Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma

Serikali imesema itaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa sera, sheria na miongozo inayohusu huduma za lishe nchini, ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi na salama kuhusu afya na lishe.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la papo kwa hapo lililoulizwa na Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe kuhusu ongezeko la watu wanaojihusisha na utoaji wa huduma za lishe bila kuwa na vibali au sifa stahiki.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na mabaraza na taasisi za kitaalamu itaendelea kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazohusu huduma za afya na lishe zinafuatwa kikamilifu ili kuwalinda wananchi dhidi ya taarifa potofu au huduma zisizo salama.

“Niwaelekeze Wizara ya Afya pamoja na mabaraza yote ya kitaalamu kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, sera na miongozo ya huduma za lishe huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini kuhusu uwezekano wa kuratibu vizuri zaidi masuala ya leseni kwa watoa huduma za afya na lishe,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojitangaza kuwa wataalamu wa lishe kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na kukua kwa utandawazi pamoja na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, pamoja na faida zinazotokana na upatikanaji wa taarifa kwa urahisi kupitia teknolojia, bado ipo haja ya kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu lishe inatolewa na wataalamu wenye sifa, weledi na vibali vinavyotambulika kisheria.

Aidha, amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watu au taasisi zitakazobainika kutoa huduma za lishe kinyume na taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakikisha wanapata huduma kutoka kwa wataalamu waliosajiliwa na mamlaka husika.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa afya za wananchi pamoja na kuhakikisha elimu ya lishe inayotolewa.


WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imepanga kujenga madarasa 1,360 kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa sera ya elimu ya miaka 10 ya lazima sambamba na kuongeza miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari nchini.

Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mazingira ya elimu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za elimu kwa wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Serikali itajenga mabweni 17 katika shule za sekondari 17 pamoja na nyumba 33 za walimu ili kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa walimu, hususan katika maeneo yenye changamoto za miundombinu.

Vilevile, vituo 50 vya walimu vitajengwa katika Halmashauri za Wilaya kwa lengo la kuongeza motisha kwa walimu na kusaidia utoaji bora wa huduma za elimu. 



Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 2.398 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na miradi mbalimbali ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Prof. Mkenda amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 2,394,423,829,000 zimeombwa kwa ajili ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46), ambapo Shilingi 697,841,881,000 ni kwa matumizi ya kawaida.

Amefafanua kuwa ndani ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi 648,082,352,000 zitatumika kwa mishahara ya watumishi huku Shilingi 49,759,529,000 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo.

Aidha, amesema Shilingi 1,696,581,948,000 zinaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Shilingi 1,337,249,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 359,332,948,000 ni fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Wizara kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) imeomba kuidhinishiwa Shilingi 3,866,993,000 kwa matumizi ya kawaida.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, kati ya fedha hizo za UNESCO, Shilingi 1,335,020,000 ni kwa mishahara na Shilingi 2,531,973,000 ni kwa matumizi mengineyo.

Ameomba Bunge kupokea, kujadili na kupitisha makadirio hayo ya bajeti yenye jumla ya Shilingi 2,398,290,822,000 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Wizara katika mwaka wa fedha 2026/2027.



Benki ya Exim Tanzania, kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) unaojulikana kama Exim Cares, imeunga mkono huduma za afya katika Hospitali ya Manispaa ya Geita, ikiwa ni hatua ya kuziba mapungufu muhimu katika huduma za afya ya uzazi na dharura, huku ikithibitisha tena dhamira yake ya kuboresha ustawi wa jamii inazozihudumia.

Msaada huu ni sehemu ya mpango wa kimkakati wa benki hiyo katika uwajibikaji kwa jamii, unaolenga maeneo muhimu yakiwemo afya, elimu, ubunifu, mazingira, na uwezeshaji wa kiuchumi. Kupitia nguzo hizi, benki imetekeleza miradi mbalimbali nchini, ikijumuisha programu za msaada wa tiba, kampeni za uchangiaji damu, ufadhili wa elimu na miradi ya uwezeshaji wa jamii yenye lengo la kuleta matokeo endelevu na ya maana.

Hatua hii ndani ya Geita umechochewa na uhitaji uliobainika ndani ya hospitali, ambapo upungufu wa vifaa muhimu vya tiba umekuwa ukizuia utoaji wa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususani kwa wajawazito, watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda au wanoazaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Kwa kuingilia kati katika maeneo haya muhimu, Benki ya Exim inalenga kuimarisha uwezo wa hospitali na kuboresha matokeo ya afya kwa jamii inayozunguka.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya wa Geita, Mheshimiwa Hashim Abdallah Komba, aliipongeza Benki ya Exim na kuishukuru kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha afya ya watoto, hususan watoto njiti na wale wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Pia alibainisha kuwa, licha ya benki hiyo bado kutokuwa na faida katika tawi lake jipya la Geita, imeonyesha moyo wa huruma na uwajibikaji kwa kuweka kipaumbele katika kusaidia jamii.

Aidha, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Stanley Kafu, alisema kuwa hatua hii inaonyesha mkakati wa makusudi na unaozingatia mahitaji halisi ya jamii.

“Kupitia Exim Cares, tunahakikisha tunalenga maeneo yanayogusa moja kwa moja maisha ya jamii inayotuzunguka. Hapa Geita, tulizungumza na wadau na kubaini mapungufu mahususi katika huduma za afya ya uzazi na watoto, na msaada huu unalenga kushughulikia kwa changamoto hizi kwa njia itakayosaidia jamii” alisema.

Mwakilishi wa Hospitali ya Manispaa ya Geita, Mganga Mfawidhi Dr. Thomas Mauru, aliipokea msaada huo kwa mikono miwili, akisema unakwenda sambamba na uhitaji wa haraka katika kuboresha huduma tajwa.

“Msaada huu utaongeza uwezo wetu wa kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususan kwa Watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Unachangia moja kwa moja kuboresha ubora wa huduma za afya tunazotoa kwa jamii yetu,” alisema.

Hatua hii inaakisi falsafa pana ya Benki ya Exim ya kuhakikisha ukuaji wake unaendana na maendeleo ya jamii inazozihudumia, na kuhakikisha kwamba kila benki inavyokua, inajibu mahitaji halisi ya wananchi.

Baada ya shughuli hii ya CSR, benki hiyo inatarajiwa pia kuzindua rasmi tawi lake jipya la Geita, hatua inayolenga kuimarisha zaidi uwepo wake katika mkoa huo na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watu binafsi na biashara. Uzinduzi huo unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde.

Kama sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu, Benki ya Exim inaendelea kuwekeza katika suluhisho na ushirikiano unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, kuchochea ukuaji wa biashara na kuimarisha mnyororo wa thamani, ikionesha nafasi yake si tu kama taasisi ya kifedha, bali pia mshirika wa maendeleo ya Tanzania.

Mkuu wa Wilaya ya Geita Mh. Hashim Abdallah Komba(kulia) akikabidhiwa moja ya vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Bw. Stanley Kafu (kushoto) kwa lengo la kurudisha kwa jamii. Hafla hii imefanyika kama moja ya huduma za Benki hiyo chini ya Mpango wa Exim Cares ambapo wanatoa misaada kwa sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na mazingira. Tukio hilo limefanyika tarehe 6 May 2026, Mkoani Geita.









 

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Dkt. Neema Majule, amesema Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027 inapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika utafiti wa miamba na vyanzo vya maji ili kubaini maeneo yenye maji ya kutosha, kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Majule ameyasema hayo Mei 6, 2026 bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji, ambapo alieleza kuwa pamoja na jitihada za serikali za kutoa maji kutoka kwenye mito na maziwa, ni muhimu kufanya tathmini ya mazingira ili kuhakikisha hatua hizo haziathiri viumbe hai na mfumo wa ikolojia.

Aidha, ameshauri serikali kuboresha na kukarabati miundombinu ya maji iliyochakaa ili kupunguza upotevu wa maji na kusaidia kufikia viwango vya kimataifa, Pia ameomba Wizara kutenga mfuko maalum wa matengenezo (Maintenance Fund) utakaowezesha ukarabati wa miundombinu kufanyika sambamba na udhibiti wa upotevu wa maji.

Katika mchango wake, Dkt. Majule amesema ndoto ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma bado ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mkoa huo, amesema wananchi wa Dodoma wana matarajio makubwa kuona mpango huo unatekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa vitendo na si kubaki kwenye mipango ya maandishi pekee yaani makaratasi.





Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amewapongeza walimu wa Mkoa wa Dodoma kwa jitihada zao zilizochangia kuongezeka kwa ufaulu katika ngazi zote za elimu kuanzia msingi hadi sekondari.

Akizungumza jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa elimu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mei 6, 2026, Prof. Shemdoe amesema takwimu zinaonyesha mafanikio makubwa ya ufaulu kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Ameeleza kuwa ufaulu wa darasa la nne uliongezeka kutoka asilimia 94.6 mwaka 2024 hadi asilimia 95.9 mwaka 2025, huku darasa la saba ukipanda kutoka asilimia 87.8 hadi asilimia 93.2. Kwa upande wa kidato cha pili, ufaulu uliongezeka kutoka asilimia 86.12 hadi 88.9, kidato cha nne kutoka asilimia 92.8 hadi 94.4, na kidato cha sita kutoka asilimia 99.86 hadi asilimia 99.87.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi, viongozi na wadau wa elimu, akibainisha kuwa kaulimbiu ya mkoa huo kwenye sekta ya elimu isemayo “Uwajibikaji wangu ni msingi wa kuinua ubora wa elimu Dodoma” imechangia kwa kiasi kikubwa kutoa hamasa.

Prof. Shemdoe amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwajibikaji katika sekta ya elimu kwa kusimamia taaluma, kudhibiti utoro wa walimu na wanafunzi, pamoja na kuhakikisha miradi ya ujenzi wa madarasa, shule mpya na vyoo inakamilika kwa wakati.

Aidha, amewataka viongozi kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya elimu zinatumika kama zilivyokusudiwa, huku akihimiza ubunifu na bidii kazini ili kuongeza mafanikio zaidi.

Aidha Waziri Shemdoe amepinga vikali swala la ubaguzi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuwataka walimu kuhakikisha wanafunzi hao wanapata haki sawa ya elimu, pia amesisitiza umuhimu wa huduma ya chakula mashuleni, akiwataka wazazi kushiriki katika kuchangia chakula na Walimu kutumia maeneo ya shule kwa kilimo kwaajili yao na mengine kwaajili ya Wanafunzi ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha uhakika.

Katika suala la nidhamu, Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa adhabu kwa wanafunzi zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia umri na kosa alilofanya mwanafunzi, sambamba na kufuata miongozo iliyopo badala ya maamuzi binafsi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mkoa huo umeendelea kunufaika na maboresho ya sekta ya elimu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na kuboreshwa kwa maslahi ya walimu.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha Dodoma kupanda kutoka nafasi ya kumi hadi nafasi ya pili kitaifa kwa ufaulu, huku lengo likiwa kushika nafasi ya kwanza.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Khatibu Kazungu, ameeleza kuwa mkutano huo umelenga kutathmini utekelezaji wa mpango mkakati wa elimu wa mwaka 2025, akibainisha kuwa utoaji wa tuzo kwa walimu umeendelea kuwa chachu ya kuongeza ari ya kazi na kuboresha matokeo ya wanafunzi kila mwaka.







Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ametembelea banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa mkutano wa wadau wa elimu uliofanyika Mei 6, 2026 jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazooneshwa na taasisi hiyo, kwa lengo la kufahamu mchango wao katika maendeleo ya sekta ya elimu.

Mkutano huo wa wadau wa elimu Mkoa wa Dodoma umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, ukiwa na kauli mbiu isemayo “Uwajibikaji wangu ni msingi wa kuinua ubora wa elimu Dodoma,” na mgeni rasmi alikuwa Waziri wa TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe.











Leo hii patashika nguo kuchanika kwenye Nusu Fainali ya Mkondo wa Pili wa Europa League ambapo timu nne kushuka dimbani kuwania nafasi ya kucheza Fainali. Je nani kushinda leo?

Tukianza na mechi hii ya Aston Villa dhidi ya Nottingham Forest kutoka kule Uingereza hawa wote wanajuana vyema kabisa. Hii ni mechi ambayo ni ya kisasi kwa mwenyeji baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini kwa bao 1-0.

Mechi hii inakuja na presh ya hali ya juu kabisa kwa vijana wa Unai Emery baada ya kuangusha pointi pale City Ground. Hii inaifanya mechi ya pili kuwa ya “must win” kwa Villa, huku Forest wakicheza kwa utulivu zaidi wakiwa na faida ya matokeo ya awali lakini ni mechi ambayo Villa wanahitaji zaidi wapate matokeo ili wacheze fainali baada ya muda mrefu.

Hii ni mechi ambayo inaweza ikawa na machaguo mawili tofauti kwa timu mbili, Villa wao wanaingia uwanjani wakiwa na lengo kubwa kushambulia ili waweze kusawzisha goli mapema kabisa, lakini kwa upande wa Nottingham Forest wao wanaweza kutumia mbinu ya kujilinda zaidi kutokana an mtaji wa bao moja ambalo wanalo lakini kushambulia kunaweza kukawa kwa mbali.

Tengeneza mkwanja kupitia michezo ya Kasino ya Mtandaoni kama vile, Keno, Aviator, Poker, Roulette, Wild Icy Fruits, Super Heli na mingine kibao. Jiunge leo kwa kutembelea tovuti ya meridianbet.co.tz au piga *149*10# kisha uanze safari yako ya ushindi.

Timu hizi zimekutana mara nyingi kwenye ligi kuu na kila mmoja ameweza kushinda dhidi ya mwenzake. Lakini huku ni kwenye michuano ya Europa kila timu inaweza ikapata matokeo mbele ya mwenzake ukiachilia nafasi zao walizopo kwenye msimamo wa ligi kuu.

Nafasi kubwa ya kushinda mechi hii wanapewa vijana wa Unai kutokana na kiwnago bora ambacho wamekionesha msimu huu, lakini pia uwepo wa kocha wao ambaye haya ndiyo mashindano yake, kwani amewahi kufanya vizuri akiwa na Sevilla ya kule Hispania.

Lakini tahadhari wa Nottingham Forest pia ni kwamba kuongoza kwa bao 1 hukumfanyi atuzuie peke yake kwani wanaweza kufanya makosa ambayo yakawafanya wapoteze mechi hiyo kwani bado bao moja ni dogo na halitoshi kujilinda muda wote wa mchezo.

Hii ni mechi yenye mchanganyiko wa mbinu na akili. Villa wana ubora wa kikosi na uwezo wa kushambulia kwa nguvu, lakini Forest wana faida ya utulivu na mpangilio wa kujilinda pamoja na mashambulizi ya kushitukiza.

Matokeo yatategemea nani atakuwa na ufanisi zaidi katika dakika za mwanzo. Villa wakifunga mapema watafungua mechi, lakini Forest wakistahimili au kufunga kwanza, basi wataweza kudhibiti mwelekeo wa mechi na kufunga njia ya Villa kurejea.

Mtanange mwingine utakuwa kule Ujerumani ambapo Freiburg atamleta kwake Braga ambao walishinda mechi yao ya kwanza ya Nusu Fainali kule Ureno hivyo leo hii ni kisasi kwa mwenyeji pia. Jisajili hapa.

Braga anaingia uwanjani akiwa na faida ya bao 1, baada ya kushinda mechi ya kwanza kwa mabao 2-1 huku weenyeji wao wakiutazama mchezo huu kama wa kufa na kupona kwani hakuna kitu ambacho kitaswasaidi zaidi ya kufunga magoli mengi pekee.

Ikumbukwe kuwa Braga ni moja ya timu ambazo zinafanya vyema kule Ureno wakiwa nafasi ya 4 mpaka sasa kwenye msimamo wa ligi. Huku kwa upande wa wenyeji wao pale Bundesliga wanashikilia nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi huku wakiwa na takwimu mbaya za mechi 3 za mwisho wakiwa wamepoteza.

Hii ni mechi ya maamuzi kwa pande zote mbili huku leo hii ushindi unaweza ukaamuliwa kwa pande zote mbili hasa kama timu ina washambuliaji wazuri kwani kwenye hatua hizi magoli ndio kitu muhimu sana kuliko chochote.

Freiburg wana mfumo na uthabiti, wakati Braga wana kasi na hatari ya moja kwa moja. Timu itakayoweza kulazimisha mpinzani wake kucheza kwa mtindo usio wake itakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Hitimisho ni kwamba, Freiburg watajaribu kugeuza mchezo kuwa wa polepole na wenye udhibiti, huku Braga wakitaka kuufanya uwe wa kasi na wa wazi. Nani atafanikiwa kulazimisha mtindo wake, huyo ndiye atakayekuwa na nusu ya ushindi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa kwenye picha na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Perseus Mining Limited Bw. Rick Menell mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 06 Mei, 2026.

Perseus Mining Limited ni mwekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga, Wilayani Sengerema, Mkoani Mwanza kupitia Kampuni ya Sotta Minining Corporation Limited, inayomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde kwenye picha na Ujumbe wa Kampuni ya Perseus Mining Limited na Sotta Minining Corporation Limited mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 6 Mei, 2026.

Perseus Mining Limited ni mwekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga, Wilayani Sengerema, Mkoani Mwanza kupitia Kampuni ya Sotta Minining Corporation Limited, inayomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania.








 

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali imetangaza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo wa kisheria pamoja na sera maalum zitakazosimamia huduma za upandikizaji wa viungo, ikiwa ni jitihada za kurasimisha na kuimarisha sekta hiyo muhimu ya afya nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la kisayansi lililoandaliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa lililolenga kujadili sera, mwelekeo na mikakati ya kuendeleza huduma za upandikizaji viungo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, alisema maandalizi hayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba mwaka huu.

Amesema  kuwa uwepo wa sera na sheria hizo utaweka misingi imara ya utoaji huduma hizo kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, hali itakayosaidia kuongeza ufanisi na usalama kwa wagonjwa.

Dkt. Magembe alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, jambo linalowezesha wagonjwa wengi kupata matibabu ya hali ya juu ndani ya nchi badala ya kusafiri nje ya mipaka.

Alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa saratani ya damu pamoja na upandikizaji wa figo, huku akieleza kuwa mipango inaendelea ya kuanzisha huduma za upandikizaji wa ini na moyo katika siku za usoni.

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Magembe alisisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya, akieleza kuwa huduma za upandikizaji viungo zina gharama kubwa ambazo si rahisi kumudu bila bima.

Alifafanua kuwa gharama za upandikizaji wa uloto zinaweza kufikia shilingi milioni 75, huku upandikizaji wa figo ukigharimu takribani shilingi milioni 40, hali inayofanya uwepo wa bima kuwa nguzo muhimu kwa wananchi wengi.

Kwa mujibu wake, hadi sasa zaidi ya wagonjwa 147 wamefanikiwa kufanyiwa upandikizaji wa uloto na figo hapa nchini, hatua inayopunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa gharama kubwa za usafiri na matibabu.

Aidha, alibainisha kuwa wagonjwa wa figo wanaohitaji huduma ya kuchuja damu hulazimika kufanya hivyo mara kadhaa kwa wiki, jambo linaloambatana na gharama na changamoto kubwa za maisha, hivyo bima ya afya inaweza kuwa suluhisho muhimu kwao.

“Ni muhimu wananchi wakaona umuhimu wa bima ya afya kama wanavyochukulia bima ya magari, kwa sababu inasaidia kukabiliana na gharama kubwa za matibabu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamini Mkapa, Profesa Abel Makubi, aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, akisema hatua hiyo imewezesha kuboreshwa kwa huduma za kibingwa nchini.

Ameeleza kuwa kongamano hilo limewakutanisha zaidi ya wataalamu 150 wa afya kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ujuzi katika huduma za kisasa za matibabu.

Profesa Makubi aliongeza kuwa hospitali hiyo imejikita katika kuendeleza huduma za upandikizaji viungo na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma hizo zinapanuka zaidi.

Kwa upande wa wanufaika, baadhi ya wagonjwa waliopatiwa huduma hizo walieleza mafanikio yao, wakisema matibabu hayo yamebadilisha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Miongoni mwao ni Richard Masimba, aliyefanyiwa upandikizaji wa figo miezi sita iliyopita, ambaye alieleza shukrani zake kwa madaktari na serikali kwa kumpa nafasi ya kuendelea kuishi maisha ya kawaida.

Naye Nasra Gwota alisema kabla ya kupandikizwa uloto alikuwa akisumbuliwa mara kwa mara na kulazimika kukosa masomo, lakini kwa sasa anaendelea vizuri na kurejea katika shughuli zake za kila siku.








 

Mwamvua Mwinyi, Pwani Mei 6, 2026

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa kufuatia mgogoro wa ardhi uliotokea katika eneo la Vikawe (Lupaso), Kata ya Pangani, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza Mei 6, 2026, ofisini kwake wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge amekiri kutokea tukio hilo la uvunjifu wa amani . 

Amesema watu wasiojulikana walifika katika eneo hilo wakidaiwa kuwa na lengo la kuwaondoa wakazi wanaodaiwa kuvamia ardhi inayomilikiwa kihalali, hali iliyosababisha vifo vya watu wawili . 

Kunenge alieleza kuwa majeruhi wote wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo, mmiliki halali wa eneo pamoja na waliowatuma watu hao kwenda kuwaondoa wakazi.

Vilevile, amewataka wananchi kujiepusha na kujichukulia sheria mkononi  na uvamizi wa maeneo yasiyo yao.

“Wamiliki wa ardhi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria wanapokumbana na migogoro, ikiwemo kufikisha suala hilo katika mabaraza ya ardhi au mahakamani. 

Pia,wamiliki endapo kuna amri ya mahakama ya kubomoa nyumba, washirikishe vyombo vya dola badala ya kuchukua hatua binafsi,” amesisitiza Kunenge.

Kwa upande wake, mkazi wa Chato, Vikawe, Kidawa Hamidu, aliiomba Serikali ya Mkoa pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo ili haki ipatikane kwa pande zote.

Naye Mwenyekiti wa Vikawe Shule, Shaban Shaban, alisema mgogoro huo ulikuwepo muda mrefu na tayari vikao mbalimbali vilishafanyika kutafuta suluhu, lakini bado haijafahamika nani aliwatuma watu hao kwenda kuwaondoa wananchi.

"Coaster zilikuwa kama tano, wakiwemo watu zaidi ya 200 wakidai wametumwa kwenda kubomoa nyumba za watu waliovamia eneo hilo" 

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Siaely Moshi, alithibitisha kupokea majeruhi hao sanjali na vifo vya watu wawili wanaume, akieleza kuwa majeruhi kumi wanaendelea kupatiwa matibabu na wengine wanaendelea vizuri. 




 

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Dkt. Evaline Wilbard Munisi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira na Mahusiano) kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 06 Mei, 2026.
Viongozi mbalimbali wakiapa kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma tarehe 06 Mei, 2026. Kutoka kulia ni; Ndugu Kheri Abdul Mahimbali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Balozi Ali Jabir Mwadini, Katibu wa Rais, Mhandisi Peter Phillip Mwasalyanda Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Kuwe Bakari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Mhe. Angela Charles Kizigha, Mshauri wa Rais, Masuala ya Jamii




Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya Uapisho wa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira na Mahusiano) Mhe. Dkt. Evaline Wilbard Munisi, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 06 Mei, 2026


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali mara baada ya kumuapisha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira na Mahusiano) Mhe. Dkt. Evaline Wilbard Munisi, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 06 Mei, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi katika picha na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira na Mahusiano) Dkt. Evaline Wilbard Munisi, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma tarehe 06 Mei, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Ajira na Mahusiano) Dkt. Evaline Wilbard Munisi, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma tarehe 06 Mei, 2026.