TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimesikitishwa na kinalaani tukio lililomkumba mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la JamboLeo, Asha Kigundula wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho kati ya Simba na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili iliyopita.

Mwandishi huyo pamoja na Watanzania wengine waliokuwa Kinshasa, DRC kushuhudia mchezo wa Simba na DC Motema Pembe kwenye Uwanja wa Mashujaa ‘Stade des Martyrs’ walifanyiwa fujo ambazo hatukutarajia kama mashabiki wenye busara wangeweza kuzifanya.

Kilichotusikitisha zaidi ni hatua ya mashabiki hao kumdhalilisha mwandishi huyo bila kujali utu wake, heshima yake na thamani yake, kisa tu ni Mtanzania ambaye alikuwa uwanjani hapo kushuhudia timu ya Tanzania ikicheza.

Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana haraka iwezekanavyo kuhusiana na tukio hili ili kupata maelezo ya kina kwa vile Katibu Mkuu wa chama, Amir Mhando alikuwepo Kinshasa katika mchezo huo , hivyo atakuwa msaada mkubwa kueleza namna ya mambo yalivyokuwa.

Baada ya hapo TASWA itaangalia hatua ambazo kama chama na waandishi wa habari za michezo kwa jumla wanaweza kuchukua kwa jambo hili, kwani hata waandishi wa habari za michezo wa DRC, hawakutoa ushirikiano kwa wenzao wa hapa kama ambavyo wao walipewa wakati walipokuja Dar es Salaam na timu yao.

Kwa sasa Sekretarieti ya TASWA inafanya mawasiliano na Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Rage pamoja na Asha kuhusiana na namna bora ya kuchukua hatua za kisheria kwa jambo hili.

Tayari Rage amesema hatua ya awali atamjulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuhusiana na kudhalilishwa kwa mwandishi huyo na vurugu nyingine ambazo Simba ilifanyiwa Kinshasa na baada ya hapo tutaona hatua gani nyingine zifuatwe.

TASWA inaamini kama mashabiki wa DC Motema Pembe wangetumia kauli mbiu ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inayosisitiza amani michezoni 'Fair Play', hakika baadhi ya mambo yasingejitokeza.

Watanzania ni watu waungwana sana, tumekuwa mara kwa mara tukifanya hivyo kwa wageni wetu, hatutaki kulazimika kuharibu sifa yetu mbaya, hivyo tunaamini mamlaka husika zitafuatilia jambo hili kwa umakini zaidi.

Ahsanteni
George John
Katibu Mkuu Msaidizi TASWA
22/06/2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 22, 2011

    Bwana George Tafadhali hebu rekebisha kipengele cha mwisho (nanukuu! Hatutaki kulazimika kuharibu sifa yetu mbaya)U mimi ndo sijaelewa nifafanulie tafadhali.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 22, 2011

    "Kamati .... Itakaa ili kupata maelezo ya kina"

    Kwa nini manatoa tamko la kulaani vikali wakati hamna uhakika?
    Ingefaa mpate hayo maelezo ya kina kwanza ndiyo mtoe tamko. Huu sio uandishi wa habari hata kidogo!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 22, 2011

    Nduh, hii taarifa imetolewa na waandishi wa habari? itakuwaje mwanahabari anaandika kosa kama hili "watanzania ni watu waungwana sana, tumekuwa mara kwa mara tukifanya hivyo kwa wageni wetu,hatutaki kulazimika kuharibu sifa yetu mbaya" hivi toka lini sifa ya uungwana ikawa ni sifa mbaya? na inakuwaje muandishi wa habari anaandika "tumekuwa mara kwa marara...." badala ya "tumekuwa tukiwafanyia wageni wetu hivyo mara kwa mara"?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...