

Matembezi ya Hiari Kwa Ajili ya Changizo ya Saratani ya Matiti
Jumapili hii, tarehe 19 Octoba, kutakuwa na matembezi ya hiari yatakayoendeshwa na Taasisi ya Saratani ya Matiti Tanzania ili kuchangisha fedha kwa ajili ya wanawake walio na saratani ya matiti.
Matembezi haya ya “Kwa Pamoja Tuna Piga Mbio Kutafuta Tiba” yatakuwa ya kilomita 5, na yataanzia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja na kupita kwenye jiji la Dar es Salaam hadi kuishia kwenye Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Tunategemea kupata takriban watembeaji elfu moja (ukijumlisha wanaume, wanawake na watoto) ambao wanategemewa kutoa au kuahidi fedha kutegemeza kazi hii muhimu.
Taasisi hii inategemea kuchangisha si chini ya shilingi milioni 50 kupitia ahadi, fedha ambayo itatumika kwa ajili ya matibabu ya saratani kwa wanawake wasio na uwezo wakulipa.
Mfuko wa Susan G. Komen Kwa Ajili ya Tiba ni asasi ya saratani ya matiti iliyo na mizizi na mafanikio makubwa kule Marekani na imesaidia kuratibu na kufadhili shughuli hii. Wajumbe kutoka Komen watakuja kushiriki katika matembezi haya kutoka Marekani, pamoja na muigizaji maarufu wa kike, Gabrielle Union.
Kwenye mkutano baina ya waandishi wa habari ulioandaliwa leo na Hoteli ya Southern Sun jijini Dar es Salaam, Angela Kuzilwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Matiti Tanzania alisema, “Tunakunjua mikono yetu kwa wananchi wa Dar es Salaam ili waje kushiriki nasi katika matembezi haya maalum siku ya Jumapili.
Watieni moyo marafiki na ndugu zenu ili wawachangie fedha kwa ajili ya matembezi haya, hata kama ni kidogo tu, kwa sababu kwa pamoja tunazeza kuanza kuleta tofauti kwa maelfu ya wanawake Tanzania walio na saratani ya matiti lakini hawana namna ya kupata msaada.”
Gharama za kumtibu mtu mwenye saratani ya titi (ambayo inaweza kujumlisha garama za upasuaji, miezi kadhaa ya tiba ya saratani kwa kutumia dawa/chemotherapy, na pia, muda wa kutumia tiba ya miyonzi/radiotherapy) zinaweza kufikia shilingi za Kitanzania milioni moja, laki tatu na hamsini elfu (Tshs. 1,350,000) kwa kutegemea mazingira, garama ambazo asilimia kubwa ya wanawake wanashindwa kumudu.
Mama Kuzilwa aliendelea kusema, “Hapa tulipo, kwa mwaka tunaweza kupata wanawake wasiopungua 250 wanaofika Taasis ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya tiba. Kama tunaweza kuwachangia kiasi kisichopungua Tshs. 50 milioni tunaweza kuongeza idadi hii kwa asilimia ishirini mwaka ujao kwa kupitia mioyo ya kujitoa na bidii ya wale watakaoshiriki matembezi haya. Matembezi ya kilomita tano yanaweza kuleta tofauti kati ya uzima na mauti kwa mwanamke mwenye saratani ya matiti.”
Naye Mkurugenzi Mkuu wa hoteli ya Southern Sun, Nd. Adam Fuller, ambaye amekuwa mfadhili wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa muda mrefu alisema, “Tumefurahi sana kuandaa mkutano baina ya waandishi wa habari kwa ajili ya Taasisi ya Saratani ya Matiti Tanzania. Saratani ya matiti inaweza ikamshika mwanamke yeyote, pamoja na kuathiri wanaume wote kwa sababu sisi sote tuna mama, dada, wake na watoto wa kike.
Kama mashirika ya biashara lazima tutambue jukumu letu la kusaidia kuamsha jamii juu ya ugonjwa huu ili kwa mfano, hata wanawake tunaofanya nao kazi maofisini wajue ni nini cha kuchunguza katika miili yao na wafanyeje baada ya hapo.”
Inakadiriwa kuwa nchini Tanzania wanawake 2,500 kwa mwaka wanajisajili kwenye mikoa yote nchini kama wagonjwa wa saratani ya matiti. Hii ni asilimia ndogo sana ya wanawake walio na ugonjwa huu tayari. Asilimia yao kubwa huenda hawatambui kwamba wana saratani, hawana uwezo wa kupata tiba inayostahili ugonjwa huo na
huenda pia hawana hata nyenzo za kuwasaidia kupata msaada. Wengi wanakufa kwa upweke na maumivu makali kwa sababu hawana dawa za kupunguza maumivu na wengine wanakuwa tayari wamekwisha tengwa na familia zao.
Taasisi ya Saratani ya Matiti Tanzania ilianzishwa mapema mwaka huu ili ianze kushugulikia masuala kama haya, pamoja na kuanda mahali pa kukimbilia na kituo cha kutoa maelezo na misaada ya kimawazo au hisia kwa wagonjwa. Sababu ingine ya kuanzishwa kwa taasisi ni kwamba iwe na uwezo wa kuamsha jamii, na kushirikiana na wenzetu wenye taaluma ya tiba ili kusaidiana kuendeleza huduma kwa ajili ya wanawake wenye saratani ya matiti.
Matembezi haya ya “Kwa Pamoja Tuna Piga Mbio Kutafuta Tiba” yataanzia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jumapili hii, tarehe 19 Octoba, saa moja na nusu asubuhi. Wenye shauku ya kushiriki matembezi haya ambao bado hawajajisajili wanakaribishwa sana kujisajili siku iyo hiyo ya matembezi, wakileta ahadi za fedha zisizopungua Tshs. 25,000.
Matembezi haya yameandaliwa na Taasisi ya Saratani ya Matiti Tanzania na kutegemezwa na taasisi, asasi na mashirika yafuatayo: Mfuko wa Susan G. Komen Kwa Tiba, Hoteli ya Southern Sun, Ford Motors, Foundation for Civil Society, Monier 2000, Jamana Printers, Resolute Mining, Silver Bullet PR na IPP Media.
Kwa ajili ya taarifa za nyongeza, tafadhali wasiliana na:
Angela Kuzilwa, Executive Director
0784 443484
dats my gal... 4sho will be there kwenye hako ka-walk.... oohh god, my moyo is bouncing as twice as normal.
ReplyDelete