JK akisalimiana na Rais Mwai Kibaki wa Kenya huku marais wengine wakishuhudia kabla ya kuanza mkutano wao wa pamoja kati ya Comesa, sadc na Eac mjini Kampala Uganda jana

JK akihutubia katika mkutano wa pamoja wa nchi wanachama wa Comesa,Sadc na Eac mjini Kampala Uganda leo

Tanzania yapendekeza kuunganishwa Jumuia za EAC, SADC na COMESA
*Pendekezo latolewa na Rais Kikwete
*Lakubaliwa na yaamuliwe mchakato kuanza
*Nia ni kuundwa kwa jumuia moja kabambe ya uchumi

Na Mwandishi Maalum, Kampala

TANZANIA imependekeza kuunganishwa kwa jumuia tatu za uchumi na maendeleo za eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika, ili kuunda jumuia moja kubwa kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya eneo hilo. Pendekezo hilo limekubaliwa kimsingi.
Pendekezo hilo la kuunganisha Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC), Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), limetolewa kwanza na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi za jumuia hiyo uliofanyika leo, Jumatano, Oktoba 22, 2008.
Rais Kikwete pia ameshiriki katika mkutano huo kwenye nafasi yake ya Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Mkutano huo wa siku moja, wa aina yake kupata kufanyika katika Afrika, umezikutanisha nchi 26 za jumuia hizo tatu na umefanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort nje kidogo ya mjini Kampala, Uganda.
Miongoni mwa mambo mengine, mkutano huo wa leo umejadili na kufikia makubaliano kuhusu kuanzishwa kwa Eneo la Biashara Huru (Free Trade Area) katika eneo za nchi za jumuia hizo.

Mkutano huo pia umejadili mipango ya pamoja katika ujenzi wa miundombinu ikiwa ni pamoja na nchi hizo kuweka nguvu zao pamoja katika kutafuta fedha za kugharimia miundombinu ya pamoja.

Mkutano pia umejadili na kukubali kuondoa vikwazo vya kuwawezesha wananchi za nchi za jumuia hiyo kuwa na uhuru zaidi katika kuendesha shughuli zao katika nchi mbali mbali za jumuia hizo.

Baada ya kuwa ametoa pendekezo hilo kwenye hotuba yake ya ufunguzi, Rais Kikwete alirudia tena pendekezo hilo, zamu hii kwa maelezo ya kina zaidi, wakati wa mjadala baina ya wakuu wa nchi hizo.
Rais Kikwete amesema kuwa lisiwe tu jambo la kuzifanya jumuia hizo kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu zaidi, lakini nia hasa iwe ni kuunganisha jumuia hizo na kuunda jumuia hiyo moja “kabambe” kama alivyoiita mwenyewe.
“Kama mnavyojua Serikali ya Umoja ya Afrika inatakiwa kupatikana hatua kwa hatua. Na kama mnavyojua tulikubaliana kuwa jumuia za uchumi ziwe ndiyo msingi mkuu wa Serikali hiyo kwa maana ya kuziunganisha jumuia hizo hatua kwa hatua,” amesema Rais Kikwete.
Ameongeza: “Hivyo, kama nilivyopendekeza katika hotuba yangu, tufanye uamuzi wa kuunganisha jumuia zetu hizo tatu, ili tupate jumuia moja, yenye soko moja kubwa, yenye eneo moja kubwa ya biashara, yenye mfumo mmoja wa ushuru wa forodha,” amesema Rais Kikwete.
Amesema kuwa nia iwe ni kuwa na jumuia moja yenye nguvu kubwa zaidi kuliko jumuia tatu ambazo zinaonekana kufanya kazi moja na katika eneo dogo zaidi kwa kila jumuia.
Pendekezo hilo la Rais Kikwete limeungwa mkono na Mauritius, na nchi nyingine ikiwemo nchi mwenyeji wa mkutano huo, Uganda kupitia kwa Rais Yoweri Museveni.
Chini ya pendekezo hilo, sekretarieti za jumuia hizo zimepewa jukumu ya kuanda mapendekezo ya jinsi ya kutekeleza hatua hiyo.

Mapendekezo hayo yanatakiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuia hizo utakaofanyika katika miaka miwili ijayo.

Mapema akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Rais Kikwete amesema kuwa kwake yeye mkutano huo ulikuwa ni hatua ya kwanza katika kuunganisha jumuia hizo tatu na kuunda jumuia moja.

Ameongeza pia kuwa mkutano huo ulikuwa muhimu kwa sababu ni ushahidi kamili wa ukweli wa mahusiano ya kihistoria kati ya nchi za jumuia hizo.
“Ni jambo lisilo na maana wala tija kama kila moja ya jumuia zetu ikiendelea kuwa na eneo lake la biashara huru.

Napendekeza kuwa tutoke katika mkutano huu tukiwa na uamuzi wa kihistoria wa kuwa na eneo kabambe la uchumi – linatoka Cape hadi Cairo, kutoka Luanda hadi Djibout, kutoka Bandari ya Matadi hadi Bandari ya Dar Es Salaam.” alisema.

Amesema kuwa eneo la kiasi hicho la kiuchumi, lenye nchi wanachana 26, ndilo litakuwa manufaa kwa wananchi wetu kwa sababu “kama mnavyojua ushirikiano ni kuhusu watu,unaoendeshwa na watu kwa manufaa yao wenyewe watu.”
Rais pia ametaka nchi za jumuia hizo kuunganisha nguvu zao katika majadiliano kati ya nchi za Afrika na zile za Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu Makubaliano ya Kichumi ya Economic Partnership Agreements (EPA).
Kwa sababu ya nafasi yake kwenye AU, Rais Kikwete ndiye alimalizia hotuba za ufunguzi wa mkutano huo.

Wengine waliozungumza katika ufunguzi huo ni Katibu Mkuu wa SADC, Dk. Tomaz Salomao ambaye amezungumzia mchakato wa jumuia zote tatu katika kufikia kuitisha Mkutano wa leo, Naibu Mwenyekiti wa Tume ya AU, Erasto Mwencha; Rais Museveni akiwa mwenyeji wa mkutano huo na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa EAC.
Wengine walikuwa Rais Mwai Kibaki wa Kenya ambaye pia ni Mwenyekiti wa COMESA na Rais Kgalema Montlanthe wa Afrika Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa SADC.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. JK hana jipya hapo mkutanoni, wamtoe akahangaike na nchi yake, anafanya nini hapo? Hana ubavu wa kuelewa mambo wanayojadili hapo, atoke hapo. Michuzi mwambieni jamaa ngoma inamlalia, msimfiche, kaishiwa huyu!

    ReplyDelete
  2. Hivi naomba kuuliza wanauchumi. Uchumi wa USA na chi zilizoendeelea uki scrumble na wa nchi yetu unaharibika? Ni kwa nini? Mimi ninavyojua uchumi wetu muundo wake ni tofauti sana na miuchumi ya nchi hizo. Kwani siye wananchi wanategemea credits? mimi najua nchi yetu ni cash cash. Jumba lako au kibanda chako huna deni. Libiashara lako au kagenge kako kasamaki ni cash cash. Sikujua na sisi tunatakiwa kulia wakati watu wanalalia mahela yao kwenye magodoro kila siku. na sidhani hata kama kuna 0.001% ya watu wanaown stocks kweenye makampuni yeyote TZ na kam ni 401K hatuna.

    Najiuliza kwanii uchumi wa nchi zetu nao unashuka au ulishashuka siku nyingi ila tunatafuta sababu tu au ni misaada imepungua ndio maana tunapanic?

    ReplyDelete
  3. Wanataka kufanya econimic intergrations. na criteria za kurorm economic intergartion ni 1. No tarrif for goods from outsiders 2. Single tarrif for members and 3. Free mobility of factors of production. sasa hii ya tatu ndio itakuwa ngumu, yaani tuende zimbabwe au south kufanya kazi au kuwekeza. Na eti BALOZI NA ZANZIBAR ITAKUWEJE? MBONA WENYEWE KAZI KWA VITAMBULISHO? tutafika to no P.
    By Belas

    ReplyDelete
  4. Ni jambo la kusikitisha lakini yaliyopita si ndwele tugange yajayo!Wazo la kuyaunganisha Masoko ya EAC;COMESA;na SADC lilipaswa liwe limefanyika miaka mingi iliyopita!Lakini viongozi wetu wamesubiri mpaka Nchi Tajiri Duniani zipatwe na Janga la Kuanguka kwa Masoko ya Hisa na Mikopo ya Mabenki na hivyo kukabiliwa na misukosuko ya kiuchumi ndipo wakakumbuka 'SHUKA ASUBUHI'!Siyo vibaya.Lakini swali la kujiuliza hapa ni ,Je, ni wangapi kati ya viongozi hawa wenye mioyo safi na nia njema ya kutaka kuleta maboresho ya heri katika hali ya uchumi wa Afrika?Ni viongozi wangapi kati ya hao ambao wamedhamiria kwa dhati kabisa kuacha kuwa vibaraka wa nchi za magharibi?Ni kiongozi yupi kati ya hao aliefanikiwa kuikomboa nchi yake kiuchumi na kuifanya ijitegemee kwa kiasi kikubwa na washiriki wakubwa wa uchumi katika nchi yake wakiwa wazawa wa nchi ile?The word DICTATORS.Wangapi kati ya viongozi hao mwenye ujasiri wa kukiri kwamba yeye hana hata ile chembe ya Udikteta katika utawala wake katika nchi yake?Wangapi wamedhamiria kuheshimu misingi ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa na haki za binadamu?Kwanini huko nyuma yamekuwepo makundi hayo matatu ya EAC;SADC na COMESA licha ya ukweli kwamba wanachama wa jumuia hizo ni nchi majirani na Vipi tofauti hizo za kimsimamo leo ziwe zimetoweka?Je,zimetoweka kwa dhati au kwa lengo la kuwafanya raia wa kila nchi husika wasahau migogoro yao ndani ya nchi zao na kuanza kutafakari kuhusu hili suala jipya la Muungano wa Nchi hizo za kiafrika katika masuala ya biashara na uchumi KWA LENGO LA KUNUNUA MUDA? "Pupa" ni neno jingine.Ili Muungano huo uweze kufanikiwa basi ni lazima pawepo na mikakati itakayo kubalika na itakayo tekelezeka hatua kwa hatua bila ya kufanya mambo mengi kwa pamoja kwa pupa!Hakuna litakalo fanikiwa.When it comes to Redistribution of Natural Resources and Factor Reallocation,Africa is so divided much more than it were before 1884!

    ReplyDelete
  5. Afrika mikutano chungumzima lakini hakuna umoja. Tangu enzi za OAU na sana AU, hakuna cha maana kilichotendeka. Sababu kubwa ni kwamba karibu viongozi wote wa Afrika hawaheshimu haki za binadamu na wanaongoza kwa nguvu miaka chungumzima. Tunamwongelea Gadhafi wa Libya, Museveni wa Uganda, Wafalme wanaotumia nguvu huko Morocco, Mubarak wa Egypt, na kadhalika.

    Sisi wananchi wa Afrika, katutegemei kitu chochote mpaka viongozi hawa wakifa na kuwapa nafasi viongozi wengine wanaojua kutetea haki za wananchi na wenye nia ya kuleta maendeleo. Kuwa kiongozi kijana peke yake haitoshi, angalia Raisi Kabila wa DR Congo, anavaa suti za bei mbaya, alikuwa kijana bila ya elimu yoyote Tanzania wakati baba yake marehemu amepewa hifadhi Tanzania, leo anakula na wanajeshi mali ya nchi wakati mamilioni wanateseka na vita na njaa.

    Watawadanganya wasiokuwa na elimu, lakini watu wengi wanajua viongozi Afrika hatuna na ni sababu kubwa ya umasikini wetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...