makamanda wa polisi wakingalia mataruma na vifaa vingine vya mabehewa vilivyobambwa leo
Na Anna Nkinda wa Polisi
Jeshi la Polisi Nchini kwa kupitia kikosi chake cha Reli limekamata mataruma ya reli, reli na nati zake zenye uwezo wa kujaa mabehewa sita ya gari moshi ambayo thamani yake ni zaidi ya fedha za kitanzania milioni kumi.

Mataruma hayo ya reli, reli na nati zake yalikutwa ndani ya kiwanda cha kutengenezea nondo kijulikanacho kwa jina la A.M. Steel & Iron Mills L.T.D kilichopo eneo la Mbagala jijini D’Salaam yakiwa tayari kwa ajili ya kuyeyushwa.

Kamanda wa Kikosi cha Reli Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi Yesaya Msigwa alisema kuwa alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa raia mwema zilizofanikisha kukamatwa kwa mataruma hayo.

“Ilikuwa tarehe 16/04/2008 majira ya asubuhi nikiwa katika mkutano ndipo nilipopigiwa simu na raia mwema aliyenijulisha kuwa mataruma, reli na nati hizo yaliyokuwa yamepakizwa ndani ya gari no. T. 727 AFL aina ya Fuso yalikuwa yanashushwa kiwandani hapo kwa ajili ya kuyeyushwa na kutengenezwa nondo”.


“Mimi na vijana wangu tulifika kiwandani hapo na kukuta ni kweli mataruma hayo yanashushwa ndipo tulipowakamata watu sita ambao majina yao yamehifadhiwa ilikutunza ushahidi, ambao tunawahoji na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani” alisema Kamanda Msigwa.

Kamanda huyo aliendelea kusema kuwa baada ya kuyakagua mataruma hayo pamoja na nati zake yalikutwa yameandikwa miaka na alama mbalimbali ambazo zilisaidia kugundua kuwa ni mali ya kampuni ya Reli Nchini (RAHCO) na baada ya kuwaita wataalam kutoka (RAHCO) walithibitisha ni kweli mataruma hayo ni mali yao.

Aidha Wahandisi wa Kanda ya D’Salaam Eng. Faustin Kataraia na Bw. Maizo Mgedzi kutoka (RAHCO) walisema kuwa mataruma hayo ingawa yanaonekana chakavu ni mazima kabisa na yanatumika katika njia za reli bila kufanyiwa ukarabati ingawa baadhi yamevunjika kidogo ila yakiunganishwa yanatumika bila matatizo.

“Haya mataruma, reli pamoja na nati zake yaliyokamatwa yakipangwa vizuri yanajaa ndani ya mabehewa sita na kama shirika likiamua kuuza linauza taruma moja kwa Tshs. 13,000/= hivyo tukiyahesabu na kujua idadi yake thamani nzima itapatikana ila kutokana na wingi wake tunaamini kuwa itakuwa ni zaidi ya milioni kumi za kitanzania tulizozisema”, walisema wahandisi hao.


Wahandisi hao waliendelea kusema kuwa Kampuni ya Reli Nchini imekuwa ikipata hasara ya mamilioni ya fedha kila mwaka kutokana na wizi wa mataruma ya reli na hivyo kukwamisha utendaji mzima wa shirika hilo.

Nao vibarua wa kiwanda hicho ambao walikataa kutaja majina yao kwa kuhofia kufukuzwa kazi walisema kuwa ni muda mrefu kiwanda hicho kimekuwa kikinunua mataruma ya reli, reli pamoja na nati zake ambayo inadhaniwa kuwa yanatoka Itigi na Tabora mjini na pia yameletwa kiwandani hapo na Kampuni ya Negl L.T.D iliyopo mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam.

Vibarua hao walisema, “Kwa siku si chini ya magari matatu yanaleta vyuma chakavu hapa yakiwemo mataruma ya reli, reli na nati zake, sisi kama vibarua hatuna la kusema kwani tunadhani ni mali halali kwa kuwa serikali haisemi lolote, hivi leo tumefunguliwa macho na Jeshi la Polisi baada ya kufika hapa na kusema kuwa mali hiyo ni ya wizi na ni kinyume cha sheria za Nchi kuuza mataruma ya reli pamoja na nati zake”.


Vibarua hao ambao wanafanya kazi zao katika mazingira magumu huku wakihatarisha maisha na afya zao pasipo kuwa na vifaa vya kujikinga na hatari huku wengine wakiwa vifua wazi na kuvaa kandambili miguuni kitendo ambacho kinaweza kusababisha kuungua na moto kirahisi waliliomba Jeshi la Polisi kufanya misako ya kushtukiza katika viwanda vya chuma ili waweze kukamata mataruma mengine pamoja na nati zake.

“Kuna viwanda vingi vinavyonunua vyuma chakavu yakiwema mataruma ya reli, reli na nati kama haya yaliyokamatwa hapa tunawaomba vibarua wenzetu watoe taarifa Polisi pindi watakapoona mali kama hizi zinaletwa katika viwanda vyao kwa ajili ya kuyeyushwa kwani wauzaji na wanunuzi wanahujumu uchumi wa nchi na ni kinyume cha sheria kufanya hivyo”, walisema vibarua hao.

Wakati huohuo baadhi ya wananchi wanaoishi karibu ya kiwanda hicho waliiomba serikali kuwachukulia hatua wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda ambao wanahujumu uchumi wa Nchi kwa tama ya kujipatia fedha.

“Nadhani sasa wakati umefika kwa serikali kufuatilia kwa ukaribu zaidi biashara ya vyuma chakavu kwani watu wanaharibu njia za reli na kusababisha ajali ambazo zinapoteza maisha ya watu au treni kushindwa kufanya safari zake kutokana na kuharibika kwa reli jambo ambalo linasababisha wananchi kushindwa kusafiri kwa wakati”, walilalamika wananchi hao.



Hivi sasa hapa nchini biashara ya vyuma chakavu inakuwa kwa kasi na kupelekea baadhi ya watu wenye uroho wa fedha kufikia hatua ya kuiba mifuniko ya kufunikia mashimo ya maji machafu, vibanda vya vituo vya daladala, alama za barabarani, vyombo vya nyumbani, reli, vyuma vilivyopo katika madaraja, nati za reli, misalaba iliyokuwa makaburini na mataruma ya reli kwa nia ya kujipatia fedha

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Huu nao si ufisadi!!!!Utakuta kiwanda ni cha mhindi,Au wahindi sio mafisadi???SWALI TU.

    ReplyDelete
  2. Na nyie msitutanie hapa, hivyo vyuma chakavu vinawezaje ktutumika si ndiyo maana mnatuulia watu halafu mnateuwa tume ya mafedha kibao kuchunguza wakati ajali zinasababishwa na uchakavu na uzee wa mataruma, nati na bolt.Kama mmeshindwa kukamata watu wenye mabilioni mnawafuata hao wa vijipesa vya mboga.

    ReplyDelete
  3. siyo maratuma bwana, ni mataruma, come on!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...