Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Muhammed Seif Khatib akizungumza na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo leo wakati wa mkutano wa sita wa baraza hilo unaofanyika jijini Tanga. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Sethi KamuhandaWaziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano
Muhammed Seif Khatib akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Muhammed Seif Khatib (katikati) akiwa na viongozi na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, utamaduni na Michezo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa sita wa baraza hilo leo jijini Tanga. Picha na Aron Msigwa - MAELEZO
WAFANYAKAZI WAHIMIZWA KUTUMIA
MAJADILIANO KATIKA KUTATUA MIGOGORO.

Na Aron Msigwa – MAELEZO, Tanga

Serikali imewataka waajiri, vyama vya wafanyakazi na watumishi wa umma kutumia njia ya majadiliano katika kutatua migogoro inayojitokeza ili kuepuka uvunjifu wa amani nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Muhammed Seif Khatib wakati akifungua mkutano wa sita wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo jijini Tanga.

Amesema wafanyakazi na viongozi wanao wajibu wa kuweka utaratibu wa kutatua migogoro inayojitokeza ili kuimarisha mahusiano mazuri katika sehemu za kazi na kuwataka kuzingatia utaratibu ulioanishwa katika sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma na 19 ya mwaka 2003

Amefafanua kuwa sheria hiyo ya mwaka 2003 imeweka utaratibu na kutoa mwongozo ambao unatakiwa kufuatwa na waajiri, vyama vya wafanyakazi na watumishi wa umma kwa ujumla katika kujadili maslahi ya watumishi kisekta kupitia mabaraza ya pamoja ya majadiliano.

Amesema nchi ya Tanzania inaongozwa kwa kufuata misingi ya Demokrasia na Utawala shirikishi ambapo vikao vya wafanyakazi ni muhimu sana kupitia mabaraza ya wafanyakazi ambayo hujadili masuala mbalimbali kwa maslahi ya wafanyakazi na Taifa.

Waziri Khatib ameendelea kufafanua kuwa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya kila raia kufanya kazi na kuongeza kuwa inatoa uhuru kwa kila raia kushiriki katika kutoa maamuzi.

“Nchi yetu ni nchi ambayo wananchi wake wanaamini katika Haki sawa kwa kila Mwanadamu kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 22 ya Katiba ya nchi yetu kwamba kila raia ana Haki ya kufanya kazi na vile vile katika Ibara ya 21 kifungu cha pili, kila raia anao uhuru wa kushiriki katika kutoa maamuzi kuhusu yeye binafsi , ustawi wa jamii au Taifa” amesisitiza.

Akieleza kuhusu baraza hilo la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo linaloendelea jijini Tanga amesema kuwa baraza hilo ni chombo muhimu cha kuhimiza utekelezaji wa kazi pamoja na kusaidia kubainisha njia bora za kutekeleza malengo ya wizara kutokana na kuwahusisha wafanyakazi wenyewe .

Aidha ameogeza kuwa ushirikiano wa Baraza la wafanyakazi na menejimenti katika wizara hiyo utasaidia sana katika kuleta ufanisi na tija katika sehemu za kazi.

“Bila shaka vikao vya aina hii vinasaidia sana kupunguza madukuduku na kero za wafanyakazi hivyo kuchochea ari ya kufanya kazi na kujiletea maisha bora kwa mfanyakazi binafsi na hatimaye Maisha bora kwa kila Mtanzania” Amesema Waziri Khatib.

Ameendelea kufafanua kuwa kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ni nyenzo muhimu sana katika kuwauanganisha wafanyakazi na kuondoa migomo na migogoro na hivyo kulinda heshima na dhima kubwa iliyonayo wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa Watanzania.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Wizara ya Habari na Michezo Bw. Sethi Kamuhanda amesema mwendelezo wa vikao hivyo kwa wafanyakazi ni ishara nzuri kwani hutoa fursa nzuri kwa wafanyakazi kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji na hivyo kuleta tija na ufanisi katika utumishi wa umma.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Clement Mshana akizungumza kwa niaba ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo amesema kuwa wajumbe watayatekeleza maazimio yote yatakayoafikiwa katika mkutano huo kwa lengo la kuleta ufanisi na utulivu ndani ya Wizara.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...