JK akifungua mkutano mkuu wa saba wa umoja wa wazazi kwenye ukumbi wa Kilimani mjini dodoma leo. Shoto ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa anayemaliza muda wake, Mh. Athumani Mhina na kulia ni mkuu wa mkoa wa dodoma Dk. James Msekela.

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE
UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA SABA WA JUMUIYA
YA WAZAZI YA CCM , DODOMA, 6 JUNI 2009

Ndugu Athumani Mhina, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa;
Ndugu Khamis Suleiman Dadi, Makamu Mwenyekiti wa Wazazi Taifa;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa;
Ndugu Badru Bushako, Kaimu Katibu Mkuu wa Wazazi;
Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Umoja wa Wazazi;
Wageni Waalikwa wenzangu;
Mabibi na Mabwana:

Naomba nianze kwa kukushukuru sana wewe Mwenyekiti na viongozi wenzako kwa heshima kubwa mliyonipa kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Taifa wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ya CCM. Nawashukuru pia kwa kunipokea na kunikaribisha vizuri. Nakupongezeni pia kwa kufanikisha Mkutano wenu. Najua haikuwa kazi rahisi kama ilivyokuwa kwa Jumuiya zetu zote. Aidha, nawashukuru kwa maelezo yenu ya utangulizi na hotuba yako, Ndugu Mwenyekiti, iliyosisimua ukumbi.
Ndugu Wajumbe;
Mkutano huu, pamoja na kujadili taarifa ya kazi za Jumuiya kwa kipindi cha miaka mitano, unayo agenda muhimu ya kukamilisha safu ya uongozi wa Jumuiya ya Wazazi kwa kufanya uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya Taifa. Nawapongeza viongozi wote waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wa Jumuiya hii katika ngazi mbalimbali kuanzia kwenye matawi hadi Mikoani. Nawapongeza kwa ushindi. Hongereni sana. Nawapa pole kwa misukosuko mliyopitia maana siku hizi uchaguzi ni vita. Nawaomba mchape kazi ya kujenga Jumuiya yenu na kukipigania Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Hii ni fursa yenu ya kujipatia viongozi wazuri katika ngazi ya taifa. Watu ambao wataitoa jumuiya yenu hapa ilipo sasa na kuipeleka kwenye maendeleo makubwa. Watu ambao watasaidia kuleta utulivu na kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama, miongoni mwa viongozi na miongoni mwa watendaji.
Naomba mkumbuke kuwa katika miaka mitano hii jumuiya yenu imepita katika mtikisiko mkubwa. Katika kipindi hicho, watu wanne wamekalia kiti cha Katibu Mkuu, wawili wamekalia kiti cha Makamu Mwenyekiti na wawili tena kiti cha Mwenyekiti. Hii ni rekodi ya aina yake. Hakuna jumuiya nyingine iliyopita katika misukosuko ya namna hiyo. Uchaguzi mtakaoufanya leo ndiyo utakaoamua kama mnajitoa kwenye migogoro au mnajirudisha kule mlikokuwa. Chagueni kutoka kule.

Ni matumaini yangu kwamba sasa tutatumia fursa hii ya kupata uongozi mpya, ulio mzuri, adilifu, na unaoijua vyema Jumuiya ili kufungua ukurasa mpya katika uhai wa Jumuiya yetu hii muhimu. Napenda kuwatakia heri katika kazi hii muhimu.

Siku zote, kwetu sisi katika CCM, uchaguzi ndani ya Jumuiya zetu, kama ilivyo kwa Chama chenyewe, ni fursa ya kujiimarisha. Ninaamini kabisa kwamba mtauchukulia uchaguzi huu kwa uzito unaostahiki ili kuiimarisha Jumuiya ya Wazazi.
Wajibu wa Jumuiya
Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Wajumbe;
Kama nilivyopata kueleza huko nyuma, Jumuiya za Chama zipo kwa ajili ya kukisogeza Chama karibu zaidi na makundi mbalimbali ya watu katika jamii ya watu na nchi yetu. Jumuiya zinalo jukumu la msingi la kukipatia Chama cha Mapinduzi, wanachama, marafiki, wapenzi, washabiki na wapiga kura katika makundi hayo. Jumuiya ya Wanawake inao wajibu huo miongoni mwa Wanawake, Jumuiya ya Vijana miongoni mwa Vijana na Jumuiya ya Wazazi miongoni mwa Wazazi.

Kwetu sisi katika Chama, na hata kwenu nyinyi wenyewe, kipimo cha mafanikio ya Jumuiya yenu ni kwa kiasi gani mmefanikiwa au mnafanikiwa katika kutekeleza jukumu lenu hilo la msingi. Hii ni Jumuiya ya Chama cha siasa ambacho lengo lake la msingi ni kushinda uchaguzi wa dola ili kuongoza Serikali na taifa. Jukumu la msingi la kila jumuiya ni kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kufanikisha lengo hilo kwa jamii ya Watanzania inayowajibika nayo. Hakuna zaidi, hakuna pungufu.

Ndugu Wajumbe;
Kwa maoni yangu, katika Jumuiya zote za Chama, Umoja wa Wazazi unayo fursa kubwa zaidi ya kuwa na nguvu zaidi kuliko Jumuiya nyingine kwa sababu wigo wake wa kupata wanachama ni mpana zaidi. Jumuiya ya Wanawake upeo wake wa kupata wanachama ni Wanawake tu, siyo wengine. Hivyo karibu nusu ya Watanzania hawawezi kuwa wanachama wa UWT. Jumuiya ya Vijana ina masharti ya umri kwa wanachama wake. Ni lazima uwe na miaka kati ya 14 na 35. Hii inaondoa uwezekano wa asilimia kubwa sana ya Watanzania kuwa wanachama wa UVCCM.

Lakini, kwa Jumuiya ya Wazazi, Mtanzania yoyote aliyefikisha umri wa miaka 18 anaweza kuwa mwanachama. Tena sio lazima awe mzazi. Kwa misingi hiyo, Jumuiya yetu hii ingekuwa ndiyo kubwa kuliko zote na kiongozi wa jumuiya zote. Hata hivyo, ukweli hauko hivyo.
Kwa vigezo vya idadi ya wanachama, na kwa msisimko na harakati za chaguzi za dola, katika Jumuiya zetu tatu za CCM, inaonyesha kwamba Jumuiya hii iko nyuma kwa wanawake na vijana. Inaelekea kuwa ndiyo yenye wanachama wachache zaidi na haijafanikiwa kujitokeza katika jamii kama nguvu kubwa ya kutumainiwa kisiasa. Lazima mjiulize kwanini? Pia mjiulize mtafanya nini kuibadili hali hiyo?
Ndugu Wajumbe;
Mambo kama haya ndio yanazua mjadala na maswali miongoni mwa baadhi ya watu katika Chama chetu na jamii kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa Jumuiya hii. Nyie ndio wenye Jumuiya. Nawaomba muitafakari hali hii kwa dhati na muipe uzito unaostahili. Ni muhimu sana, ndugu zangu, kupata majibu mazuri kwa maswali na hisia hizi kuhusu Jumuiya yetu hii.
Ndugu zangu;
Mawazo hayapigwi rungu bali hushindwa na mawazo yaliyo bora zaidi. Pingeni kwa hoja na vitendo hii dhana ya kwamba Jumuiya ya Wazazi ipo ipo tu. Kuna mawazo kwamba wanaonufaika ni watendaji wa Jumuiya waliopata ajira na viongozi wake waliopata fursa za uwakilishi au ushiriki kwenye vikao vya Chama. Tunatetea lakini lazima na nyie muonekane na msikike. Nawaomba sana msiyapuuze haya ninayosema kwasababu mjadala huo upo na wakati mwingine mimi nimekuwa nauzima lakini sijafanikiwa kuunyamazisha.

Suala la Elimu
Ndugu Wajumbe;
Mbegu iliyozaa Jumuiya yetu hii ilipandwa wakati wa harakati za kupigania uhuru. Chama cha TANU kwa nia ya kuwapitia fursa ya elimu watoto wa Waafrika waliokuwa wanabaguliwa na mfumo wa kikoloni, ilianzisha Tanganyika African Parents Assocation kwa kifupi TAPA. TAPA ilijenga shule za msingi ambazo walisoma watoto wa Kiafrika walionyimwa fursa ya elimu hiyo. Ilifanya kazi nzuri wakati ule wa kudai uhuru na hata baada ya uhuru wakati ambapo shule za msingi zilikuwa hazijaenea sana nchini. Bila ya shaka baadhi ya wajumbe wa Mkutano huu wanaweza kuwa wamepata elimu yao ya msingi kwenye shule za TAPA.
Miaka kadhaa baada ya Uhuru na hasa baada ya Azimio la Arusha na vuguvugu la maendeleo vijijini, shule za msingi zikaenezwa karibu kila kijiji. Wakati huo Jumuiya yetu ikafanya uamuzi wa kuacha kushughulika na elimu ya msingi. Ikakabidhi shule zake kwa Serikali na kuelekeza nguvu zake katika kuendeleza ya elimu ya Sekondari. Kwa muda mrefu sasa, Jumuiya ya Wazazi imekuwa ikijenga, kumiliki na kuendesha shule za Sekondari katika mikoa mbambali nchini. Naambiwa kwamba Jumuiya yetu ina shule za sekondari 70 kote nchini.

Ndugu zangu;
Hivi sasa, mazingira ya utoaji wa elimu ya Sekondari nchini, na hasa umilikaji na uendeshaji wa shule za Sekondari, yamebadilika sana. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kumekuwepo na ushindani mkubwa kutoka sekta binafsi na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutoka Serikalini.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la shule za sekondari za Serikali kutokana na ujenzi wa sekondari za kata kwa kushirikiana na wananchi. Matokeo yake ni kuongezeka sana kwa shule za sekondari nchini za watu binafsi na Serikali.
Kwa mfano, kuanzia mwaka 1999 hadi 2008, shule za Sekondari zisizo za Serikali zimeongezeka kutoka shule 382 hadi shule 759 sawa na asilimia 98% wakati shule za Sekondari za Serikali zimeongezeka kutoka 444 hadi 3,039 ikiwa ni ongezeko la asilimia 584% .

Ndugu Wajumbe;
Mafanikio haya makubwa ni matokeo ya sera nzuri na msukumo mkubwa wa Serikali ya CCM kwenye elimu iliyofungua milango ya ushiriki wa watu binafsi na wa wananchi kwa kushirikiana na Serikali.

Kutokana na kuongezeka sana kwa shule za sekondari za Serikali, kitu ambacho bado kinaendelea, biashara ya elimu ya Sekondari iliyokuwa nzuri sana wakati ule shule za Serikali zilipokuwa chache sana nchini, sasa siyo nzuri tena. Wapo watu binafsi kadhaa wenye shule binafsi za sekondari ambao wameanza kupata matatizo ya kupata wanafunzi na walimu. Wamekuwa wanashindwa kulipa mikopo waliyokopa kutoka kwenye mabenki.

Matatizo haya yameibuka na kushamiri baada ya kuanza kuenea sekondari za kata. Hali itazidi kuwa mbaya siku za usoni pale shule hizo zitakapozidi kuongezeka na kuimarika kwa walimu na vifaa vya kufundishia ikiwa ni pamoja na vitabu na maabara za masomo ya sayansi. Shule za watu binafsi na zile za taasisi na za Jumuiya yetu zitazidi kupata ugumu wa uendeshaji na kupata wanafunzi na walimu.

Wapo watu binafsi ambao wameomba Serikali kuzichukua shule zao. Wapo pia, walioomba Serikali kuchukua sehemu ya gharama za uendeshaji hasa mishahara ya walimu. Zipo taasisi ambazo tayari zimeshakabidhi shule zao Serikalini. Kwa mfano, Mufindi Education Trust na Mbinga Education Trust wamekabidhi shule zao kwa Serikali.

Ndugu Wajumbe;
Hali hii ya ugumu wa uendeshaji wa shule pia imezikumba shule za Sekondari za Wazazi. Zipo shule za Jumuiya yetu ambazo zinapata taabu ya kupata wanafunzi na walimu. Madeni nayo yanazidi kuwa makubwa. Hadi sasa, shule zetu zinadaiwa jumla ya shilingi bilioni 3.3. Deni hili ni kubwa na linaendelea kukua. Sote tunajua ukweli kwamba, kwa hali ya sasa ilivyo katika Jumuiya yetu kulilipa deni hili ni tatizo gumu sana.

Ndugu zangu;
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kwa nyakati mbalimbali imejadili hali ya Jumuiya ya Wazazi na uendeshaji wa shule za sekondari. Vikao hivyo vya juu vya Chama chetu vilifikia uamuzi kuwa wakati umefika Jumuiya yetu iache kujihusisha na umilikaji na uendeshaji wa shule za sekondari. Nyakati zimebadilika. Ukweli ni kwamba yale mazingira yaliyoifanya Jumuiya ya Wazazi kuachana na kujihusisha na shule za msingi yamejirudia kwa shule za Sekondari.

Wananchi wamehamasika na kupanua elimu ya sekondari hivyo wamejitokeza kwa wingi kuchangia ujenzi wa shule za Sekondari na hali hiyo haitarudi nyuma. Jumuiya yetu haina uwezo wa fedha na rasilimali kushindana na kushinda katika mazingira haya. Hivyo lililo la busara kufanya ni kujitoa sasa kabla mzigo wa uendeshaji na hasa madeni hayajatuelemea na kugeuka kuwa aibu kwa Jumuiya na kashfa kwa Chama mbele ya wananchi.
Hatari iliyo mbele yetu ni dhahiri, si jambo la kughushi. Jambo la busara kufanya kwa upande wetu ni kusoma alama za nyakati na kuchukua hatua muafaka kama tulivyofanya kwa elimu ya msingi tulipojitoa.

Ndugu Wajumbe;
Najua zipo hisia miongoni mwa baadhi yetu za kutopendezwa na uamuzi huu wa Chama. Sipendi Jumuiya yetu hii ikawa mfano wa msemo wa wahenga wa “asiyesikia la mkuu, mguu huota tende”. Nawasihi ndugu zangu tuelewe kwamba uamuzi huo umefanywa kwa nia njema. Haukuwa rahisi lakini ilikuwa hapana budi baada ya kuangalia mbali na kuwa wa kweli kwa hali halisi na mazingira tuliyonayo sasa na mwelekeo wa kule tuendako.
Kwa maoni yangu, Jumuiya yetu haina sababu ya kujisikia vibaya kuachia shule za sekondari. Badala yake tunatakiwa kuufurahia na kuupokea kwa moyo mkunjufu uamuzi huo kwani inathibitisha kuwa malengo yetu yametimia.
Kama tulivyofanya kwa elimu ya msingi, ambapo tulikabidhi shule zetu baada ya kuona kuwa Serikali inatimiza ipasavyo wajibu wake, tufanye hivyo kwa Sekondari. Kuna ushahidi kwamba Serikali imezinduka na kufanya yale yaliyotufanya tujenge na kuendesha shule za Sekondari.

Sasa Serikali na wananchi ambao ndiyo Wazazi wenzetu wamepokea vyema mwito wetu na shule nyingi zimejengwa na zinaendelea kujengwa. Shabaha yetu ya kutaka watoto wetu wengi wapate elimu ya sekondari imetimia. Sasa ni wakati muafaka wa kuiachia Serikali iendelee kama tulivyofanya kwa elimu ya msingi miongo miwili iliyopita.

Ndugu wajumbe;
Imezungumzwa hapa kwamba tusifanye makosa kama ya siku za nyuma ya kukabidhi mali za Chama Serikalini. Ndugu zangu hakuna aliyetoa uamuzi wa kukabidhi bure mali za Chama na Jumuiya kwa Serikali. Mali hizo zitakabidhiwa kwa kulipiwa thamani halisi ya majengo na vifaa. Hivyo Jumuiya haitakula hasara. Italipwa malipo stahiki na itazitumia fedha hizo kwa kufanyia shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na kuwa na miradi ya kiuchumi.

Malezi ya Vijana
Ndugu Wajumbe;
Napenda pia kuitumia nafasi hii kuwasihi viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wazazi kutambua kuwa tunazo shughuli nyingine nyingi muhimu za kufanya zaidi ya kumiliki na kuendesha shule za sekondari. Tunayo kazi muhimu ya malezi ya vijana wetu. Jumuiya yetu, sasa ielekeze nguvu zake katika kukabiliana na matatizo ya mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana wetu na jamii kwa jumla. Tujikite katika kujenga na kuendeleza malezi mema kwa vijana wetu ili wawe raia wema na wenye tija kwa jamii.

Sote ni mashahidi kwamba jamii yetu nchini inakabiliwa na matatizo makubwa sana ya kuongezeka kwa matukio ya kukosa uadilifu miongoni mwa vijana wetu: utovu wa nidhamu, kukosa heshima, matumizi ya madawa ya kulevya, uzururaji, na tabia nyinginezo zinazoenda kinyume na maadili yetu ya Kitanzania.
Jumuiya ya Umoja wa Wazazi inao wajibu maalum na ningependa kuona kuwa inaifanya kazi hii kwa vitendo, sio kwa maneno. Lazima Jumuiya yetu ionekane kufanya kazi hii ndani ya jamii. Ipo kiu kubwa ya kazi hiyo kufanyika na ni kilio cha wengi: wakubwa kwa wadogo, wanawake kwa wanaume.

Kufanya hivyo ni miongoni mwa shabaha zetu za msingi za Jumuiya yetu lakini hatujatimiza ipasavyo wajibu huo. Nawasihi sasa tufanye. Tutaungwa mkono na kupendwa na jamii yote ya Watanzania. Tutajiongezea upendo na uhalali miongoni mwa wananchi wa nchi hii. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumejiweka mahali pazuri pa kutimiza shabaha za CCM za kuiunda jumuiya yetu hii.
Jumuiya Haijafutwa

Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Wajumbe;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kuitumia nafasi hii kuwatoa hofu kuwa Chama hakijaamua kuifuta Jumuiya ya Wazazi. Ni kweli wapo watu wanaotaka iwe hivyo. Tusiwalaumu wala kugombana nao. Hiyo ni haki yao ya kidemokrasia na wala hamna sababu ya kuumizwa kichwa nalo.
Lililoamuliwa na Chama ni lile linalohusu shule za sekondari ambalo nimeshalieleza kwa kirefu. Naomba uelewa wenu na ushirikiano wenu. Ni jambo lenye maslahi kwa Jumuiya na Chama chetu kwa jumla.

Napenda kuwahakikishia kwamba CCM inaitegemea sana Jumuiya ya Wazazi katika kujijenga na kujiimarisha ndani ya umma wa Wazazi wa nchi hii. Napenda kuona na ndiyo matumaini ya Chama kuona Jumuiya inajibeba na kutimiza wajibu wake huo kwa ufanisi mkubwa.
Hivi sasa haijafikia viwango vinavyotarajiwa. Lakini naamini mnaweza. Semeni kama alivyosema Rais Obama wa Marekani: “Yes, we can!” Inawezekana timizeni wajibu wenu.

Ndugu Wajumbe;
Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nategemea sana mchango wa Jumuiya ya Wazazi uonekane kwa dhahiri katika kukitafutia na kukipatia ushindi Chama cha Mapinduzi. Vilevile, nategemea mchango mkubwa wa Jumuiya ya Wazazi katika kukiletea ushindi Chama cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010. Muanze sasa kujipanga vizuri. Kanzu ya Ijumaa hufuliwa Alhamisi. Muwe Makini kwenye Kuchagua.

Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Wajumbe,
Naomba nimalize kwa kuwasihi kuwa muwe makini katika kuchagua viongozi wenu. Mnachagua watu wa kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo. Mkifanya kosa mtalijutia. Kila mjumbe ampe kura yake mtu anayeamini yeye kuwa ataisaidia Jumuiya kusonga mbele. Usichague mtu kwa kuambiwa na mtu au mzee fulani maarufu. Usimpigie mtu kura kwa sababu ya uhodari wa mpiga debe wake au wakala wake.
Hivi mtu ambaye amehongwa kwa ajili unategemea asemeje? Usimpigie mtu kura kwa sababu amekuhonga. Anayehonga hafai. Amepoteza sifa ya uadilifu. Aliyenunua kura kwako hakuthamini na wala hatokujali akipata. Yeye akipata atahangaikia kurudisha pesa yake. Unajua ataipata wapi, ni humu humu kwenye Jumuiya. Matokeo yake badala ya fedha kutumika kutekeleza malengo ya Jumuiya zinafidia gharama ya uchaguzi ya Mwenyekiti na Wajumbe wake.
Anayeendesha kampeni za kuwachafulia wenzake majina na sifa zao naye kama anayehonga hafai. Hivi huwezi kunadi sifa za mtu unayemuona anafaa bila kuchafua jina la mwingine? Ndugu zangu, tujiulize Jumuiya yetu na Chama chetu tunakipeleka wapi?

Mwisho kabisa, nawapongeza tena kwa kufanikiwa kufanya mkutano huu. Umechelewa lakini hatimaye umefanyika. Pengine kuchelewa kwake kumewapa muda wa kuwajua vizuri zaidi wagombea, hivyo mtafanya uamuzi bora zaidi. Nawatakia heri katika kuwapata viongozi bora, na sio bora viongozi.
Sote tutakaporudi majumbani mwetu tuendelee kukisemea na kukipigania Chama chetu. Tuendelee kuhimiza moyo wa upendo na mshikamano miongoni mwa wana-CCM.

Asanteni kwa kunisikiliza!
Kidumu Chama cha Mapinduzi!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 07, 2009

    MKUU WA WILAYA, NIMEFULAHIA MATUMIZI YA NENO NDUGU KATIKA HOTUBA HII, JAPO BADO WANASEMA WASIVYOTENDA. NA PIA MTAZAMO WA KIKWETE KUHUSU SHULE BINAFSI ZA SEKONDARI NAFIKIRI SIO SAHIHI, KWANI ZA SERIKALI ZIMEZIDI KUDOLOLA NA SIO ZA BINAFSI.
    TUMPONGEZE KWA KUTUMIA NENO NDUGU BADALA YA NENO MHESHIMIWA AMBALO NAFIRI SIO SAHIHI KULITUMIA KWA WATU WASIO NA HESHIMA KATIKA JAMII.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 07, 2009

    Kwenye Chama tunatumia neno Ndugu nasiyo Mheshimiwa. Mheshimiwa ni neno la mtaani watu wanapenda kuwaita hao vigogo, na siyo neno rasmi la Chama

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 07, 2009

    huu ni mkutano wa wazazi wa upande wa ccm au tanzania nzima? na kama ni tanzania nzima ccm inahusika vipi? mbona nchi zingine maraisi huwa wanatumikia wana nchi wote bila kutumia nembo za chama chao mpaka wakati wa uchaguzi ukirudi tena? nini tofauti ya tanzania na mataifa mengine?

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 07, 2009

    angalia hotuba ya obama aliyoitoa kwa jumuiya ya waislamu duniani au katika hotuba zake; ni fupi, zisizojaa uongo na unafiki kama huu msururu wa siafu wanaokwenda kuhamia chakula cha malkia wao.
    haya mambo ya "kuchonga" sana utadhani kuna watu wana muda wa kusikiliza masalo yenu yasiyo na mpango. mwenzio gordon brown anakiona kindumbwendumbwe bongo naako kungekuwa na wakali wa siasa, ungepiga chini mchinga!! walahi vile.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 08, 2009

    Nina mtazamo tofauti kidogo na mheshimiwa kwenye suala la ufuaji wa kanzu, ningefurahi sana kama kanzu ya Ijumaa ingefuliwa Jumamosi, ikae safi kuisubiri Ijumaa nyingine. In short, watafuta kura mje mapema zaidi tushirikiane, hakika ukifika muda wa kura tutakupa, siyo uje leo ili kesho tukuchague..big no!

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 08, 2009

    mjomba....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...