📍TANESCO yawapa wazazi na waalimu elimu ya nishati safi ya kupikia kwa umeme
📍Jiko la Nishati safi ya kupikia latolewa kuendelea kuhimiza matumizi ya kupika kwa umeme
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, TANESCO Mkoa wa Kigamboni ilitoa elimu ya matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia katika Shule ya Msingi Malaika iliyopo Kigamboni.
Elimu hiyo ilitolewa wakati wa siku maalum ya ufunguzi wa shule tarehe 13 Januari, 2026 (Back to School), iliyowakutanisha wazazi na walimu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya, alisema kuwa lengo la kutumia fursa hiyo ni kuhakikisha wazazi na waalimu wanapata uelewa wa kina kuhusu faida za kutumia nishati ya umeme kupikia akibainisha faida zake kuwa ni nishati salama, gharama nafuu na rafiki kwa mazingira.
“Shirika linakenga kuhakikisha wazazi na walimu wanaelewa kuwa kupikia kwa umeme ni salama, ni nafuu na kunalinda afya pamoja na mazingira. Tukibadili mtazamo wetu leo, tutakuwa tumewekeza kwenye maisha bora ya baadaye,” alisema Tumaini.
Vile vile, ili kuunga mkono utekelezaji wa matumizi ya nishati safi ya umeme katika taasisi za elimu, TANESCO ilikabidhi jiko la umeme aina ya Pressure Cooker lenye ujazo wa kilo 15 kwa uongozi wa shule hiyo ambalo litawarahisishia kupika shuleni hapo.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malaika Bw. Ahmed Abdallah Fataki aliishukuru TANESCO Mkoa wa Kigamboni kwa msaada huo na kuahidi kulitumia kikamilifu, hatua itakayosaidia kuachana na matumizi ya nishati zisizo salama shuleni hapo.
“Jiko hili litatusaidia sana kuboresha huduma za chakula kwa wanafunzi na kutuondolea utegemezi wa nishati zisizo salama. Tunaishukuru TANESCO kwa kutukumbuka na kutuunga mkono katika ajenda ya nishati safi,” alisema Bw. Fataki.
Nao wazazi wa wanafunzi hao walionesha mwitikio mkubwa kwa kutembelea banda la TANESCO kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuahidi kuacha matumizi ya nishati zisizo salama, ili kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.


.jpeg)


.jpeg)















.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)



.jpeg)


























