jk akipozi na kamati ya profesa wangwe baada ya kuwasilisha ripoti yao jana ikulu
Kamati ya kukusanya maoni kuhusu uharakishwaji wa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki, jana ilimemkabidhi Rais Jakaya Kikwete ripoti yake katika hafla fupi iliyofanyika ikulu.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Profesa Joseph Wangwe amesema asilimia 75.9 ya Watanzania waliohojiwa wamesema hakuna sababu ya kuharakisha uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki ili hali ni asilimia 20.8 ndio waliotaka kuharakishwa kwa shirikisho hilo.

Professa amemweleza Rais kwamba jumla ya Watanzania 65.000 walipata fursa ya kutoa maoni yao na kwamba kamati yake ilitembelea mikoa yote 26 na wilaya zote pamoja na kukutana na makundi yote muhimu ya kijami kama ambavyo Rais alivyokuwa ameagiza.

Mwenyekiti huyo wa kamati amefafanua kwamba ukusanyaji wa maoni hao umechukua muda mrefu kutokana umuhimu wa jambo lenyewe lakini pamoja na kuzingatia maagizo waliyopewa na Rais Jakaya Kikwete.

Amefafanua kwamba njia mbalimbali zilitumika katika ukusanyaji wa maoni hayo zikiwamo za mikutano ya hadhara, madodoso, radio, televisheni na tovuti.

Aidha Profesa Wangwe amebainisha kwamba taarifa hiyo ambayo imo katika vitabu viwili pamoja na mkanda wa video imegawanywa katika maeneo makuu mawili – ambayo ni ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Katika Siasa, Professa anaeleza kuwa elimu ya ufahamu kuhusu Shirikisho ni jambo ambalo lilisisitizwa na wananchi wakati wakitoa maoni yao .

“Kuhusu Demokrasia na Utawala Bora, wananchi walionyesha wasiwasi wao kama nchi jirani zina demokrasia na utawala bora kiasi cha kuridhisha kuwa na shirikisho. Lakini pia suala la kero za muungano lilijitokeza huku wananchi wakishauri kwamba kero hizo zipatiwe ufumbuzi kabla ya kuingia kwenye shirikisho” akasema.

Ameeleza kuwa katika sababu hizo za kisiasa, wananchi pia walielezea wasiwasi wao kuhusu tofauti za kiitikadi kwamba bado kunatofauti ambazo ni lazima zishughulikiwe.

Kwa upande wa uchumi na maendeleo ya Kijamii, Professa Wangwe anasema, Watanzania wengi wamekuwa na wasiwasi katika mambo manne.

Kwanza ni tofauti za kiuchimi kati ya Tanzania na Kenya, pili uwezo wa ushindani wa kibiashara na hasa soko la ajira, tatu umuhimu wa kuweka misingi mizuri ya kiuchumi na nne umiliki wa ardhi na maliasili.

“Kwa wale wanaosema tuharakishe uundwaji wa shirikisho nao walielezea faida mbalimbali kuhusu shirikisho hilo .


"Lakini pia Mheshimiwa Rais kuna maswali mengine yaliyojitokeza ambayo hayahusiani na mambo ya shirikisho ni ya kitaifa nayo pia tumeyaweka kwenye ripoti hiyo” alieleza Profesa Wangwe.

Akihitimisha maelelezo yake, Professa Wangwe amemweleza Rais kwamba katika mchakato huo wa kukusanya maoni hayo wananchi waliihoji kamati kama maoni yao yangefikishwa kwa Rais kama yalivyo na kama yatafikishwa, je yatafanyiwa kazi?

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa baada ya kamati kukamilisha kazi yake, sasa kazi iliyobaki ni ya serikali na kuongeza kuwa ripoti hiyo itawasilishwa katika Baraza la Mawaziri na Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Professa Ibrahimu Msabaha.

“Baada ya kuwasilisha katika Baraza la Mawaziri, Wizara husika watakutana na wenzao na Sekretariati ya Afrika Mashariki,” akasisitiza Rais Kikwete.
Amesema Rais “Ninawashukuru sana kwa kazi nzuri na kwa ripoti hii nzuri mliyonikabidhii, nawashukuruni kwa uvumilivu maana hata kusikiliza nako kunahitaji uvumilivu, nina imani wako baadhi ya wananchi waliokuwa wakali sana kuhusu mchakato huu na wakawafokea kama vile nyie ndio mlioliamua jambo hili. Mmemaliza kazi yenu sasa kazi iliyobaki tuachie sisi”.

Kuhusu kama Serikali itayazingatia na kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wananchi, Rais Kikwete amewahakikishia wananchi kwamba serikali imeyapokea maoni yao na itayafanyia kazi kama ambavyo wameshauri.

Kamati ya kukusanya maoni kuhusu uharakishwaji uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki ilianza kazi yake mwezi Oktoba mwaka jana na imekamilisha kazi yake Julai 13, 2007

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 14, 2007

    Watu 65,000 tu?
    Watanzania walio na umri zaidi ya miaka 18 ni kama asilimia 50 (kama watu 17,500,000) kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002. Kitakwimu hiyo sampuli ni ndogo mno kuweza kuitolea maamuzi manake ni asilimia 0.4 ya watanzania walau wenye umri wa mika 15 na kuendelea. Inawezekana kama wangetumia sampuli kubwa ya kutosha si ajabu watu wasiopenda kuharakishwa kwa shirikisho wangekaribia asilimia mia moja! Hata hivyo, kiasi fulani picha imepatikana licha ya juhudi za kufunika ukweli.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 14, 2007

    Tunaomba kamati hiyo iliyotukuka kabisa ituambie ni kiasi gani cha kodi zetu wametumia kwa kipindi chote hicho.Na kisha wananchi tutafanya tasmini ya kuona kama kulikuwa na ulazima kuwa na kamati kwa kitu kilichokuwa wazi kama hicho.Maana ya Malima na Mengi zilimwagwa 100M. Mmh,jamani,sisi kweli upole umetuzidi !!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 14, 2007

    Kaka Michuzi kama umekosea jina la bosi wangu wa zamani Wangwe. Ni Profesor Samweli Wangwe sio Joseph... asante!!

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 15, 2007

    Mbona kwenye hiyo maada sijaona kipengele kinachohusu usalama wa jamii na umoja? Kenya wenyewe kwa wenyewe wanamatabaka sana na migogoro hiyo siyo tishio kwa nchi nyingine?...

    ReplyDelete
  5. Du Michu,hao wazee kabla hawajaanza iyo kazi hawakuwa na matumbo ya hivyo tunavyowaona sasa, Hivi kweli hizo sio Kodi zetu mzee, naungana na muungwana wa kwanza kuomba tupewe takwim halisi ya faranga za kitanzania zilizotumiwa na kamati hiyo ya kuratibu european union ya Africa mashariki.Mambo mengine tutaelezana baada ya kupata takwim halisi za faranga

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 15, 2007

    Republic of East Africa ni ndoto ya alinacha,mi nashangaa kwani tuli bother hata kukusanya maoni,it is simply unworkable.Looks like wakenya,waganda,warundi na wanyarwanda wanatamani sana tena sana kuungana na sisi, na kama hivyo ndivyo ilivyo basi waje tuungane lakini tu form THE GREATER REPUBLIC OF TANZANIA,makao makuu Dar,lugha rasmi kiswahili,makao makuu ya bunge dodoma, jeshi litaitwa GTPDF makao makuu Lugalo etc na Rais wa Tanzania atateua wakuu wapya wa mikoa ya kenya,uganda,rwanda na burundi.atakayetaka kuleta mambo ya mungiki,mauaji ya kimbari etc moja kwa moja ni detention without trial.are they ready?if not waachane na sisi.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 16, 2007

    HUYO KIJANA ALIYESIMAMA MSITARI WA MBELE MIKONO AMAIFUNGA MAENEO YA SEHEMU ZAKE ZA NDOA NI MHE.ZITTO KABWE? NASIKIA JAMAA KICHWA KISHENZI....

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 17, 2007

    Zitto kweli ni kichwa, ila siri kubwa ya Zitto ni kusoma kwa bidii na kutafuta habari mpya kila kukicha. Zitto hakubali jambo kirahisi lazima ahoji ili apate ufafanuzi. Ndo maan unaambiwa sceptism is sometimes very important, it will drive you to search and seek more and clarified informations. Come on guys sisi wote ni vichwa ila wengine ni wavivu wa kufikiri na kutafuta habari!!!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...