Amina Abdalla wa Culture Music Club akiimba wimbo wake wa 'Kibali' katika Sherehe za maridhiano na umoja wa kitaifa zinaendelea katika kijiji cha Kangagani, Pemba.
Bahati Hamadi (kushoto) akiimba wimbo wa 'Vijumbajumba' na Malik Wastara
Sherehe za maridhiano na umoja wa kitaifa zilizoandaliwa na taasisi ya Swahili Center zinaendelea kwa kasi ambapo kwa Jumamosi iliyopita, magwiji wa Taarab kutoka vikundi mchanganyiko vya Unguja na Pemba vilirindima katika kijiji cha Kangagani, Pemba.
Katika onesho hilo ambalo lilifanyika katika uwanja wa Skuli ya Kangagani, Wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wapenzi wa Taarab kutoka sehemu mbali kama vile Chake, Kambini na hata kutoka Mkoani waliliminika na kujimwaga katika burudani hizo zilizoanza saa 2 usiku.
Baadhi ya wasanii maarufu walioshiriki katika onesho hilo ni kama vile Bi. Fauziya Abdalla (Nadi Ikhwan Safaa), Taymour Rukun (Kalcha Music Club), Ali Said ‘Wazera’ (Light Star), Malik Hamadi ‘Wastara’ (Kiuyu-Minungwini), Makame Khamis Nyange ‘Prof. Gogo’ (Maendeleo Taarab) na wengine wengine kutoka vikundi vya Unguja na Pemba.
Kwa kuibusha hisia za mashabiki wao, wakali hao wa Taarab asilia walipiga vibao vingi vinavyopendwa vikiwemo ‘Ahadi’ (Fauziya Abdalla), ‘Kibali’ (Amina Abdalla), ‘Watu Wananiuliza’ (Sameer Basalama), ‘Mtoto wa Mjini’ (Fatma Ali Faki), ‘Mgomba’ (Said Dokoa), ‘Mpewa Hapokonyeki’ (Bahati Hamadi), ‘Vijumbajumba’ (Malik Hamadi Wastara) na Lulu (Prof. Gogo).
Katika kuutambulisha mradi huo kwa waliohudhuria onesho hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Center Bw. Kheri Abdalla Yussuf, aliwajulisha wapenzi hao wa sanaa kuwa dhamira ya mradi huo ni kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa nchini Zanzibar kupitia sanaa za utamaduni zenye burudani na mafunzo kwa jamii yote.
Mradi wa 100% Zanzibari (tafsiri; Mzanzibari asilimia mia moja) umekuwa ukifanya maonesho katika Mikoa ya Unguja na Pemba kufuatia kambi za kisanii zinazoshirikisha fani za Taarab, Ngoma za Utamaduni na michezo ya Kuigiza. Shangwe hizo zimekuwa zikifanyika kwa awamu katika sehemu mbali mbali ambapo kwa hiki hii zitahamia katiak kijiji cha Nungwi, Mkoa Kaskazini Unguja.
Swahili Performing Arts Center (Kituo cha Sanaa za Maonesho cha Waswahili) ni taasisi ya iliyoanzishwa kwa dhamira ya kuchangia katika maendeleo ya sanaa za maonesho asilia za Zanzibar pamoja na zile za mwambao wa Waswahili kupitia uwezeshaji (wasanii), uzalishaji wa kazi za sanaa, maonesho na ushirikishaji jamii. Dira ya Swahili Center ni kuurejeshea hadhi utambulisho wa utamaduni wa Kiswahili.
Mradi wa 100% Zanzibari umedhaminiwa na Ubalozi wa Norway pamoja na kampuni ya mawasiliano ya Zantel.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...