Majaji wa mdahalo uliozihusisha shule 8 kutoka Dar es salam na Pwani wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wanafunzi wakati wa mdahalo huo. Shule ya sekondari Jangwani iliibuka na ushindi kwa upande wa Dar es salaam wakati mkoa wa Pwani shule ya sekondari Minaki iliibuka na ushindi.
Bernadeta Charles mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule ya sekondari Baobab iliyoko mkoani Pwani akiwasilisha mada kuhusu Haki ya Mtoto kulindwa kwenye mdahalo uliozishirikisha shule nane za sekondari kutoka mkoa wa Pwani na Dar es salaam katika ukumbi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jana jioni jijini Dar es salaam.


Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi. Mary Massay akiongea na wanafunzi wa shule za sekondari kutoka Mkoa wa Pwani na Dar es salaam walioshiriki mdahalo wa Haki za Binadamu na Utawala Bora ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani yatakayofanyika kitaifa Desemba 10 visiwani Zanzibar.


Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mdahalo uliojadili mada mbalimbali kuhusu Haki za Binadamu na Utawala Bora wakifuatilia kwa makini mdahalo huo jana jioni jijini Dar es salaam. Washindi katika mdahalo huo watelekea visiwani Zanzibar ili kuchuana na wanafunzi wa shule zilizochaguliwa ili kuwapata washindi watakaotangazwa kitaifa katika kilele cha Siku ya Haki za Binadamu Duniani Desemba 10 mwaka huu, Zanzibar.

Picha na Aron Msigwa,
habari na Anna Nkinda - Maelezo
Wanafunzi wa shule za Sekondari hapa nchini wametakiwa kuzijua haki zao za msingi ambazo zitawasaidia kupata mahitaji yao ya muhimu bila ya kunyanyaswa na watu wachache ambao hawapendi kuzifuata haki za binadamu na utawala bora.

Wito huo umetolewa jana na Mary Massay ambaye ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora wakati wa mdahalo wa wananafunzi wa shule za sekondari kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuhusu haki za binadamu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo uliopo jijini Dar es Salaam.

Massay alisema kuwa ofisi za tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora imekuwa ikichapisha vitabu, majarida na vipeperushi mbalimbali vinavyoelezea haki za binadamu katika makundi mbalimbali hivyo basi kama wanafunzi hao watakuwa na bidii ya kusoma machapisho hayo yatawasaidia kujua haki zao.

Alisema, "Hivi sasa tume ya haki za binadamu na utawala bora imeamua kutokuwaacha nyuma watoto kwani nao ni wanajamii na ni sehemu ya haki za binadamu hivyo basi inawafundisha mambo ya muhimu kuhusiana na haki za binadamu ili nao watakaposhika madaraka hapo baadaye wajue la kufanya".

Aliendelea kusema kuwa wananchi wengi katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa na uelewa mkubwa kuhusu haki za binadamu na utawala bora jambo la muhimu lililopo ni kuzilinda na kuzitetea haki hizo.

"Ni jukumu la watanzania wote kujua haki za binadamu ni zipi kwani katika maisha tunayoishi kila siku haki za binadamu zipo. Kwa mfano unaweza kujiuliza Je shuleni watoto wanapewa nafasi ya kuchangia? Wazazi wanawashirikisha watoto wao katika mambo mbalimbali ya familia?, kama hakuna ushirikishwaji wa watoto basi haki za binadamu hazifuatwi hapo", alisema Massay.

Kaimu Mtendaji huyo aliwataka wanafunzi hao kujifunza kutokana na yale watakayoyasikia kutoka kwa wenzao kwenye mdahalo huo pia aliwaahidi kuipeleka elimu kama hiyo kwa shule zingine za msingi na sekondari zilizopo nje ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Nao wanafunzi walioshiriki katika mdahalo huo walisema kuwa hivi sasa wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kutokuwapa watoto wao haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kutokuwapeleka shule na kuwanyima uhuru wa kushirikiana na watu wengine.

Wanafunzi hao walisema kuwa wananchi wengi walioko mikoani hawajui haki zao za msingi hivyo basi tume hiyo inawajibu wa kuwapatia taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambazo zitawasaidi kufahamu haki zao.

Shule zilizoshiriki mashindano hayo kutoka mkoa wa Pwani ni Minaki, Bagamoyo, Baobab na FilbertBay kwa upande wa mkoa wa Dar es Saam ni Makongo, Kibasila, Jangwani na Al-muntazir ambapo wazungumzaji 24 walijadili mada tatu zilizokuwa zinajadiliwa na kupatikana washindi wawili kutoka shule za Minaki waliopata asilimia 71.6 na Kibasila waliopata asilimia 57.3.

Fainali za mashindano hayo zitafanyika tarehe 09/12/2009 kwa kuwashindanisha wanafunzi wa shule nne, mbili kutoka Tanzania Bara na mbili kutoka Visiwani ambapo zawadi zitatolewa kwa washindi wa kwanza, wa pili na wa tatu tarehe 10/12/2009 ambayo ni kilele cha maadhimisho ya siku ya haki za binadamu Duniani.

Mada zilizojadiliwa katika mdahalo hupo ni Haki ya mtoto kulindwa ni jukumu la wazazi pekee, je wazazi walaumiwe kwa kutokutimiza wajibu wao?, Elimu juu ya haki za binadamu kwa wananchi ni jukumu la Serikali pekee. Je wananchi wa Tanzania wanaufahamu wa kutosha juu ya haki na wajibu wao? na Raia wote wa Tanzania huzaliwa huru na wote ni sawa? Je makundi maalum ya raia wa Tanzania yanafaidi haki zao za msingi?

Hadi sasa shughuli mbalimbali zimeshafanywa na tume ikiwa ni maandalizi ya kuazimisha siku hiyo ambazo ni midaharo kuhusiana na haki za binadamu, warsha ya haki za binadamu, semina kwa wahariri wa vyombo vya habari, haki za binadamu na wafanyabiashara na kutoa warsha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Sherehe za maadhimisho hayo zitafanyika kitaifa kwa mara ya pili hapa nchini huku ikiwa ni miaka 61 tangu kuanzishwa kwa siku ya haki za binadamu Duniani tarehe 10/12/2009 visiwani Zanzibar na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Abeid Aman Karume ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, kemea aina zote za ubaguzi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...