HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI, SHINYANGA, MEI MOSI, 2006
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi na Ujenzi (TAMICO) na Mratibu wa Sherehe za Mei Mosi Mwaka huu;
Mheshimiwa Fredy Masasi;
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Nchini,
Mheshimiwa Nestory Ngulla;
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana,
Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe;
Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mheshimiwa Asha Abdallah Juma;
Waheshimiwa Mawaziri;
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa;
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga;
Waheshimiwa Wabunge;
Waheshimiwa Mabalozi;
Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO)
Mheshimiwa Ali Ibrahim;
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri (ATE)
Mheshimiwa Dr. Aggrey Mlimuka;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi Wenzangu;
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Wananchi na
Ndugu Wafanyakazi;
Naomba nianze na shukrani. Kwanza, tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana leo katika sherehe za mwaka huu za siku ya Wafanyakazi Duniani zinazofanyika hapa Shinyanga. Tumshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kutujalia uwezo, nguvu na maarifa na hivyo kutuwezesha kufanya kazi ya kuendeleza maisha yetu binafsi na kuijenga nchi yetu kwa ufanisi na mafanikio.
Pili, nawashukuru viongozi wa Vyama Huru vya Wafanyakazi kwa kunipa heshima hii ya kipekee ya kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika siku ya leo. Nimefurahi na kufarijika sana kwa kupewa fursa ya kujumuika nanyi wafanyakazi wenzangu katika kusherehekea sikukuu hii muhimu ya wafanyakazi duniani.
Ndugu Wafanyakazi;
Naipongeza Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe kwa kazi nzuri ya kuratibu mahusiano kati ya Serikali, Wafanyakazi na Waajiri kupitia vyama vyao. Nampongeza pia Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Asha Abdallah Juma, kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha sherehe hizi.
Aidha, naupongeza Mkoa wa Shinyanga na wakazi wake wote, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Brigedia Jenerali, Dr. Johanness Balele, kwa mapokezi mazuri, maandalizi mazuri na maonyesho ya kufana ya sherehe hizi.
Ndugu Wananchi na Ndugu Wafanyakazi;
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya wageni wenzangu, napenda kuitumia nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Shinyanga kwa mapokezi makubwa na mazuri yaliyojaa upendo tele.
Jambo hilo limenipa faraja kubwa sana. Nilipokuja hapa wakati wa kampeni mlikuwa wengi sana lakini leo mmetia fora. Hongereni sana.
Ndugu Wananchi;
Tumejumuika hapa kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi ambayo inaadhimishwa duniani kote siku ya leo. Hivyo basi hotuba yangu inatakiwa ihusu maadhimisho haya. Lakini kwsa sababu maalum nimeongeza mambo mawili. Kwanza, kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi na kunipa heshima ya kuongoza Taifa letu. Ni mara yangu ya kwanza kufika hapa tangu uchaguzi mkuu kumalizika Desemba 14, 2005. Pili, nimeonelea nitumie fursa hii kuijumuisha maneno ya hotuba yangu ya mwisho wa mwezi Aprili katika hotuba yangu ya leo. Kama mnavyojua, nilistahili kufanya hivyo jana lakini niliamua nifanye leo pamoja na kuzungumzia masuala ya Mei Mosi.
Shukrani kwa Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga
Ndugu Wananchi;
Napenda sasa kutumia nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa mkoa huu wa Shinyanga kwa heshima kubwa mliyonipa ya kunichagua kuiongoza nchi yetu. Nawashukuru pia kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi na hivyo kukiwezesha kuendelea kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ndugu Wananchi;
Wakati wa kampeni za uchaguzi niliwaomba mchague kwa mithili ya mafiga matatu. Mlifanya hivyo kasoro katika jimbo moja tu la Bariadi Mashariki ambapo mtani wangu na mtani wa CCM, Mheshimiwa John Cheyo alichaguliwa kuwa Mbunge. Naambiwa pia kuwa kati ya Kata 166 Mkoani tumeshindwa Kata 26. Nimefurahishwa sana na ushindi huu mnono. Ahsanteni sana.
Ndugu Wananchi;
Mmeonyesha imani kubwa sana kwangu na kwa chama changu cha CCM. Watu husema: “Imani huzaa imani”na “mcheza kwao hutuzwa”. Napenda niwahakikishie kuwa nami pia nitawalipa kwa imani. Nitajitahidi kwa uwezo wangu wote alionijalia Mwenyezi Mungu na kwa kutumia mamlaka mliyonipa kutimiza ahadi zangu kwenu. Natambua vyema methali ya Kiswahili isemayo: “Ahadi ni deni”. Hivyo nami ninalo deni kwenu na kwa wananchi wa Tanzania ambalo ninao wajibu wa kulilipa.
Ndugu Wananchi;
Kazi ya kutekeleza ahadi za CCM zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi na zile zangu nilizozitoa hapa na kwingineko nchini tumeshaianza. Mawaziri wote na wizara zote wamekamilisha mipango ya utekelezaji wa Ilani kuhusu sekta zao wanazoziongoza. Bajeti ijayo utekelezaji unaanza. Tutafanya hivyo kwa bajeti zote tano za kipindi cha uongozi wangu na wa Chama chetu.
Ndugu Wananchi;
Nilipokuja mkoani hapa mwaka jana wakati wa kampeni niliwaahidi kuwa mkinichagua mimi na Chama Cha Mapinduzi pamoja na mambo mengine tutatekeleza mambo yafuatayo:
1. Kujenga daraja la mto Simiwi;
2. Kukamilisha ujenzi wa barabara za Shinyanga - Mwanza, Shinyanga – Nzega, na Tinde – Isaka, kwa kiwango cha lami;
3. Kutengeneza barabara za Shinyanga – Maswa – Meatu hadi Bariadi; na
4. Kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mkoa huu.
Ahadi hizo ninazikumbuka na kama nilivyosema mchakato wa kuzitekeleza tunaendelea nao.
Ndugu Wananchi;
Pale tutakapokwama tutafahamishana ili kila mmoja wetu ajue sababu za kukwama. Napenda kutumia nafasi hii pia kuwakumbusha viongozi wenzangu wa kuchaguliwa yaani, Wabunge na Madiwani, nao pia wasisahau ahadi walizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi. Nawaomba wazifikishe kwa Halmashauri zao ili zijumuishwe katika mipango ya wilaya. Zile ambazo zimewazidi kimo Wabunge watuletee taifani ili na sisi tuone namna ya kusaidia. Tafadhalini wananchi wapendwa, wakumbusheni Wabunge wenu na Madiwani wenu kama wamesahau ili waziainishe ahadi hizo kwenye mipango ya Halmashauri zenu ili zipate kutekelezwa mapema.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza na wafanyakazi nchini, naomba niwashukuru kwa kunichagua. Nina hakika wengi wenu mlinipigia kura, tena kura nyingi tu. Ushindi mnono nilioupata ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kura zenu. Nawashukuruni sana kwa imani kubwa mliyoionesha kwangu. Nawaahidi kuwa nitajitahidi kuwatumikia kwa kadri ya uwezo wangu wote. Naomba mzidi kuniunga mkono, kuniombea dua kwa Mwenyezi Mungu na sote tufanye kazi kwa juhudi na maarifa ili shabaha yetu ya kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania itimie.
MASUALA YA KITAIFA
Hali ya Chakula Nchini
Ndugu Wananchi;
Naomba nitumie nafasi hii kuwapeni pole sana wananchi wa Shinyanga kwa tatizo la upungufu mkubwa wa chakula lililoukumba mkoa wenu msimu huu. Mkoa huu ni moja ya mikoa michache hapa nchini iliyoathirika sana na uhaba wa chakulauliosababishwa na hali ya ukame. Serikali, kwa kutambua uzito wa tatizo lenu ilichukua hatua zote muhimu kuhakikisha kuwa mnapatiwa chakula cha msaada mapema. Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Lowassa alikuja hapa Mkoani Shinyanga kujionea wenyewe ukubwa wa tatizo na kuona jinsi zoezi la usambazaji wa chakula cha njaa kwa waathirika lilivyokuwa linaendelea. Natambua kuwa bado hamjavuna na hivyo wengi wenu bado mnahitaji msaada mpaka mavuno. Tutaendelea kufanya hivyo mpaka tuvuke salama.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na kwamba hali ya chakula nchini bado siyo ya kuridhisha sana, kwa ujumla kuna matumaini ya hali hiyo kuimarika zaidi katika msimu huu. Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo yote nchini zinatupa matumaini hayo. Nimeona jitihada zenu katika kilimo. Nawaomba tushikilie msimamo wetu huo huo wa kutunza mashamba yetu ili mavuno yawe mzuri. Tukifanya hivyo tutakuwa tumemfurahisha Mwenyezi Mungu ambaye tumemuomba sana atujalie mvua na kutuitikia. Wito huo huo nautoa kwa Watanzania wote kwani karibu nchi nzima mvua za masika zilizoanza mwezi Machi zimekuwa nzuri. Tuzitumie vyema mashambani mwetu.
Ndugu Wananchi;
Juhudi zetu za kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa, ilikuwa ni shughuli pevu. Ilikuwa ni kazi nzito na yenye gharama kubwa. Tathmini ya mwisho iliyofanywa Februari, 2006 ilionyesha kuwa zaidi ya watu 3,776,000 walikuwa wanahitaji msaada wa chakula. Mpaka sasa Serikali imeshasambaza zaidi ya tani 57,000 za mahindi zilizowapunguzia ukali wa tatizo ndugu zetu hao. Kati ya chakula hicho, tani 14,955 zimetolewa bure kwa watu ambao hawana uwezo wa kununua chakula hata kwa bei nafuu ya shilingi 50 kwa kilo. Hivi karibuni Serikali iliagiza kutoka nje tani 42,000 za mahindi. Mahindi hayo yameanza kuwasili na tayari yameanza kusambazwa kwenye mikoa yenye upungufu wa chakula.
Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru viongozi na Watendaji wote wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri waliyoifanya kunusuru maisha ya Watanzania wenzetu katika baa hili. Pongezi maalum kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Lowassa kwa uogozi wake mahiri wakati wote wa tatizo hili mpaka sasa.
Ndugu Wananchi;
Katika kipindi hiki pia, wafanyabiashara wameingiza nchini jumla ya tani 147,379 za mahindi. Aidha, wameingiza tani 96,960 za ngano na tani 37,000 za mchele kuchangia juhudi za Serikali. Nao pia nawashukuru kwa juhudi zao hizo ambazo zimepunguza makali ya tatizo hilo nchini na hasa mijini.
Napenda pia kuitumia fursa hii kutoa shukrani maalum kwa wahisani wa ndani na wa nje waliochangia kuongezea nguvu za Serikali kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula nchini. Nawashukuru sana kwa moyo wao wa huruma na upendo. Wahisani wa ndani walichangia jumla ya shilingi 5,802,526,070/=. Kati ya hizo, fedha taslimu ni shilingi 4,480,136,070/= na shilingi 1,332,390,000/= ni thamani ya vyakula na vitu vingine vilivyotolewa Wahisani wa nje nao tayari wametoa jumla ya shilingi 10,039,538,810/=. Kati ya fedha hizo, shilingi 2,926,650,000/= zimekabidhiwa kwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa ajili ya kununulia madawa ya kuulia wadudu na mbegu. Kiasi kilichosalia cha shilingi 7,112,888,810/= kimekabidhiwa kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya kununulia na kusambaza chakula cha njaa nchini.
Wiki hii, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) litaanza zoezi la kusambaza tani 5,400 za mahindi kwa watu wasio na uwezo wa kununua chakula kwa shilingi 50/= kwa kilo kwenye wilaya chache zilizoathirika zaidi na uhaba wa chakula. Napenda kusisitiza kuwa chakula kinachoendelea kutolewa bure ni kwa wale tu wananchi walioathirika sana na ambao hawajaanza kuvuna chakula chao wenyewe hadi sasa.
Ndugu Wananchi;
Sina budi kutoa pongezi na shukrani maalum kwa kitendo cha aina yake kulichofanywa na wananchi wenzetu cha kuchangia kiasi kikubwa cha fedha na chakula kusaidia wananchi wenzao wenye shida. Ni mara ya kwanza jambo hili kufanyika na imeleta sura mpya ya uwajibikaji na moyo wa kujali wa Watanzania wazalendo. Nawashukuru kwa moyo wao wa huruma na wametuwekea heshima mbele ya mataifa na wananchi. Wahenga wamesema “Kutoa ni moyo na wala si utajiri”. Nawaomba waendelee na moyo wao huo ambao ni wa kuigwa na kila mtu mwenye mapenzi na nchi yetu.
Upatikanaji wa Umeme
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Tatizo lingine kubwa ambalo limekuwa linalikabili taifa letu katika miezi ya hivi karibuni ni upungufu wa umeme uliopelekea tuwe na mgao wa umeme nchi nzima. Kama nilivyowafahamisha mara kadhaa, Serikali imeendelea na jitihada zake za kushughulikia tatizo hili. Leo hii nafurahi kusema kwamba hali imekuwa nafuu kiasi kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Uzalishaji umeme umeongezeka kutoka megawati 265.5 zilizokuwa zinazalishwa mwishoni kwa mwezi Machi mwaka huu hadi kufikia megawati 546 mwishoni mwa mwezi uliopita. Ongezeko hili ambalo limesaidia kupunguza makali ya mgao wa umeme limetokana hasa na kuongezeka kwa maji kwenye mabwawa ya Kihansi na Kidatu. Lakini, hali ya Bwawa la Mtera bado ni mbaya sana. Mpaka sasa maji yameongezeka kwa karibu mita mbili tu na kufikia mita 688.95 mpaka majuzi. Bado kina cha maji ni pungufu kwa mita 9. Hakuna matumaini ya kujaza kiasi hicho katika msimu huu wa mvua ambao sasa unaelekea ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Hali hiyo mbaya ya maji katika Bwawa la Mtera inaashiria kuwa tatizo la upatikanaji wa umeme nchini litaendelea kuwepo. Kwa sababu hiyo basi, tegemeo letu kubwa katika muda mfupi ujao bado liko katika kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Vilevile, lipo katika ununuzi na upatikanaji wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi. Bahati nzuri mchakato wa kupata mitambo hiyo upo katika hatua nzuri za kiutekelezaji. Ni matarajio yangu kuwa kama mambo yakienda kama ilivyopangwa katika kipindi cha miezi michache ijayo hali itarejea na kuwa ya kawaida. Mipango yetu ya muda wa kati na muda mrefu ya kukabiliana na tatizo la umeme nayo inaendelea vizuri.
Ongezeko la Bei ya Mafuta
Ndugu Wananchi;
Ongezeko la mara kwa mara la bei ya mafuta limeendelea kuwa tatizo kwa uchumi wa nchi yetu. Upande mmoja ongezeko hilo linaongeza mzigo katika matumizi ya akiba yetu ya fedha za kigeni katika uagizaji. Upande mwingine, linaathiri utulivu wa bei za bidhaa na huduma nchini. Hatuna matumaini ya kushuka kwa bei za mafuta ila muelekeo wake ni kupanda zaidi. Naomba nirudie wito wangu wa kuwaomba wananchi wenzangu kuwa waangalifu na wabanifu katika matumizi ya mafuta.
Tatizo la Uhalifu
Ndugu Wafanyakazi;
Katika hotuba yangu pale Dodoma, nilielezea jitihada tunazoendelea nazo kukabiliana na tatizo la uhalifu nchini. Juhudi hizo zinaendelea na ushirikiano wa karibu wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeongeza uwezo wa kudhibiti uhalifu. Hata hivyo ujambazi bado upo na uovu wao na ukatili wao unaendelea kusikika hapa na pale kama ilivyotokea hapa majuzi. Napenda kurudia tena kuwahakikishia kuwa hatutalegeza uzi mpaka ushindi upatikane. Inshallah tutashinda tu kwa sababu tunasimamia haki na wao wanasimamia uovu. Hivi karibuni nimeagiza pia kuwa katika mapambano dhidi ya uhalifu, tatizo la biashara ya madawa ya kulevya nalo walishughulikie kwa ari, nguvu na kasi ile ile.
Nawaomba wananchi wote tuendelee kushirikiana kwa karibu na Jeshi letu la Polisi na vyombo vingine vya usalama katika mapambano haya. Ushirikiano wenu mpaka sasa umewezesha mafanikio ya kutia moyo yaliyopatikana. Tuendeleze ushirikiano huo kwa manufaa yetu sote.
Rasilimali ya madini
Ndugu Wananchi;
Nimeona pia Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yetu utajiri mkubwa wa madini. Tunayo madini ya kila aina yakiwemo dhahabu, almasi, madini ya vito na kadhalika. Sekta ya Madini ni moja ya sekta muhimu katika kuharakisha kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi na wananchi wake. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imefanya kazi nzuri na kubwa ya kushawishi watu na makampuni makubwa kuja kuwekeza hapa nchini.
Matokeo ya jitihada zote hizi siyo tu kwamba makampuni makubwa ya uchimbaji madini kutoka nje yameweza kuja kuwekeza hapa nchini, bali pia mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa taifa letu umeongezeka. Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kwamba mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 45 mwaka 1995 hadi kufikia dola milioni 693 mwaka 2004. Aidha, takwimu za awali zinaonyesha kwamba mauzo ya madini nje kwa mwaka 2005 yanatarajia kufikia dola za Marekani milioni 800 kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia.
Vile vile mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.4 mwaka 1995 hadi asilimia 3.2 mwaka 2004. Pia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kutoka sekta ya madini umeongezeka kutoka shilingi 454 milioni mwaka 1995/6 hadi kufikia shilingi 23,810 milioni mwaka 2004/5.
Tunayashukuru makampuni makubwa ya nje yaliyokubali kuja kuwekeza kwenye sekta ya madini hapa nchini ambayo yameiwezesha Tanzania kuwa nchi ya tatu barani Afrika baada ya Afrika ya Kusini na Ghana katika uzalishaji madini aina ya dhahabu. Tunayashukuru kwa kutuletea mitaji na teknolojia ya kisasa ambayo imetuwezesha kuchimba madini ambayo huko nyuma tulishindwa kuyachimba kutokana na uwezo wetu mdogo kwenye maeneo hayo. Tunayashukuru pia kwa kutoa ajira kwa wananchi wetu. Nimeelezwa kuwa idadi ya Watanzania wanaofanya kazi moja kwa moja kwenye migodi mikubwa hapa nchini sasa inafikia watu 8,300 na idadi hii inaendelea kuongezeka kila mgodi mpya unapoanzishwa.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuyahakikishia makampuni hayo na wawekezaji wengine kuwa, Serikali inathamini sana mchango wao katika kuinua uchumi wa nchi yetu na tutaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye sekta ya madini na nyinginezo. Ni matumaini yangu kuwa ushirikiano uliopo hivi sasa kati ya makampuni hayo, wenyeji waishio maeneo jirani na migodi, na Serikali kwa ujumla utaendelea na kuimarika zaidi. Aidha, tunakaribisha watu na makampuni mengi zaidi kuja kuwekeza nchini mwetu kwani bado tuna raslimali kubwa ya madini ardhini ambayo haijachimbwa.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa, bado Taifa halijanufaika vya kutosha na raslimali hiyo hasa kwa upande wa kodi ya mapato na mambo mengineyo. Sheria ya Madini na mikataba tuliyowekeana imekuwa na upungufu wa hapa na pale. Nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini, ikishirikiana na Wizara ya Sheria na Katiba, Wizara ya Uchumi, Mipango na Uwezeshaji na Wizara ya Fedha na Mashirika husika yaiangalie upya sheria hiyo na mikataba ili tufanye marekebisho stahiki.
Lengo langu ni kutaka sisi wenye raslimali nao tufaidike. Kwa jinsi ilivyo sasa inaelekea yule mwenye fedha, mitaji na teknolojia ndiye anayenufaika zaidi kuliko sisi wenye raslimali tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Hii si sawa. Si jambo jema upande mmoja tu ndio unaofaidi. Si haki. Tunataka haki itendeke.
Maslahi ya watumishi wa Umma
Ndugu Wafanyakazi;
Hii ni Mei Mosi yangu ya kwanza tangu mnipe heshima ya kuongoza nchi yetu. Hivyo, napenda nitambue na kuwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kulijenga Taifa hili changa. Nawapongezeni kwa dhati kwa jinsi mnavyoshirikiana na Serikali na waajiri wenu katika kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali nchini. Nyinyi ni wadau na wahimili muhimu wa uchumi wa Tanzania. Ahsanteni sana kwa mchango wenu adhimu na nawaombeni mzidishe juhudi na kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kupunguza umaskini unaolikabili Taifa letu. Ninyi kama Wafanyakazi, ndiyo kichocheo na kiungo muhimu katika ujenzi wa nchi yetu.
Ndugu Wafanyakazi;
Naelewa mazingira magumu yanayowakabili katika utendaji wa kazi zenu. Nayatambua matatizo yanayohusiana na uduni wa maslahi yenu, uhaba wa nyezo za kazi na vikwazo mbalimbali vya uwajibikaji. Nafahamu jinsi matatizo hayo yasivyojenga motisha na kupunguza tija ya mfanyakazi. Nilipoongea na Uongozi wa TUCTA walinieleza kwa kina faraja zenu na karaha zenu.
Ndugu Wafanyakazi;
Pamoja na upya wangu katika nafasi hii, naelewa jinsi gani Serikali imekuwa ikishughulikia matatizo na kero za Wafanyakazi. Naelewa kwa kiasi gani imefanikiwa au kutofanikiwa kuboresha mazingira ya kazi, kukuza motisha na kuongeza tija ya uzalishaji mali nchini. Nawapongezeni pia wafanyakazi kwa kutambua kuwa Serikali imekuwa inajitahidi kuyashughulikia matatizo ya wafanyakazi wa umma na wengineo kwa kiasi cha uwezo wa mapato yake na uwezo wa uchumi wa Taifa letu.
Napenda kuwaahidi kuwa nitafanya kila niwezalo kuendeleza juhudi hizi ili wafanyakazi waishi maisha bora zaidi.
Uboreshaji mishahara
Ndugu Wafanyakazi;
Katika risala yenu mmelieleza kwa uzito na kina tatizo la msingi la udogo wa mishahara ya wafanyakazi nchini. Ni kweli, mishahara ya wafanyakazi kwa ujumla ni midogo na haikidhi mahitaji yao ya maisha. Mimi na wenzangu Serikalini tunaelewa vyema athari za mshahara usiokidhi mahitaji kwa mfanyakazi na kwa kazi aifanyayo. Lengo la Serikali ni kukabiliana vilivyo na tatizo hilo kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Nia ya Serikali ni kufanya hivyo ili wafanyakazi waweze kuishi maisha ya heshima.
Ndugu Wafanyakazi;
Kwa ajili hiyo tumeamua kuanza mchakato utakaotuelekeza katika kumlipa mfanyakazi mshahara ambao utamfanya aishi maisha ya heshima. Swali kubwa hapa ni namna ya kufikia ulipaji wa mshahara huo. Kuna masuala mengi ambayo hayana budi kuangaliwa na kuzingatiwa kwa pamoja ili kuiwezesha Serikali kufikia uwezo wa kumlipa mfanyakazi mshahara wa kiwango hicho cha kukidhi mahitaji yake ya kila siku. Katika kutekeleza hili, Serikali imekusudia kufanya mambo yafuatayo:-
Moja: Kuunda Tume ya Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma ambayo itashughulikia uchambuzi wa suala zima la mishahara na maslahi ya wafanyakazi na kupendekeza hatua za kuchukua.Tume hii nitaitangaza wiki ijayo na itafanya kazi katika muda usiozidi miezi sita. Mara baada ya kumaliza kazi yake, mapendekezo ya Tume hiyo yatashughulikiwa mapema iwezekanavyo na uamuzi juu ya hatua za kuchukua utafanywa kwa umakini unaostahili.
Pili: Hata hivyo, wakati tume hiyo ikifanya kazi zake Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuboresha mishahara ya kada mbalimbali za wafanyakazi katika mwaka wa fedha wa 2006/07.
Tatu: Serikali itahakikisha kuwa Mabaraza ya Kisekta ya mishahara ya Kima cha Chini cha mishahara yanaendelea kuundwa. Kwa ajili hiyo naiagiza Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kuongeza kasi ya uundwaji wa mabaraza hayo. Kasi ya sasa hairidhishi.
Suala la ajira:
Ndugu Wafanyakazi;
Tunatambua kuwepo tatizo kubwa la ajira nchini. Kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ni moja ya agenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne. Mikakati inakamilishwa na muda si mrefu Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana italifahamisha Taifa. Dhamira ya Serikali ni kuongeza ajira kwa Watanzania. Ajira zipo za kuajiriwa katika Serikali na Sekta binafsi na zipo ajira za kujiajiri wenyewe. Serikali imedhamiria kuweka mazingira mazuri ambayo yatawezesha kukuza ajira nchini ili Watanzania wanufaike na kupunguza dhiki ya maisha.
Ndugu Wafanyakazi;
Katika risala yenu mmelizungumzia tatizo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na watu wengi nalo ni lile la kuajiri wageni katika nafasi ambazo zingeweza kufanywa na Watanzania. Napenda kuwahakikishia kuwa, tutakuwa makini na wakali kwa ajira za namna hiyo. Tutasimamia kwa karibu kanuni na taratibu zilizopo kuhusu ajira za wageni nchini. Upo ulegevu fulani fulani ambao tumekusudia tuurekebishe miongoni mwa wahusika Serikalini na kwenye makampuni. Lakini, ni kweli pia kwamba, ajira ya wageni ipo sana katika maeneo ya kada za kati yaani mafundi mchundo (technicians) ambapo nchini kuna upungufu. Ni vyema tuelewe kuwa, tatizo hili linakuzwa na upungufu wetu wa kutokuwa na vyuo vya kutosha vinavyotoa mafunzo ya kada za kati hasa mafundi mchundo na kadhalika. Hatuna budi kutilia mkazo mafunzo ya namna hiyo kwa kuendeleza vyuo vilivyopo na kuanzisha vingine kama hapana budi. Hata hivyo, Serikali haitatoa vibali kwa ajira za namna hiyo mahali ambapo Watanzania wapo na wanaweza kufanya kazi hizo.
Ubinafsishaji wa mashirika
Ndugu Wafanyakazi;
Nilipoongea na Uongozi wa TUCTA hivi karibuni, walionyesha kutoridhika kwao na ubinafsishaji wa mashirika yanayotoa huduma za kijamii na kiuchumi. Risala yenu nayo imesisitiza tena kilio hicho. Napenda niwahakikishie, Wafanyakazi na Watanzania wenzangu, kuwa Serikali haina mpango wa kubinafsisha mashirika yote makubwa yanayotoa huduma za kijamii na kiuchumi (public utilities). Badala yake Serikali inao mpango wa kufanya marekebisho mbalimbali katika mashirika hayo. Katika marekebisho hayo baadhi ya shughuli zinaweza kubinafsishwa au kukodishwa. Dhamira kubwa ya Serikali ni kutafuta mbinu za kuimarisha uendeshaji wa shughuli za mashirika hayo ili yaweze kuboresha utoaji wa huduma zao. Ni ukweli ulio wazi kwamba mashirika yetu mengi yana matatizo makubwa ya uendeshaji.
Ndugu Wafanyakazi;
Serikali haina nia kabisa ya kubinafisha mbuga za wanyama. Ni jambo ambalo halijafikiriwa kabisa na sijui kama litafikiriwa. Mbuga ni urithi wa taifa letu na hatukusudii kuzibinafsisha.
Pamoja na hayo napenda kusisitiza kuwa Serikali haitarudi nyuma katika sera ya mageuzi ya kiuchumi. Hatukusudii kurudia katika kufanya shughuli za uzalishaji mali na biashara. Hiyo ni shughuli itakayofanywa na sekta binafsi, serikali itafanya kazi ya kuboresha mazingira ili sekta binafsi istawi nchini.
Suala la Pensheni
Ndugu Wafanyakazi;
Pensheni ndiyo maslahi pekee ya mfanyakazi anapostaafu kutoka katika utumishi wake wa Umma. Hivyo basi, naelewa masikitiko yenu kama mambo hayako sawa. Serikali inatambua kuwepo kwa tofauti mbalimbali za ulipaji wa pensheni kwa wastaafu kutokana na kuwepo mifuko tofauti ya pensheni na yenye masharti tofauti. Serikali inakubaliana na rai yenu ya kutaka tofauti hizo ziondolewe na usawa uwepo. Napenda kuwahakikishia kuwa tumesikia kilio chenu na tutashughulikia ipasavyo. Naamini hatimaye mtafurahi. Nafurahi kuwaarifu pia kuwa suala la mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa tumeshaanza kulishughulikia. Lengo letu ni kuubadili mfuko huo nao uwe ni wa pensheni tofauti na ilivyo sasa. Naomba mvute subira kwani subira yavuta heri. Mambo yatarekebishwa kwa manufaa ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa.
Ushirikishwaji katika maamuzi
Ndugu Wafanyakazi;
Suala la ushirikishwaji wa wafanyakazi katika utoaji wa maamuzi yanayohusu utendaji katika sehemu za kazi halina mjadala. Umuhimu wake kwa upande wa kuongeza uwajibikaji, ufanisi na tija unaeleweka. Agizo la Serikali Na.1 la mwaka 1970 lilitambua umuhimu huo na kuweka msingi na utaratibu wa ushirikishwaji wa wafanyakazi katika utoaji wa maamuzi sehemu za kazi. Nimesikia kilio chenu kuhusu mapungufu yaliyopo. Nawahakikishieni kwamba, Serikali itasimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa Agizo hilo. Nitasisitiza kuzingatiwa kwa agizo la kuwateua wawakilishi wa wafanyakazi kuwa wajumbe katika Bodi za mashirika ya umma.
Aidha, tunatambua umuhimu wa uwakilishi wa makundi ya jamii katika Bunge. Bahati nzuri jambo hili linatekelezwa vizuri hapa nchini kwa uwakilishi wa wanawake. Ndugu zanguni, katika mfumo wa demokrasia ya uchaguzi na sasa katika siasa za vyama vingi nafasi ya upendeleo zina ukomo wake kwa makundi ya kijamii. Upendeleo maalumu kwa wanawake unatokana na muafaka wa kimataifa na kikanda. Muafaka huo unaelekeza kuwepo kwa asilimia 30 mpaka 50 ya wanawake katika nafasi za uamuzi mojawapo ikiwa ni Bunge la nchi. Hivyo, enyi wafanyakazi wenzangu, napenda kuwashauri kuwa, wale wanaopenda kujihusisha na siasa katika ngazi ya Ubunge, wakagombee katika majimbo yao au sehemu za makundi maalum, kwa wale ambao ni wanawake.
Ndugu Wananchi na
Ndugu Wafanyakazi;
Sisi ni Serikali mpya. Tuna miezi minne tu tangu tuanze kazi. Tunaongozwa na kaulimbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya. Lakini ili tuweze kwenda kwa kasi na msukumo mpya, tunahitaji sana ushirikiano na msaada wa kila mmoja wenu. Nawaomba muiunge mkono Serikali yenu kwa kuchapa kazi kwa bidii na maarifa ili safari yetu ya kuelekea kwenye Tanzania yenye neema kwa wote iwe fupi zaidi.
Naamini uwezo huo mnao. Historia ya nchi yetu imejaa mifano mingi mizuri ya mchango mkubwa wa wafanyakazi kwa uhai na maendeleo ya taifa letu. Wakoloni walipotuvamia na kututawala kwa mabavu, ni nyinyi wafanyakazi mliosimama kidete kupambana nao na kudai uhuru wa nchi yetu. Wengi wa mashujaa wa mapambano hayo, akiwemo Mzee wetu Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa, walitoka miongoni mwenu.
Baada ya uhuru, wafanyakazi mmekuwa pia mstari wa mbele katika kazi ngumu na nzito ya kujenga nchi yetu. Maendeleo tunayozungumzia na kujivunia leo yana mchango mkubwa wa wafanyakazi kwa ushirikiano na Watanzania wote. Hakuna mafanikio yoyote ya nchi yetu ambayo hayakuchangiwa na ninyi wafanyakazi.
Ni kwa msingi huo, mimi nina imani kubwa nanyi. Nathamini sana mchango wenu na nawategemeeni sana katika kufanikisha majukumu mazito mliyonikabidhi ya kuliongoza taifa letu kutoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi kwenye neema.
Nataka kuwathibitishia kuwa daima nitashirikiana nanyi kwa hali na mali. Katika risala yenu hapa mmezungumzia mambo mengi na mazito. Baadhi tayari nimeyagusia lakini kwa mengine yaliyobaki nataka niseme tu kwamba tumesikia, tumeyapokea na tutayafanyia kazi. Naamini hakuna lisilowezekana wala hakuna jambo lisilokuwa na ufumbuzi. Hivyo tutaendelea kuwasiliana na kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa mambo yote mliyoyaeleza. Waziri mhusika Profesa Jumanne Maghembe yuko hapa, naamini naye amesikia vizuri. Atafuatilia kwa karibu.
HITIMISHO
Ndugu Wafanyakazi;
Nilikusudia leo kusema machache. Sina hakika kama nimetimiza ahadi yangu hiyo kwenu. Hata hivyo naomba nimalize kama nilivyoanza. Nawashukuru sana wafanyakazi na wananchi wote kwa juhudi kubwa na nzuri za kujenga taifa letu. Nawashukuru nyote kwa kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Nawashukuru pia kwa uelewa na uvumilivu wenu katika kipindi ambacho tumekuwa tukikabiliwa na changamoto mbalimbali. Nawaomba muendelee na moyo huu wa ushirikiano ili kwa pamoja tujenge uchumi na Taifa imara.
Wahenga walisema: penye nia pana njia. Basi sote tuwe na nia moja ili twende njia moja ya kuelekea kwenye Tanzania yenye maendeleo. Na linalowezekana leo, lisingoje kesho. Inawezekana Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Asante Michuzi, Hotuba hii imejaa kauli za Kikasisi zaidi. Kikwete anaonyesha kufahamu kuhubiri Injili zaidi ya Hotuba za umma. Lakini ana muda mfupi bado ofisini hivyo naunga mkono hoja ya kukubaliana na mahubiri yake na kujenga subira. Kikubwa nafurahi ukweli wa kuona makosa na kuyasema bila uoga na kuahidi kupambana nayo. Mungu ibariki Tanzania, Ibariki Afrika na watu wote wenye nia njema ya maendeleo Duniani.
ReplyDeleteRais ana mtu maalumu wa kutayarisha hotuba zake hata kama naye anachangia lakini wako watu mahususi wa kuandaa speech ya Rais.
ReplyDeleteBado ni hotuba nzuri sana kwa mtazamo wangu.
Ni nzuri sana, lakini amesahau vita dhidi ya majambazi wa kutumia kalamu, I mean Wala rushwa ambao ndio wanaokwamisha jitihada zetu za kusonga mbele
ReplyDeletemichuzi na wanablog wote, hii hotuba ndefu sana kwangu kuweza kuisoma napenda lakini siwezi kabisa, kuna awezae kunisaidia kunipa hints tuu? tafadhali iwapo tu itawezekana
ReplyDeletenatanguliza ahsante.
Ahsante Michuzi kwa hotuba hii.Mengi aliyoyasema sio mageni zaidi ya hilo la tume ya kuangalia upya maslahi ya wananchi.Binafsi sidhani kama hilo linahitaji tume wakati wizara husika zipo na watumishi ni wa kutosha.Nilipokubaliana naye vizuri ni pale mwisho aliposema "Inawezekana,timiza wajibu wako" Hilo ndio la msingi ambalo sisi,kama wananchi,tunatakiwa kulizingatia.
ReplyDeleteWewe anony unayeomba kupewa hint hebu ona aibu. Na hili ni tatizo la watanzania wengi; ni wavivu mno wakusoma lakini wakati huo huo wanajifanya wajuvi kwelikweli. Sasa wewe hapo unaomba hint hizo halafu uende kijiweni: Rais kasema hivi, Rais kasema vile, ooh kumbe hata hotuba yenyewe hujaisoma. Watanzania tuna kazi!
ReplyDeletehebu toa hint hapo acha maneno wewe, si bora unipe hata hiyo hint kuliko niwe sielewi kabisa kinachoendelea.
ReplyDelete