JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIABUNGE LA TANZANIA | ||
Simu Na. 022 2112065 Fax Na. (255) 022 2112538 E-mail: tanzparl@parliament.go.tz | | Ofisi ya Bunge S.L.P. 9133 DAR ES SALAAM |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
_______________
YAH: TAARIFA POTOFU YA GAZETI LA DIRA YA MTANZANIA TOLEO LA JUMATATU, 20 – 26 JUNI, 2011 ‘ SAKATA LA POSHO ZA WABUNGE’ SPIKA MAKINDA MBUMBUMBU ‘Utafiti wabaini anasimamia asichokijua
magwiji wa Bunge washangaa tamko lake’.
1.0 UTANGULIZI
Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesikitishwa sana na habari potofu na yenye dharau iliyochapishwa na gazeti la Dira ya Mtanzania, lenye usajili ISSN No. 1821-641, Toleo Namba 89 la Jumanne Juni 20 -26, 2011 lenye kichwa cha habari ’SAKATA LA POSHO ZA WABUNGE’ SPIKA MAKINDA MBUMBUMBU pamoja na vichwa vidogo vya habari vyenye kusomeka ‘Utafiti wabaini anasimamia asichokijua’ magwiji wa Bunge washangaa tamko lake’ nk katika ukurasa wake wa kwanza na iliyoendelea pia katika Ukurasa wa 2.
Pamoja na Vichwa vya habari hiyo, Katika taarifa hiyo Mwandishi wa gazeti hilo amedai kuwa;
i. Spika wa Bunge, Anne Makinda hana uelewa wa kutosha wa jinsi mbunge anavyoweza kupoteza wadhifa wake
ii. Pia Spika wa Bunge haelewi mfumo wa malipo ya Posho za Wabunge
iii. Spika hana mamlaka ya kumfukuza Mbunge yeyote anayekataa kusaini Fomu za kuchukua posho ya kikao.
2.0 MAJIBU YA HOJA POTOFU ZILIZOTOLEWA
Ofisi ya Bunge ingependa kuwaarifu wananchi kwamba habari hiyo iliyoandikwa na gazeti la Dira ya Mtanzania ni ya dharau na haina ukweli wowote na imeandikwa kwa nia mbaya ya uchochezi na kuharibu sifa aliyonayo Mhe. Spika Bungeni na kwa watanzania kwa ujumla.
Ili kuondoa upotofu wa taarifa iliyotolewa na gazeti hili, Ofisi ya Bunge ingependa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa kama ifuatavyo;
i. Sio kweli kwamba Mhe. Anne Makinda hana uelewa kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge. Mhe. Makinda amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 30 Bungeni na kwa kipindi hicho chote ameshika nyadhifa mbalimbali Bungeni na Serikalini. Aidha akiwa Naibu Spika ameongoza kamati ya Bunge iliyoshiriki marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007.
Kwa mantiki hiyo anazifahamu vyema Kanuni za Bunge na ana uzoefu na uendeshaji wa shughuli za Bunge kwa muda mrefu kuliko hata idadi kubwa ya wabunge wapya waliopo Bungeni. Katika utendaji wake, hafanyi kazi kwa kuvutwa na hisia bali husimamia uendeshaji wa Bunge kwa Mujibu wa Kanuni za Bunge ambazo tunashaka hata kama mwandishi wa gazeti hili anazifahamu vyema.
Ni kwa kuzingatia hilo aliwaeleza bayana Waandishi wa habari siku alipofanya nao mahojiano ambapo mwandishi wa gazeti hili pia hakuwepo, kuwa taratibu la kuchukua posho kwa Mbunge huenda sanjali na kusaini mahudhurio Bungeni (Mbunge anayehudhuria Bunge ndiye anayelipwa posho), kwa maana huwezi kumlipa posho Mbunge asiyekuwepo Bungeni. Mahudhurio ya Mbunge ni pale anaposaini fomu ya Mahudhurio. Kwa mantiki hii, kanuni zinamtaka bayana kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge.
Kanuni ya 143 inatamka kuwa:
(1) kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati ni wajibu wa kwanza wa kila mbunge.
(2) Mbunge yeyote atakaeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza Ubunge wake kwa mujibu wa ibara ya 71 (1) ya katiba na Spika ataiarifu Tume ya Uchaguzi.
(3) Mbunge atakapokosa kuhudhuria nusu ya vikao vya Mkutano mmoja bila ya sababu ya msingi atapewa onyo.
Hivyo basi kwa mantiki hiyo, Mbunge atakayeshindwa kusaini fomu za mahudhurio kwa mtiririko huo hapo juu atakuwa amepoteza sifa zake za kuwa Mbunge kwa mujibu wa Kanuni.
ii. Aidha ni kwa uvivu wa kufikiri au kwa makusudi kabisa, mwandishi wa gazeti hili ameandika yale aliyohisi ni sahihi na kufanya utafiti katika kiwango ambacho hajaeleza ni kwa kutumia vigezo gani bila hata kujaribu kuuliza misingi halisi aliyoizungumzia Mhe. Spika kuhusu uhalali wa mahudhurio ya Mbunge sanjali na ulipwaji wake posho awapo kazini.
Hivyo madai ya kuwa Spika hana madaraka ya kumfukuza Mbunge Bungeni hayana mantiki na wala madaraka ya Spika kuhusu kumfukuza Mbunge hayakuwa sehemu ya mahojiano na waandishi na Spika wa Bunge kama anavyodai, na Kanuni zimeeleza bayana kazi za Spika Bungeni. Kumbuka madaraka ya Spika, wajibu wa Wabunge na hata Miongozo mingine Bungeni huratibiwa kwa mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge.
Hatujui lengo la mwandishi ni lipi hasa kwa kuweza kutoa taarifa zenye upotoshaji mkubwa kwa umma na zenye kuleta dharau kwa kiongozi wa Bunge na Bunge kwa ujumla kwa kuzingatia kuwa kiongozi huyu amechaguliwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
3.0 HITIMISHO
Ofisi ya Bunge inapenda kuwaarifu wanahabari wote kuwa Idara yake ya Habari imekuwa ikitoa ushirikiano wa kutosha kuwaarifu waandishi kwa taarifa zozote wanazohitaji na inasikitishwa kwa kiasi kikubwa na uandishi unaojali hisia na wenye kulenga uchochezi badala ya kuelemisha.
Licha ya mwandishi wa habari hii kutokuwepo Dodoma na wala hakushiriki mahojiano hayo na Mhe. Spika, habari husika iliyoandikwa imelenga kutoa taarifa potofu bila kushirikisha hata upande wa pili kwa ufafanuzi. Kwa kuzingatia hilo Ofisi ya Bunge inamtaka Mhariri wa Gazeti la Dira ya Mtanzania kuomba radhi kwa uzito ule ule waliotoa habari yao ya kupotosha umma.
Deogratios Egidio
Kny: KATIBU WA BUNGE
21 Juni, 2011
Deo Mbona na wewe unapotosha zaidi? kanuni ya 142 (2) inasema mikutano mitatu mfululilo... ndo mbunge anaweza akakosa ubunge na si vikao vitatu kwa mantiki hiyo mbunge anatakiwa akose mkutano wa bajeti, the wa mwezi wa 9 na november ndo atakosa ubunge na si mahudhurio ya siku tatu.
ReplyDeleteNiliwahi kusema hoku siku za nyuma na Mhe. Ben Mkapa aliwahi kusema wakati akiwa pale Magogoni kwamba Tanzania hakuna waandishi wa habari bali kuna wanaonukuu habari.
ReplyDeleteKwa mwandishi wa Habari na kuwa mnukuu habari ni vitu viwili tofauti.
Sasa kwa sababu wamezoea kuwa wanukuu habari siku wakiambua kutaka kuwa waandishi wa habari matokeo yake ndo hayo kuandika UONGO.
Maana mwandishi wa habari ni mtafiti, mfukunyuku, mpekeke, mpekuaji, mtafutaji mwenye uwezo wa kuainisha kile anachokisikia kwa kwa kutumia Katiba, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali
Lakini hawa wa kwetu hapa ni wanukuu habari ambao hawana haja ya kuwa watafiti, kazi yao ni kumsikiliza fulani kasema nini kisha wanashika kalamu na kuandika
"akasema" "akasisitiza" akaongeza" alisema" aliongeza" "akahoji" n.k n.k
Nunua magazeti ya leo soma uone wanavyoandika kisha nunua magazeti kama ya Kenya au Uganda linganisha na magazeti ya TZ. Kwa kifupi Magazeti ya TZ ni kama Kaseti iliyorekodiwa maneno ya msemaji magazeti mengine [Kama ya Kenya na Uganda yameandikwa na waandishi].
Kazi ya wanukuzi habari wetu hapa TZ ni kufukuzia soda pale Idara ya Habari Maelezo huwezi kuwakuta mitaani wakitafuta habari, huwezi kuwakuta Maktaba wakitafuta habari kwa kusoma na kufanya utafiri, kazi yao ni kufukuzia posho mara habari zao zikitoka kwenye Gazeti utawaona wanakwenda kwa mtu ambaye habari yake wameinukuu, utawasikia
"Mzee umeona gazeti la leo?" Basi mhariri alitaka kunibania lakini kasifu sana ulivyosema. Basi kazi yao ndo hiyo.
Wanachefua, wanakera, wanatia KINYAA kama matapishi ya Mlevi wa Pombe ya "KOMONI"
Siyo kama nawasema
wewe uliona wapi Mwandishi aliyepata "division" 4 akaweza kuwa mtafiti kwa kusoma miezi 6 kwenye vinavyoitwa vyuo vya Uandishi wa habari?
Nawatakia kazi njema.
Magulu
Germany
1.Nina mashaka na kilichoandikwa hapa katika mtizamo yakinifu ufuatao,
ReplyDelete[a]Kichwa cha habari kinatuhumu taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti husika toleo la JUMATATU.
[b]Sehemu ya utangulizi inatuhumu taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti husika toleo la JUMANNE.
[c]Bunge kama chombo,taasisi na mhimili uliopo kisheria,ofisi yake inapokuwa inatoa taarifa za kibunge kwa umma,inatumia barua yenye nembo ya Bunge.Cha kushangaza taarifa hii haina nembo ya bunge letu Tukufu.
Kwa mantiki hiyo,ofisi iliyotoa taarifa hii,haipo makini hivyo kupotosha uhalisia wa mambo.Siku nyingine kuweni makini katika kazi za umma.
Umefika wakati sasa nyie watumishi wa Bunge mkafanya kazi zenu bila kuangalia maslahi ya vyama vyenu, hapo kulikuwa hakuna haja ya kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari wala nini, mlitakiwa mchukue
ReplyDeleteHATUA ZA KISHERIA KWENYE MAMLAKA ZINAZOHUSIKA. Sasa hapa mnaleta hii taarifa eti awaombe radhi kwani taratibu hamzijui au kwa kuwa nyie ingawa mnafanya kazi huko lakini mmeweka mbele maslahi ya vyama vyenu. Peleka kunakohusika huyo mwandishi, aende akathibitishe huko aliyoyasema.
watu wamevamia fani kwa kutokuwepo ajira msiwalaumu jamani michuzi we niwasiku nyingi ndugu yetu waelimishe vijana walioingia kwenye fani hiyo kwa kupunguza ukali wamaisha kwani kazi hiyo haikuwa nia na lengo lao imetokea tu jamani mimi binafsi siwalaumu wapo wengi hao sio huyo tu wasaidieni hao
ReplyDeleteMama Makinda amekuwa ni kama mwalimu mkuu na wabunge watoto wa shule anawakemea kama atakavyo.
ReplyDeleteLengo la Bunge siyo kuleta mvuto kwa watu ni kujadili hoja bila woga kwa maslahi ya wenye nchi siyo kutetea watawala tu.
Sipingi tatizo la uandishi wa Habari usizingatia weledi, lakini pia its not fair kuwahukumu waandishi wa habari wote tena kwa kauli kali kama iliyotolew na Magulu. tupo waandishi wa habari ambao tunachukia ukiukwaji wa weledi na nina hakika tunatimiza kazi zetu vizuri, na ndio maana watanzania hawajasema hawahitaji vyombo vya habari na waandishi wake. I'm sorry kama comment hii imekuudhi MAGULU lakini, kwa kweli nimesoma comment yako nimesikitika sana kwa jinsi ulivyotujumuisha wote.
ReplyDeleteNadhani sio katika uandishi wa habari tu watu wanakosea, wanakosea hata katika fani nyingine Mfano, Uhasibu baadhi yao wanatuhumiwa kwa wizi, Udaktari baadhi yao wanasahau mikasi ndani ya mwili wa binadamu na wengine wanapasua kichwa badala ya mguu, na wanasiasa nao akiwemo Rais baadhi yao wanakosea. Lakini sio vizuri kuwajumuisha na kuwaita matapishi. Vaa uhusika kwamba nawe ungekua mwandishi wa habari unayefanya kazi yako vizuri halafu mtu akasema maneno kama hayo akijumuisha waandishi wa habari wote ungejisikiaje? Basi kama haifai hata sie tunaohenya huku vijijini kupaza sauti za wakulima wa Namtumbo, Tunduru, Nanguruwe ama Mpanda kule, hatuoni Soda wala posho ya Maelezo tunajisikia vibaya tunaposikia kashfa za makanjanja zinatujumuisha na sie
Anyway ni mawazo yangu tu, yanaweza kupingwa pia.
Michuzi naomba uifikishe Post hii kwa heshima ya waandishi wa Habari wote wanaofanya kazi zao vizuri, vinginevyo itakua ni kuwavunja moyo na hata wanaotaka kuingia katika fani hii wakiwa na taaluma nzuri wanakata tamaa na kuingia fani zingine, sie tutabaki peke yetu na hao wanaotuhumiwa kwa mishiko na soda za watoa taarifa (sources)
NAWASILISHA KWA MASIKITIKO POST HII