

Na Mwandishi wa OMH
KWA muda mrefu, kampuni nyingi za ubia kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa kimataifa ziliongozwa na wataalamu kutoka nje ya nchi.
Lakini sasa, upepo umegeuka, baadhi ya kampuni hizo zinaongozwa na wazawa — na matokeo yake yanaonekana wazi, kimkakati na kifedha.
Tanzania inashuhudia kizazi kipya cha viongozi wazawa wakiongoza katika nafasi ya Afisa Mtendaji Mkuu kampuni kubwa kama Benki za NMB na NBC, Puma Energy Tanzania, na Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER).
Ruth Zaipuna (Benki ya NMB) — Mtanzania wa kwanza kuongoza benki hiyo. Ameongeza gawio la serikali kutoka Sh16 bilioni wakati alipoteuliwa Agosti 2020 hadi Sh68.1 bilioni mwaka wa fedha wa 2024/25, ongezeko la asilimia 325.6.
Theobald Sabi (Benki ya NBC) — Amebadilisha taswira ya NBC, akipandisha gawio la serikali kutoka Sh1.3 bilioni hadi Sh10.5 bilioni, ongezeko la asilimia 707.7.
Fatma Abdallah (Puma Energy) — Mtanzania mwenye uzoefu wa kimataifa, ameongeza gawio kutoka Sh8 bilioni hadi Sh13.5 bilioni, ongezeko la asilimia 68.8.
Mohamed Mohamed (TIPER) — Ameongeza gawio la serikali kutoka Sh1.5 bilioni hadi Sh5.5 bilioni, ongezeko la asilimia 267.
Mabadiliko haya yanaakisi dira ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), chini ya uongozi wa Bw. Nehemiah Mchechu.
Kufikia Juni 9, 2025, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa imekusanya Sh1.028 trilioni kutoka kwenye gawio na michango ya taasisi za umma na kampuni za ubia ongezeko la asilimia 68 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, na asilimia 34 zaidi ya makusanyo ya jumla ya mwaka wa fedha 2023/24.
Huu ni ushahidi kwamba watanzania wanaweza kuongoza, wanaweza kutekeleza, na wanaweza kutoa matokeo makubwa katika kampuni za ubia kati ya serikali na wawekezaji wa kigeni.
“Lengo letu si kuweka wazawa tu katika nafasi za juu za uongozi, bali kuhakikisha uongozi wao unaleta tija, uwajibikaji na maslahi ya taifa kwa muda mrefu,” alisema Bw. Mchechu.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...