Katika kuadhimisha miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, mwaka 2007, tuliandaa shindano la kutafuta kijana mwenye kipaji cha biashara, katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. Mafanikio yalikuwa makubwa sana.
Tuliweza kupata mapendekezo mengi, na baada ya uchambuzi yakinifu tukapata washindani watatu, ambapo baada ya mchuano wa mwisho, tuliweza kupata mshindi mmoja ambaye aliondoka na kitita cha dola elfu mbili za kimarekani, na kompyuta.
Mwaka huu mshindi atapata dola elfu tano za Marekani, pamoja na Kombe.
Shindano hili ni kwa ajili ya vijana wenye umri kati ya miaka 16 hadi 24 na kwamba washiriki wanapaswa kuandika mchakato wa aina ya biashara ambao utafafanua jinsi watakavyoiendesha kwa bajeti ya fedha ambazo zitatolewa kama zawadi ya kwanza.
Hakika shindano hili mwaka jana lilivutia wasikilizaji wetu wengi sana, na hata katika siku ya kutoa zawadi, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, mbali na kuiopongeza BBC kwa shughuli pevu kama hiyo, aliomba shindano kama hili lirudiwe, na sisi bila hiana, tumefanya hivyo.
Tofauti na mwaka jana, mwaka huu shindano hili litakuwa na awamu mbili:
Awamu ya kwanza: Kila nchi itakuwa na shindano lake, ambapo atapatikana mshindi mmoja katika nchi husika.
Awamu ya pili: Hii ndio fainali yenyewe. Washindi kutoka kila nchi husika, watapambana katika fainali hii.
Nchi sita za Afrika Mashariki na Kati zitahusika katika shindano hili, nazo ni: Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Fainali itatangazwa moja kwa moja katika matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, kupitia kipindi chake maarufu - Dira ya Dunia, na pia kwenye mtandao bbcswahili.com.
Faidika na BBC 2008, Sheria na Kanuni za shindano
1. Shindano hili linaendeshwa na BBC.
2. Shindano ni kwa ajili ya raia na wakazi wa Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Washiriki lazima wawe na umri wa kati ya miaka kumi na sita (16) na ishirini na nne (24) wakati wa shindano. Washiriki watalazimika kuonesha uthibitisho wa umri na uraia wao.
3. Mchanganuo utakaowasilishwa usizidi maneno 1,500 (Elfu moja na mia tano). Na uwasilishwe kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza tu.
4. Michanganuo itakayowasilishwa haitorejeshwa, hivyo mshiriki ahakikishe anahifadhi nakala. Mchanganuo uwe kazi halisi ya aliyeuandaa, na usivuke mipaka ya hakimiliki, au kuathiri mtu yeyote na kwa njia yoyote.
5. Washiriki watambue kuwa, BBC haitahakikisha kuifanya michanganuo iliyowasilishwa kuwa siri, hivyo waandaaji hawana budi kuamua ni yapi wanataka kuyaweka katika michanganuo yao. BBC haitahusika na lolote katika hilo.
6. Mchanganuo utumwe kwa BBC kupitia anuani iliyopo kwenye wavuti bbcswahili.com/faidika, au kutumwa kwa posta au kuwasilishwa katika ofisi za BBC zilizopo katika nchi zinazoshiriki kwenye shindano hili.
7. Michanganuo yote itapitiwa kwa uangalifu na michanganuo mitatu kutoka kila nchi itachaguliwa.
8. Michanganuo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda itachambuliwa kwa pamoja, na kwa siku moja.
9. Washindi watatu kutoka kila nchi watalipiwa gharama zote na BBC za kushiriki katika fainali ya nchi husika.
10. Washindi wa kitaifa, watachujwa na majaji watakaoiwakilisha BBC na jamii ya wafanyabiashara ya eneo la Afrika Mashariki katika nchi husika. Mshindi katika taifa husika, atalazimika kutetea mchanganuo wake na kuwashawishi majaji, katika matangazo ya moja kwa moja ya BBC.
11. Mshindi wa kwanza kutoka kila taifa, ataalikwa na BBC kushiriki katika fainali, itakayofanyika Kampala Uganda. Wshiriki watapambanisha michanganuo yao mbele ya majaji, katika fainali itakayotangazwa moja kwa moja kupitia BBC na bbcswahili.com.
12. Shindano limeanza rasmi Jumatatu, Aprili 21 2008.
13. Mwisho wa kupokea michaganuo ni tarehe 16 May 2008. Michanganuo itakayofika baada ya tarehe ya mwisho haitahusishwa kwenye shindano. Ushahidi wa kutuma mchanganuo hautatumika kama kigezo cha kupokelewa kwa mchanganuo.
14. Michuano ya kitaifa itafanyika katika wiki inayoanza Jumatatu Juni 2 hadi Ijumaa Juni 6 kama ifuatavyo:
14.1 Jumatatu Juni 02, 2008: Bujumbura, Burundi.
14.2 Jumanne Juni 03, 2008: Kigali, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
14.3 Jumatano Juni 04, 2008: Dar Es Salaam, Tanzania.
14.4 Alhamisi Juni 05, 2008: Nairobi, Kenya.
14.5 Ijumaa Juni 06, 2008: kampala, Uganda.
15. Fainali ya shindano hili itafanyika Juni, 2008.
16. Wafanyakazi wa BBC hawaruhusiwi kushiriki katika shindano kama washindani. Kila mshiriki awasilishe mchanganuo mmoja tu. Atakayewasilisha zaidi ya mchanganuo mmoja atakuwa amejiondoa kwenye shindano.
17. BBC ina haki ya kuondoa mshiriki yeyote, wakati wowote, iwapo itaona kanuni zimekiukwa.
18. Kila mshindi, atazawadiwa taji maalum. Fedha taslimu hazitatolewa. Maelezo na jinsi zawadi zitakavyotolewa yanaweza kubadilishwa wakati wowote.
19. Washindi wa pili na wa tatu, katika michuano ya kitaifa, kila mmoja, atazawadiwa cheti maalum cha kutambua ushiriki wao katika shindano hili.
20. Mshindi wa kwanza atajinyakulia zawadi ya juu kabisa katika shindano, ambayo ina thamani ya dola elfu tano za Marekani na taji maalum. Fedha zitakuwa zikitolewa kwa mujibu wa mahitaji ya bajeti. Maelezo na jinsi zawadi zitakavyotolewa yanaweza kubadilishwa wakati wowote. Zawadi hizo na fedha haziwezi kubadilishwa na kupewa mtu mwingine, na wala hakuna njia nyingine zaidi ya kupata zawadi, kinyume na maelekezo ya BBC.
21. Washindi katika ngazi zote, watajulishwa kupitia matangazo ya BBC ya moja kwa moja. Kuingia kwa washiriki katika shindano hili, kunamaanisha washindi katika ngazi zote watakuwa radhi kurekodiwa sauti na picha zao, na kurushwa na BBC duniani kote, bila ya kibali, na vile vile kutumia michanganuo yao kwa ajili ya kulitangaza shindano na BBC.
22. Kwa kuwasilisha michanganuo, washiriki wanathibitisha kuwepo kwao katika fainali zote katika shindano hili. BBC inahifadhi haki za kubadili au kurekebisha sheria hizi, au hata kufuta kabisa shindano hili iwapo italazimika kufanya hivyo.
23. Michanganuo itachanguliwa kwa njia ya usiri na majaji, na uamuzi wao ndio wa mwisho. Hakutakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kuhusu matokeo kati ya washiriki na majaji.
24. Kanuni na miongozo hii inarandana na sheria za Uingereza na mahakama za Uingereza ndio mipaka ya msingi. Kwa kuingia katika shindano hili, mshiriki atakuwa amesoma na kuelewa kanuni hizi, na kukubaliana nazo, na kuzifuata kama inavyotakiwa.
PS: Kama namna gani vipi hujaelewa na nini....nenda:
/specials/1430_faidika/index.shtml


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...