Ankal, nakuomba wakumbushe wadau wetu tulikotoka, enzi zetu ambazo sasa zinaingia kwenye "ya kale dhahabu"!

Posti hii inatoka kwa yule yule aliyeandika ile "kumbukumbu ya Edward Moringe Sokoine". Basi leo tulikuwa tunazungumzia picha moja toka kwenye blogu ya Bakari Msulwa (mawio-shineshine.blogspot.com)basi ile kutaja tu jina la Msulwa, doh, ndo tukawa tumemchokoza Monsignor Phabby akaandika hii kumbukumbu yake, yaani dah, jamaa sijui alimeza memory chip ya 2GB? manake dah. Soma mwenyewe! Ni kumbukumbu bin kumbukumbu. Tunawakumbuka waliokuwa wakitukosha roho enzi hizo!
Subiwww.wavuti.com

Wahenga walisema ya kale ni dhahabu, leo naomba niwakumbushe baadhi ya watangazaji wetu mahiri waliokuwa wakilitumikia taifa katika kutupasha habari, kutuelimisha, na kutuburudisha. Ni kumbukumbu ya muda mrefu kidogo hivi nitakapowasahau wengine tafadhali karibuni sana tukumbushane ili tuwakumbuke na kuwaenzi hawa wanahabari wetu mahiri katika eneo la utangazaji miaka hiyo.

Alikuwepo David Wakati (Mkurugenzi) – pamoja na vipindi vingine alikuwa maarufu zaidi kwenye kipindi cha Nipe habari. Kisha kuna Ahmed Kipozi -Taarifa ya habari na External Service, Khalid Ponera – Maarufu kwenye Zilipendwa Jumapili asubuhi subuhi kwenye na robo mara baada ya taarifa ya habari na matangazo ya vifo, Nassoro Nsekeli akitangaza majira asubuhi saa kumi na mbili na nusu na saa tatu usiku. Hapo kwa mwanafunzi majira ikikukuta bado upo nyumbani unajua umeshachelewa shule siku hiyo jiandae kwa bakora. Pia kulikuwa na Sarah Dumba (Mkuu wa Wilaya) –maarufu kwenye taarifa ya habari, Salim Seif Nkamba mwenyewe akijiita SS Mkamba maarufu kwa taarifa ya habari pia, Salim Mbonde akitangaza mpira huyu tulikuwa tunaamini eti alikuwa mnazi wa Simba, Ahmed Jongo (Mungu Amrehemu) – tuliamini alikuwa mnazi wa Yanga kwelikweli tukawa tunawekeana utani eti Jongo kasema Simba bila sisi mbili halafu Hassan Mkumba akipiga matangazo ya vifo baada tu ya taarifa ya habari.

Walikuwepo pia Chalz Hilary mwenyewe akiwa hataki aitwe Charless huyu ndo pro mwenyewe wa mpira kabla ya kuhamia Radio One na kujichukulia umaarufu mpaka kufikia kuitwa mzee wa Macharanga, Julius Nyaisanga- Brazamen wa RTD miaka hiyo. Akitangaza Club Raha Lete Show utamsikia mimi ni mtangazaji wako wa kawaida uncle J Nyaisanga ukipenda ni super tall...adios Sayonara (sasa hii sayonara nikawa siielewi nikawa nasema adios ‘seremala’), Siwatu Luwanda –alikuwa maarufu kwenye mama na mwana Jumamosi saa tisa na dk 2 na marudio Ijumaa jioni na mahiri kwenye taarifa ya habari. Ilikuwa ni mwiko kwa motto kukosa hiki kipindi. Halafu akawepo Bibi Debora Mwenda -mtaalamu mwenyewe wa mama na mwana enzi za ua jekundu, binti chura, Salama Mfamao akituletea taarifa ya habari na mchana mwema, Christina Chokunogela wakiichangamsha RTD enzi hizo maarufu kwenye ombi lako eti muombaji wimbo anasema tafadhali mtangazaji usiniweke kapuni, naomba nipigie wimbo wa Solemba....maana kila nikiusikia wimbo huu hata kama nilikuwa nakula huacha kula mpaka wimbo uishe ah...

Halafu alikuwepo Chisunga Steven mzee wa kanda ya Ziwa Magharibi alikuwa mtaalamu wa Ugua pole na akituripotia habari za RTC Kigoma kuzigagadua Simba au Yanga, Pale Arusha alikuwepo Batty Kombwa - Mzee wa Arusha huyu yeye alikuwa mtaalamu wa Wakati wa Kazi ile mida ya asubuhi mchana kabla ya saa sita. Inapofika kwenye wataalamu wa kutangaza mpira, Dominic Chilambo (Mungu amrehemu)- ndiyo alikuwa kipenzi changu. Huyu Mzee wa TP Lindanda wana Kawekamo alikuwa ananikosha sana utamsikia Marsha kwakeee Massatu, anampelekea Kitwana Seleman kwake Mao Mkamy Ball Dancer kwake Beya Simba anarudisha pembeni kuleee kwake Edward Hizza ...enzi hizo Pamba inakanyaga acha tu. Alijua sana kuipamba Pamba na alikuwa na mapenzi ya kweli kwa hiyo timu. Baadaye akaja Bujaga Izengo wa Kadago alikuwa na sauti fulani hivi mtaalamu wa Taarifa ya habari , Edda Sanga (Mkuu wa wilaya sasa) -Mama na Mwana alikuwa na sauti ya upole hivi ya kimama hasa wakati mwingine akitangaza External Service, Aloycea Maneno- akitangaza kwa umahiri kabisa Ombi lako, Mama na Mwana, na CheiChei Shangazi...

Wengine ambao siwezi kuwasahau ni Barnabas Mluge (jamaa alikuwa mnazi wa CDA huyu acha tu enzi hizo zikitamba pamoja na Kurugenzi na Waziri Mkuu- Ukimsikia ameanza watoto wa Nyumbani CDA ya Dodoma hapo basi mjue Simba au Yanga mshalala hapo. Walikuwepo pia Omar Jongo (mpira), Mohamed Amani (Mohamed Dahman), Idrissa Sadallah -kanda ya nyanda za juu kusini akiifagilia Tukuyu Stars huyu, Abisay Steven wa Kanda ya Ziwa Nyasa yeye na Majimaji humtoi huyu. Hapo akiwapamba akina Celestine Sikinde Mbunga, Octavian Mrope, Dadi Athuman, Samli Ayoub ‘beki mstaarabu’...acha tu, Peter Makorongo na sauti yake nzito hivi akiwa Arusha kule kabla hajaamishiwa Mtwara, Angalieni Mpendu maarufu sana kwenye hisia na muziki kipindi kilichojichotea washabiki wengi kwa ule umahiri wake wa kupangilia stori na muziki, Titus Phillipo, Nazir Mayoka, Abdul Ngalawa (taarifa ya habari na mazungumzo baada ya habari yamewajia kutoka redio Tanzania DSM….halafu anaanza stori fulani mwisho unapewa ujumbe wa siasa ni kilimo, ujamaa na kujitegemea, mtu ni afya, na vitu kama hivyo), Juma Ngondae, Mohamed Kissengo, Malima Ndelema, Abdala Mlawa alikuwa mtaalamu mwingine huyu wa ombi lako, Hendrick Michael Libuda mtaalamu wa Mkoa kwa Mkoa, Mikidadi Mahmoud maarufu sana kwenye kutangaza mpira, Rosemary Mkangala (External Service na taarifa ya habari), na Abdala Majura kabla hajahamia Radio One na kisha BBC. Halafu kule Zanzibar alikuwepo Yusuph Omar Chunda, zaidi namkumbuka kwenye kipindi cha michezo mida ile ya saa mbili kasorobo hivi nyakati hizo Small Simba na KMKM zikitamba kwelikweli kabla ya kuja Miembeni na Malindi.

Halafu kuna Michael Katembo huyu jamaa vipindi vyake alikuwa anavipamba mpaka utapenda kusikiliza tumbuizo asilia na mkoa kwa mkoa. Pale Mbeya baadaye akaenda Nswiiiiiima Ernest maarufu sana kwenye Majira na kuripoti matukio, halafu kanda ya ziwa alikuwepo Nathan Rwehabura. Siwezi kumsahau Jacob Tesha mwenye sauti nene yenye mkwaruzo hivi maarufu sana kwenye taarifa ya habari na External Service. Akisoma habari utapenda maana anasoma kwa utulivu na umahiri mkubwa. Lakini mwisho wa yote alikuwepo Ben Kiko, mzee mwenye mbwembwe na madoido ambaye kila ukisikia sauti yake ni lazima uvutike kumsikiliza. Waliokuwepo wakati wa vita ya Kagera wanasimulia jinsi walivyokuwa hawakosi kuketi pembeni ya redio zao kumsikiliza huyu bwana mkubwa akiwapa simulizi ya jinsi wazee wetu wa JWTZ walivyokuwa wakimvurumusha Amin.

Ama kwa hakika ya kale ni dhahabu na haina budi kutunzwa hata kwa kukumbukwa na kuenziwa tu. Asanteni sana watangazaji wetu, Taifa daima litawakumbuka.

Na Monsignor Phabby

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 32 mpaka sasa

  1. kweli "old is god" na hizo gigs mbili halali!

    ReplyDelete
  2. Mume Wangu, Mikanjuni TangaApril 17, 2010

    Sikuona jina la Abdul Omar Massod( Marehemu), ambaye alukuwa mtangazaji mashuhuri wa kipindi cha michezo cha saa mbili kasorobo na pia alikuwa katibu mwenezi wa Yanga. Wazee wa uwanja wa Fisi walikuwa wanamsikiliza hata saa tisa usiku huku wakiendelea kulamba kinywaji.

    ReplyDelete
  3. Mie ni mpenzi wa dhati wa hii blog lakini leo nimeona nami nitokee kwenye maoni kwa kweli nimeguswa sana na hii habari ya ya kale ni dhahabu. Nimefurahishwa mno kukumbushwa watangazaji wetu wa Redio pekee wakati huo. Alipotajwa Ben Kiko kwa kweli nimekumbuka mengi mno na hasa ile vita ya kumuondoa Nduli Amini. Asanteni Sana

    ReplyDelete
  4. Umenikumbusha mbaalisana mdau. Asante sana kwa kumbukumbu hii. Mungu akubariki. "we can feast from our memories!"

    Mdau wa Namanyere

    ReplyDelete
  5. Enzi hizo watu walikuwa wazalendo kweli.

    ReplyDelete
  6. kweli ya kale ni dhahabu, umenikumbusha mbali sana Mdau, unakumbuka kipindi cha ugua pole kila jumapili saa tatu baada ya kipindi cha watoto wetu?

    ReplyDelete
  7. Mmemsahau mtangazaji Akadoga Chiledi na sauti yake nzuri ya kunguruma.( Old is gold mwe)

    ReplyDelete
  8. Ni Club la Leo Show...

    ReplyDelete
  9. DUH HUYU JAMAA ANA KUMBUKUMBU SANA SIJUI KAZITOA WAPI?.. AMA KWELI KUTUNZA HISTORIA NI MUHIMU SANA, YAANI WENGINE TULIKUWA TUMESHAWASAHAU KABISA WATU MAHILI KAMA HAO. INABIDI KAKA TIDO MHANDO AWAFANYIE ANGALAU KA-GET TOGHETHER FULANI HIVI WALIOSALIA ILI ANGALAU KUWAENZI JAMANI.
    ASANTE SANA MDAU.

    ReplyDelete
  10. Mkuu wa Libeneke nashauri uwasiliane na wahusika waiweke hii article kwenye makumbusho yetu.

    Maana ni jambo la aibu sana nchi yetu haina electronic archives kabisa! Huyu jamaa ameelezea 90% ya RTD ya enzi hizo na inahistahili kutunzwa kama kumbukumbu.
    Imagine leo hii uki google majina ya hao watu ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa historia ya media industry yetu wala hawapatikani, ni ajabu sana!
    I also recommend that this article should be published so it can be available for electronic search engines!

    ReplyDelete
  11. Mwari Wangu, Kwa Wakwere LugobaApril 18, 2010

    Mnakumbuka mbwembwe za Ben Kiko siku alipofunga goli katika mechi moja iliyochezwa pale uwanja wa Jamhuri?? Huyu jamaa alijifagilia mpaka ikawa noma.

    ReplyDelete
  12. Mbona tumemsahau yule alikuwa anatangaza ngoma za utamaduni. KATEMBO. Mungu amlaze pema peponi. Huyu na Uncle Nyaisanga nadhani walianza wakati mmoja RTD. Dada yangu Sango Kipozi akisoma habari utachoka. Walipohamia Dom na mme wake Radio Dom ilinawiri. Liyongo kwenye habari utachoka.

    Tuseme ukweli wakati huo hatukuwa na radio nyingine zaidi ya KBC ya akina Mambo na vipindi vya huu ni uungwana?? Nakumbuka kila J. pili tukiwa tunakula chakula cha mchana hapo nyumbani baada ya misa ya mchana utasikia je, huu ni uungwana??? Leonard Mambo.

    Uncle J, kaka Kipozi, dada Sango (tulikuwa wote Dom nakumiss sana), Marehemu Katembo tunamiss ngoma zako hasa zile za watani wa jadi wa musoma.

    ReplyDelete
  13. kaka umemsahau marehemu iddi rashidi mchatta ,na majina haya kaka yalivutia wenyewe wakiyatamka kwa urefu Nswimwa ernest maraso, Bujaga izengo kadago sasa hivi makelele tu.

    ReplyDelete
  14. jamaa upo fit! Hongera sana! umenifurahisha sana ulipomtaja Abdul Ngalawa! huyu jamaa alikuwa kila siku ananivuta sebuleni kwa baba kumsikiliza nikitegemea ni hadith km za Bibi Debora! akianza tu story za kilimo au siasa nilikuwa naishiwa nguvu! Michael Katembo naye alitisha kwa nyimbo za asili!

    ReplyDelete
  15. Nae jamaa wa mtaani Dunstan "Tido" Mhando nae je? Enzi hizo alikuwa ni "brazzaman" wa nguvu na memba kiongozi waTangaline. Pia umemsahau Marehemu Saidi Omari Kassongo, hakuna atakae msahau huyu jamaa aliyeanza kama messenger tu na wala hajapata elimu ya kutosha lakini alikuwa na mdomo na mastori na upenzi wa mziki wa hali ya juu. RIP kaka Kassongo!!

    ReplyDelete
  16. Patrick TsereApril 18, 2010

    Hukumtaja mtangazaji KIHEMBA na mkewe Halima Kihemba (Mkuu wa Wilaya sasa Kibaha). Betty Chalamila(?) sasa ni Betty Mkwasa (Mkuu wa Wilaya Bahi).

    Kweli Old is Gold. Mimi nakumbuka mwaka 1965 wakati huo Mikidadi Mdoe (kwa sasa ni marehemu) ndiye akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Sauti ya TBC kabala haijawa RTD, walikuwepo watangazaji machachari ambao walifariki wote watatu kwa kugongwa na treni eneo la Shauri Moyo wakitokea kazini Sauti ya TBC. Hao walikuwa Salehe Ali,Kwegy Munthali wakiwa pamoja na Sulemani Maneno (?). Hao walikufa pale pale. Siwezi kusahau Daressalaam yote ilishikwa na majonzi. Hao vijana wakati ule walikuwa watangazaji wenye sauti za kuvutia sana. Mwingine alikuwa ni Raymond Chihota akitangaza kipindi ambacho kila kijana wa wakati ule alikuwa anakipenda. Kikiitwa Chipukizi Club. Hiki ndiyo kilikuwa muasisi wa mabugi jijini Dar. Baada ya Zimbabwe kupata uhuru Raymomnd alirudi kwao Zimbabwe. Sasa ni marehemu

    ReplyDelete
  17. Mwe.Mwana siku ya Ijumaa mida ya nane na dakika mbili mchana ilikuwa lazima nichelewe shule kwa sababu ya MAMA NA MWANA.Halafu hiyo mkoa kwa mkoa ilikuwa ni shule tosha ni kama vile mtu ushafika ufipani vile kumbe bado.Aisee.

    ReplyDelete
  18. dah! kwa hakika hii imeenda shule!
    vitu murua amevikumbusha hapa..
    ghafla umsikilize yule bwana wa huko kwenye mpira wa miguu, ukute ni simba na yanga..basi wewe utasikia "chama na mongellah, mogellah na chama wasikilizaji,lalalala goo! dah! kumbe mpira upo kati kati ya uwanja!!!!..mara mechi nyingine,unasikia "kampira na mpira kampira na mpira lalalalaa! dah unatoka nje pale!!!"....jamaa walikuwa wataalam. yule mama wa mama na mwana, alifanya watoto tupiganie redio mkulima siku ikifika!!
    enzi hizo nyimbo zimetulia saana,mfano "alfajiri upepo wa bahari umenijia...","zuwena","kifo","mwanameka" nk..baada ya taarifa ya habari,unasikia,"kama sio juhudi zako nyereree.." dah!! mara mnarushwa na kipande cha hotuba baba wa taifa... kudadeki!!
    hii imetulia sana!!
    mohsein

    ReplyDelete
  19. mama na mwana!!
    zile hadithi zilikuwa ni movies tosha,kwanza home tulikuwa hatuna TV,basi ukiisogelea radio ukasikiliza kwa makini unajikuta unaona movie fulani hivi,hadithi ikiisha kabla ya kufika mwisho(mara nyingi ilikuwa hivyo) hukawii kukosa raha!! au usikie sijui shule gani imeenda kumtembelea yule mama kule studio, unawachukia bila kujua hahha!! natamani kusikia hata kale ka wimbo kake, kalikuwa kanavutia sana!

    ReplyDelete
  20. Kaka umemsahau Dustan Tido Mhando kwenye michezo mida ya mbili kasoro robo.

    ReplyDelete
  21. hii kwweli imekwenda shule; wadau naomba mnikumbushe lolote kuhusu majira na mikingamo. hii nayo ilikuwa kali. bila ya kusahau migoma kabla ya taarifa ya habari na majira

    ReplyDelete
  22. Asante sana mdau kwa kutukumbusha mbali tulikotoka. Mwingine ni Swedi Mwinyi alikuwa akitangaza mpira na kusoma taarifa ya habari.

    ReplyDelete
  23. Duuh aisee hii ripoti imetulia.The best article of the year so far by far!!I was smilling all the way when reading it.MICHUZI,I think you should recognize such kind of contributors at the end of the year!

    ReplyDelete
  24. Michuzi,
    For the first time, mada iliyounganisha blog!
    Labda kwa vile watoto wadogo waropokaji hawana cha kuchangia!

    ReplyDelete
  25. Naomba ku-conclude. Ukweli ni kwamba, hisia za namna hii ni za kawaida katika maisha ya binadamu. Hata wale ambao ni wadogo sasa hivi watawakumbuka hivi hivi na kuwa miss watangazaji wa sasa (ambao nyie madai si mahiri). Wala hakuna jipya. Ni "nostalgia" tu hii.

    ReplyDelete
  26. KUNA MTU YOYOTE ANAKUMBUKA PWAGU NA PWAGUZI

    ReplyDelete
  27. ...mguu pande moja.. mguu sawa moja.. nyumaas geuka moja mbili tatu moja kushotoos geuka moja mbili tatu moja.... lol nikikumbuka kula kiapo cha chipukizi naumwaga mbavu ati nyumas geuka ha ha haaaa!

    ReplyDelete
  28. Naam, old is gold. Chaguo la msikilizaji ilikuwa kipindi nikipendacho sana. Malima ndelema...!
    Ua jekundu enzi zile ukikosa, umekosa bonge la muvi...
    Asante mdau kwa kutukumbusha mazuri ya zamani

    ReplyDelete
  29. Bro Michu tusisahau pia bwana Sekione Kitojo akituburudisha kwa mambo ya mipira, akirusha kipindi toka uwanja wa kirumba Mwanza

    ReplyDelete
  30. Umemsahau DOMINIC CHILAMBO---- alikuwa RTD kanda ya ziwa Mwanza, baadae alihamishiwa Mbeya, Kanda ya nyanda za juu kusini ambako alienda kufariki. R.I.P alikuwa akitangaza mpira wa Pamba sports club hutaki kuacha redio...

    ReplyDelete
  31. NA GODFREY MNENE TUSIMSAHAU. HII HABARI SI YA ZAMANI SANA. NI YA MIAKA YA KATI YA MWISHO YA 70 NA KUENDELEA NYUMA YA HAPO RTD HAIKUWA NA OFISI MIKOANI WATANGAZAJI WOTE WALIKUWA DAR, NI BAADAYE TECHNOLOGIA ILIVYOKUWA INAKUWA NCHINI NDO WAKAANZA KUSAMBAZA WATANGAZAJI KIKANDA NA MIKOA.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...