Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego (Kushoto) akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa baraza hilo.Wengine kutoka kulia ni Hassan Bumbuli Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) na Ruyembe Mulimba, Mratibu wa program hiyo.
Muandaaji wa Muziki kutoka Studio za MJ, Joachim Kimario ‘Master J’ (Kulia) akichangia mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa, BASATA.Kulia kwake ni muandaaji mwenzake Allan Mapigo.
Mtangazaji wa vituo vya redio na TV vya East Africa Anna Peter hakuwa nyuma katika kutoa dukuduku lake kwani lawama zilielekezwa kwa watangazaji kwamba, wamekuwa chanzo cha kudidimia kwa muziki wa kizazi kipya.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa la BASATA wakifuatilia kwa makini mjadala kwenye jukwaa hilo mapema wiki hii.

Na Mwandishi Wetu

Waandaaji mahiri wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini Joachim Kimario (Master J), Lamar na Allan Mapigo wamedai kwamba,muziki wa kizazi kipya maarufu kwa jina la Bongo Flava umepoteza muelekeo na juhudi za makusudi zinahitajika katika kuurudisha kwenye mstari na kuupa utambulisho wa kitanzania.

Wakizungumza katika mjadala mkali kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa, waandaaji hao wa muziki walitupa lawama kwa watangazaji wa vituo vya redio na TV kwamba ndiyo chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa muziki huo kwa kile walichoeleza kwamba, hakuna utaratibu wa kuchuja nyimbo kabla ya kwenda hewani na baadhi hawana utaalam wa kazi zao.

Aidha, waliongeza kwamba pamoja na wao kujitahidi kuandaa midundo kwa kufyonza kutoka jamii za kitanzania, wasanii wa hapa nyumbani wamekuwa ni wa kuiga kila kitu wanapoingia studio na hawako tayari kubadilika wanapoelekezwa hali ambayo imeufanya muziki uhame kutoka kuwa wa jamii ya Tanzania na kuwa ule wenye kunakiri kila kitu kutoka nje hususan Marekani.

“Kwa sasa wasanii wanachokifanya ni kusikiliza muziki wa nje na kuja kuingiza kwenye muziki wao.Wamekuwa wakikopi kila kile msanii wa nje anachofanya kuanzia kuvaa na kuimba, wanataka wafanane na Jay Z hata wakija studio wanataka watengenezewe sound (midundo) kama ile ya nje” alisema Lamar kutoka Studio za FishCrab.

Kwa upande wake Master J ambaye ni mmiliki wa Studio za MJ alisema kwamba,siku hizi wanamuziki hawaangalii mazingira ya jamii za kitanzania tofauti na zamani, wamekuwa ni wa kuimba mambo yasiyofaa na yasiyopatikana katika jamii yetu bali ile ya Marekani hali ambayo imezidi kuutokomeza muziki wa kizazi kipya.

“Zamani tulikuwa na Hip Hop kama za akina 2 Proud ambaye kwa sasa anajiita Mr.Two (Sugu).Walikuwa wanaimba Hip Hop yenye kubeba matatizo halisi ya jamii ya Tanzania , Sugu aliimba nyimbo kama mikononi mwa polisi, miaka chini ya 18 na zote mbali ya kugusa matatizo yaliyopo ya jamii zilipendwa na kufanya vizuri tofauti na sasa” alisisitiza Master J
Aliongeza “Ujio wa redio na televisheni zisizozingatia utaalamu (professionalism) kwa watangazaji wake bali swaga (ujanja ujanja) na vipaji tu vya kuongea ni moja ya sababu ya kupoteza dira kwa muziki na hapo ndipo mambo yalianza kuharibika”.

Katika Jukwaa hilo la Sanaa pamoja na waandaaji wa muziki hao kutoa michango yao kuhusu mwenendo wa muziki wa kizazi kipya nchini, Mtaalam wa muziki John Ndumbaro alitoa maelezo ya kina kuhusu sekta hiyo ya sanaa ambapo mada ilikuwa ni Changamoto Katika Kutengeneza Muziki wenye Utambulisho wa Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Uzuri ni kwamba bado tuna wasanii wachache ambao wameendelea kuiheshimu sanaa. Lakini, kwa bahati mbaya, hawapewi nafasi wanayostahili kwenye vyombo vya habari; kama MJ na Lamar walivyosema hapo juu.

    Ma-DJ ambao wanaendelea kutuletea UPUUZI huu tunawafahamu. Sasa, tuwafanye nini? Vyombo vya habari ambayo vinaajiri watu ambao hawana ujuzi wowote kuhusu muziki navyo tunavifahamu.

    Wakati tunarusha lawama, nadhani itakuwa vizuri tukijiangalia sisi wenyewe pia. Kwani tukisusia kazi za wasanii wabovu wanaopewa promo kutokana na "swagga" tu, itakuwa vipi? Labda wanafanya wanachofanya ili kukidhi soko la watu wanaopenda vitu vya fasta-fasta.

    Wanaoipenda Bongo Hip Hop sio vibaya mkichungulia hii playlist:

    http://vijana.fm/about/projects/bila-sanaa/

    ReplyDelete
  2. SOSSY FORREALFebruary 15, 2011

    STEVE NYABERO Umeongea Ukweli Mtupu hapo Mtu mzima.

    Na LAMAR hajakosea , msanii anamuiga JAY Z na anabebwa na MaDJ Uchwara.
    JOH MAKINI ndio ANAONGOZA KuMkopi JAY Z

    ReplyDelete
  3. Hii inatokana na ule utamaduni wa MaDJ kusimamia wasanii (Management) na hivyo hulazimika kuwapa nafasi za upendeleo bila ya kujali ubora wa kazi. Wakati mwingine ni suala la "Kitu Kidogo" yaani msanii anapeleka nyimbo na anaacha na elfu 50 ili kazi yake ipewe upendeleo.
    Vile vile wasanii wengi wa kizazi kipya ni vijana wasio na ajira wala elimu yya kutosha hivyo hulazimika kufanya kazi amabazo wanahisi zitwapa mafanikio ya haraka.

    ReplyDelete
  4. Vituo vya redio vimekuwa vingi na bado vnaanzishwa kila siku,hiyo si vibaya ni maendeleo,tatizo linakuja kwenye huu utitiri wa watangazaji ambao hawajui hata muziki wao wamekazana ku promot miziki ya ajabu ajabu bila hata kuangalia ubora wa muziki,lawama zaidi ziende kwa watangazaji,na baadae ziwarudie wasanii wa kizazi kipya,wengi wao hawana ule ujuzi wa kuujua muziki vizuri,wamevamia fani hii tu kwa kuwa wanaona wenzao wanarekodi na kupata majina,pesa haraka haraka,lakini unakuta muziki huu haudumu kamwe,unakuta wimbo unasema"paka kapanda baiskeli,na kuku kavaa raizoni????"sasa hizo ni nyimbo kweli??ndio maana zamani redio Tanzania walikuwa na kamati ya kufuatilia nyimbo na miziki kwa ujumla kabla ya kurekodi.tuangalie mambo haya kabla muziki wa Tanzania haujaangamia.mwanamuziki mkongwe.
    "Majuu"

    ReplyDelete
  5. Mambo gani haya, Sossy? Unataka wale wa kamati wa 'taarifa za kiitelejensia' waanze kunisaka mzee?

    Kuhusu suala la elimu ya kutosha, mbona kina Jay Mo, Daz Nundaz, Solo Thang, Juma Nature na wengi kibao walikuwa wanaandika mashairi mazuri miaka ya tisini, wakati wapo O-level? Baadhi walianza kupata umaarufu wakiwa kidato cha pili. Inakuwaje leo hao hao wa kidato cha pili au cha tatu ghafla wanashindwa kuumiza vichwa? Ukishafikiria na kujibu hayo basi utaelewa tatizo liko wapi hasa.

    Muziki ni sanaa; mhusika anahitaji kipawa kwanza. Kama unavyojua, shule zetu hazifanyi chochote kukuza vipaji vya vijana. Kwa kifupi, watu ambao hawana vipaji na ufahamu wa mambo yanayotokea kwenye jamii ndio wanapewa kipaumbele sasa hivi (sio wote lakini).

    Jiulize itakuwa vipi mmoja wa "wabana pua" akipelekwa kwenye jopo la manguli wa muziki duniani.

    Au, kama upo ughaibuni, wasikilizishe marafiki zako kutoka Afrika na mabara mengine nyimbo mbili kutoka Tanzania: Free Soul (Grace Matata) na wimbo wowote ule wa mmoja wa "wabana pua". Halafu, subiri matokeo.

    Kama 'wataalamu' walivyosema, kama huko juu kungekuwa na "vichwa" vinavyoweza kupembua kipi ni pumba na kipi ni mchele, basi tusingefika hapa tulipo. Tumeimbishwa "kuku kapanda baiskeli" mpaka wagumu tusiopenda upuuzi tukaanza kuupenda. Baada ya wiki hivi tunajishtukia na kuficha kaseti (kama ulikuwa tayari umeinunua).

    Wahusika wafanye jaribio dogo tu: waanze kuajiri watu wawili-watatu ambao watachukulia kazi za wasanii (muziki) kama sanaa; sehemu ya fasihi. Watu hao wapewe vipindi vyao - hata kama ni mara moja kwa wiki. Nina uhakika hawa watu watakuwa wanapiga nyimbo tofauti kabisa kulinganisha na kinachopewa nafasi sasa hivi!

    Wale wanaofuatilia muziki wa "Kizazi Kipya", mmeshawahi kusikia wimbo wa Solo Thang 'Sikati Tamaa'? Umeusikia mara ngapi kwenye radio stations zetu?

    Wimbo wa Bonta 'Nauza Kura Yangu', je? Au huu haupigwi kwasababu hauna "kiitikio kizuri"? Mbona Fid Q ameghani "Mwanamalundi" bila kiitikio? Lakini watu wanaomuelewa wanaupenda kinoma! (Wimbo upo kwenye hiyo playlist niliyoitaja hapo juu.)

    Kitu kizuri ni kwamba, bado kuna wasanii ambao wameendelea kuheshimu sanaa, na hiyo inatia moyo...

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...