JK akipewa ujumbe kabla ya kupokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi John Mutinda Mutiso wa Kenya leo Ikulu, Dar
JK akipokea hati za utambulisho toka kwa Balozi Juan Manuel Gonzalez De Linaries Palou wa Hispania
Balozi Yudhistiranto Sungadi wa Indonesia akikabidhi hati za utambulisho kwa JK
Balozi Kadri Sander Gurbuz wa Uturuki.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Juni 5, 2009 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi wanne ambao wataziwakilisha nchi zao katika Tanzania, na baadaye kufanya mazungumzo na mabalozi hao.

Katika shughuli hiyo iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi John Mutinda Mutiso wa Kenya, Balozi Juan Manuel Gonzalez De Linaries Palou wa Hispania, Balozi Yudhistiranto Sungadi wa Indonesia na Balozi Kadri Sander Gurbuz wa Uturuki.

Akizungumza na Balozi Mutiso baada ya kupokea hati zake za utambulisho, Rais Kikwete amesifia uhusiano mzuri ulioko kati ya Tanzania na Kenya, na kusema kuwa Serikali yake inatarajia kuendeleza uhusiano mzuri wa utendaji kazi ambao ulikuwapo kati ya Tanzania na balozi wa Kenya aliyemaliza muda wake.

Naye Balozi Mutiso amempongeza Rais Kikwete kwa kukamilishwa kwa mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria hadi Shinyanga na Kahama uliofunguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Rais Kikwete.

Balozi huyo pia amempongeza Rais Kikwete kuhusu uzinduzi wa kivuko kikubwa kuliko vyote nchini cha Mv Magogoni kilichozinduliwa jana, Alhamisi, Juni 4, 2009 na Rais Kikwete mjini Dar es Salaam.

Balozi Mutiso amesema kuwa kwa miaka saba Kenya imeagiza kivuko kutoka nje lakini mpaka sasa hakijapatikana wakati kile cha Mv Magogoni kimejengwa hapa hapa nchini katika muda mfupi tu.

Mwakilishi huyo wa Kenya vile vile amesifia juhudi za Rais Kikwete katika kusuluhisha mzozo mkubwa wa kisiasa nchini Kenya mwanzoni mwa mwaka jana.

Katika mazungumzo na Balozi Juan Manuel, Rais Kikwete ameishukuru Serikali ya Hispania kwa msaada wake katika maendeleo ya kusambaza umeme vijijini katika Tanzania, na kuiomba nchi hiyo kuendelea kuunga mkono jitihada hizo za Tanzania kusambaza umeme nchini.

Rais Kikwete vile vile ameishukuru Serikali ya Indonesia kwa msaada wake wa kuanzisha na kuendeleza Kituo cha Mafunzo ya Wakulima cha Mkindo (MFTC) ambacho kina uwezo wa kufundisha wakulima 18 kwa wakati mmoja.

Naye Balozi Gurbuz wa Uturuki amemwambia Rais Kikwete kuwa nchi yake inataka kuimarisha uhusiano wake na Tanzania katika nyanja za elimu, kilimo na afya pamoja na kuimarisha biashara na shughuli za uchumi kati ya nchi hizo mbili.

“Tunataka kuongeza uhusiano wetu wa kiuchumi. Tunataka makampuni ya Uturuki kuja kuwekeza katika Tanzania. Tunataka kuongeza nafasi za wanafunzi wa Tanzania kusomea katika vyuo vikuu vya Uturuki hasa kwenye ngazi za shahada za uzamili na uzamivu,” Balozi huyo amemwambia Rais Kikwete.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 05, 2009

    JK safari iyooo kwenda kuzishukuru nchi wa kutuletea Mabalozi wapya.
    I`m just say.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 06, 2009

    hawa mabalozi ambao sisi hatuna mabalozi kwao wanafata nini? Spain/Indonesia/Turkey dhidi ya Tanzania ni nani anamuhitaji mwenzake zaidi? Nilidhani sisi ndio tuweke mesenja wa kuwakilisha maombi ya hisani huko kwao, sio wao waje. Wanasakanya nini hawa kwetu?

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 06, 2009

    hahahaha! Iam just say too! tehtehteh!

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 08, 2009

    HAHAHA NAMFAGILIA WA UBATANI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...