Pichani ni Mwenyekiti wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania Walter Bgoya,akizungumza wakati wa tamko la kupinga kubadilishwa kwa mfumo wa matumizi ya vitabu vingi kwenda kimoja mashuleni wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
MSIMAMO WA WACHAPISHAJI VITABU WA TANZANIA (PATA) KUHUSU MFUMO WA MATUMIZI YA KITABU KIMOJA BADALA YA MFUMO WA VITABU VINGI MASHULENI

Tarehe 21 Januari, 2010 katika mkutano wa Wadau wa Elimu huko Dodoma, ambao PATA (Chama cha Wachapishaji Vitabu Tanzania ambacho kingetegemewa kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inakichukulia kuwa mshiriki wake katika elimu) hakikualikwa, hata baada ya kuomba kialikwe kama mtazamaji tu, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alitoa kauli zifuatazo:
· Kwamba kushindwa kwa kiasi kikubwa katika mtihani wa mwaka 2009 kumesababishwa na matumizi ya vitabu vingi kwa pamoja katika mashule yetu, jambo ambalo linawachanganya wanafunzi na pia walimu. (TBC TV – Jambo Tz. Program ya 22/01/2010)
· Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi isiendelee kutumia vitabu hivyo shuleni.
· Serikali itaanzisha mfumo wa kitabu kimoja kwa somo moja katika kila daraja kote nchini.
· Mtihani ni mmoja kwa nchi nzima na kwa hiyo kitabu kiwe kimoja tu.
· Shule zisijishughulishe na ununuzi vitabu.

Chama cha Wachapishaji Vitabu Tanzania (PATA) kimeshtushwa na kauli ya Mheshimiwa Waziri, kuwa ati wingi wa vitabu, wala si uchache wa vitabu, ndio sababu ya watoto kufeli mitihani. Inawezekana Mheshimiwa anamaanisha kitu tofauti, kwa sababu hata maktaba ambazo kawaida hufurika vitabu vya kila aina, intaneti yenye mamilioni ya mitandao ambayo imesheheni kila taarifa uitakayo ya jambo lolote unaloweza kulifikiria vyote hivyo ni vyanzo vikubwa vya maarifa. Je, vitu hivyo vyote vinawezaje kuwa chanzo cha kuchanganyikiwa? Ikumbukwe kwamba vitabu anavyovizungumzia Mheshimiwa Waziri vimepitishwa na Wizara tena baada ya kukaguliwa kwa taratibu maalumu zilizowekwa na kuchujwa ipasavyo.

Zaidi ya hayo, PATA inaomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba matumizi ya “kitabu kimoja kwa mtihani mmoja” yamepitwa na wakati. Mtindo kama huo wa kufunza na kujifunza unachochea kukariri na kuhifadhi ili tu kufaulu mtihani na wala haumsaidii mwanafunzi kupata elimu ya kweli. Isitoshe, mtindo huo unakwenda kinyume na mtaala mpya wa mwaka 2005 uliotolewa na wizara yake. Mtaala mpya huu ni badiliko kamili la mfumo mzima wa kujifunza. Msingi wake ni kumpa mwanafunzi nafasi ya kujifunza kwa udadisi, awe na stadi za kumwezesha yeye mwenyewe kupata majibu sahihi ya maswali mbalimbali na akili inayokaribisha mawazo tofautitofauti. Hayo yote yanapatikana kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya kupatia taarifa pamoja na vitabu vingi, intaneti na njia zote za mawasiliano. Kwa kweli, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakuwa haiendi sambamba na mtaala wake mpya ambao imeuanzisha hivi karibuni.
Kwa hali hiyo, tunaomba wananchi waelewe yafuatayo:

UKWELI KUHUSU MATUMIZI YA VITABU VINGI SHULENI
· Vitabu vyote vinavyotumiwa mashuleni vimekaguliwa na kupitishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia kitengo chake maalumu cha kukagua na kupitisha vifaa vya elimu (EMAC).

· Kitengo hicho maalumu cha kukagua na kupitisha vifaa vya Elimu (EMAC) kina wataalamu kutoka Taasisi ya Elimu, Chuo Kikuu cha DSM, Wakurugenzi mbalimbali wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wataalamu wa somo husika toka kitengo cha wakaguzi, walimu na wadau wa elimu mbalimbali. Kitengo hicho kinaongozwa na Ofisa Taaluma Mkuu wa Wizara na kina wataalamu waliobobea kwenye taaluma zao wasiopungua 15.
· Kinyume na hoja zinazotolewa kusudi ili kupotosha, shule hazipewi vitabu wala hazilazimiki kununua vitabu vyote vilivyopitishwa na Wizara kwa kila somo. Ukweli ni kuwa walimu ndio wenye kupembua na kuchagua miongoni mwa vitabu vingi vinavyopatikana sokoni na kisha huchagua kitabu cha kiada kimoja tu ambacho kinamfaa kwa mahitaji yake na uwezo wake wa kifedha.
· Ukweli ambao wazazi, wanafunzi na walimu wanauelewa ni kwamba jambo muhimu linalochangia wanafunzi kufeli kwa wingi ni uchache wa vitabu vya kiada na ziada katika mashule ya Serikali. Ukweli mwingine ambao Wizara inaujua lakini inaukwepa (kusudi?) ni kwamba kuna vitabu vingi vyenye thamani ya karibu shilingi bilioni 60 za Tanzania kwenye mabohari, kwa kipindi cha miaka 2 sasa, badala vitabu hivyo kuwepo madarasani kote nchini. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilithibitisha ukweli huu kwa barua yao No. D/EMAC/PATA. Vol. 11/201 ya tarehe 18 Des. 2008.
· Mfumo wa matumizi ya vitabu vingi maana yake hasa ni kuwa walimu wana fursa ya kuchagua miongoni mwa vitabu vilivyopo ambavyo vimeidhinishwa. Mfumo huu hauna uhusiano na vile inavyoongelewa kwamba vitabu visivyofaa husukumizwa mashuleni na wanafunzi hulazimishwa kuvitumia vyote kwa pamoja. Ukweli ni kuwa Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya Mwaka Mpya alikiri kuwa upo upungufu wa vitabu mashuleni, sababu ya hali duni. PATA inaunga mkono kauli ya Rais ambayo ni kinyume na wazo la kuwa shuleni kuna vitabu vingi.
· Hutokea mara chache kuwa baadhi ya vitabu ambavyo vimepitishwa na EMAC, kweli visingepitishwa, na vimepenya katika chujio hilo. Hapo ndipo inapoonekana faida ya kuwa na vitabu vingine sokoni; vitabu visivyoridhisha vinachujwa na kutoweka.

NIA YA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI KUANZISHA MFUMO WA KUTUMIA KITABU KIMOJA
· Kwa kuwa vitabu vyote vimepitishwa katika chujio la EMAC, vimetathminiwa na kupata angalau kiwango cha chini cha ufanisi, jaribio la kuchagua kitabu kimojawapo miongoni mwa hivyo kunaweza kuleta tuhuma ya kuwepo kwa “mipango” hasa katika mwaka wa uchaguzi (kuondolewa kwa ada za mtihani, katika mkutano huohuo kumeleta tuhuma za “mipango ya uchaguzi”) kwa kuwa wale wachapishaji ambao watakuwemo katika “orodha mpya” papohapo watamilikishwa ukiritimba uliohalalishwa na Serikali!
· Mfumo wa kitabu kimoja, kwa mchapishaji mmoja (TPH), mchapaji mmoja (KIUTA/PRINTPAK), mwandishi mmoja (TIE) na msambazaji mmoja (TES) ulikuwapo hapa nchini katika miaka ya 60 hadi 90, na sote tunajua jinsi mfumo huo ulivyoshindwa kabisa. Je, Wizara haielewi haya?
· Wizara hiyohiyo ikajenga mfumo mpya wa kutumia vitabu vingi baada ya utafiti wa muda mrefu, na uwekezaji mkubwa wa watu binafsi, serikali, wafadhili na hata Benki ya Dunia. SIDA ndio hasa iliyomimina mabilioni ya shilingi katika mradi wa majaribio ya uchapishaji (PPP) ambao umezaa mfumo wa matumizi ya vitabu vingi uliotoa ufumbuzi wa tatizo sugu la matumizi ya kitabu kimoja.
· Mfumo huo wa kutumia vitabu vingi hatimaye ukazaa vitabu bora kwa bei ya wastani. Wakati wa mfumo wa kitabu kimoja kulikuwa na uhaba wa vitabu, na leo hii tatizo (tuliite tatizo?) ni upatikanaji wa vitabu vingi na vizuri.
· Tutawezaje kumuokoa mwanafunzi kutokana na madhara ya “kitabu kimoja” kisichofaa wakati hatuna kitabu mbadala? Je, hakutakuwa na chombo kama kile cha EMAC cha kuthibitisha ubora? Hata kama kitakuwepo, kwa nini tudhanie kuwa kitakuwa bora zaidi kuliko EMAC tuliyonayo sasa?
· Kuanzishwa kwa mfumo wa kitabu kimoja ndio kitakuwa chanzo cha vifo vya makampuni mengi ya uchapishaji ya hapa Tanzania, na pia kupoteza ajira nyingi za Watanzania, kodi ya mapato na vipaji vya kazi, kuporomoka kwa maduka ya vitabu kote nchini kama ilivyokuwa zama za “kitabu kimoja”. Matokeo yake ni ukiritimba mwingine wa kuzalisha vitabu visivyokuwa na ubora kwa gharama kubwa kwa Serikali. Hali hiyo itafanya vipaji vya waandishi wazuri wa Taifa letu vipotee.
· Msaada mkubwa wa hali na mali ulitolewa na wafadhili wetu na Serikali yetu katika kufanikisha mfumo wa “vitabu vingi”. Makampuni ya wananchi na pia ya kigeni yaliwekeza katika juhudi ya kufanikisha mfumo wa vitabu vingi. Nani atawafidia gharama zao?

SUALA LA SHULE KUTOKUENDELEA KUNUNUA VITABU VYAO WAO WENYEWE
· Katika mfumo wa sasa wa vitabu vingi shule huchagua na kununua vitabu vinavyolingana na mahitaji yao.

· Kamati za shule zina wajibu wa kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika katika mazingira ya uwazi.

· Ni kweli kwamba baadhi ya viongozi wa shule wasio waaminifu wanashirikiana na wauzaji wa vitabu wasio waaminifu na shule kuuziwa “vitabu hewa”. Pia kuna mtindo wa kurudufu vitabu ambavyo ni hakimiliki ya watu wengine na kuviuza shuleni.

· Ikiwa shughuli hii ya kununua vitabu watapewa Viongozi wa Elimu wa Wilaya, hapo ndipo “rushwa kubwa” itakaposhamiri kama ilivyokuwa hapo zamani. Viongozi hao watakubaliana na wasambazaji, na kununua vitabu kulingana na asilimia kubwa zaidi atakayopewa na muuzaji. Idadi ya ‘vitabu hewa’ itaongezeka maradufu. Kadhalika itakuwa vigumu kwa shule za mbali kuchukua vitabu vyao kutokana na utaratibu wa ugavi, wakati hivi sasa wauza vitabu hufikisha vitabu popote wanapoweza kuviuza.

· Ingefaa mfuo uliopo sasa uendelee kwani kuna vyombo husika kuchunguza na kufuatilia matumizi ya mali ya umma kama vile PET. Vyombo hivyo viko hai sasa na Serikali ndio yenye wajibu wa kuviwezesha ili vifuatilie na kuchunguza kwa makini matumizi ya mali ya umma.

RIPOTI YA MSHAURI HURU NA KONGAMANO LA WAZI
Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya uchapishaji wa vitabu na mashirika ya nje na ndani, Mshauri Huru aliteuliwa ili kutafiti na kutathmini kwa kina mchakato mzima wa vitabu na athari za kurejea katika mfumo wa zamani wa kitabu kimoja. Ripoti ya Mshauri huyo itatolewa kwenye kongamano la wadau wa elimu linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni. Ripoti hiyo itakuwa na ufafanuzi wa kina na wa kitaalamu kuhusu maswali, majibu na matokeo yanayoambatana na mabadiliko yanayopendekezwa katika sera ya vitabu. Kadhalika, Benki ya Dunia nayo tayari imeshaweka mshauri wake mahasusi kuandaa ripoti kuhusu suala la matumizi ya kitabu kimoja.
Kwa ushauri wa PATA, na pia kutokana na ripoti ya Mshauri Huru, wafadhili wetu wakiwemo Benki ya Dunia, SIDA, DFID, UNESCO, UNICEF na EU wamekubali kuchangia maandalizi ya Kongamano la Wazi la vitabu ambalo litahudhuriwa na watumiaji na wahusika wakuu wa vitabu pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. PATA inaamini kwamba Kongamano hilo lina umuhimu wa pekee katika kuisaidia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufikia uamuzi tanzu, uliojadiliwa kitaalamu, utakaoweza kuongoza maendeleo muhimu ya elimu ya Taifa na yanayokubalika na wananchi. Ikiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itatoa uamuzi wa harakaharaka bila kuzingatia mchango mkubwa uliotolewa na washirika wetu wakuu wa maendeleo, ambao kwa kipindi kirefu msaada wao umekuwa ni uti wa mgongo wa Bajeti ya Taifa, hasa katika elimu, utazusha wasiwasi na mashaka kuhusu nia na pia uwezo wa Wizara katika kutekeleza sera thabiti zilizotokana na utafiti na uchambuzi wa kina uliokwishafanyika.

HITIMISHO
PATA inatoa ombi kwa Serikali yetu tukufu kufikiria tena kuhusu sera mpya ambayo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi anataka kuilazimisha katika tasnia hii. Ni vema tulipe nafasi kongamano hilo la wadau wote wa elimu ambalo litafadhiliwa na washirika wetu wa maendeleo litoe mwanga wa kitaalamu kuisadia Wizara ili ifikie uamuzi tanzu juu ya jambo hili muhimu, utakaokubalika na wadau wa Elimu ya Taifa letu na utakaoleta ufanisi wa nchi yetu kwa ujumla.
PATA inaamini kuwa kuchagua kitabu kimoja tu si jambo la busara, hakuna sababu ni kupinga maendeleo, na ni kinyume kabisa na sera ya Serikali yenyewe juu ya uwekezaji na pia inapingana na mwongozo wa PPRA (Public Procurement Regulatory Authority) na FCC (Fair Competition Commission). Isitoshe, hivi sasa mazungumzo yanaendelea katika nchi zote wanachama wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) yenye lengo la kusawazisha MTAALA WA ELIMU wa nchi wanachama. Punde si punde, mtaala huo utabadilika ili uwe na uwiano wa pamoja wa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika elimu. Je, ni busara hivi leo kufanya badiliko kubwa kama hilo halafu kulibadili tena chini ya makubaliano ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki?

Imesainiwa kwa niaba ya PATA:
Ian Ben Moshi
Mwenyekiti-PATA
02/02/2010

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 18 mpaka sasa

  1. Ni kama wehu hivi kutumia kitabu kimoja. Tatizo kubwa ni hii mitihani "ya taifa" ta tangu enzi za ukoloni. Taifa la watu milioni karibu 40 eti wanafunzi wanafanya mtihani mmoja. Waingereza walotuacha na huo mfumo bila shaka wao hawautumii. Kama kulikuwa na ajenda za ujamaa za kusaidia watu wote tuwe na mawazo hayo hayo, ujamaa haupo tena. Hakuna nchi iliyoendelea inayofanya mambo kama sisi jamani!!! Tumia vitabu vingi, ua mfumo wa kijinga wa National Exams - iwe mitihani ya kanda au mikoa inayofuata "viwango" vilivyowekwa kwa ngazi ya taifa

    ReplyDelete
  2. Hakuna serikali tukufu ingali inafisaidi wajenga nchi.
    TAPA msiwe nawasiwasi, kama mlivyogundua baada ya Oktoba 2010, sera ya vitabu vingi itarudishwa.

    ReplyDelete
  3. Seems to be a business war but let students have choices.

    Wizara wangekuwa wanachagua vitabu vya msingi vya kufundishia na mitihani itoke huko huko lakini siyo kuzuilia uwepo wa vitabu vingi.

    Watunzi wanatofautiana katika kuelezea mada zao. Waacheni wanafunzi wachague vitabu vya kununua kulingana na uelewa wao.

    ReplyDelete
  4. Kaka Michu kuna kipindi nilisoma malalamiko ya mama mmoja kwenye blog yako akilalamika hawa watunzi wa vitabu, kuwa kitabu alichomnunulia mtoto cha mazoezi kilikuwa na makosa mengi sana, akawasiliana na mwandishi wa kitabu hakuwa na ushirikiano mzuri, nachanganyikwa kwani na mimi naona vitabu vikizidi vingine vinawapotosha watoto hasa wanaojiandaa na mitihani!

    ReplyDelete
  5. Kwa hakika msimamo huu uliotolewa na Waziri tena aliye na karama ya Uprofesa inastusha kama si kusikitisha,

    Inapaswa kujiuliza kama je nia yetu wanafunzi wafaulu kwa uwingi tu kwa kukariri pasipo uelewa tena uliomithilika kwa dunia yetu hii ya leo iliyojaa kila aina ya ushindani katika suala zima la taaluma au wawe na changamoto na wafaulu kwa kuweza kupata uelewa sadifu wa masomo na maswala yanayohusu ushindani yakinifu katika dunia ya leo,

    Tuamke Watanzania, tufumbue macho, tuangalie zaidi ya pale upeo wa macho yetu ufikapo bali tutakiwapo,

    Mungu Ibariki Tanzania, Uwape hekima, busara, na upeo ulio angavu zaidi ya vyeo au shahada walizonazo kama si kusadikika nazo,

    Matukio OleAfrika Aranyande Chuma

    ReplyDelete
  6. Nielewavyn mimi mkeshahoi ni kwamba kuna kitabu cha KIADA na vitabu vya ZIADA. Nashawishika kuamini waziri anamaanisha kitabu kimoja cha kiada kwa shule zote nchini. Na mwalimu yeyote anayetaka anaweza kuongeza vitabu vya ziada kwa wingi apendavyo. Ikiwa hivyo ndivyo basi namuunga mkono profesa kwa asilimia 100. Utitiri wa vitabu vya KIADA unatuchanganya walimu, wanafunzi na wazazi kwa ujumla wetu. Na pengine unachangia ufaulu mdogo, nasema pengine kwavile sijafanya utafiti kuthibitisha.

    ReplyDelete
  7. Ndio ni muhimu kukawa na vitabu kadhaa vya kufundishia na hii aina maana kuwa ni lazima kitabu kimoja kitumike nchi nzima!! bali kukiwa na mwongozo wa vitabu kadhaa itasaidia sana katika kukuza elimu yetu. hii ya kuachia nguvu ya soko la vitabu ifanye kazi, tutakuja kujikuta katika mataizo makubwa sana hapo baadae. mtu anaweza kuw ameenda shule na kuelimika lakini alichojifunza hakipo kabisa katika dunia ya leo!! kumbe kajifunza vitu vya kufikilika na tayari ana shahada yake!!! kazi hapo.

    ReplyDelete
  8. PONGEZI kwa waziri wa ELIMU!!!
    Biashara ya vitabu imeingiliwa kama biashara ya pharmacy na nyinginezo,kwani wachapa vitabu huwa wanapeleka CHINA kufyatua hivyo vitabu,vingi vina spelling mistakes,havina ubora wa content.na wapitishaji wa wizarani wanapewa hongo,hivyo wanaaprove vitabu bila kuvipitia kwa kina.
    USHAURI:
    Wizara itoe vitabu i.e content ya vitabu,viwe na hatimiliki ya serikali,au public creative commons license.viwekwe online katika website ya wizara.
    kampuni zinazotaka kuchapa na kusambaza ziwe huru kutoa nakala hizo zilizotolewa na kurasimishwa na wizara ya elimu.

    By Mzalendo

    ReplyDelete
  9. Mi naona huo mfumo wa kutumia aina moja ya vitabu kwa darasa au vidato vyote Tanzania ni mzuri as unaleta uniformity ktk shule zote nchini na kwamba kila shule itumie vitabu vyake vyenyewe inachanganya wanafunzi hata wasahihishaji.
    Huko miaka ya nyuma tulikua tunatumia vitabu vya aina moja baina ya mashule na tulikua ok. Siku hizi kutoa vitabu ni biashara. Hongera Waziri kwa uamuzi sahihi

    ReplyDelete
  10. NINASHANGAA KUONA KUNA WATU HAWAELEWI MFUMO BORA WA ELIMU UNAHITAJIKA KUWA VIPI HUSUSAN KATIKA SWALA LA VITABU.
    naamini prof yuko sahihi kabisa, maana kinachozungumziwa sio kupiga marufuku vitabu vingi,bali ni kuwa na uniformity kwasababu mtihani unakuwa uniform,hivyo majibu na uwelewa unatakiwa kupimwa kwa kutumia source moja ya information waliyotakiwa kupewa.
    hata katika nchi za huku pia hilo liko wazi,kunakuwepo na muongozo unaoonyesha ni vitu gani mwanafunzi wa level gani anapaswa kuvielewa na kuvujibu,na ni vitabu gani anavyotakiwa kuvitumia ili kujibu anachopaswa kujibu. kinachobakia sasa ni vitabu vya ziada kulingana na uwezo na matakwa ya ziada ya mwanafunzi.lakini kujibu ni lazima ajibu kwa kutumia kitabu kilichowekwa kwa ajili ya hilo.
    nadhani tunaelewana,tusiwachanganye wanafunzi na walimu prof yuko sahihi kabisa.

    ReplyDelete
  11. Nami naungana na waliomsapoti waziri. Hawa jamaa wa TAPA wanafanya biashara. Hawajali kitabu kama kimechapishwa vizuri mistake kibao. Huyu mzee anapinga kwa kuwa ameishaacha kusomesha, watoto wake wote wamesomes nje ya nchi.Watoto wetu anataka kuwafungia kanyaboya. Serikari iwatumie vizuri wataalamu wa masuala ya elimu waangalie ni lipi la kufanya.

    ReplyDelete
  12. Kaka Michu,
    Naomba tena nitumie hiki kichwa changu kuwaelimisha wadau jambo moja au mawili kuhusu hili swala la vitabu;
    (1) Suala la kupanga/kutunga Mitaala na kutoa "reference materials" ni la Mamlaka husika "hapa ni Serikali/Wizara" na kamwe haliwezi eti kupewa wachapisha vitabu waamue au waishawishi au wailazimishe serikali,
    (2) Kuwa na mfumo wa Kitabu kimoja au viwili (main reference) ni utaratibu wa kawaiada na hauko katika mashule peke yake. Ni mfumo ulio duniani kote kuanzia elimu ya awali hadi PhD. Kila eneo la usfundishaji lina kitabu kimoja au viwili vikuu (main reference) ambavyo lazima uvisome na mtihani ukija lazima utoke eneo hilo. Vingine tunaviita suplementary books....na hawa wanaoitwa wachapishaji lazima walielewe hilo. Hata hapo katika chuo chetu kikongwe MLIMANI, SOKOINE, MUHIMBILI na Hivi vichanga kuna mfumo huo kila fani ina kitabu au vitabu ambavyo ni Main reference....SIWAELEWI hawa WAFANYABIASHARA....

    (3) Mimi naona huu utaratibu wa kutaka shule iwe biashara iz not a good idea.Lazima tuheshimu mamlaka husika ambazo hufanya tafiti, na kutoa mwelekezo wa vitabu gani vitumike..."kiada na Ziada".
    Ankali..wale wote wal;iosoma enzi kabla ya huu utandawazi kuja wanakumbuka kulikuwa na vitaju au mada ambazo kila mwanafunzi akisoma anakamata uelewa fulani na inakuwa accross the board, then ukijisomea vitabu vingine vya ziada unaelweza zaidi. Hapa nakumbuka vitabu kama vya "KULI", the River Between, African Child, Songs of Lawino, Great Pond....na hadithi maalum kama vile "Hawala ya Fedha", "Sadiki na Sikiri"..nk.nk.nk Kaka Tanzania tulikuwa mbali ila wajanja wanataka kudharau mfumo uliokuwepo ambao bado uko mathubuti unahitaji 'ukarabati kidogo tuu"

    .....Sipendi biashara iingilie shule..na sikubaliani na hawa wachapishaji

    ReplyDelete
  13. Uncle Matukio hapo juu, umeongea vema. Kweli karne ya leo Tanzania nzima tuimbe shairi moja tu la 'sungura karukaruka na sizitaki mbichi hizi?' huko ni kurudi nyuma. Nchi zote zimevuka huko. Hapo kwa watani wetu Kenya wao wana vitabu vya kiada 6. Kesho wakipitisha mtaala mmoja kwa jumuia ya afrika mashariki yote. Tutashika mkia. Kama hatujui maana ya kitabu kimoja (single) cha kiada na vitabu vingi(maltple)vya kiada , tufanye utafiti.

    ReplyDelete
  14. Kwa maoni yangu naona kuna mkanganyiko wa mambo; mfumo wa kitabu kimoja? au mfumo wa vitabu vingi? Hilo ni suala moja. Ubora wa vitabu katika mifumo yote hiyo miwili ni suala jingine. Suala la tatu ni nani anayeidhinisha kitabu kutumika katika shule. Kwa mfano je, publisher anaweza kuuza kitabu chake shuleni bila kitabu hicho kuwa kimeidhinishwa na mamlaka ya serikali? Suala la nne ni gharama ya vitabu. Je, hivi sasa serikali inaweza kugharimia huo Prof. Maghembe anaouta utitiri wa vitabu? La mwisho ni mamlaka gani inapaswa kununua vitabu na kuvisambaza shuleni?
    Huo mfumo wa kitabu kimoja kwa kila somo kwa kila ngazi nchi nzima si mgeni. Huo ndio uliokuwa mfumo katika enzi za Ujamaa. Taasisi ya Elimu (wakati ule) ilikuwa ndiyo mamlaka pekee iliyokuwa na jukumu la kuandika vitabu. Vitabu hivyo havikupitiwa na mamlaka yoyote nyingine kutazama kama vinafaa, kama vina makosa au vinaendana na mitaala na umri na uwezo wa wanafunzi. Baada ya hapo miswada ilipelekwa Tanzania Publishing House ambako ilihaririwa lugha tu lakini siyo maudhui (content) na baada ya hapo ilipelekwa kwa mpiga chapa mmoja tu Printpak, shirika la serikali. Baada ya vitabu kutoka vilipelekwa vyote Tanzania Eiimu Supplies ambao ndio pekee waliokuwa na jukumu la kuvisambaza.Huo ndio mfumo uliokuwepo na matokeo yake yalikuwa mabaya kiasi kwamba ilibidi serikali iubadilishe. Vitabu havikuwa vizuri kitaaluma, havikuwa imara kimuundo na havikuwapo vya kutosha. Ilifika mahali kitabu kimoja kikawa kinachangiwa na watoto 20, na sehemu nyingi hasa mikoani hakukuwepo na vitabu kabisa.
    Hiyo ndiyo historia ya mfumo wa kitabu kimoja. kwa kuwa serikali ilikuwa imezama sana katika kumiliki tasnia (industry) ya vitabu, na kwa kuwa matokeo yake yalikuwa mabaya ajabu, na halafu itikadi ya soko huria ilipoingia uamuzi ukachukuliwa katika tasnia hii kama ilivyokuwa kwa nyingine kuwa serikali ijitoe kabisa katika mlolongo mzima wa uandishi, uchapishaji, uchapaji na biashara ya vitabu, kwa kifupi serikali isijihusishe na biashara ya vitabu. Hiyo ikawa ndiyo sera mpya ya serikali ambayo sasa Kikwete anamtumia Maghembe kuiondoa ii warejeshe ile ya miaka ya nyuma.
    Kazi muhimu na ya lazima kwa serikali ni kutayarisha mitaala, na mihutasri ya masomo. Baada ya hapo ni kazi ya wachapishaji kutafuta waandishi wa vitabu, wahariri, wachoraji wa vielelezo, wachapaji na wauza vitabu.

    Serikali iliweka utaratibu mwingine muhimu sana. Ili kitabu kiweze kutumika shuleni, kwa vile vya shule za msingi, sherti ya kwanza ilikuwa ya miswada yote ya vitabu kupitia Baraza la Kiswahili ili kuhakikisha kuwa Kiswahili kilichotumiwa ni sanifu na hakina maneno yasiyostahili kuwa katika kitabu cha walengwa wa umri fulani. Wachapishaji wanalipia kazi hiyo. Baada ya hapo, muswada wa kitabu ukiwa na muhuri wa "kinafaa" kwa upande wa lugha inabidi upelekwe EMAC (Educational Materials Approval Committee) katika Wizara ya Elimu ambako sasa unapitiwa na wataalamu wa somo husika kwa kutumia kila kigezo muhimu cha taaluma: usahihi wa maudhui, ubora wa vielelezo, usawia na mitaala na muhutasari wa somo, ubora katika kujali masuala ya kijinsia, masuali na mazoezi na kadhalika. Kama muswada (manuscript) una upungufu mdogo katika vigezo hivyo unarudishwa kwa mchapishaji ili ufanyiwe masahihisho na uipelekwe tena kwao kwa kupewa cheti cha ithibati. Kama upungufu wake ni mkubwa basi unatupiliwa mbali. Hata baada ya wataalamu wa somo kuupitia na kuona unafaa, lazima upitiwe na kamati yote ya watu 15, chini ya mwneyekiti wao ambaye ni Kamishna wa Elimu na wote kwa pamoja waseme unafaa. Ukipita, mchapishaji anapewa cheti cha ithibati ambacho lazima kipigwe chapa ndani kwenye kurasa za kwanza. Bila ya hivyo kitabu hakiwezi kuingia darasani hata kidogo na mwalimu hawezi kukinunua.

    Inaendelea...

    ReplyDelete
  15. Maoni yanaendelea...

    Huo ndio utaratibu wa kupitisha kitabu. Sasa, hata kama vitabu ni vitano au kumi, vikisha pitishwa na EMAC maana yake ni kuwa chochote kile kinafaa kabisa kwa matumizi ya shule zote na kinakidhi mahitaji ya huo mtihani mmoja.Mitihani haitungwi kutokana na (textbooks). Inatungwa kulingana na mtaala na mihutasari. Umuflisi wa elimu yetu ni huu wa kusoma kwa ajili ya kushinda mitihani na siyo kuelewa na kufikiri, kudadisi na kujitafutia vyanzo mbalimbali vya maarifa.

    Mfumo wa Multi-textbook umepanua tasnia ya uchapishaji. Maduka ya vitabu yalikuwa yamekufa,sasa yamefufuka. vitabu vinapatikana kdogo nafuu kuliko ilivyokuwa. Si bora kukawa na tatizo la wingi kuliko lile la uhaba?

    Uhuru ni kuwa na chaguo. Si ubora wa uchache na ubaya wa wingi. Suala ni kuwa kama kitabu kimoja hakitoshelezi matakwa yako, unachagua kingine ili mradi vyote vimepitishwa na EMAC na kukubalika kutoa elimu kwa watoto wa darasa lako. Halafu mbona kuna shule za binafsi zinazotumia mitaala ya Cambridge School Certificate na ya International Baccalaureat. Maghembe anawaamulia kitabu kimoja cha kutumia? Kwa lazima?

    Yule mama aliyekuta kitabu kimoja chenye makosa kibao alieleza kilikuwa kitabu cha Kampuni gani? Je, kilikuwa na cheti cha ithibati? Kama kilikuwa na cheti hicho, si Wizara ya Elimu iliyokitoa Na si Wizara inayoteua EMAC? Bila ya kujua ni kitabu kipi na ni mchapishaji yupi si vizuri kusema kuwa vitabu vyote ni hovyo. Halafu hivi Taasisi ya Elimu (Tanzania Institute of Education) itakapopewa na Maghembe ukiritimba wa kuandika, kuhariri na kuchapisha vitabu, nani atafanya kazi inayofanywa na EMAC sasa hivi? Au hiyo sasa itafutwa? Mbona hivi sasa mmoja wa wajumbe wa EMAC ni kutoka TIE? Halafu kuna ambaye hajaona vitabu vilivyotolewa tayari na TIE? Mbona ni aibu tupu! Kwa hiyo amka, kitabu si kizuri kwa sababu ni kimoja na kimetolewa na serikali. Na vitabu si vibaya kwa sababu nivingi!

    Shule hainunui vitabu vya kila mchapishaji. Inanunua kitabu kimoja na hata hicho ni kitabu kimoja kwa watoto sita hadi saba na sehemu nyingi nchini ni kitabu kimoja kwa watoto hadi kumi na nne. Ruzuku ya vitabu ni chini ya shilingi 5,000 kwa mtoto kwa mwaka kwa mahitaji yote ya vitabu na stationery. Hivyo vitabu vyote shule itavinunua na nini? Tangu alipoingia Maghembe Wizarani textbooks hazijanunuliwa! Janja ya kuficha ukweli, hakuna vitabu shuleni na hiyo ni sababu moja ya hakika pamoja na ile ya migomo na malalamiko ya walimu yaliyokithiri katika muda wa Maghembe, ya matokeo mabaya ya 2008 na 2009. Siyo vinginevyo.

    Juu ya ununuzi wa vitabu. Huko nako historia ni ile ile. Ukiritimba wa Tanzania Elimu Supplies ulirithiwa na ukiritimba wa serikali kupitia Ma DEO. Kwa sababu ya uchache wao walishirikiana na wachapishaji wenye uchu kununua vitabu vyao tu. Yaani DEO fulani anakubaliana na publisher mmoja percent yake halafu ananununa vitabu vya huyo publisher peke yake. Kwa hiyo biashara ikawa si biashara ni ufisadi mtupu. Kutokana na hilo na malalamiko ya walimu na wachapishaji waliokuwa wakikataa ufisadi huo na pia kwa sababu ilikubalika kuwa katika mfumo wa vitabu vingi wa kuchagua kitabu kinchofaa zaidi ni mwalimu, madaraka yakapelekwa shuleni na walimu wakapewa mafunzo ya kupima na kuchagua kitabu kinachofaa kwa kila somo. Tanzania ina wilaya chache na Ma DEO wachache ukilinganisha na shule zaidi ya 17,000 za msingi. Unaweza kuwaweka mfukoni wachache huwezi kuwaweka mfukoni 17,000 na ukijaribu itakugharimu kiasi kikubwa sana kiasi kuwa biashara haitakuwa na faida. Ndiyo sababu kuna utata hapa. Kuna mshiko mkubwa kwa wachache na ndiyo sababu wachache wanataka warejeshewe himaya yao.

    Ulisikia pahali ambapo vitabu si biashara katika nchi ya itikadi ya ubepari? Sasa wachapishaji wa Tanzania kufanya biashara ya vitabu ni la kushangaza? Si bora vitabu ambavyo haviui? Pharmacy zinazouza dawa za bandia mbona zinaendelea kuwepo? Na hizi ziliibukaje? Zamani hazikuwepo kwa sababu dawa zilitolewa bure na ziikuwepo za kutosha.

    Kama haya hayasaidii basi tutaendelea.

    ReplyDelete
  16. Watu msichanganye habari, mtaala ndio unakuwa mmoja. Lakini vitabu vyaweza kuwa tofauti.Halafu shule au walimu waweza kushauri vitabu gani vinafaa.

    Kwa mfano, kitabu cha darasa la kwanza kinachofundisha 2+2 = 4.
    Na kingine kinafundisha hivyo kwa kutumia picha ya vijiti viwili + vijiti viwili = vijiti vinne. Yote ni sawa.

    ReplyDelete
  17. Watanzania tusidanganyike hata kidogo, kitabu kimoja hakiwezi kuleta tija na wala kujenga uelewa mpana wa mtoto kama tuonanyo kwenye nchi za wenzetu. Mimi naomba niulize ishu ni vitabu au ni upungufu wa walimu na hasa vijijini?
    Mimi naamini tatizo lipo kwenye ufundishaji kwani mimi ni mmojawapo niliyetokea kijijini miaka ya 1990, hapo tulikuwa na kitabu kimoja lakini ukiangalia shule zingine mwalimu anamaliza sylabus, na nilipokuwa nasoma nikiwa darasa la sita mpaka unakwisha nilifikia sura ya tatu kati ya sura nane hadi kumi kwa baadhi ya masomo. sasa niambie kama ntaweza kujibu mtihani kama mwenzangu aliyemaliza sura zote nakufanya mazoezi ya ziada kwenye zaidi ya kitabu kimoja.
    Na ninaamini kwa sasa hali ni mbaya zaidi has huko vijijini na ukizingatia ndo kila siku walimu wanakuwa wanafatilia maslahi yao mijini bila mafanikio.
    Tutafanye maamuzi kwa uelewa mpana zaidi ili tuweze kuendeleza elimu na si kutoa maoni kwa sababu tu hujui mazingira mazima ya elimu yetu ya kibongo. Na mimi ninaamini mwanafunzi aliyesooma vitabu zaidi ya kimoja uelewa wake nitofauti na aliyesoma kitabu kimoja.
    Ushauri wa bure tusiyumbishe elimu yetu tena kwa kila kukicha tunaleta mabadiliko ya siyo ya msingi, ni juzi tu tumetoka kwenye matatizo ya elimu ya mungai ambayo pengine madhara yake ndo pia yanachangia kufeli kwa wanafunzi wengi kwenye mitihani yao.
    Mdau
    Makimu

    ReplyDelete
  18. kwi!kwi!kwi!kw kweli bongo tambarale kamanda wa ffu kanena

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...