Msanii maarufu wa filamu nchini James Michael (JB) akiwaeleza wajumbe wa kikao kazi cha nane cha sekta ya Utamaduni ushuhuda juu ya mafanikio yake binafsi kwenye tasnia ya filamu.Alitoa historia na changamoto zilizomkabili.

Msanii Mrisho Mpoto akitoa ushuhuda kuhusu sekta ya sanaa nchini na hali ya wasanii kwa ujumla mbele ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Vijana na Michezo,Dkt.Nchimbi.Upande wa kushoto wa waziri ni Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni,Profesa Hermans Mwansoko.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Vijana na Michezo Dkt.Emmanuel Nchimbi katika picha ya pamoja na washiriki baada ya kufungua rasmi kikao kazi cha nane cha sekta ya utamaduni nchini kinachoendelea jijini Mwanza.
Na Mwandishi Wetu,Mwanza
Waziri wa Habari,vijana,utamaduni na Michezo Dkt.Emmanuel John Nchimbi jana Jumanne amekifungua rasmi kikao kazi cha nane cha sekta ya utamaduni nchini kinachoendelea jijini Mwanza huku akitoa miezi sita kwa vazi la taifa kuwa limepatikana.

Pamoja na kutoa miezi hiyo sita kwa vazi la taifa kuwa limepatikana,Dkt.Nchimbi aliwahimiza watendaji wa sekta ya utamaduni kusisitiza matumizi ya sanaa za asili katika kada mbalimbali hapa nchini huku akitaka kasi iongezwe katika ukusanyaji wa takwimu mbalimbali zihusuzo wasanii na sekta ya utamaduni kwa ujumla.

“Moja ya mambo ambayo niliyaacha wakati nikiwa naibu waziri wa wizara hii ni suala la vazi la taifa,mchakato wake umekuwa ni wa muda mrefu sijui kwa nini.Sasa naagiza vazi hilo la taifa lipatikane ndani ya miezi sita kunzia sasa” alisisitiza Dkt.Nchimbi.

Aidha,aliwataka wasanii nchini kubuni sanaa zilizo bora, zenye kubeba maadili ya mtanzania na zinazoweza kuuzika kimataifa ili kuweza kujiongezea kipato.Pia alitaka elimu zaidi kutolewa kwa wasanii ili wajue umuhimu wa mikataba katika kazi zao.

Awali, akimkaribisha mheshimiwa waziri kwenye Kikao hicho,Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni,Profesa Hermans Mwansoko alisema kwamba, Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo imepata waziri kijana na sahihi ambaye atakuwa ni chachu ya mabadiliko katika sekta ya utamaduni.
Pia alimpongeza waziri aliyekuwa kwenye wizara hiyo,Mh.George Haruna Mkuchika ambaye kwa sasa amehamishiwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa utendaji wake huku akipongeza uteuzi wake kwenye wizara hiyo mpya ambapo sasa maafisa utamaduni wote watakuwa chini yake na yeye anaifahamu vema sekta hii nyeti nchini.

Akizungumzia kikao cha nane cha utamaduni kinachoendelea jijini hapa,Profesa Mwansoko alisema kwamba, kinalenga kujadili masuala mbalimbali yahususuyo sekta hii ikiwa ni pamoja na changamoto sugu zinazoikabili na baadaye kuja na njia mbadala za utatuzi.

Kikao cha sekta ya Utamaduni kinachoendelea jijini Mwanza kitafikia tamati Ijumaa ya Desemba 12, 2010 na jana wajumbe walipata wasaa wa kuelezwa hali ya tasnia ya filamu nchini ikiwa ni pamoja na kupata ushuhuda wa msanii maarufu wa filamu James Michael (JB).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. Hatuwezi kupata Vazi la Taifa bila ya kuwa na viongozi wanaopenda taifa. Kwani watu wengi wanaangalia viongozi kama role model na sio mkae mtengeneze vazi na kulipigia kura. This is just coming as you have leaders as role models ambao wanaonyesha vazi fulani ndio identity yao. Tafadhali msipoteze muda wenu fuatilia dunia nzima utaona haikutokea kwa kutoa amri au kuwashindanisha watu.....!!!

    ReplyDelete
  2. Vazi la taifa halibuniwi bali hutokana na mavazi wanayovaa wananchi wanaojali utamaduni wao. Tumekwisha kuwa na mavazi mengi sana tukianzia na yale yaliyokuwa yakivaliwa na wanasiasa wetu mara tu baada ya uhuru na kutelekezwa kwani yalikuwa yanasili ya Ghana kwa Nkhuruma. Wapo watu ambao waliwahi kubuni na kuzawadiwa lakini hayakuwa na utamaduni wetu; Bahati mbaya wengi wetu nhatuupendi wala kuujua utamaduni wetu hivyo mavazi wa asili ya makabila yetu tunayaona kuwa ni ya kishamba sasa sijui hilo vazi jipya litakuwa ni la nani, wakazi wa mjini tu, wanaccm tu, wabunge tu au wanaokwenda nje ya nchi? Ninauhakika baadhi ya makabila wanayo mavazi yao sijui kama yatapigwa marufuku kwani hayatakuwa rasmi. Mwisho labda kurahisisha mambo vazi analovaa Nchimbi liwe ndilo vazi rasmi la taifa. Kwa kifupi vazi la taifa halipatikani kwa amri.

    ReplyDelete
  3. Vazi la Taifa la nini jamani, hebu nielimisheni mimi mbumbumbu?

    ReplyDelete
  4. Jamani mbona badal ya kwenda mbele twarudi nyuma? Hivi vazi la taifa ni la kulazimishwa? Vazi la taifa ni ridhaa ya wavaaji na si jukulu la serikali. Kazi ya serikali ni kuliendeleza tu. Najiuliza: 1.Hivi hilo limo katika hadidu za rejea alizokabidhiwa Mhe. Waziri? 2. Je limo katika ilani ya CCM ili ilitimize kabla ya uchaguzi? kama sivyo na hata kama ndivyo, nafikiri kuna mambo mengine muhimu zaidi ya kufanyiwa kazi. Hili la vazi si LAKUSHURUTISHWA. Washabiki wa hilo labda waangalie historia na kuona jinsi akina Sankara na wengine walivyojaribu na kukwama.

    ReplyDelete
  5. Ninamuunga mkono Khadijah kwa asilimia mia. Mimi ni mmojawapo ya wadau ambao wamekuwa wakitoa maoni yao katika blogu hii kwa kuangalia viongozi wa kitaifa wanavyovaa na pia kwa kusoma maoni ya baadhi ya wadau wanaolalamika kila wakiona mtu (mwanamume) hakuvaa suti ya ulaya katika hafla rasmi. Kwa kumuunga mkono Khadijah nitoe mfano wa suti ya kiafrika iliyoshika kasi katika kizazi cha kwanza cha viongozi wa nchi za Afrika baada ya uhuru (1960s-1980s). Akina Nyrere hawakukaa chini na kupiga kura, bali walivaa suti hiyo na ikawa kama ni kaida na hatimaye ikatambuliwa kama vazi rasmi na kuingizwa kwenye nyaraka za protokali kama vile vazi linaloruhusiwa katika hafla rasmi za kitaifa. Suti ya afrika ilikuwa utambulisho wa Afrika na ushahidi kwamba waafrika nao wanaweza kubuni kitu chao. Zaidi ya hapo, ubunifu uliendelea kujidhihirisha kwa wabunifu wa mitindo kuja na staili mbalimbali. Hicho ndio tunakita sustainable creativity angaa katika uwanja huo. hakuna anayekaa chini kupiga kura. Ushahidi ni ni hapa kwetu suti ya afrika ilianza kama ilianza kutokuwa na ukosi, ikachukua ukosi (ikijulikana kama kaunda suit)na mikono mifupi, na staili mbalimbali za mifuko na vifungo, na leo hii imechukua mikono mirefu pamoja na staili mbali mbali za mifuko na vifungo - ni maridhawa pamoja na kwamba imefanywa second class. Kwa maoni yangu huwa namuona Rais JK anaappear more of a statesman akiwa amevalia suti hii kuliko anavyokuwa amevaa suti ya ulaya ambapo anaonekana kama mwigizaji - Washington/London-approved business attire!!!!

    ReplyDelete
  6. Dalili tosha kuonyesha jinsi tusivyo na vipaumbele...kuna masuala mengi ya msingi hatujayatatua tunakimbilia kulazimisha "vazi la taifa". Viongozi wetu kila mara huibuka na kauli zenye utata. Kuna haja ya hawa viongozi kutafuta ushauri kabla ya kubwabwaja maneno...oh mara vazi la taifa, oh...mara viongozi tusivae suti....

    ReplyDelete
  7. Wed Dec 15, 04:18:00 PM, umeandika, "Kwa maoni yangu huwa namuona Rais JK anaappear more of a statesman akiwa amevalia suti hii kuliko anavyokuwa amevaa suti ya ulaya ambapo anaonekana kama mwigizaji - Washington/London-approved business attire!!!!"

    Mwanaharakati mmoja wa mjini Kingston, Jamaika, aliandika akilalamika msafara wa Rais Kikwete kuingia hapo kisiwani wakati wa usiku. Zaidi, alilaamika kumuona Rais Kikwete akiteremka kutoka nadi ya ndege huku amevalia suti ya k-Magharibi.

    Mwanaharakati huyo, aliandika, "the man did not even cut a dash' ..."

    Alitegemea sana awasili wakati wa mchana sio usiku ili apokelewe na watu wengi.

    Wanaharati wengine waJamaika wanapenda sana kuvaa mashati ya vitenge au dashiki; ndio maana ya kumlaumu Rais Kikwete kuvaa hiyo suti ya ki-magharibi.

    ReplyDelete
  8. Tanzania haijawahi kushurutishwa kuwa na vazi la Taifa. Tuna makabila zaidi ya 120 na dini tofauti na kila mtu yuko huru kuvaa anavyotaka. Huu ukomunist Nchimbi anautoa wapi? Kwamba unaamka asubuhi na kutoa amri watu wawe na vazi la taifa? Je vitu kama hivi vinahitaji kujadiliwa kwenye Bunge ambalo linawakilisha wananchi na kutunga sheria? Hatuhitaji kuwa na uniform kuonyesha patriotism. Tanzania inakwenda mbele sio kurudi nyuma.

    ReplyDelete
  9. Tunataka maji safi, umeme, ajira, kuboreshwa kwa mfumo wa elimu, viongozi bora, mikataba wazi ya uwekezaji na kadhalika na sio vazi la taifa. Teyari tunavaa vazi la taifa linaitwa umasikini.

    ReplyDelete
  10. Wadau dhana ya vazi la taifa haina maana ya kuwalazimisha watu wsivae jinsi wanavyopenda - sio ukomunisti wala nini - bali ni vazi ambalo watanzania watatarajiwa kulivaa katika shughuli/hafla rasmi za kiserikali/kidola (something close to business attire in western culture - ambayo ndio imetokea kuwa vazi rasmi kwa dunia nzima). Kwa mfano vazi la taifa la marekani ni suti kama unayoona Mhe JK anatinga kila anapokuwa katika hafla rasmi kama vile kuwaapisha mawaziri au kuhutubia bunge. Suti hiyo hiyo ndio Maseneta wa Marekani huwa wanatarajiwa kuvaa wakiwa ndani ya ukumbi wa mijadala!! Hilo ndilo vazi la taifa la Marekani. Wadau wa utamaduni wanacholilia ni kwamba tunaweza kubuni suti ya kitanzania (hawasemi mavazi ya jadi kwa sababu utamaduni hukua na kubadilika na pia huwa kielelezo cha ubunifu wa jamii) ambayo ndio hiyo tutatarajia kumwona Rais akiwa amevaa wakati anahutubia bunge, wakati anawaapisha mawaziri, wakati anampokea Rais wa Marekani (kumbuka Rais wa Ghana alipompokea Rais Obama alikuwa amevaa nini? - hilo linaweza kukueleza kwa nini waGhana wako mbele yetu hatua zaidi ya kumi- creative mind, innovative mind, proud of themselves, more democratic, nk.

    ReplyDelete
  11. Mitumba inatutosha na hatuna hata pesa ya kuinunuwa, na imeshauwa viwanda vyetu. Tunahitaji umeme na maji safi sasa, matibabu na elimu kwa watoto wetu.

    ReplyDelete
  12. Hata siku moja vazi la taifa halibuniwi na hata siku moja huwezi pigia kura vazi la taifa.

    Muangalie Mpoto vazi l;ake ni zuri lenye utambulisho wa afrika na urudi kwa waziri na suti ya kimagharibi.

    Chakuchekesha hata muziki wa Tanzania hatuna yaani huwezi kwenda sehemu mtu akasema mziki wa Tanzania huo zaidi waweza kujua wa tanzania kwa kuwa tu unaimbwa kiswahili.

    Bongo kweli ukiwa waziri mtelemko ni kuamuru hata visivyohitaji amri.

    Ndio maana Bongo kuna wawekezaji wa kichina wanauza karanga za kukaaanga na kitchen utensils kariakoo hii yote ni kwa sababu wanatakiwa kusimamia mambo ya msingi wamelala tu

    ReplyDelete
  13. Wewe Thu Dec 16, 02:31:00 AM hakuna mdau anayesema kuhusu kulazimishwa kuva bali wanasema vazi hilo halipatikani kwa kutoa amri, pia tusiwe kama kuku kwa wepesi wa kusahau kwani wakati wa Sumaye akiwa waziri mkuu liliwahi kuwepo shindano la kupata vazi la taifa na mshindi kupatikana na kuzawadiwa;Ninakumbuka vazi hilo lilikuwa linabendera ya taifa sasa tutamtaka huyo mshindi arudishe zawadi yetu! Au Nchimbi halipendi kwa sababu yeye hakushirishwa au kwa sababu halina bendera ya ccm? Hivi akija waziri mwingine naye atataka vazi jingine la taifa si tutajikuta kuwa taifa la kubuni vazi la taifa na si mambo mengine muhimu tunayotakiwa kuyabuni?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...