Mgombea urais kwa tiketi ya
CHADEMA Dk. Wilbroad Slaa


Ndugu wana JamiiForums, Mtandao wa IssaMichuzi, wana FaceBook na mitandao mingine na Watanzania wenzangu wote kwa ujumla mtakaosoma ujumbe huu, Salaam toka Mbeya Vijijini, ndio tumeanza mikutano midogo ya kufunga kazi asubuhi hii na tutahitimisha baadaye.

Ninashukuru sana kwa maneno ya heri kwa siku yangu ya kuzaliwa hapo jana na ningekuwa sina shukrani kama ningeacha ipite bila kusema asante kwa maneno mema mliyonipatia humu na kwenye facebook na hata waliopata nafasi kwa njia ya simu. Ninawashukuru vile vile kwa mashauri mbalimbali, na pia kwa sala na dua zenu.

Ninashukuru sana na ninaona fahari kuwa ni mwanachama mwenzenu.

Kampeni zote zinaisha leo na kesho ni siku ya Uchaguzi Mkuu kama mnavyofahamu. Kwa upande wangu nimetembelea karibu maeneo yote ya nchi yetu kubwa, nimekutana na watu mbalimbali na nimeona mengi. Nimeona mengi yenye kutia matumaini na faraja na nimena mengine ya kuhuzunisha na kukatisha tamaa. Yote kwa ujumla yake yamenipa picha ya kuelewa zaidi Taifa letu hasa kuhusu mafanikio tuliyoyapata mpaka hivi sasa na changamoto tulizonazo.

Ninaelewa vizuri zaidi sasa kupitia mang’amuzi binafsi hali ya Taifa letu ilivyo na ya kwamba ni lazima tubadili mwendo na huko tunakokwenda maana tutafika mahali ambapo tutashindwa hata kujiuliza tulifikaje. Watu makini hawawezi kuendelea na njia ambayo wanajua wamepotea. Kuendelea kung’ang’ania kwenda wakati mnajua mmeshapotea ni kutukuza kiburi cha kujiona. Taifa letu limepotea njia na hata kama tukijitahidi kwa nyimbo na masimulizi mbalimbali kuhalalisha huko tunakokwenda bado tutakuwa tumepotea.

Ni kwa sababu hiyo nilipoombwa kugombea Urais nilitambua uzito wa mzigo huu mkubwa kwani utahusiana moja kwa moja na kubadilisha mwelekeo wa taifa letu na kuanza kutengeneza pale palihorabiwa, kuinua kilichoanguka na kumwagilia kilichoanza kunyauka. Hili linahitaji mawazo mapya, uthubutu wa kiuongozi na mtazamo mpya wa nini Taifa letu linahitaji. Ndugu zangu, Taifa letu linahitaji mabadiliko makubwa ili tuweze kujipa sisi wenyewe na watoto wetu nafasi ya kuweza kufanikiwa huko mbeleni.

Mabadiliko haya siyo mabadiliko ya mapambo yaani kuhamimisha maua na vitambaa sebuleni wakati nyumba inanuka na nichafu. Wote mliosikiliza au kumwangalia mgombea mwenzangu jana ni wazi hana ahadi ya mabadiliko yoyote makubwa isipokuwa mwendelezo wa yale yale yaliyotufikisha hapa. Ni kutokana na hilo natambua kuwa kura ya kesho siyo kura ya kawaida; siyo kura kama ya 2005 au ya miaka kabla yake.

Kura ya kesho ni kura ya kuchagua kuendelea na vile tulivyo kwa miaka mitano ijayo au kubadilika ili tuanze upya kwa njia sahihi na kwenda ambako sote tunakujua tunataka kwenda. Ninaamini tunachohitaji ni mabadiliko yatakayoanzisha mwamko wa kuanza kulijenga upya taifa letu. Hili ndilo lililonifanya nikubali pale Chama changu kiliponiomba ninyanyue bendera ya Chadema kwenye uchaguzi huu katika nafasi ya Urais.

Naweza kuwaahidi mengi na kwa maneno matamu ya kila aina. Hata hivyo ninawaahidi kitu kimoja kwa uhakika wa asilimia 100. Mkinichagua kuwa Rais wenu na mkiwashawishi ndugu, jamaa na marafiki zenu kufanya hivyo nami nikachaguliwa, nitawapatia uongozi ambao utaifanya miaka 49 iliyopita kuwa ni ya masimulizi ya njozi za jinamizi kwani nitaongoza timu ya watu ambao watakuwa wamejitokea muda, elimu, ujuzi na vipya vyao katika kujenga taifa letu upya. Katika miaka mitano ijayo tutafanya mambo ambayo CCM na utawala wake imeshindwa kufanya kwa karibu miaka hamsini.

Tutawapa nafasi Watanzania hatimaye nao wafurahia matunda ya uhuru wao na vile vile kuweza kuanza kujenga Taifa la kisasa ambalo litakuwa ni tamanio nakinara cha mabadiliko ya kiutawala, kiuchumi na kiutendaji katika Bara letu. Tuna uwezo, tuna sababu na tuko tayari kuwatumikia.

Naomba sana kura zenu hapo kesho ili niwe Rais wenu katika awamu ya tano. Kura yako ina nguvu ya kubadilisha mwelekeo wa taifa letu. Usiuze, usiache kuitumia na pale utakapoitumia itumie kwangu, kwa wagombea Ubunge Chadema na wagombea wetu wa Udiwani ili tuweze kuhakikisha yote tuliyowaahidi tutayatimiza na zaidi.

Msiwe na shaka, hata toka Ikulu nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa mitandao hii na kuwapa taarifa mbalimbali moja kwa moja na kujibu maswali mtakayokuwa nayo kuhusu serikali yenu pale inaponipasa mimi kutolea kauli. Asanteni!!

Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. Happy birthday our president from 1st November 2010. Expecting many from you Dr.

    ReplyDelete
  2. God bless Tanzania,bariki uchaguzi,bariki wapiga kura wafanye uchaguzi sahihi kwa mtu sahihi kwa masirahi ya nchi yetu na vizazi vyote.Amen.
    "CHAGUA MTU SI CHAMA"

    ReplyDelete
  3. Kila ninaposoma au kusikilza hotuba zako napata faraja na matumaini mapya ya kuwa yupo mtu anayeweza kutambua,kuona, kukemea kwa dhati na kusema ukweli kwamba nini tunahitaji watanzania kwa sasa.

    Hakuna ubishi kuwa mabadiriko ndiyo yanayotakiwa na labda kikubwa nikuombee inshallah mwenyezi mungu akuongezee nguvu, hari na uishi miaka mingi zaidi ili siku moja uone basi watanzania tunafika kule tunakostahili tukiwa katika mstali mnyoofu.

    Umejitahidi sana na mimi kama kijana siku zote nimekuwa nikijifunza kutoka kwako na nikitamani watanzania na viongoze wetu wote basi tungekuwa wakweli kwetu wenyewe na si kuhubiri tusichokiamini.

    Inasikitisha sana, kama leo hii naulizwa nini hali ya nchi huko nilikopita natoa majibu yanayostahili kutolewan ama na mamlaka ya hali ya hewa tanzania (TMA) ama na watu wa food security.

    Ni aibu kwa Taifa zima na sisi sote wanafiki tunaopiga makofi ya kinafiki, ili muda uende. Imefika wakati tukemeane wenyewekwa wenyewe kuanzia majumbali hadimashuleni.
    Jukumu ni letu watanzania kupiga makofi na kushanglia kama kawaida yetu bila kujali kilichosemwa kuwa kina tija au maana hasa kwetu kama watanzania au kusema sasa tutapiga makofi mara chache iwezekanavyo na pale tu panapostahili makofi na vifijo.

    ReplyDelete
  4. Ushundi ni wako baba. Nuru mpya ya Tanzania!!!

    ReplyDelete
  5. Nakushukuru saaaana Mr. Ankal kwa kuweka ujumbe huu wa Raisi mtarajiwa na makini kwenye blogu hii ya jamii, japo umebana mambo kadhaa mpaka dakika ya mwisho.

    Sasa tupime, tuamue wapi tunataka kwenda. Baadaye tusiwalaumu watani wetu wa jadi, au wageni wawekezaji kwa hali tutakayokuwa nayo hapo baadaye.

    Uamuzi uko mikononi mwetu, kama kweli tumepata elimu-dunia vizuri, maamuzi yetu hapo kesho yatakuwa ya kimapinduzi!!

    Hapa tumeombwa kura, tofauti na baadhi ya wagombea wengine wanaongea mpaka mwisho bila kusema wanataka nini!!

    ....na ukiombwa, usiwe myimi!!

    Vidumu vyama vyote!!

    ReplyDelete
  6. Mtanzania asiye na woga, MwanzaOctober 30, 2010

    Sisi wenye upeo wa kuona mbali tunakubaliana moja kwa moja na maelezo yote uliyotupa na kwa hakika KURA zetu ni kwa CHADEMA tu.
    Tatizo ninaloliona mbele yetu ni woga wa Watanzania wenzetu wa kubadilika hata wakati wa hatari, lakini safari hii watabadilika .
    Mungu Ibariki CHADEMA
    mUNGU ibariki TANZANIA

    ReplyDelete
  7. Kauli nzito, Mungu afanikishe azima ya kulinusuru taifa letu

    ReplyDelete
  8. Uliombwa ili ulete mabadiliko ya haliambayo umeiona wakati wa ziara za kampeni, mbonaunajichanganya? Kikwete amefanya mengikatika nchi yetu, uchumi umekuwa mkubwa,wa pili sasa africa mashariki, vigogo wamefikishwamahakamani kwa mara ya kwanza katika historia yetu, uhuru wa watu, mitandao, magazeti na vyombovingine haujawahikutokea, amani zanzibar just to mention a few. Wananchi tuchague Amani,tusichague ukoo, ukabila na udini. Tusidanaganyike na ahadi za uwongo kwa dhahiri,upunguze kodi za bidhaa halafu ugharamie huduma za jamiibure inawezekanaje? Tuchague Maendeleo na elimu bora. Tumchague Kikwete apate zaidi ya asilimia 90 safari hii!

    ReplyDelete
  9. Dr. Slaa anajigamba, "Katika miaka mitano ijayo tutafanya mambo ambayo CCM na utawala wake imeshindwa kufanya kwa karibu miaka hamsini."

    Maneno matamu; ahadi tamu! Labda ya kuingiza kimada hapo Ikulu! Ikulu ni patakatifu! Kamwe kuingiza vimada hapo Ikulu!

    Hivi nikweli kuwa TANU/CCM haikumfanyia chochote huyo Dr. Slaa?

    ReplyDelete
  10. Dr. Slaa asante kwa kututumia salamu.

    Good luck Dr. Slaa & God bless you!!

    (US Blogger)

    ReplyDelete
  11. NDUGU ZANGU WATANZANIA TUBADILIKE NA TUMJARIBU HUYU JAMAA KIUKWELI TUMESHA POTEA NA TUKIFANYA KOSA MIAKA MITANO IJAYO HALI ITAKUWA NGUMU KIASI HATA MKATE UTALIWA KWA KUTEGEMEA RUSWA SIO MSHAHARA TAFADHALINI TUMCHAGUE SLAA ILI TUOKOE WATOTO WETU NA WAJUKUU WETU

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...