KIKWEKWEREKWE
Hodi hodi blogini kaka michuzi naingia
Mimi wako muhisani ujumbe nakuletea
Kufuga nimetamani kuku ninawatajia
kaka kwako kweli kiko kikuku kikwekwerekwe.
Kama hakipo nyumbani basi chukuwa hatua
Wasomi nipatieni kama mtajionea
Kokote kitafuteni kikuku nahitajia
kaka kwako kweli kiko kikuku kikwekwerekwe.
Nimeshinda vijijini kikuku naulizia
Kikokoriko jamani kisiwe chenye udhia
Manyanyu kwangu sifani msije kuniletea
kaka kwako kweli kiko kikuku kikwekwerekwe.
Kishingo pia sidhani kama kweli kitafaa
Sikutumwa ugangani kufuga nimeamua
Ukweli nimetamani nasina nyengine njia
kaka kwako kweli kiko kikuku kikwekwerekwe.
nilijaribu zamani boi nikajifugia
wakangia maradhini mafua kuwaumbua
wakafa wote kwanini nimebadilisha nia
kaka kwako kweli kiko kikuku kikwekwerekwe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Ama kweli Michuzi wadau umepata !! Dada yetu si useme tuu unatafuta Rijali , na utowe picha yako sisi hatujui hicho cha kwanza kwa nini kiliumwa mafua. Sema nakusifu kwa Usanii shairi limetulia.

    ReplyDelete
  2. Kikuku cha namna gani, bora Jongwe jifugia
    Atawika mtaani, Kuchi mbegu maridhia
    Kidume cha fani, na masubwi ayajua
    kwani unashida gani, spring chicken kulilia?

    Kuchi yuko makini, si rahisi kukimbia,
    Aina ya bukini, ni wazuri kwa tabia,
    bara na visiwani, waheshimika sawia
    Atawika mtaani, mbegu maridhia.

    Vikuku taabani, nguvu pumzi huwaishia,
    Siha yao matatani, sote twawaharumia
    Kuchi wa bukini, kama punda milia
    Musuli imesheheni, hakika utafurahia.

    Vumilia jamani, kuchi utajipatia
    Subiri hata mwakani, ogopa kiruka njia
    Kunguru sije tamani, mwanzo kuangamia
    kikuku cha nini, Kuchi utajipatia?

    ReplyDelete
  3. KIKWEKWEREKWE ??!!!

    Karibu blogini hadi barazani ingia
    Sisi wako wahisani ujumbe tumepokea
    Kufuga umetamani kuku umetutajia
    Kama kweli kiko kikuku kikwekwerekwe?.


    Utakipata bwawani, kama umedhamiria
    Wasomi blogini, mada wameistukia
    Imeingia akilini, kikuku wahitajia
    kama kweli kiko, kikuku kikwekwerekwe?.

    Umeshinda vijijini, kikuku kukiulizia
    Kikuku makini, kisije leta udhia
    Hutaki purukushani miwaya kukuletea
    Kama kweli kiko kikuku kikwekwerekwe?.


    Kwa sura usidhani, kama kweli maridhia
    Si elimu au fani, huwezi kutambua
    Ukweli kwa darubini,hakika utajua
    Angaza kwa Salmini, Amrefu jipimia
    Hapo ndo yakini, kikwekwerekwe kungamua

    Usijaribu kizamani, sura kutangulia
    Au tajiri mjini, jina zuri kuvutia
    Taingia maradhini mafua kujiuumbua
    Mauti harakani, hatari kukurubia
    Yataka ndo yakini kikwekwerekwe kungamua.

    '''Mdau Bonde la Mpunga'''

    ReplyDelete
  4. hayo maoni ma3, hujaridhia?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...