Tume ya Taifa ya UNESCO yakutana na BAKITA, BAKIZA na TATAKI kujadili ushirikiano wa maendeleo ya Kiswahili

Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na viongozi na wataalamu kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), kwa lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano wa kitaasisi katika kukuza nafasi ya lugha ya Kiswahili katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Kikao hicho cha pamoja cha kiofisi kimewakutanisha wawakilishi wa taasisi hizo nne kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika masuala yanayohusu maendeleo ya Kiswahili, kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha juhudi za kitaifa na kutumia fursa zinazopatikana katika majukwaa ya kimataifa.


Katika mazingira ambayo lugha zina nafasi muhimu katika mawasiliano, utamaduni na ubadilishanaji wa maarifa, uratibu wa kitaifa ni nyenzo muhimu katika kuendeleza nafasi ya Kiswahili na kuongeza mwonekano wake katika majukwaa mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Kupitia kikao hicho, washiriki walikubaliana kuendelea kutumia mifumo na fursa zilizopo za kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza nafasi ya Kiswahili, sambamba na kuzingatia misingi rasmi ya usanifishaji na maendeleo ya lugha hiyo.

Ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya UNESCO, BAKITA, BAKIZA na TATAKI unaunganisha majukumu na utaalamu wa taasisi hizo katika masuala ya lugha, taaluma, utafiti na maendeleo ya Kiswahili. Ushirikiano huo ni muhimu katika kuweka msingi wa uratibu wa pamoja kuhusu fursa zinazoweza kuchangia kukuza lugha hiyo katika ngazi ya kimataifa.

Aidha, hatua hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa taasisi za kitaifa katika kuendeleza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, maarifa na utamaduni, huku ikiimarisha juhudi za kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kupata nafasi katika mazingira yanayozidi kuunganishwa kupitia mawasiliano ya kimataifa.

Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa katika kutekeleza majukumu yake yanayohusiana na maeneo ya UNESCO, ikiwemo mawasiliano na taarifa, kwa kuzingatia fursa za ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Tume ya Taifa ya UNESCO — Kuimarisha ushirikiano wa kitaifa kwa maendeleo ya lugha, maarifa na utamaduni.
Na Byera Deus, Biharamulo

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kuhakikisha mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Nyakanazi–Nyakafundikwa, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera, analipwa Sh milioni 600 ifikapo Desemba mwaka huu ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo unaotarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 42,000.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 2.9, ambao hadi sasa umefikia asilimia 78 ya utekelezaji.

Amesema kazi kubwa za ujenzi zimekamilika, huku shughuli zilizobaki zikihusisha kukamilisha vituo vya kuchotea maji ili kuwezesha wananchi kuanza kupata huduma hiyo ifikapo Desemba mwaka huu, endapo malipo kwa mkandarasi yatafanyika kwa wakati.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji inayoukabili mji wa Nyakanazi, ambao unaendelea kukua kwa kasi na kuwa na mahitaji makubwa ya huduma za kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa Nyakanazi ni eneo muhimu kiuchumi na kijiografia, likiwa lango la wageni wanaoingia na kutoka katika nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hivyo upatikanaji wa maji ya uhakika ni muhimu kwa wakazi na wageni wanaopita katika eneo hilo.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa malipo ya wakandarasi kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa, akilitaka RUWASA kuhakikisha wakandarasi wa ndani wanaotekeleza miradi hiyo hawakwami kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Biharamulo, Mhandisi Lucas Matina, amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji na miundombinu mingine ya mradi, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kukamilisha vituo vya kuchotea maji ili huduma iweze kutolewa kwa wananchi wa Nyakanazi na maeneo jirani.

Amesema licha ya mradi kufikia asilimia 78 ya utekelezaji, mkandarasi amelipwa Sh milioni 700 pekee kati ya gharama zote za mradi, huku akiwa anadai zaidi ya Sh bilioni 1.4, hali inayohitaji hatua za haraka ili kukamilisha kazi zilizobaki.

Naye Mkurugenzi wa Mipango wa RUWASA Makao Makuu, Mhandisi Enock Wagala, amesema wakala huo unafanyia kazi agizo la Naibu Waziri, huku Sh milioni 600 zikitarajiwa kulipwa ifikapo Desemba mwaka huu ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi.

Amesema RUWASA inatambua umuhimu wa mradi wa Nyakanazi–Nyakafundikwa katika kutatua changamoto ya maji safi na salama kwa maelfu ya wananchi, kutokana na ukuaji wa mji huo na ongezeko la mahitaji ya huduma za kijamii na kiuchumi.







Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa majengo mapya ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ya juu kupitia uwekezaji wa kimkakati unaolenga kupanua fursa za elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 425, sawa na takribani shilingi trilioni moja, katika kuimarisha elimu ya juu nchini kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), huku Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa kikinufaika na uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 30.

Amesema uwekezaji huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ongezeko la wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari linaendana na upatikanaji wa nafasi za elimu ya juu, akibainisha kuwa tangu mwaka wa fedha 2021/2022, Mkoa wa Iringa umepokea zaidi ya shilingi bilioni 175 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi hizo.

Katika kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa, Mheshimiwa Ndejembi ameuagiza uongozi wa Chuo hicho kusimamia kwa umakini, uwazi na uadilifu fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha ujenzi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora. Amesema Serikali haitavumilia matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma, kwani kila shilingi inayowekezwa katika elimu inapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, akizungumza wakati wa kumkaribisha Makamu wa Rais, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya uwekezaji mkubwa na wa kihistoria katika sekta ya elimu ya juu, akieleza kuwa kupitia Mradi wa HEET, jumla ya Taasisi 20 za elimu ya juu nchini zimenufaika na ujenzi wa maabara 309, hosteli 26, maktaba, kafeteria na ofisi 1,177, pamoja na ukarabati wa majengo 48, hatua inayofungua ukurasa mpya katika kuboresha mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji, tafiti na ubunifu nchini.

Profesa Mkenda amesema mafanikio hayo hayaishii katika ujenzi wa majengo pekee, bali yameambatana na upanuzi wa wigo wa elimu ya juu kwa kuanzishwa kwa kampasi mpya katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa ya Manyara, Kagera, Lindi, Njombe, Katavi, Kigoma, Mwanza, Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Tanga, Singida, Mara na Ruvuma pamoja na Zanzibar. Amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi, kupunguza changamoto ya umbali na gharama za masomo, pamoja na kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata elimu na ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa, amesema chuo hicho kimeendelea kupiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya elimu kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30.4, inayojumuisha majengo ya sayansi, maabara ya fizikia, midia anuwai na elimu maalumu, hosteli za wanafunzi pamoja na maktaba. Ameeleza kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2026, ujenzi wa majengo manne yanayofadhiliwa kupitia Mradi wa HEET ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.

Mkwawa ni miongoni mwa vyuo muhimu vinavyoandaa walimu wa sayansi na masomo mengine hapa nchini. Kuongezeka kwa mabweni, maabara na madarasa ya kisasa kutaongeza idadi ya wanafunzi wanaoweza kudahiliwa na kuimarisha mafunzo ya vitendo kwa walimu watakaofundisha vizazi vijavyo






















Na. Joseph Mahumi, Bangkok, Thailand

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na Tanzania, hususan katika ufadhili wa miradi ya kimkakati, maendeleo ya rasilimali watu, nishati na miundombinu ya usafirishaji, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.

Mhe. Balozi Omar aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nishati, akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia juhudi za kupanua upatikanaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati, sambamba na mpango wa Mission 300 unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika.

“Tanzania imenufaika na ufadhili wa IDA-20 wa karibu dola bilioni sita za Marekani, huku chini ya IDA-21 tukipangiwa dola bilioni 2.54 za Marekani na ahadi za ufadhili zinazozidi dola milioni 760, huku miradi mingine ikiendelea kuandaliwa kwa ajili ya utekelezaji” alisema Mhe. Balozi Omar

Akizungumzia ukubwa wa ushirikiano wa sasa kati ya Tanzania na Benki ya Dunia, Mhe. Balozi Omar amesema kuwa thamani ya miradi 33 inayotekelezwa kupitia ushirikiano huo imefikia zaidi ya dola bilioni 8.8 za Marekani, ambapo miradi 30 ni ya kitaifa na mitatu ni ya kikanda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na usafirishaji Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika eneo la usafirishaji, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika kuboresha Ushoroba wa Kati (Central Corridor), kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha bandari, reli na miundombinu mingine ya usafirishaji ili kurahisisha biashara na kuongeza fursa za uwekezaji.

“Serikali inalenga kuubadilisha Ushoroba wa Kati kutoka njia ya usafirishaji na kuufanya kuwa Ushoroba wa Maendeleo na Ustawi wa Kiuchumi (Economic Prosperity Corridor), kwa kutambua na kuendeleza fursa za uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu hiyo.” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa Tanzania inathamini mchango wa Dkt. Kibwe katika kufanikisha majukwaa muhimu ya kimataifa yaliyofanyika nchini, yakiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Human Capital Summit) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Julai 2023, pamoja na Mkutano wa Mapitio ya Katikati ya Kipindi cha Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa (IDA) uliofanyika Zanzibar mwezi Desemba 2024.

Ameeleza kuwa mikutano hiyo imeipa Tanzania fursa ya kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya maendeleo ya Afrika na kimataifa, hususan katika kuboresha rasilimali watu, ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kukabiliana na changamoto za maendeleo barani Afrika.

Mhe. Balozi Omar alieleza matumaini ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mkurugenzi mpya atakayechukua nafasi hiyo Bi. Lonkhululeko Magagula, atakayechukua nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, ameipongeza Tanzania kwa hatua zilizopigwa katika kuimarisha ushirikiano wake na Benki ya Dunia, akibainisha kuwa thamani ya miradi ya maendeleo kati ya pande hizo imeongezeka kutoka takribani dola bilioni nne alipokuwa akianza majukumu yake hadi kufikia kiwango cha sasa.

Alisema mafanikio hayo yanaonesha hatua kubwa iliyofikiwa katika kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akieleza kuwa akiwa Benki ya Dunia, anajivunia kushuhudia Tanzania ikifikia hadhi ya nchi yenye uchumi wa kipato cha kati.

Dkt. Kibwe alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kutumia fursa za uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya sekta ya madini, akieleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi 30 zinazozingatiwa katika mpango wa Benki ya Dunia unaolenga kuimarisha maendeleo ya sekta ya madini na rasilimali zake.

“Mpango huu unajumuisha maeneo muhimu matatu ambayo ni kuimarisha utawala na usimamizi wa sekta ya madini, kuendeleza miundombinu inayowezesha uchimbaji na usafirishaji wa madini, pamoja na kuongeza upatikanaji wa mitaji na uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Dkt. Kibwe.

Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano na washirika wake wa maendeleo ili kutumia fursa za ufadhili, uwekezaji na utaalamu katika kutekeleza miradi ya kimkakati na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, na maafisa wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto) akiwa katika picha na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, walipokutana na kufanya mazungumzo, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa tatu kushoto), Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (wa tatu kulia), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kulia), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe (wa pili kulia), Mkurugenzi Mbadala wa Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki ya Dunia, Bi. Lonkhululeko Magagula, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo yao, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, walipokutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, jijini Bangkok, nchini Thailand)



Na Mwandishi Wetu, Pwani

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Kimanzichana Kusini, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, na kuchangia Sh milioni tano kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Ujenzi wa ofisi hiyo unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh milioni 34 hadi kukamilika kwake, huku kazi za ujenzi zikiwa zimefikia hatua ya upigaji wa sakafu.

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake wilayani Mkuranga, leo Oktoba 18, 2026, Kihongosi ameipongeza CCM Kata ya Kimanzichana Kusini kwa juhudi za kujenga ofisi hiyo, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha shughuli za chama katika ngazi ya kata.

Aidha, amesema Wilaya ya Mkuranga imepiga hatua katika maendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma, akitaja mabadiliko ya makazi ya wananchi na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Mkuranga, ikiwemo huduma za umeme, maji na afya kupitia hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati.

“CCM itaendelea kuwa chama kinachoongoza kwa sababu ni chama kinachotekeleza ahadi zake. Kimeahidi kuleta maendeleo kwa wananchi na kimeendelea kuyatekeleza,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa maboresho katika sekta ya afya yamepunguza changamoto ambazo wananchi, hususan wanawake wajawazito, walikuwa wakikabiliana nazo walipokuwa wakitafuta huduma za kujifungua.













Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ndugu Ramadhan Ali Kimara, amesema amedhamiria kufunga kamera za CCTV katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato ili kudhibiti upotevu na kuongeza uwazi.

Akizungumza na wakusanya mapato tarehe 18 Oktoba 2026, Kimara amewasisitiza kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji, uadilifu na ufanisi. Amefafanua kuwa kamera hizo zitasaidia kuimarisha usimamizi wa mapato na kurahisisha kazi zao.

Aidha, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili, hususan upungufu wa vitendea kazi, huku akiwahimiza kushirikiana kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinaboresha huduma kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya Kibiti.




Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema zoezi la uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara limekamilika kwa mafanikio makubwa, ambapo imegunduliwa gesi asilia inayotarajiwa kuongeza kiasi cha nishati hiyo kutoka futi za ujazo trilioni 57.54 zilizopo sasa.

Amesema Serikali inatarajia kuzindua visima hivyo wiki ijayo katika Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara, ambapo pia itatangaza kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa kutokana na shughuli hizo za uchimbaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 18, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Mhe. Homera amesema visima hivyo, viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti, vimechimbwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na mwekezaji, kampuni ya M&P.

Amesema ugunduzi huo unazidi kuiwezesha Serikali kuwa na nishati ya gesi asilia kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.

Mhe. Homera ameongeza kuwa Serikali kupitia TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.

Ameeleza kuwa shughuli za uchukuaji wa data za mitetemo zinaendelea katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na zinatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku maandalizi ya uchorongaji wa kisima cha uzalishaji na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yakiendelea katika Kitalu cha Ntorya.

Kuhusu maendeleo ya Kitalu cha Ntorya, Mhe. Homera amesema ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka Ntorya hadi Madimba umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kuanza mapema mwaka 2027 na kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku.

Ameeleza kuwa TPDC inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi katika usambazaji wa gesi asilia majumbani na kwenye magari (CNG), ambapo hadi Septemba 2026, jumla ya vituo 22 vilikuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma.

Katika hatua nyingine, Homera amesema wiki ijayo Serikali inatarajia kusaini na kukabidhi leseni mpya za utafutaji mafuta na gesi asilia (PSA) kwa TPDC, hatua itakayoliwezesha shirika hilo kuendelea na shughuli za utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali hizo nchini ambapo Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi atakuwa mgeni rasmi.

Akizungumzia sekta ya umeme, Mhe. Homera amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka na kufikia Megawati 4,646 kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia, jua na nishati nyingine mbadala, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo huo hadi Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Amesema katika kuimarisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu, Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Kishapu II wenye uwezo wa Megawati 100 ukiendelea.

Aidha, miradi mingine yenye uwezo wa zaidi ya Megawati 600 ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi.

Kuhusu miundombinu ya usafirishaji umeme, Waziri huyo amesema Serikali imekamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma tangu Septemba 2026, ambao umeimarisha ubora na kiwango cha umeme kinachofika katika mikoa ya Magharibi na Kaskazini mwa nchi.

Ameongeza kuwa Mradi wa Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwa Novemba 2026 na kuunganisha Mkoa wa Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza, huku Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga ukitarajiwa kuwashwa Februari 2027 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na maeneo ya viwanda ya Mkuranga.

Aidha, amesema utekelezaji wa Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa na kuondoa changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.






MBIO za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimezindua rasmi msimu wake wa 25 (Silver Jubilee) katika hafla iliyojaa hamasa kubwa iliyofanyika katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, ikiweka msingi wa wikendi ya kihistoria ya mbio mjini Moshi mnamo Februari7, 2027.

​Akizungumza KAtika hafla hiyo, Waziri Mkuu mstaafu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, alipongeza mbio hizo kwa kufikia hatua hiyo kubwa ya robo karne ya ubora na mchango wake mkubwa katika kuhamasisha utamaduni wa michezo na utalii wa michezo.

​"Kufikisha miaka 25 ni mafanikio ya kipekee yanayoonyesha udhibiti, maono, na ushirikiano bora na Serikali ya Tanzania," alisema Mhe. Majaliwa.

​Alibainisha kuwa Kilimanjaro Marathon mara zote imekuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya wanasayansi na wanariadha wa ndani.

​Pia alizipa changamoto mbio nyingine nchini kote kuiga mfano huu wa kipekee, kwani lengo linapaswa kuwa kukuza mabingwa wengi zaidi wa Kitanzania katika miaka 25 ijayo.

​Mhe. Majaliwa alisisitiza kuwa mbio hizi zina faida kubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania huku akiongeza kuwa ndio tukio kuu la michezo la kimataifa nchini Tanzania.

"Inapokusanya zaidi ya washiriki 13,200 na idadi sawa ya watazamaji kutoka zaidi ya nchi 60, mbio hizi zinakuwa chachu kubwa kwa sekta ya ukarimu, usafirishaji, na biashara ndogondogo mjini Moshi na maeneo ya jirani," alisema.

​Aliwahimiza washiriki na wageni watakaohudhuria msimu huu wa miaka 25 kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vikuu vya utalii vya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro na Zanzibar.

​Mhe. Majaliwa pia alitoa shukrani za dhati kwa wadhamini wote: mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager (Mbio za Km 42), YAS (Mbio za Nusu Marathon Km 21), na CRDB Bank (Mbio za kujifurahisha za Km 5); wadhamini rasmi wasaidizi: Coral Paints, Kilimanjaro Natural Mineral Water, na TPC Sugar; washirika rasmi GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement, ALAF Limited, Salinero Hotel - Kilimanjaro, na Harleys Deep Heat and Deep Freeze; pamoja na wasambazaji rasmi Kibo Palace Hotel Arusha na Keys Hotel Moshi.

​Mwakilishi wa Kilimanjaro Premium Lager) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania, Bi. Khensani Mkhombo, alieleza kujivunia kwa kampuni hiyo kushirikiana na mbio hizo kwa miaka 25—moja ya udhamini mrefu na wenye mafanikio makubwa zaidi wa michezo wa makampuni nchini Tanzania.

​"Kwa miaka 25 ya ajabu, Kilimanjaro Premium Lager imesimama bega kwa bega na tukio hili la kiwango cha kimataifa kusherehekea utamaduni wa Kitanzania, michezo, na roho ya jamii iliyo hai," alisema.

"Ili kusherehekea hatua hii ya robo karne, wanariadha na wageni watarajie wikendi isiyosahaulika iliyojaa matukio ya kusisimua, huduma za ukarimu, na sherehe mjini Moshi.

Tunawasihi washiriki kujisajili mapema kupitia www.kilimanjaromarathon.com au Mixx BY YAS pindi lango la usajili litakapofunguliwa, kwani nafasi za ushiriki ni chache."

​Mwakilishi wa Kampuni ya YAS, Woinde Shisael, alithibitisha tena azma ya YAS ya kuendelea kuwezesha mbio hizo na kuwasihi watu wengi zaidi kujiunga na mbio za mwaka huu.

​"Kwa miaka 25, Kilimanjaro Marathon imeunganisha wanariadha, familia, jamii, na dunia kupitia Tanzania. Kama Mdhamini Rasmi wa Nusu Marathon, tunajivunia kuwezesha viunganishi hivi kupitia Mtandao wetu wa 4G na 5G Ya Viwango, tukisaidia watu wengi zaidi kushiriki katika uzoefu huu wa kipekee huku tukisaidia jamii zenye afya bora, kuwezesha vijana, na kuhamasisha nia inayoisukuma Tanzania mbele.

"Tunawaalika washiriki wote kutoka nnadi na nje ya mipaka ya Tanzania kujiunga nasi mjini Moshi kwa sherehe za kihistoria za miaka 25."

​Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa CRDB Bank, Bw. Muhumuliza Buberwa, alisema CRDB Bank inajivunia kuendeleza ushirikiano wake na tukio hili kama mdhamini rasmi wa Mbio za kujifurahisha za Km 5 (Fun Run).

“Mbio za Km 5 zinahusisha watu mbalimbali – familia, vijana, na wakimbiaji wa mara ya kwanza – kuwa sehemu ya hadithi hii ya kipekee ya Kitanzania.

" Tunawapongeza Kilimanjaro Premium Lager na washirika wote kwa hatua hii kubwa.”

​Waandaaji, Kilimanjaro Marathon Company Limited, wamethibitisha kuwa usajili katika kategoria zote za mbio utafuata mfumo wa atayeanza kufika ndiye atakayehudumiwa kwanza (first-come, first-served).

​Mara tu idadi inayotakiwa itakapofikiwa, usajili utafungwa mara moja.

Wanariadha wanahimizwa kujisajili mapema ili kujihakikishia nafasi na kuepuka kutoridhika.

​Mbio za 25 za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon, zikiwa na kaulimbiu ya “Mbio ya Watu”, zitafanyika Jumapili, 7 Februari 2027, zikianzia katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

​Tukio hili limeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited, huku usafiri wa wageni wa kimataifa na masoko ya kimataifa yakiendelea kuratibiwa na Wild Frontiers Events.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kiwanda cha Geofields kilichonzishwa na wazawa kwa ajili ya huduma migodini ya Wire Mesh.
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Geofields Tanzania Limited, Denis Dillip akitoa maelezo kuhusiana kiwanda hicho kinachomilikiwa na watanzania kwa asilimia 100 kuwa sera za nchi zimewezesha wazawa kuwa sehemu ya kutoa huduma katika sekta ya madini.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akizungumza kuhusiana na umhimu wa kiwanda Geofields katika kunufaika na ajira kwa kwa watanzania wakiwemo wananchi wa Bagamoyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Masoko was Chama cha Watoa Huduma Migodini (TAMISA) Dkt Sebastian Ndege akitoa maelezo kuhusiana matokeo ya wazawa kuanzisha kiwanda cha kutoa huduma migodini.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza katika uzinduzi wa Kiwanda cha Geofields kilichonzishwa na wazawa kwa ajili ya huduma migodini ya Wire Mesh.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TAMISA Japhet Mussa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa ya watanzania kuwa na nguvu ya kutoa huduma migodini.

*Geofields yazindua kiwanda cha Wire Mesh mgodini

Na Mwandishi Wetu Pwani
WAZIRI wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amefungua rasmi kiwanda cha Geofields Tanzania Limited cha kuzalisha bidhaa za Wire Mesh zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini, kilichopo Kerege, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, chenye uwezo wa kuzalisha vipande zaidi ya 100,000 kwa mwaka.

Uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanyika Oktoba 17, 2026, unaashiria hatua muhimu katika kukuza uzalishaji wa ndani wa vifaa vinavyotumika migodini, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Kiwanda hicho kinaendeshwa na Geofields Tanzania Limited kupitia kitengo chake cha Geofields Underground Support (GUS), kinachojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji chini ya ardhi migodini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Geofields Tanzania Limited, Denis Dillip, amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kukidhi mahitaji ya migodi nchini, huku kampuni ikiendelea kuweka mikakati ya kupanua uzalishaji na kuongeza ushindani katika masoko ya Afrika Mashariki na kimataifa.

Dillip amesema kampuni hiyo tayari imefungua tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hatua inayolenga kupanua wigo wa biashara na kuongeza nafasi ya kampuni katika soko la kikanda.

Ameeleza kuwa kampuni imewekeza katika teknolojia na utaalamu ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya kimataifana na hasa katika kulinda usalama na maisha ya wafanyakazi chini ya migodi. Aidha, amesema uwepo wa wataalamu wenye mafunzo kutoka Australia na China unalenga kuimarisha ujuzi, teknolojia na uwezo wa juu wa uzalishaji wa kampuni.

Aidha, Dillip ameishukuru Serikali, hususani Wizara na Tume ya Madini kwa kuweka sera nzuri za maudhui ya ndani (Local Content), akieleza kuwa sera hizo zimekuwa chachu ya uwekezaji na kuimarisha ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Amesema hatua hiyo muhimu pia imechangiwa na ushirikiano kati ya Geofields Tanzania Limited na kampuni yake mbia ya African Underground Mining Services (AUMS), pamoja na washirika wake wa Australia, kampuni za Perenti na Barminco. Aidha, ameishukuru Geita Gold Mine (GGM) kuwa miongoni mwa wadau wakubwa watumiaji wa bidhaa zetu na kushirikiana nasi kuhakisha kuwa tunafikia dhumuni la serikali la sera ya maudhui ya ndani na ushirikiswaji wa watanzania katika shughuli za migodi.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo una mchango muhimu katika kuendeleza uzalishaji wa ndani, kuhamisha teknolojia na utaalamu, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani unazingatia viwango vya kimataifa.

Katika suala la ajira, Geofields Tanzania Limited ina jumla ya wafanyakazi 105 ina mpango wa kuongeza nafasi zaidi za ajira kwa Watanzania kadri shughuli za uzalishaji zitakavyoendelea kupanuka. Hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya viwanda, kukuza ujuzi wa kitaalamu na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia fursa zinazotokana na uwekezaji huo.

Akizindua kiwanda hicho, Waziri wa Madini Mh, Mavunde amepongeza uwekezaji huo na kueleza dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na utengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji madini barani Afrika.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani ili kuongeza uwezo wa kampuni za Kitanzania kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya migodi nchini na katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na maelekezo yaliyochangia kuimarisha sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Pia, Waziri Mavunde amewahimiza Watanzania kuunganisha mitaji na nguvu za kibiashara ili kutumia fursa zinazopatikana katika mnyororo wa manunuzi wa sekta ya madini. Amebainisha kuwa takribani shilingi trilioni 5.1 zinahusishwa na mnyororo huo, huku sehemu kubwa ya shughuli hizo ikitajwa kujikita katika kampuni zisizozidi sita.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanislaus Nyongo, amesema mkoa huo una viwanda vikubwa na vidogo 1,768, akieleza kuwa uwekezaji wa Geofields unaongeza mchango wa mkoa katika kukuza sekta ya viwanda nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesisitiza umuhimu wa kampuni hiyo kutoa kipaumbele kwa wakazi wa Kerege katika fursa za ajira zitakazotokana na uwekezaji huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janeth Reuben Lekashingo, amesema mafanikio ya sekta ya madini yanapaswa kupimwa pia kwa ukuaji wa kampuni za Kitanzania, ajira zinazozalishwa, viwanda vinavyoanzishwa, uhamishaji wa teknolojia na ongezeko la uzalishaji wa ndani.

Top News