Mkuu wa wilaya ya Rombo Peter Toima akizungumza na wanahabari ,kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Moshi Musa Samizi.

Na Dixon Busagaga,Kilimanjaro

MKUU wa wilaya ya Rombo, Peter Toima amesema baadhi ya polisi na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) ndio kikwazo katika kudhibiti uvushaji wa mahindi kwenda nchi jirani ya Kenya .

Baadhi ya magari ambayo yalishikiliwa na jeshi la polisi baada ya
kukutwa na shehena ya mahindi yakisafirishwa kuelekea wilayani Rombo
 Toima ameyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari,aliouitisha kuzungumzia biashara hiyo ya mahindi, mkutano ambao ulihudhuriwa pia na Samizi ambaye ni mwenyekiti wa wakuu wa wilaya za mkoa Kilimanjaro.

Alisema wapo baadhi ya vijana wasio waaminifu wa TRA na polisi wanaohongwa na wafanyabiashara kuruhusu mahindi yavushwe kwenda Kenya na kufanya zoezi la kuzuia kuwa gumu.

Mkuu huyo wa wilaya, alisema wafanyabiashara hao sasa wamebuni njia mpya mbili mpya ambazo ni Kitobo-Same-Ziwa Jipe-Kenya na Sanya Juu-Ngaranairobi-Olmolok wilayani Siha hadi -Kikelelwa wilayani Rombo na baadaye kuingia Kenya.
Malori yaliyokamatwa yakiwa yamepaki pembeni mwa barabara.
“Tumefanikiwa kudhibiti mchana lakini malori yanavuka usiku wa manane…kama wanapitisha tani 400 za mahindi kwa siku kwenda Kenya hivi tangu biashara hii waanze ni shehena kiasi gani imevushwa kwenda Kenya?”alihoji Toima.

Alifafanua kuwa wilaya yake ina upungufu wa tani 4,000 za nafaka katika vijiji vya maeneo ya tambarare ambavyo ni Shimbi Mashariki,Ibukoni, Kiraeni, Msaranga, Mahorosha na Leto na hakuna tatizo la njaa Rombo.

Toima alisema uongozi wa serikali wilaya ya Rombo hauwezi kukubali mahindi yasemekane yanapelekwa Rombo wakati mahindi hayo hayauzwi katika masoko ya wilaya hiyo na badala yake huvushwa kupitia njia za panya 320 kwenda Kenya.

Mkuu huyo wa wilaya alisema serikali imeanza kuchunguza madai kuwa baadhi ya polisi waliohamishwa wilayani humo baada ya kuhusishwa na vitendo vya rushwa hawajaondoka na ndio wanaowasaidia wafanyabiashara hao.

Kwa upande wake, Samizi aliwataka polisi kutafuta taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini wafanyabiashara wanaoendelea na uvushaji huo wa mahindi usiku kwa kutumia pikipiki, baiskeli, malori na pick-up ili waweze kukamatwa mara moja.

Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa wananchi wa mkoa Kilimanjaro wametoa ushirikiano mkubwa wa kuzuia mahindi hayo kwenda ya nchi na akavipongeza vyombo vya habari kwa namna vilivyofichua biashara hiyo ya mahindi.

“Kama chakula kingekuwa kinakwenda kwenye masoko ya Rombo isingekuwa tatizo na hata bei ya mahindi ingeshuka, lakini mahindi haya hayaendi Rombo kinachofanyika Rombo inatumika kama kisingizio tu,”alisema Samizi.
Mizigo iliyokamatwa.

Inakadiriwa kuwa malori kati ya 200 na 300 huvuka kila siku kwenda Kenya kupitia njia za panya zilizotapakaa katika wilaya za Moshi Vijijini na Rombo huku baadhi ya polisi na maofisa wa TRA wakidaiwa kugeuza biashara hiyo kuwa mradi.

Nyumba za kulala wageni katika mji mdogo wa Himo zinadaiwa kufurika wageni wakiwemo raia wa kigeni na wafanyabiashara wa mahindi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi huku polisi wakionekana kuzidiwa nguvu wafanyabiashara hao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 05, 2011

    Kwa nini serikali imzuie mkulima kuuza mahindi au bidhaa yeyote katika soko au sehemu anayoamini atapata faida nzuri? Kama serikali inataka zoezi hili lifanikiwe basi na waanze kununua hayo mahindi wao wenyewe kwa bei nzuri kama ambayo wakenya wako tayari kununua.

    Uko wapi uhuru wa kuuza kilichochako? tangu lini mahindi yamekuwa mali ya taifa? Mkulima anahangaika kila kukicha shambani, muda wa kuvuna unapofika anategemea kujipatia riziki yake bila ya uonevu wa serikali. Kama serikali inataka kuanzisha kodi ya mahindi yanayopelekwa nje ya nje na waanzishe lakini sio kuzuia kuuzwa kwa bidhaa hii nje ya nchi. Wakulima wana familia zao ni wajibu wao kuuza mazao yao kwa bei nzuri itakayowanufaisha wao na familia zao tu!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 05, 2011

    WEWE ANONY WA 05:02; UJUE KWAMBA NCHI INALAZIMIKA KUDHIBITI UUZAJI WA CHAKULA HASA PALE KINAPOUZWA NJE YA NCHI KWA LENGO LA KUHAKIKISHA KUWA AKIBA YA NDANI YA NCHI IPO YA KUTOSHA; NA SI KUFUNGULIA RUHUSA YA KUUZA POPOTE HALAFU UNASIKIA NCHI INA UHABA WA CHAKULA. ANGALIA SKENDO ZINAZOWAKUTA WAKENYA; WAMEUZA RESERVE; SASA WANAPIGANA VIJEMBE. NI KWELI MKULIMA ANA HAKI YA KUUZA; LAKINI UJUE HATA MTU AKIPELEKA NAFAKA SOMALIA AU SUDAN ATAUZA KWA BEI YA JUU; KAMA ANAWEZA KUFIKISHA HUKO; KWA SABABU KUNA UHABA; HIVYO UDHIBITI NA UHABA UNAFANYA BEI ZINAKUWA JUU; NA SERIKALI HAIWEZI KURUHUSU SOKO HOLELA NDANI NA NJE; LAZIMA IWE NA MSIMAMO. MIMI BINAFSI NAUNGA MKONO SWALA LA KUDHIBITI; JAPO WACHACHE WATAFANIKIWA KUVUSHA KAMA HIVYO; ILA UPUNGUFU UNAWEZA JUDHIBITIWA.
    ASKARI WA ROMBO HASA HUKO KIKELELWA TARAKEA NDIO WALA RUSHWA HASWAA; WANAWASAIDIA HATA WAFANYABIASHARA KUKAA MPAKANI NA KUSIMAMIA MAZOEZI YA KUVUSHA YAENDE SALAMA. RUSHWA NI UGONJWA KTK JESHI LA POLISI. LINAHITAJI KUSAFISHWA!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 06, 2011

    Serikali isipige marufuku kuuza mahindi nje. Iwapo kenya ni soko zuri la mahindi kutoka Tanzania, kwa nini Serikali isiweke utaratibu maalumu ambao utalenga katika kuzalisha mahindi zaidi???

    Jamani kupata soko la bidhaa zako nje sio rahisi, soko kama hili la mahindi Kenya ni la kuliwekea mipango endelevu; tuzalishe mahindi zaidi ya kututosha sisi Watanzania na Wakenya pia...why not!!!???

    Haya mambo ya zuia zuia..yamepitwa na wakati.

    Mkulima, Morogoro.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...