Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Bwana Shanes Martin Nungu akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika uwanja wa michezo wa Mkwakwani Tanga leo wakati wa kilele cha sherehe za kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
Kijana Safari Antony kutoka Geita Mwanza akimweleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete matumizi ya mashine ya kukobolea mahindi aliyoitengeneza na kuileta kwa maonesho katika viwanja vya Tangamano,mjini Tanga katika kilele cha sherehe za Mwenge wa uhuru zilizofanyika kitaqifa mkoani Tanga

Kiwanda kipya chaanza kujengwa Tanga, bei ya saruji kuporomoka
Na Mwandishi Maalum, Tanga

UHABA wa saruji na bei kubwa za bidhaa hiyo nchini vinatarajiwa kuwa historia katika miaka miwili ijayo, kufuatia kuanza uzalishaji wa kiwanda kipya cha saruji ambacho ujenzi wake umeanza leo (Jumanne, Oktoba 14, 2008) katika eneo la Maweni, Tanga.

Ujenzi huo umeanzishwa leo na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika sherehe ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho kitakachoanza uzalishaji Oktoba, 2010,
na kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 4,000 kwa siku. Ujenzi huo utachukua miezi 24.

Kiwanda hicho kinajengwa na Kampuni ya Athi River Mining Ltd (ARM) yenye makao yake nchini Kenya, na kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi kuliko kingine chochote cha uzalishaji saruji katika eneo la Mashariki mwa Afrika kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,500,000 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Pradeep Paunrana amemwambia Rais Kikwete kwenye sherehe hiyo:
“Kupitia uzalishaji huu wa tani 4,000 kwa siku, tunapenda kukuhakikishia kwamba uhaba wa saruji litakuwa ni historia, bei zitakuwa za ushindani na zitakuwa bei halisi badala ya bei za sasa za saruji zinazoongozwa na uhaba wa bidhaa hiyo.”

Mkurugenzi huyo amesema kuwa kampuni yake ambayo imekuwa na shughuli nchini kwa miaka sita iliyopita, imevutiwa kuwekeza zaidi katika uchumi wa Tanzania kutokana na kugundua mvuto wa uchumi huo.

“Mheshimiwa Rais, baada ya kuwa tumeonja utamu wa uchumi wa Tanzania, na maisha yanayozidi kuwa bora kila siku kwa kila Mtanzania, lilikuwa ni jambo la dhahiri kabisa kuingia katika uzalishaji wa saruji hapa nchini,” amesema Praunrana.

ARM ambacho kwa miaka sita iliyopita imekuwa inazalisha chokaa inayotumiwa katika uchimbaji madini nchini, inazalisha bidhaa za viwandani katika Afrika Kusini, Zambia na Kenya, ambapo kampuni hiyo pia inazalisha saruji.

Mkurugenzi huyo amemwambia Rais Kikwete kuwa ARM imeamua kuwa uzalishaji wote wa siku ya kwanza Oktoba 2010, yaani tani 4,000 ama malori 125 ya saruji, itatolewa yote kwa Rais Kikwete ambaye ataamua kuitumia atakavyo kwa miradi ya kijamii aitakayo.

Kiwanda hicho kipya kitaifanya Tanzania kuwa nchi pekee katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika kuwa na viwanda vinne vya saruji.

Viwanda vitatu vilivyoko kwa sasa ni Tanzania Portland Cement Company (TPCC) ama Twiga Cement cha Dar Es Salaam, Simba Cement cha Tanga na Mbeya Cement cha Mbeya.
TPCC ndiyo kiwanda cha kwanza cha saruji Tanzania kilichofunguliwa Agosti 8, mwaka 1966 na Baba wa Taifa, Mwalimu JK Nyerere.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo ya leo, Rais Kikwete ameipongeza ARM kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika uzalishaji wa saruji ambao sasa utaiwezesha Tanzania kuzalisha tani 3,000,000 kwa mwaka baada ya kuwa kiwanda hicho kimekamilika katika miaka miwili ijayo.
Pamoja na kwamba uzalishaji saruji nchini umekuwa unaongezeka, bado uwiano wa saruji na idadi ya wananchi wa Tanzania umebakia ndogo.

Amesema kuwa mwaka 2005 wakati wananchi wa Tanzania wanakadiriwa kufikia milioni 37, matumizi ya saruji yalikuwa sawa na kilo 37 kwa kila Mtanzania kwa mwaka.

“Matumizi haya bado ni madogo ikilinganishwa na matumizi ya saruji nchini Kenya ambayo ni wastani wa kilo 56 kwa mtu mmoja kwa mwaka. Nchini Afrika Kusini, matumizi haya yanafikia wastani wa kilo 400 kwa mtu mmoja kwa mwaka.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. He! Mhishimiwa Misupu kumbe mwenge wa Uhuru bado upo!! Naona bora sasa wauite mwenge wa Ufisadi maana umepoteza mwelekeo wake. Zamani tulikuwa tunaimba shuleni "Sisi tumekwisha uwasha mwenge....Pale ambapo hakuna matumaini, ulete tumaini".Yako wapi matmaini, uko wapi upendo n.k kama watu hawawajali wenzao. Wanatenga bajeti kwaajili ya kukimbiza mwenge wakati hakuna la maana linalofanyika zaidi ya kugawana hizo fweza.Kila kiongozi anayekuja madarakani tunazani atakuwa mzuri, kumbe afadhali wa jana.Basi kama mwenge unamurika uanzie kuwamurika mafisadi wote uwapandishe juu ya mlima Kilimanjaro na kuwatupa makorongoni waka$??*#e mbali.Maana wananikera sana.
    Mdau, Cardiff

    ReplyDelete
  2. HUYU KIJANA KAFANYA KAZI KUBWA SANA. LAKINI HAWEZI KUPATA HATA SENTI MOJA KUTOKA KWA JAKAYA. NCHI ZA WAKWELI ANATUZWA KAMA MILLION 100 YA KUIPELEKA JAPAN AU CHINA KWA UCHUNGUZI ZAIDI, KISHA ANAPATA WAHANDISI AMBAO ATASHIRIKIANA NAO KUIBORESHA HII MASHINE. BAADA YA HAPO ATAWEZA KUINGIA MKATABA NA KIWANDA CHA KUTENGENEZA MASHINE KAMA HIZO KWA KIWANGO CHA JUU ZAIDI NA WATATENGENEZA MASHINE NYINGI. KIJANA ATAFAIDIKA KUWA MILIONEA NA TANZANIA ITAPATA SIFA KWANI MASHINE ITAWEKEWA ALAMA INAYOSEMA" MADE IN TANZANIA" ASSEMBLED IN JAPAN OR CHINA.
    THANKS
    MAWAZO!!!

    ReplyDelete
  3. HII NI HADITHI, HAIWEZEKANI NA ITASABABISHA SARUJI KUPANDA BEI KWA VISINGIZIO VIPYA VITAKAVYOANZISHWA, IKIWA MAFUTA, UMEME GHARAMA ZA UENDESHAJI NA KUPANDA KWA BEI YA SARUJI DUNIANI! TUMEZOWEA AHADI FEKI KWANI MITAMBO YA KUZALISHA UMEME NAYO TULIAMBIWA HIVYOHIVIVYO LAKINI SASA TUKO WAPI.

    ReplyDelete
  4. HUU MWENGE UNA FAIDA GANI KWA NCHI YETU. MBONA MIMI SIONI UMUHIMU WAKE ZAIDI YA KUGHARIMU MAMILIONI YA PESA AMBAZO ZINGEWEZA KUTUMIKA KWA SHUGHULI MUHIMU ZA KUSAIDIA JAMII? KUNA MTU YE YOTE ANAFANYA HESABU YA GHARAMA ZAKE (MAGARI MENGI YA SERIKALI YANAYOTUMIKA, GHARAMA ZA MAHOTELI NA MINUSO,WAKATI MWINGI NA MASAA YA KAZI YANAYOPOTEZWA)

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...