mwanakijiji sasa hivi kaniletea ujumbe ufuatao. kwa vile tarishi hauwawi nami naumwaga kama ulivyo...
Wanafunzi wa kitanzania wapatao 29 waliotelekezwa na serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwenye vyuo vya nchini Ukraine hatimaye leo wameamua kufanya kile walichotishia miezi michache iliyopita, nacho ni kujisalimisha na kuomba hifadhi kwenye Ubalozi wa Uingereza jijini Kiev, nchini Ukraine. Wanafunzi hao wamegoma kuondoka ubalozini hapo hadi wapatiwe jibu la uhakika na serikali ya Tanzania.
Ubalozi huo tayari umeshakubali kuwapokea vijana hao mapema asubuhi. Uamuzi huo umefikiwa baada ya serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Sayansi na Elimu ya juu kuwakana wanafunzi hao na kutowatambua licha ya kuwaahidi mikopo ya masomo tangu mwezi wa tisa mwaka jana. Kwa mujibu wa wanafunzi hao waliozungumza na KLH News ambao tayari wako njiani kuelekea Jijini Kiev kwa treni toka vyuo mbalimbali sababu kubwa ya uamuzi huo ni kuwa:

[*]a. Wanaishi katika maisha magumu ambayo yanatishia siyo tu usalama wao bali pia afya zao. Mara moja tayari wameshaitiwa vyombo vya usalama kuwachunguza.
[*]b. Vyuo vyao vikuu vimewapa tarehe 20 ya mwezi huu kama tarehe ya kufutwa chuoni na hapo kuwa wahalifu na kuweza kukamatwa na kufungwa
[*]c. Mmoja wa wanafunzi alishanganyikiwa kutokana na msukumo wa matatizo hadi kuitiwa madaktari wa magonjwa ya akili. Hali yake licha ya kutengemaa lakini bado yuko nusu nusu.
[*]d. Jitihada za wanafunzi hawa kuwasiliana na viongozi wa wizara zimekwama baada ya kuzunguzwa zungushwa na viongozi wa wizara hiyo akiwemo Waziri wa Wizara hiyo Prof. Msolla ambaye amefikia kukata simu kila vijana hao wanapojitambulisha. Wizara hiyo hiyo imeshindwa kushughulikia matatizo ya wanafunzi wengine walioko nje ya nchi wanaokabiliwa na matatizo yanayolingana au kukaribiana na yale ya Ukraine. Miongoni mwa wanafunzi walioko katika hali mbaya ni wale wa Cuba, na wale Urusi.
[*]e. Jitihada za wazazi wa vijana hao kuwasiliana na viongozi wa Bodi ya Mikopo na wizara imeshindikana baada ya serikali kusema kuwa "haiwatambui" vijana hao na hivyo kuwafanya wazee hao kushindwa kujua wafanye nini isipokuwa kuanza hatua za kisheria dhidi ya wizara na wahusika wengine. Madai haya ya kutowatambua yalithibitishwa na Prof. Msolla mwenyewe alipozungumza nami mapema leo. Na nilipomuuliza kama wizara au bodi ya mikopo haikutoa ahadi yoyote kwa vijana hao alikataa kujibu na kukata simu na kuizima kabisa. Sehemu ya mahojiano yangu na Prof. Msolla yatasikika kesho.
[*]f. Ubalozi wa Uingereza Ukraine uliipa serikali ya Tanzania ofa ya kuwasaidia kuwalipia vijana hao na kuwapa misaada mingine ya kibinadamu endapo tu serikali ya Tanzania itaandika barua ya kurudisha fedha hizo kwa serikali ya Uingereza. Serikali ya Tanzania haikuwapa jibu hadi leo.[*]g. Balozi wa Tanzania Urusi ambaye pia anatuwakilisha Ukraine amejitahidi kufanya mambo mengi ambayo yangefanywa na wizara hadi amefikia mahali pa kuwaambia wanafunzi hao hana jingine la kufanya na kuwataka "waombe Mungu".
[*]h. Ahadi ya serikali ya kutuma ujumbe kwenda nchi hizo (usiniulize pesa za ujumbe huo zitatoka wapi) kwenda kuangalia matatizo hayo mwanzoni mwa mwezi huu imefutwa na hakuna ahadi nyingine au mpango unaoeleweka wa kufanya ziara hiyo.
[*]i. Bodi ya mikopo ya elimu ya juu imekuwa ikibadili badili taratibu na kushindwa kabisa kuja na utaratibu wa haki, unaoeleweka na wenye mantiki katika kushughulikia tatizo la elimu ya Juu Tanzania. Matatizo yanayotokea kwenye vyuo vikuu nyumbani na yaliyosababisha wanafunzi kugoma ni matokeo ya bodi goigoi, isiyo makini, isiyojua inachofanya, na isiyo na uwezo wa kushughulikia suala zima la elimu ya juu. Bodi hii ni aibu kwa Taifa, ni kashfa iliyochosha, na ni mfano wa ukiritimba uliokithiri. Ni lazima ivunjwe.

Ni kutokana na mambo hayo yote, vijana wetu, watoto wetu na wa Watanzania wenzetu wamefikia kikomo cha ustahimilivu wao na uungwana wao. Majaribio yote ya kutatua tatizo hili kimya kimya yameshindikana.
Wakati wa kumwajibisha Prof. Msolla, Mama Katunzi, na wakuu wa Bodi ya Mikopo umefika. KLH News inasimama upande mmoja na vijana hawa kwa kitendo chao ambacho kingeweza kuepukika lakini kutokana na kiburi na ubabe wa serikali (ambao umeendelezwa) imebidi wakichukue.
Hisia ya viongozi wa serikali kudhani wanaimiliki Tanzania na wana maamuzi ya mwisho ni lazima ioneshwe kuwa ni hisia iliyopotoka na isiyo na nafasi tena katika jamii yetu. Viongozi ni watumishi na wanatakiwa kuongoza.
Katika hili wameshindwa kabisa kuongoza na badala yake wamebakia kupiga kelele za "ukuu wa serikali" wakionesha wazi kutojali hatima ya watoto wa wenzao!!
Unganeni nami, na kwa mlio mmoja kuitisha kujiuzulu kwa Prof. Msolla na Mama Katunzi, na kuvunjwa kwa bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Mahojiano na wanafunzi hao na pia Waziri wa Elimu ya Juu Prof. Msolla yanasikika kwenye KLH News http://www.mwanakijiji.podomatic.com
Mwenyeji - KLH NewsSauti ya Watanzania kwenye Mtandao!
Hatulali - Daima tuko Macho!!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 21 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 18, 2007

    Serekali ya Uingereza inahusikaje na mabo hay kama si umtonya wa hawa vijana ?
    Waje hapa (UK) tusaidiane kubeba kama wanaona tunafaidi !
    Dunia ya leo wala si nchi nyingi zinazolipia vijana wao masomoni n'gambo kwa elimu ya juu bila kueleza mikakati ya kukusanya madeni baada ya masomo!
    Hawa vijana wana wakati mgumu sana wenzao dar walikuwa wanagoma juzi tu ,bora wao hawakujisalimisha na "kuchagua kaka "
    Kila la kheri wadogo zangu

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 18, 2007

    Poleni vijana kwa kupigishwa kwata na wizara ya elimu ya juu Tanzania. Ndo hivyo mwenye shibe hamtambui mwenye njaa.

    Watanzania woote tunajua enzi zile walizosoma viongozi woote hawa wanaoatamia madaraka sasa walisoma buure. nyakati hizo walikuwa wakiingia mabwalo wanakula mavyakula, wanajichotea matunda wanakula tena kwa starehe zote, mawali haya wakishiba wanaaza kutengeneza snowman huku wasichana wao wakiviringa wali na kurusiana wakicheza ready. Ukizunguka mlango wa nyuma unakuta wapishi nao wakitia mikuku, mi-blue band na vikorokoro vingine katika makapu yao tayari kwa kupeleka nyumbani. Walitunzwa haswa kama watu watakaoleta ukombozi kwa wenzao siku za baadaye. Leo hii mwe!!!!

    Hivi sasa wamejishibia zao kwa mamishara makubwa ya serikali. Wanachokifanya ni kuwakoromea watoto wanyonge chuo kikuu wanaoitafuta elimu. Maendeleo Tanzania ni Dar na katika miji kadhaa tu lakini maskini ya Mungu ukienda vijijini tangu miaka ile nasoma primary school baaaado kuko vile vile tu. Sasa bila kuwasaidia watu na kuwaelimisha kwa karibu sijui tutafikaje huko maendeleoni? May be hadi mwaka 2,100.

    Poleni, nadhani vijana mmejifunza -usiamini mikataba na serikali. Mngerudi nyumbani na kusomea UDSM labda watawasikia- na UD napo ni kifukuto tu. Labda mtafute scholarship na kwenda nchi zingine mkamalizie masomo yetu.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 18, 2007

    Nimezungumza tena na wanafunzi hao wakidamkia nje ya ofisi za Ubalozi wa Uingereza, wamelala nje na baridi.. na wengine wamepatwa na mafua... hali ni mbaya.. na serikali iko kimya. Nimezungumza na Waziri Mkuu Bw. Lowassa ambaye alichokisema itakuwa ni nukuu nitakayoenda nayo Kaburini...! sijawahi kukatishwa tamaa na kiongozi namna hiyo.. anyway..amesema Naibu Waziri wa Elimu ya Juu yuko Ukraine... sijui kama ni kikazi au vinginevyo...na sijui kama anapanga kukutana na hao vijana au la...

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 18, 2007

    Hii serikali ya sasa ni ya MABISHOLOLO wala haiwajali wananchi wa chini zaidi ya kuzidi kuwakandamiza !!! Kwani waliopata MENO kabla ndio watakaokula nyama siku zote !! Tena afadhali hata serikali ya AWAMU ya tatu pamoja na kwamba walikuwepo waliokuwa walafi LAKINI sio kama hii ya sasa ambayo VIONGOZI wanajali maslahi yao binafsi dhidi ya walalahoi !! Hao watoto walioenda kusoma UKRAINE lazima watakuwa walipata BARAKA zote za Wizara husika, sasa inapofikia hasa huyo Prof. uchwala ambaye alitumia pesa nyingi kumuondoa mbunge wa zamani wa KILOLO, Mh. Mwamoto, ili apate hiyo nafasi aliyonayo na kujisahau na kuwajibu wanafunzi hao ovyo utadhani atakaa kwenye wadhifa HUO alionao mpaka KIFO chake kitakapomfikia !!!! Haya mambo yafanywayo ndio yanafanya wananchi hasa WALALAHOI wamkumbuke hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba HAKUNA aliye kuwa MKOMBOZI wa WATANZANIA kama yeye !!! MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU WABARIKI WALALAHOI !!!

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 18, 2007

    hawa watotot wanatafuta umaarufu wa fujo bora wangeimba bongo flava, wameenda ubalozi wa uingereza kufanya nini sasa? pumbafu kama hawana hela na hawataki kupiga box warudi nyumbani full stop
    sie wanatucheka jinsi migongo ilivyopinda kwa ajili ya box
    michuzi unatujazia tu nafasi tumeshachoka na upuuzi wao hawa kula kulala wanafikiri maisha ni tonge mdomoni till to the end let 'em learn

    ReplyDelete
  6. Inatia huruma sana.Nina hasira sana na hawa wezi,nimewachoka na wizi wao midomo iliyojaa uongo na unafiki na kiburi.Wanapashwa kuchomwa moto!......

    Ngoja niachie hapa maana nina hasira sana na hawa wezi wa Tanzania.Hasira zikipungua nitarudi tena

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 18, 2007

    wewe ananymous unavyosema kuhusu kupiga mabox unadhani kila nchi foreigners wanaruhusiwa kupiga mabox,,wewe shukuru mungu hata hilo box umelipata la kubeba,,,km ulikuwa huna cha kuandika bora ungenyamaza sio kuwasema eti wanatafuta umaarufu,,,
    Mi nawatakiwa hao watoto kila la kheri ktk kudai haki zao,Mungu awalinde na kuwaongoza!

    ReplyDelete
  8. Hivi jamani huyu msola ni mungu mtu!!!!mbona anaonekana ni mtu jeuri sana????Yaani ndo kwanza mwaka unaisha lakini jeuri anayoenyesha ni ya kiwango cha juu????au wanafunzi anaowakatia simu si ndo angepaswa asikilize matatizo yao na kutafutia ufumbuzi?????

    ReplyDelete
  9. KAULI YA JAJI MKUU SAMATA IWE CHANGAMOTO KWA WADAU WA SHERIA NCHINI

    Katika mamabo ambayo watanzania tumekua tukijigamba na kutembea vifua mbele ni AMANI iliyotawala nchini tangu tulipopata uhuru karibu miongo minne na nusu iliyopita..Nchi yetu imetokea kua kimbilio la wageni kutoka nchi majirani ambapo hapakaliki kutokana na kutoelewana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na vita vya kimakundi au kimatabaka kati ya watawala na wananchi wao.

    Sina haja ya kuingia kwa undani katika hali tete inayoendelea kwa majirani zetu ila kwa kuanzia mada iliyobeba kichwa cha habari hapo juu niliona ni busara kugusua kwa uchache maswahibu yanayowakumba wenzetu katika siasa zao na mifumo ya utawala na ya kutetetea haki zao.


    Jana Mheshimiwa jaji mkuu Barnabas Samatta aligusia juu ya umuhimu wa vyombo vya sheria hasa mahakama katika kudumisha amani ya nchi husika kwa kuweka bayana kua...nanukuu "Iwapo jamii itapoteza imani kwa mahakama zetu ndio itakua mwanzo wa kupoteza amani nchini" Inawezekana ikaonekana ni sentensi fupi na iliyozoeleka lakini suala linabaki kua ni jitihada zipi zimefanyika katika kunusuru hali hiyo isitokee???Tunafanya nini ili kuhakikisha wananchi wetu hasa wale waliokata tamaa hawapotezi imani kwa vyombo vyetu hivi ambavyo ni mhimili muhimu katika utawala wa kidemokrasia na wenye kuheshimu haki za binadamu????

    Kauli hii imekuja wakati muafaka wakati kukiwa na malalamiko mengi juu ya ubabaishaji unaofanywa na vyombo hivi katika kutetea haki za wanyonge.....Kumekua na ucheleweshaji wa kesi katika kiwango cha kukatisha tamaa na hata mara nyingine kutolewa maamuzi ambayo wakati mwingine yamekua yakizua mjadala juu ya umakini wa vyombo vyetu hivi..Sina nia ya kubeza kila jema linalofanywa na na mahakama zetu ila ni katika kuleta changamoto kwenye mchakato wa wadau kuelekea kwenye ujenzi wa jamii wenye kuheshimu haki za wananchi wenzetu..

    Kumekua na migogoro mingi kati ya mtu na mtu,jamii na jamii,wananchi na serikali,wafanyakazi na waajiri wao,wanafunzi na uongozi wao lakini je "nii hatma ya kelele na tofauti zitokanazo na misuguano ya makundi hayo"?? Siku zote binadamu amekua na tabia ya kujaribu njia mbadala pale anapoona nia na mitazamo yao haiendi sawa na kama walivyotaraji....vitendo vya kuchoma vibaka moto ni kielelezo kirahisi cha kuelezea kuchoshwa na ufanisi wa baadhi ya taasisi au asasi zilizokabidhiwa majukumu ya kusimamia mambo kama hayo....Kwanini raia ambaye amechoshwa na tabia ya jambazi sugu au vibaka wazoefu asiamue kuchukua sheria mkononi wakati kila wanapopoleka malalamiko yao kwenye vyombo husika,hakuna maamuzi ambayo yataonekana kukidhi kero za walalamikaji!!!!!!

    Kuna kesi nyingi katika sekta ya madini kati ya wachimbaji wadogo wadogo na wamiliki wa makampuni ya kigeni,kuna kesi nyingi kati ya wafanyakazi na waajiri wao ambazo bado mwisho wake haujulikani,wastaafu kila siku wanatanga na njia katika kufuatilia haki zao lakini bila matumaini yoyote katika yale mambo wanayodai ambayo asilimia 90% ni ya msingi!!!!!! Siku za karibuni kumekua na zoezi la bomoa bomoa katika jiji la Dar Es Salaam na asilimia kubwa ya wahanga wa tatizo hilo ni machinga.....vibanda vyao vingi vilipitiwa na sulubu hiyo...Sina nia ya kubeza zoezi hilo kwani mantiki yake iko wazi kabisa 'Kupendezesha mandhari ya jiji' hili ni jambo jema na linapaswa kupongezwa na kila mtu lakini swali la msingi ambalo linastaajabisha kila watu makini ni "Kwanini baadhi ya vibanda viachwe" Katika gazeti tando la michuzi alipiga picha ya moja ya vibanda hivyo na kuhoji uhalali wa kuwepo kwake????Watu wengi walichangia na kusema pengine ni cha mkubwa flani!!!je wakubwa hawapaswi kuguswa na sheria????je hao ndo wanapaswa kua juu ya sheria????

    Iko mifano mingi ambayo inatia kichefuchefu katika utekelezaji wa mambo ambayo ni ya manufaa kwa wananchi...Nani hajui kua karibu asilimia 60 ya vituo vya mafuta vilivyopo katika jiji la Dar Es Salaam vipo kinyume na sheria???Je wasimamizi wa sheria hizo wako wapi??? au tunataka wananchi waanze kuamini kua hizo ni miradi ya watunga sera na sheria ambao pia wamepewa ruhusa ya kuzivunja???Ni kwanini majibu ya maswali haya yasipatiwe ufumbuzi wa haraka katika kurudisha imani ya wananchi kwa watawala wao?????

    Kwa kumalizia napenda kutoa tu changamoto kwa serikali yetu kua makini katika kusimamia na kutatua kero za wananchi wake ili waendelee kua tayari katika kushiriki kikamilifu utekelezaji wa mipango ya maendeleo yao....Naamini kubwa na serikali ya mheshimiwa baba JK kwahiyo chondechonde watendaji msimwangushe katika nia yake njema ya kujenga nchi moja inayoheshimu haki na yenye kuweka mazingira ya kila mmoja kufaidi matunda ya uhuru...Ubabe wa baadhi ya watendaji hayana nafasi kwasasa kwani mwisho wake hautupi matumaini yoyote mazuri.....Mfano mzuri tunao kwa migomo inayoendelea kwa wanafunzi wa elimu ya juu....hii kwangu ni ishara ya kuchoshwa na ubabaishaji wa baadhi ya watendaji.....Nadhani itabidi tuanze kujadili nia ya mtu kama Proffessor msola katika kutumikia wananchi wa jamuhuri yetu hii.....Inatia hasira pale unaposikia WAZIRI flani msomi anawakatia simu wananchi wake eti kwasababu amechoshwa na kero zao!!!!!!!Hili naomba niliongelee siku nyingine...


    Naomba kuwasilisha..

    ReplyDelete
  10. AnonymousMay 18, 2007

    Sisi wanafunzi wa Cuba tulishapata mikopo yetu kama tulivyoomba, baada ya kupata msaada mkubwa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam na Ubalozi wa Tanzania Ottawa Canada. nawaomba wanafunzi wenzetu wa Kiev wasivujike moyo waendelee kufuatilia masuala yao

    ReplyDelete
  11. AnonymousMay 18, 2007

    Kaka au ni dada samahani kwa kukukosoa kwakweli hawa watoto si mabogas,ni binadamu anaejaribu kutafuta msaada juu ya shida zinazowakabil kutokana na kuiamini serikali ya bongo...ikiwa serikali yao haiwajali na wameshafika hadi huko na kuanza masomo yao hadi hapo walipofikia unadhani ni mchezo?????
    ulitaka warudi huku waimbe bngo flava kwani ndo maisha hayo????kila mtu akiamuwa kuimba bongo flava je hizi kazi yengine watafanya nani bila kisomo ndugu????na ukitazama kazi za sasa hivi ni CV kwenda mbele zaid ya hapo unakuwa mlalahoi kama mimi.samahani sanaa kwa kukukosoa ndugu lakini serikali ya tanzania ipo kwenye dilema bado,haijijui nibora kutoweka kitu ambacho mnajijuwa hamuwezi kukitekeleza rather than kuwatupa vijana wa taifa lakesho namna hiyo kwenye serikali za watu na kupatwa na majanga ya namna hii...
    kwakweli prof inathibitisha kabisa kama mnawasaliti vijana kwa kitendo cha kuwakatia simu na kutotaka kuwasaidia vijana wetu,ni bora msiwape vijana matumaini ya kuendelea kusoma na wakati hamjiwezi jaman...tafadhali prof wasaidie vijana kabla hujatumbukia kwenye shimo la makaa ya moto..wangekuwa watoto wenu nyinyi mlokuwa serikalini mngekubali wateseke kiasi hiki????SIDHANI KWAKELI.kuweni waungwana na mtimize wajibu....

    ReplyDelete
  12. AnonymousMay 18, 2007

    Kwanini wanaomba ubalozi wa uingereza? Si wangeomba hifathi hiyo nchi waliopo?
    Serikali ya uingereza inahusikaje? Kuna maubalozi mangapi mpaka wakimbilie uingereza...Mnofu mkubwa ehe

    ReplyDelete
  13. AnonymousMay 18, 2007

    Rudini nyumbani. Kama mnasema nchi hizo hazina hata kazi basi rudini home.

    Mlipopata hizo nafasi mlijua nchi mnayoenda kuwa hazina tajira? Na kama mnapata kichaa nchi za watu kwanini msirudi tu home?

    Mambo ya kusomeshana yangisha. watu wanataka loana wakati wakipewa hawalipi sasa mnataka hiyo fund iwe inaongezeka kutoka wapi. Wakulaumiwa ni hao wanaomaliza nakutolipa hela ili ziwasomeshe wengine na sio nchi.

    Mngeenda UN kwanini uingereza? Acheni kutafuta umaarufu.. Kwani uingereza ni baba wa Tanzania?
    Nyie ujinga umewazidi. Mbona hamkukimbilia ubalozi wa USA au mmejua jinsi walivyo anti immigrant kwa sasa mkajua huko hamtasikilizwa.
    Isiwe tabu hata wengine tunateseka kuliko nyie tu.

    ReplyDelete
  14. AnonymousMay 18, 2007

    Wewe anoy 2:45 ni wasomi wangapi hawana ajira bongo? Siku hizi kusoma sio asset ya nchi tena ni asset yako. Kwa hiyo mbinu na jinsi ya kupata mikopo ni wew na wazazi waliokuleta hapa duniani sio nchi tena. Nchi inatakiwa kuwasaidia kupata basic education tu.
    Na kama unataka ikusaidida unatakiwa uombe kwa utulivu sio kutishia migomo na kwenda kwenye maubalozi ya nchi nyingine. Na kwa taarifa hamna nchi inayokubali watu wa TZ kama asylum.

    ReplyDelete
  15. AnonymousMay 18, 2007

    Anon wa 2:45:00 pm unapoteza nguvu zako bure kujaribu kuelimisha watu ambao hawako tayari kuelemika. Wengi wanaopinga watoto wa maskini wasipate elimu ni wale ambao wana hofu kwamba watapoteza nafasi zao kwa hao maskini au hawapendi wengine waje wapate nafasi ktk jamii.

    Pia WENGI wanaopinga ni wale ambao, KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE, hawakupata BAHATI/HAKI ya kufadhiliwa na serikali ktk level ya elimu ya chuo kikuu.Kwa ufupi hawakupata elimu ya chuo kikuu au waliipata baada ya "kubeba mabox" sana; au walilipiwa na wazazi/ndugu zao wenye uwezo sasa inawauma kwanini wengine walilipiwe (am sorry, WAKOPESHWE) na serikali.

    Tanzania haitaendelea kama watu hatutaacha wivu na ubinafsi.Elimu ukiipata wewe peke yako na wengine wakakosa ina manufaa gani?

    Think twice!

    ReplyDelete
  16. AnonymousMay 18, 2007

    Hivi kwa nini huyu Msola na bodi yake ya MAKOPO tusiwafukuze kama mbwa mwizi?, wanawanyanyasa wadogo zetu sanaa.Sisi ndo waajiri wa aliyeajiri hiyo jeuri anamfanyia nani?

    ReplyDelete
  17. AnonymousMay 18, 2007

    Jamani finally watu wanauona ubaya wa Msola eeh? Mi nimekulia Morogoro, nimesoma SUA (Sokoine University of Agriculture) toka shule ya msingi wakati Msola anapanda cheo na kuwa Vice-chancellor was SUA, that man yaani haambiliki! akiamua ameamua, na ni mtu mbaya sana, hasa kwa wanafunzi. Nakumbuka wakati wa migomo, enzi hizo sie wadogo mambo Msola aliyokuwa anayafanya- na alikuwa anaogopwa balaa. Na hajaacha mpaka leo mie sasa mtu mzima namaliza chuo. Nilishangaa sana wakati alipochanguliwa kuwa waziri, hivi Kikwete angekuwa mpigania maslahi ya walalahoi angechagua mtu kama yule kuwa waziri wa elimu? mmh au atasema alikuwa hajui mambo ya Msola? Na huu ni mwanzo, ngojeni msikie...

    ReplyDelete
  18. AnonymousMay 18, 2007

    Miye nampenda msola ..kama mayor Bloomber wa NY city. Hataki ujinga anaenda na law...mambo ya kubebana migingoni yaishe.

    Kopa lipa fanya kazi ulipwe hamna cha bure ulimwengu huu.

    ReplyDelete
  19. AnonymousMay 19, 2007

    Arise Sir Julius Kambarage Nyerere,sorry to say this, but our beloved Tanzania has gone to the dogs,the motherland seems to be galloping backwards. KAMBARAGE tunalia

    ReplyDelete
  20. AnonymousMay 20, 2007

    Samahani mwanakijiji,
    kwa nini hao wanafunzi wasiende ubalozi wa bongo huko Russia?
    Kunaniiiiiiiiiiiiiii?

    ReplyDelete
  21. AnonymousMay 21, 2007

    MTAJIJUUUUUU......MTAJIJUUUUU. FUNGASHA VIRAGO RUDINI HUKU MKUTANE NA FFU UDSM. MTAJIJUUUUUU NA ELIMU YENU YA JUUUUUUUUUU. Hata nyie mkipata elimu mi nikija ofisini kwenu mtanijibu hivyo huku mkidai...en elimu bwana, soma kijana teh...teh... teh teh... halafu unamwita mtoto wa mjomba wako ambaye umempa kazi ya mgambo ofisini...."MWAKINYUNYU hebu kuja hapa ondoa hii taka taka sina shida ya kuona hiii...ok" na kidhungu chenu cha UKRAINE!!!!FYUUUUSSSSSSSSS

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...