
Na Mwandishi Maalum, New York.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya jummane limepiga kura ya kusitisha ujumbe wa Libya katika Baraza la Haki za Binadamu.
Kusimamishwa huko kunatokana na ombi lililowasilishwa na Baraza la Haki za Binadamu lenye makao yake Geneva, Usiswi, baada ya Baraza hilo kukutana siku ya ijumaa wiki iliyopita na kuamua kwa kauli moja kuiondoa Libya katika ujumbe wa Baraza hilo.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepigia kura ombi hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na matumizi ya nguvu za kupita kiasi kunakofanywa na Rais wa nchi hiyo, Muammar Al Quadhafi dhidi ya wananchi wake wanaoandamana kwa amani wakimtaka aachie madaraka.
Ilihitajika Theruthi mbili ya kura kutoka kwa wanachama 192 wa UM ili kupitisha uamuzi huo.
Uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, umekuja ikiwa ni takribani siku tatu tu zimepita tangu Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa mataifa, nalo kupitisha siku ya jumamosi tamko la kumwekea vikwazo Muammar Quadhafi na washirika wake .
Pamoja na kuweka vikwazo, Baraza Kuu la Usalama pia limeiagiza Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuchunguza kama kunavitendo vyovyote vya makosa ya kijinai dhidi ya binadamu.
Katika upigaji kura wa Jumanne ni Venezuela tu ambayo ilielezea kusita kwake kuhusu upigaji kura huo kwa kile ilichotaka ufanyike uchunguzi kwanza. Hata hivyo hatua hiyo ya Venezuera na haikuathiri upigaji wa kura hiyo.
Akizungumza kabla ya upigaji kura kuanza,Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Joseph Deiss, aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo, kwamba hadhi na heshima Jumuia ya Kimataifa, ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ya Baraza Kuu la Usalama na Baraza la Haki za Binadamu vilikuwa katika mashaka.
“ huu ni wajibu wetu kwa watu wote wanawake kwa wanaume ambao wanahangaika kudai kuheshimiwa kwa haki zao na ambao leo hii wako katika hatari kubwa, matumaini yao hayapashwi kupotea bure” anasema Bw. Deiss.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akizungumza kabla ya upigaji kura, yeye alisema hatua mbalimbali zilizochukuliwa na vyombo vya juu vya Umoja wa Mataifa zilikuwa zinapeleka ujumbe muhimu, ujumbe wa kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria na hakuna msamaha kwa yeyeyote anayefanya vitendo vya jinai dhidi ya bindamu.
Akasisitiza kuwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya jinai lazima watambue kuwa wataadhibiwa na kwamba misingi ya haki na uwajibikaji utadumishwa.
Ban Ki Moon ameonya juu ya kuendelea kwa ongezeko la hali ya machafuko na mahitajio ya misaada ya kibinamu huku akionyesha wasiwasi kuhusu taarifa za kwamba serikali ya Libya imefungulia maghala ya silaha na silaha hizo kuangukia mikononi mwa maharamia na magenge ya wahalifu ambayo yamekuwa yakitumia silaha hizo dhidi ya waandamanaji.
Akizungumzia kuhusu idadi ya watu ambao wamepoteza maisha, Ban Ki Moon anasema mpaka sasa hakuna taarifa sahihi, ingawa inakadiriwa watu 1,000 wanaweza kuwa wamepoteza maisha na maelfu wengine wakiwa wamejerushiwa, aidha amesema karibu watu 150,000 tayari wamekimbilia nchini Tunisia na Misri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...