inaendelea kukua, ikiathiri viumbe wa majini na kutishia uchumi wa jamii ya kisiwa hicho.
Ailars Lema, Mhifadhi Bahari kutoka Mafia Island Marine Park (MIMP), anaeleza kuwa taka ngumu, hasa plastiki, zimeendelea kuwa changamoto kubwa ndani ya maeneo ya hifadhi baharini.
Aina hizi za taka hutokana zaidi na shughuli za kibinadamu kama matumizi ya chupa za plastiki kama boya kwa wavuvi na wakulima wa mwani, pamoja na shughuli za utalii.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka wa fedha 2023/2024 zilizokusanywa na MIMP, jumla ya tani 1.7554 (sawa na kilo 1,755.4) za taka ngumu hasa plastiki zilikusanywa kutoka maeneo mbalimbali ndani ya hifadhi.
Anasema kiasi hiki kinamaanisha wastani wa kilo 146 kwa mwezi, ama zaidi ya kilo 4.8 kila siku.
“Taka nyingi zilizokusanywa zilihusisha chupa za maji, vifungashio vya bidhaa, vipande vya nyavu na plastiki zinazotumika kama boya,” anaeleza Ailars.
Ailars anabainisha kuwa licha ya changamoto hizo, Mafia ina nafasi ya kuwa mfano wa mafanikio katika uhifadhi wa bahari kutokana na hatua zinazochukuliwa kwa sasa.
Anaeleza kuwa bahari safi si tu msingi wa uhai wa viumbe wa majini, bali pia msingi wa afya, uchumi na maisha ya vizazi vijavyo.
“Ikiwa tutatunza mazingira, mazingira yatatufaa, lakini tukiyapuuzia, tutabeba mzigo wake sisi na watoto wetu,” anasisitiza Ailars.
Amesisitiza haja ya ushirikiano baina ya wananchi, wavuvi na wadau wa mazingira ili kukomesha utupaji hovyo wa plastiki na taka nyingine kwenye bahari.
Vilevile takwimu kutoka shirika lisilo la kiserikali la Sea Sense zinaonyesha kuwa mwaka 2021, zaidi ya kilo 2,200 za taka ngumu zilikusanywa kwenye fukwe za Mafia wakati wa kampeni ya usafi wa Pwani.
Taka hizo zilijumuisha plastiki, nyavu zilizotupwa, chupa na mifuko ya plastiki ambazo ni tishio kubwa kwa viumbe kama kobe wa baharini wanaofika Mafia kutaga mayai.
Licha ya uchafuzi wa taka, mabadiliko ya tabianchi nayo yanachangia kuporomoka kwa matumbawe, ambayo ni makazi muhimu ya samaki na viumbe wengine wa baharini.
Kupungua kwa matumbawe kunapunguza pia idadi ya samaki,huku uvuvi, ikiwa chanzo kikuu cha kipato kwa wakazi wa Mafia.
“Samaki wanapungua ukilinganisha na miaka ya nyuma, inabidi tuvuke mbali zaidi baharini, wakati mwingine nyavu zinashika taka nyingi,” anasema Juma Omari, mvuvi kutoka Kijiji cha Kilindoni.
Mvuvi na mkazi kama Juma hukabiliwa na mtego wa mazingira, hawana rasilimali za kutosha kubadili njia zao za maisha, lakini ni waathirika wa moja kwa moja wa uchafuzi wa bahari na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika kukabiliana hali hiyo, mnamo Oktoba 2025, Mafia ilifanya kikao cha kuandaa mpango mkakati na mpango kazi wa kudhibiti taka ngumu na plastiki.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Dkt. Seleman Kataga, alitoa wito kwa wananchi na wadau kushirikiana kikamilifu kutekeleza mpango huo ili kuokoa mazingira.
Kwa upande wake, Ofisa Afya wa Wilaya ya Mafia, Othman Masanga, alieleza kuwa ana matumaini mpango huo utaboresha shughuli za kiuchumi kama utalii, ambao unategemea mazingira safi na salama.
“Kisiwa chetu kinazungukwa na bahari na hutegemea uvuvi na utalii, hivyo, mpango huu utasaidia kuhifadhi bayoanuai na kuimarisha uchumi,” anasisitiza Masanga.
Abdul Amrani, kutoka kikundi cha Takataka Dampo, aliunga mkono mpango huo akisema utasaidia kutekeleza maazimio ya kuzuia kuenea kwa plastiki.
Kwa mujibu wa Gladness Lauwo, Ofisa kutoka taasisi ya FORUMCC, kuundwa kwa mfumo jumuishi wa udhibiti wa taka ni fursa muhimu ya kutekeleza mradi wa “Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu”, unaoratibiwa na FORUMCC kwa kushirikiana na IUCN, Ofisi ya Makamu wa Rais, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, wadau wa mazingira na wananchi.
Nae Dkt. Robert Katikira, mshauri wa mradi wa PWANI YETU kutoka Shirika la Ujerumani la Ushirikiano wa Kimataifa (GIZ), anaongezea waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kulinda mazingira kwa kutumia kalamu zao kuhamasisha umma kuhusu ulinzi wa bahari na kupambana na utupaji holela wa taka.


.jpg)
.jpg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...