Na Veronica Kazimoto – MAELEZO

Kesho ni siku ya kitaifa ya kupanda miti ambapo maadhimisho haya kwa mwaka huu yatafanyika katika ngazi za mikoa yote Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Maimuna Tarishi. Maadhimisho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa ni mwaka ambao umetangazwa na Umoja wa Mataifa kama Mwaka wa Kimataifa wa Misitu pia ni mwaka ambao Tanzania inaadhimisha miaka 50 ya uhuru.

”Tukumbuke pia kuwa huu ni mwaka wa kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Hivyo, tutaadhimisha siku hii kwa kutathmini tulikotoka, tulipo na tunapokwenda kuhusiana na hali ya misitu”, imefafanua taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kila mtanzania anatakiwa atathmini athari anazopata kutokana na ufyekaji na uharibifu wa misitu ili aamue kwa dhati kuihifadhi misitu kwa ajili ya kuwanufaisha watu wa kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Bi. Tarishi amesema, kila familia haina budi kuanzisha bustani ndogo yenye miche inayolingana na idadi ya wanafamilina ambayo ni rahisi kuitunza miche hiyo kwa kutumia maji yanayopatikana nyumbani.

Katibu Mkuu huyo anafafanua kuwa, njia nyingine ya kuongeza kiwango cha upandaji miti ni kupanda mbegu moja kwa moja ardhini kwa baadhi ya miti hasa katika mikoa iliyoko katika nyanda za juu hapa nchini kama Tanga na Iringa.

“Wakati mwingine siyo lazima miche yote inayopandwa itoke bustanini. Njia nyingine ya kustawisha miti ni kutumia miche inayojiotea yenyewe ardhini kama maotea. Miche hiyo inapandwa katika sehemu zilizokusudiwa ikiwa bado midogo. Njia hii inatumika hasa kwenye sehemu zenye mvua nyingi na udongo tifutifu,” amebainisha Bi. Tarishi.

Katika taarifa yake, Bi. Tarishi anasema, aina nyingine ya kustawisha misitu ni kutenga na kulinda eneo kutokana na uharibifu wa kimazingira ili mbegu ziote zenyewe (natural regeneration), njia hii imefanikisha shughuli za kustawisha misitu na malisho ya mifugo mkoani Shinyanga.

“Wananchi wa Shinyanga wanatumia utaalam wao wa jadi unaojulikana kwa jina la Ngitili wa kutenga maeneo na kuyapumzisha ili mbegu zijiotee zenyewe, matokeo yake mkoa huu umeongeza zaidi ya hekta 500,000 za ardhi ambayo ilikuwa imeharibika kabisa hapo awali,” Bi. Tarishi anasema.

Bi. Tarishi amewapongeza wananchi wanaostawisha miche ya miti bila kutegemea ile inayostawishwa katika bustani za serikali, kwa sasa asilimia 70 ya miche ya miti yote inayopandwa inatokana na juhudi za wananchi wenyewe.

Maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupanda Miti yalifanyika kwa mara ya kwanza tarehe Mosi Januari mwaka 2001 kutokana na Waraka wa Waziri Mkuu Namba 1 wa mwaka 2000 uliomtaka kila mwananchi kupanda miti kwa manufaa yake ambapo mwaka jana Siku ya Taifa ya Kupanda Miti iliadhimishwa kitaifa Aprili Mosi mkoani Shinyanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...