Ban Ki Moon, akiapishwa na Bw. Joseph Deiss Rais wa Mkutano Mkuu wa 65. Katika kiapo hicho cha kuingia kazini Ban Ki Moon alitumia Katiba ya Kwanza kabisa ( Original Charter) ya Umoja wa Mataifa, Katiba hiyo, ambayo ililetwa rasmi kwa shughuli hiyo inahifadhiwa katika Maktaba Kuu ya Congress iliyoko Washgton DC. Ban Ki Moon anakuwa Katibu Mkuu wa Nane kuongoza Umoja wa Mataifa, mkutano huo wa kumteua na kupitishwa kwa Ban Ki Moon ulihudhuriwa pia na Msaidizi wake wa Karibu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akitembea kuelekea Meza Kuu huku akiinama kwa heshima kama ishara ya kuwashukuru Mabalozi waliokuwa wakimshangilia kwa nguvu mara baada kutangazwa rasmi kwamba ameteuliwa na kupitishwa kwa kauli moja na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ( General Assembly) Kuongoza Umoja wa Mataifa kwa mhula wa pili utakaoanza rasmi Januari 2012 na kumalizika Desemba 2016.

Na Mwandishi Maalum

Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amepitishwa kwa kauli moja kuendelea na jukumu la kuongoza Umoja wa Mataifa kwa mhula wa pili.

Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ( General Assembly) ,wenye wajumbe 192 ulimpitisha Ban ki Moon katika mkutano wake uliofanyika jana jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York ,Marekani.

“Ninatangaza rasmi kwamba mkutano mkuu umemteua na kumpitisha kwa kauli moja, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kuendelea na wadhifa huo kwa mhula wa pili” akatangaza Bw. Joseph Deiss Rais wa Mkutano Mkuu wa 65 wa Umoja wa Mataifa.

Kauli hiyo iliwafanya Mabalozi na wasaidizi wao waliofurika ndani ya ukumbi Mkuu wa Umoja wa Mataifa ( General Assembly Hall), kushangilia kwa nguvu. Hali iliyoonyesha kukubali kwamba Ban Ki Moon ambaye amekiongoza chombo hicho kwa miaka minne na nusu alikuwa anastahili kuendelea na wadhifa huo.

Makofi na nderemo viliongezeka zaidi pale Bw. Joseph Deiss alipomkaribisha rasmi Ban Ki Moon kujongea Meza kuu.

Na kwa unyenyekevu mkuu, Ban Ki Moon akiwa amezungukwa na walinzi wake alitembea kuelekea meza hiyo, huko akiinamisha kichwa chake kama ishara ya kupokea kwa mikono miwili makofi na nderemo kutoka kwa Mabalozi na wasaidizi wao.

Hafla ya Kuteuliwa na kupitishwa kwa Ban ki Moon, ilihudhuriwa pia na msaidizi wake wa karibu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro.

Mhula wa pili wa Katibu Mkuu Ban ki Moon unaanza rasmi Januari 2012 na utamalizika Desemba 31, 2016. Ban Ki Moon anakuwa katibu Mkuu wa Nane kuongoza Umoja wa Mataifa tangu kuasisiwa kwake.

Baada ya wawakilishi wa makundi mbalimbali kutoa maelezo ya kwa nini wanadhani Ban Ki Moon alikuwa anastahili kuendelea na wadhidha huo.

Ban Ki Moon akiwa amezungukwa na wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama, na wenyeviti wa kamati sita ambazo ziko chini ya Mkutano Mkuu.Alikula kiapo kwa kunyoosha mkono wake wa kulia huku wa kushoto ukiwa umeshikilia Katiba ya kwanza kabisa ( Original Charter) iliyounda Umoja huo.

Katiba hiyo ililetwa moja kwa moja kutoka Maktaba Kuu ya Congress iliyoko Jijini Washgton DC ambako ndio inakohifadhiwa.

Shamra shamra na Utaratibu wa kumteua na hatimaye kupitishwa kwa Ban Ki Moon kuendelea na wadhifa huo. kulitanguliwa na kusomwa kwa Azimio lililo wasilishwa na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine lilielezea kwamba Baraza Kuu la Usalama lenye wajumbe 15 wakiwamo watano wa kudumu lilikuwa linapendekeza Ban Ki Moon achaguliwe tena kuendelea na wadhifa wake kwa kipindi cha pili.

Baraza Kuu lilikutana June 17 katika mkutano wake wa siri ambao ndio uliompitisha rasmi Ban Ki Moon kuendelea na wadhifa huo.

Kabla ya Baraza Kuu kumpitisha makundi ya kanda nchi za Afrika, Asia, Ulaya , Ulaya mashariki , Marekani ya kaskazini na kusini yalitangulia kumpitisha katika vikao vyao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ilikuwa miogoni mwa viongozi wa nchi za mwanzo kabisa, kutangaza hadharani kumuunga mkono Ban Ki Moon aendelee na wadhifa wake kwa mhula wa pili.

Akitoa shukrani zake baada ya kuapishwa, Ban Ki Moon amesema, kwa moyo mmoja anatoa shukrani zake kwa Umoja wa Mataifa kwa kumuamini na kumtaka aendelee na wadhifa huo. Akasisitiza kuwa hiyo ni heshima kubwa sana kwake.

Akaeleza kuwa atajitahidi kwa kadri ya uwezo wake na kwa kushirikiana na wanachama wa UN kuzikabili changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia hivi sasa.

Akasema anaamini kwamba, katika kuzikabili changamoto hizo, kunahitajika ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja na kwamba hakuna taifa linaloweza kujidai kwamba linaweza kwenda au kufanya kivyake vyake bila ushirikiano na wengine.

Akasema daima ataendelea kuwa mnyenyekevu na msikivu na kuzingatia maslahi na matakwa ya nchi wanachama. Ili hatimaye chombo hicho muhimu kiwekeze kikidhi kiu na mahitaji ya wananchi wanaounda Umoja wa Mataifa.

Kwa ujumla wazungumzaji wote walieleza kwamba, Ban ki Moon alikuwa anastahili kuendelea kipindi cha pili kwa sababu kadhaa zikiwamo za kumudu vema majukumu yake.

Majukumu hayo ni, kusimamia misingi, kanuni na taratibu zinazoainishwa ndani ya Katiba ya UN, na amekuwa kiungo muhimu katika kutetea, kusimamia na kutekeleza kwa dhati dhana ya uwazi na uwajibikaji wa pamoja.

Sababu nyingine ni kwamba Ban Ki Moon amekuwa mtetezi wa wanyonge wasiokuwa na sauti, kasimamia kidete masuala ya amani, ulinzi na usalama, ulinzi wa raia dhidi ya udhalimu na kutetea haki za wanawake kwa kuanzisha taasisi mpya inayoshughulikia masuala yao ( UN WOMEN).

Aidha Ban Ki Moon anaelezwa kama kiongozi ambaye amekuwa kiungo muhimu katika , kusimamia changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, usitishwaji wa silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia, kupiga vita umaskini, huduma za afya na kusimamia suala zima la maendeleo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 22, 2011

    Daima ataendelea kuwa mnyenyekevu, msikivu na kuzingatia matakwa ya wanachama!
    Nionavyo mimi, Ban Ki Moon hakustahili kuungwa mkono na viongozi wa Afrika na kwa mtazamo wangu hata rais wetu Mhe. Kikwete alikosea kumuunga mkono hadharani. Bahati mbaya sikupata nafasi ya kuchangia juu ya hili kama nilivyokuwa nimepanga lakini rais alikosea. Kwa mtazamo wangu mimi, rais si tu kwamba alikosea lakini kama ningekuwa ni yeye, pale Dkt Asha Rose Migiro alipokuja siku za karibuni, ningemshawishi ajiuzulu na kazi yake ya unaibu katibu mkuu ili kujenga heshima miongoni mwa wana wa Afrika.
    Kwa kweli UNO ninavyoiona mimi, ni umoja ambao uko zaidi kwa maslahi ya mabepari wa Ulaya na Marekani na ndio maana ulifanya haraka kupitisha azimio kwa maslahi ya NATO kuendelea na uvamizi katika ardhi ya Libya. NATO hao hao ili kuungaunga muonekano wao, baada ya kugundua wanakosea katika Libya wakapunguza kasi mashambulizi na kuingilia machafuko ya Ivory Coast ambayo yalikuwepo kabla ya Libya lakini hawakuyaingilia mpaka walipoona kama sababu ya kuungwa mkono kuwa wanafanya haki hivyo na waendelee hata Libya.
    Hivyo mimi naiona UNO ni chombo cha wachumia matumbo ya wakubwa na inaendekeza maguvu ya wakubwa kiasi kwamba yamekuwa (maguvu hayo) miongoni mwa vyanzo vya ugaidi. Lakini mbaya zaidi na dharau kwa viongozi wa Afrika, ni UNO kuendelea kuacha fujo za NATO hata pale viongozi wa Afrika walipokuwa wakitafuta suluhu ya kidemokrasia katika mzozo wa Libya. NATO kuendelea kuishambulia Libya kunapingana na matakwa ya Umoja wa Afrika ya kutounga mkono aina ya mapinduzi ya serikali iliyowekwa na wananchi, hivyo kwa kuwa UNO inashindwa kukemea NATO viongozi wa Afrika hawakupaswa kuunga mkono kuongozi wa Umoja unawaowadharau waafrika, tena ni afadhali wangekaa kimya. Hapa Ban Ki Moon anakiri kuwa "ataendelea kuwa mnyenyekevu na msikivu na kuzingatia matakwa ya wanachama" hata kama ni pamoja na kuingia vitani bila kufuata taratibu, huyu si kiongozi analiestahili kuendelea madarakani.
    Hapa si maanishi kama Gaddaf ni msafi sana kiasi cha kutetewa. Awe ama ni msafi ama ni mchafu wananchi wa Libya ndio wana haki ya kuamua hatima yake lakini pia kwa kutumia taratibu na kanuni zilizopo si kwa mitindo inayosababisha uharibufu wa chi kama ilivyo sasa. Kama ingelikuwa ni Afrika ya aina ya uongozi wa Mwl Nyerere tusingeona aina ya viongozi wanafiki kama alivyo Rais Museven ambae aliandika tahariri kwenye gazeti la serikali kupinga uvamizi wa NATO halafu asubuhi akatangaza kuzizuia mali za Libya zilizoko nchini mwake, hii ndio hali inaochagiza muonekano wa vita hii kuwa ya matumbo zaidi kuliko maslahi halisi ya usalama wa watu wa Libya. Sasa viongozi wa kiafrika kuunga maslahi ya vita vya aina hii ni kuhalalisha aina hii UNO kuachia aina hii ya ubadilishanaji wa madaraka kwa kuharibu maisha, miundombinu na uchafuzi wa mazingira. Ni utaratibu wa kishenzi usiojali ustaarabu.

    sesophy@yahoo.com

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...