JK na Mama Salma Kikwete wakiwa wamefuatana na Makamu wa Rais Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere mchana wa leo wakitokea Marekani kwa ziara ya kikazi. Chini JK akiongea na D. Shein na Mh. Pinda kabla ya kuondoka uwanjani
Rais arejea baada ya ziara ya mafanikio

Na Mwandishi Maalum

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amerejea nchini leo (Jumatatu, Septemba Mosi, 2008) mchana, baada ya kumaliza ziara ya kikazi yenye mafanikio makubwa katika Marekani, kwa mwaliko wa Rais George W Bush.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar Es Salaam, Rais Kikwete amelakiwa na viongozi mbali mbali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein.

Rais Kikwete ambaye alimbatana na mkewe, Mama Salma Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na mawaziri wengine, aliondoka nchini Jumatatu iliyopita, Agosti 25, mwaka huu, 2008, kwa ziara hiyo ya kikazi.

Miongoni mwa shughuli zake kuu kwenye ziara hiyo ya siku tatu, Rais Kikwete alishiriki katika mkutano wa kutangazwa rasmi kuwa Chuo cha Kimataifa cha Wanyamapori katika Afrika (International Conservation College, Tanzania Campus) kitajegwa mjini Arusha.

Chuo hicho kitajengwa na taasisi ya kimataifa ya kutunza wanyamapori ya International Conservation Caucus Foundation (ICCF).

Rais pia alitembelea makao makuu ya Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani la USAID, ambako ilitangazwa misaada mbali mbali ya kusaidia jitihada za maendeleo ya Tanzania.

Miongoni mwa misaada hiyo ni mkopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 20 kudhamini shughuli za wakulima wadogo wadogo nchini, na msaada wa kiasi cha dola za Marekani 623, 580 kusaidia kujenga uwezo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Mkataba wa makubaliano ya msaada wa EWURA ulitiwa saini na Waziri Membe kwa upande wa Serikali, na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Biashara (USTDA), Leocardia Zak kwa niaba ya Serikali ya Marekani.

USAID pia ilitangaza msaada wa dola za Marekani milioni 1.5 kwa ajili ya kuipatia Tanzania vitabu vya kufundishia masomo ya sayansi katika shule za sekondari, na kiasi cha dola nusu milioni kwa ajili ya mafunzo ya walimu na ujenzi wa maabara tatu za kufundishia lugha ya Kiingereza.

Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Bush katika Ikulu ya Marekani.

Mazungumzo hayo yalifuatiwa na chakula cha mchana, na baada ya hapo Rais Bush alimtembeleza mwenyeji wake katika maeneo na vyumba mbali mbalui vya Ikulu ya Marekani ya White House.

Rais pia alishuhudia utiaji saini wa mkataba wa msaada ambako Marekani itasaidia ujenzi wa vituo viwili vya kisasa vya kupambana na ugonjwa wa ukimwi kwa watoto.

Vituo hivyo, vitajengwa Mwanza na Mbeya, chini ya Mpango Mahsusi wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi wa PEPFAR, utaoshirikiana na taasisi binafsi ya Baylor International Pediatric AIDS Initiative katika ujenzi huo na utoaji wa nyenzo nyingine kwa ajili ya kujenga uwezo zaidi wa Tanzania kupambana na ukimwi.

Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss-Kahn ambaye aliipongeza Serikali ya Kikwete kwa jinsi ilivyoshughulikia na kumaliza tatizo la upotevu wa fedha katika Malipo ya Akaunti ya Nje (External Payments Account –EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Strauss-Kahn alimwambia Rais Kikwete kuwa Tanzania haikuwa nchi ya kwanza kukumbwa na tatizo hilo, lakini ilikuwa imeonyesha mfano na njia kwa jinsi ilivyolishughulikia tatizo hilo.

Alisema kuwa kwa kadri IMF inavyohusika, suala hilo sasa limemalizika na ukurasa wa EPA kufungwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. Ni furaha kubwa kusikia safari ya Rais JK na ujumbe wake huko Marekani imekuwa ya mafanikio makubwa sana! Tunaomba Mwenyezi Mungu amwongezee nguvu na busara ili aweze kufanya safari nyingine nyingi kama hizo katika siku za usoni.
    Ugomvi wangu ni kauli ya IMF. Tunashukuru kusikia kuwa IMF kwa kadri inavyohusika, ukurasa wa EPA umefungwa(na bahati nzuri hizo tuliisha hakikishiwa kuwa hizo pesa hazikuwa za mfadhili wala mkopo kutoka kwao). Lakini tungependa kuihakikishia IMF kuwa kwa vile sisi Watanzania ndio tunajua uchungu wa kukwapuliwa pesa zetu na hao wenzetu wachache, ukurasa wa EPA ndio kwanza umefunguliwa upya!!!!!! Tunaifahamu vizuri IMF isivyojali maslahi ya wananchi po pote pale ilipoingiza sera zake.

    ReplyDelete
  2. hahhahaha
    ASANTE IMF yaani hapo mmewafunga pingu wale ambao kutwa kucha wanapiga hodi eti serikali ya usimamishiwe misaada. Inafurahisha kuwa mmeridhika.

    KAZI kwetu, pesa zinarudi vipi lini hiyo mapambane wenyewe

    POLE RAIS wetu kwa kazi ngumu. Mungu akutie nguvu, sasa pumzika huu ni mwezi mtukufu.

    ReplyDelete
  3. WADAU NAOMBA MSAADA WA MAWAZO, MIMI NINA RAFIKI YANGU AMBAYE NI MTU MWEMA SANA KWANI HUTUPA OFA ZA BIA TUWAPO BAA HIVYO NI MTUMIAJI MZURI WA PESA KWANI HAFUJI, LAKINI NYUMBANI KWAKE MKE NA WATOTO WAKE HAWANA CHAKULA. JE NIMLAMU KWA HILI.

    ReplyDelete
  4. shopping ya idd kwa kwenda mbele, lol, aaah kwa raha zao!!

    ReplyDelete
  5. Itifaki imezingatiwa? Naona mama salma ndiye aliyetangulia mbele badala ya Mh.Okwete katika moja ya picha hapo juu. It reminds me of Lucy Kibaki who disembarks from the plane first instead of the prezoo.

    ReplyDelete
  6. Michuzi, samahani, wakati JK anaenda Marekani na aliporudi kavaa nguo zile zile, ina maana anakuiga wewe unapovaa hiyo fulana yako?

    ReplyDelete
  7. WEWE ANONYMOUS HAPO JUU UNAEOMBA MSAADA WA MAWAZO MIMI NAKUPA HUU HAPA... WEWE NI RAFIKI MKIA WA FISI UKISHIRIKI UTAKUFILISI,KAMA KWELI WEWE UNGEKUWA NI RAFIKI WA KWELI HATA HIYO OFFER YAKE UNGEITOLEA NJE... WEWE SIO RAFIKI BALI NI MNAFIKI MPENDA VYA BURE.....HABARI NDIO HIYO!!!!!NINA HASIRA SANA NA MIJITU KAMA WEWE MNATUTESA SISI NA WATOTO.

    ReplyDelete
  8. Makamu wa Raisi, Waziri Mkuu, na Mawaziri, wote wanakwenda uwanja wa ndege kumpokea Raisi?!!

    hivi huko siyo kupoteza muda wa kazi jamani??!!

    ReplyDelete
  9. Wadau naomba mnisaidie. Mh. Rais (soma rahisi) amekwenda Marekani kwa ziara ya siku tatu. Sasa siku tatu ni zipi? Nahesabu naona rahisi amekaa nje ya nchi siku 8, kama sikosei alitumia usafiri binafsi, basi sanasana angekuwa nje ya nchi siku tano. Naomba msaada.

    Moja ya mafanikio yanazumgumziwa ni utiaji sahihi wa kuanzisha university ya wanyama pori, hilo kweli ni jambo la furaha, lakini ilibidi kweli rais aendee? Mbona hakutia sahihi yeye basi?

    ReplyDelete
  10. Ukurasa wa EPA hauwezi kufungwa rasmi na IMF!Eti nini,IMF? IMF ndiyo kitu gani kwa watanzania? IMF ndiyo iliyompigia kura Rahisi wetu aiongoze nchi? Sasa naona tumefilisika akili na mawazo pia.Msije mkadhani EPA imekwisha.No,Never!Mpaka wahusika wafichuliwe hadharani na wafikishwe mbele ya sheria.Tutamvumilia Rahisi wetu iwapo tu atawafukuza kazi wote wale ambao wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na EPA na vyanzo mbalimbali!Lakini siyo kwa kibali cha IMF,NO Please!inatosha.Pesa mchukue,basi hata akili zetu pia mzichukue msukule?Hilo halitawezekana Rahisi wetu na Wapambeez!

    ReplyDelete
  11. WEWE 12:36PM 02/09/2008 INAELEKEA DARASA LAKO LINA UTATA KUWA MAKINI KWANI HILO NI FUMBO JUU YA EPA, WAKATI JK ANASIFIWA NJE WANANCHI NDANI TUNALALAMIKA HII NI SAWA NA BABA MTOA OFA NA SIFA NYINGI NJE WAKATI MKE NA WATOTO WAKE WANALALAMIKA KWA KUKOSA CHAKULA NA WAPEWA OFA WAKIDAI KUWA SIKWELI KUWA FAMILIA YA MTOA OFA HAILISHI FAMILIA YAKE!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...